Kutoka Tume ya Nyalali hadi Samia: Mnyika asimulia hotuba ya Lissu

Lissu: Lengo la kualika waandishi wa habari kwa sehemu hiyo lilikuwa nini?
Mnyika: Lengo lilikuwa kuwapa nafasi ya kuchukua habari na kuzifikisha kwa umma kuhusu madai yetu ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria ili kuwezesha uchaguzi huru na wa haki chini ya kaulimbiu ya No Reforms, No Election; bila ya mabadiliko hakuna uchaguzi.
Lissu: Unaposema hotuba ya mwenyekiti ndiyo ilikuwa ndefu, unamaanisha nini?
Mnyika: Katika muda wa masaa matatu, masaa mawili na zaidi alizungumza mwenyekiti wa chama.
Lissu: Waeleze majaji hotuba hiyo ndefu ilihusu nini.
Mnyika: Mwenyekiti alieleza historia ndefu ya madai ya kutaka haki kuanzia kabla na baada ya Tume ya Rais maarufu kama Tume ya Nyalali kati ya mwaka 1991 na 1992. Aliendelea kuzungumzia mabadiliko ya kikatiba na kisheria ya kuwezesha uchaguzi huru na wa haki yaliyokataliwa na serikali ya chama kimoja wakati huo, CCM.
Lissu: Suala lingine nililolizungumzia?
Mnyika: Alieleza madhara ya kutofanyika kwa mabadiliko hayo kuanzia uchaguzi wa mwaka 1995.
Pia alieleza maoni ya tume nyingine zilizoundwa kushughulikia mambo ya kikatiba wakati wa uchaguzi. Alitaja Tume ya Kisanga, akataja Tume au Kamati ya Bomani, na akaeleza kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba kati ya mwaka 2011 hadi 2014, maarufu kama Tume ya Warioba, na jinsi CCM ilivyotumia wingi wake katika Bunge la Katiba kukwamisha mchakato huo.
Pia alieleza madhara ya kukosekana kwa mabadiliko hayo kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, uchaguzi wa vijiji na vitongoji wa mwaka 2019, uamuzi wa Chadema kujitoa kwenye uchaguzi baada ya wagombea wengi wa Chadema kuondolewa kwenye uchaguzi, na yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo yeye alikuwa mgombea urais.
Alieleza baadhi ya wagombea kuenguliwa kwa mapingamizi yasiyokuwa na msingi, na wale waliobaki kufungiwa kampeni. Pia alieleza kuwa siku ya kura mawakala wa Chadema waliondolewa vituoni katika maeneo mengi na kwamba kura ziliingizwa kwenye vituo vya kupigia kura zikiwa zimeshapigwa.
Pia alieleza kuhusu hatua ambazo chama kilichukua baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 wakati huo mwenyekiti wa chama akiwa Freeman Mbowe, akidai mabadiliko ya kikatiba na tume huru ya uchaguzi. Alisema matokeo yake ni Mbowe kubambikizwa kesi ya ugaidi na kukaa rumande gerezani kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2022.
Alieleza kuwa baada ya kesi hiyo kufutwa na Mbowe kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu mwaka 2022, ndipo mazungumzo kati ya Chadema na CCM pamoja na serikali yalipoanza.
Akaeleza kuwa katika mazungumzo hayo upande wa Chadema uliwasilisha kwa mdomo na kwa maandishi mapendekezo ya maeneo ya marekebisho ya kikatiba ili kuwezesha uchaguzi huru na wa haki. Alisema baada ya mwaka mmoja wa mazungumzo, upande wa CCM na serikali ulijibu kwa mdomo kukataa mapendekezo yote ya marekebisho ya Katiba yaliyolenga kuwezesha uchaguzi huru na wa haki, na hatimaye mazungumzo yakavunjika.
Lissu: Subiri, waeleze waheshimiwa majaji hayo mazungumzo na mapendekezo yalikuwa yanahusu uchaguzi gani?
Mnyika: Yalikuwa yanahusu uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Lissu: Waeleze majaji ushiriki wako katika mazungumzo hayo.
Mnyika: Mimi nilikuwa miongoni mwa timu iliyokutana na Rais tarehe 22 Mei 2022. Katika kikao hicho, mapendekezo ya namna ya kukwamua na kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya yaliwasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa wakati huo, Freeman Mbowe.
Lissu: Waeleze majaji kulikuwa na nini baadaye?
Mnyika: Mapendekezo ya hoja nyingine kumi za mazungumzo, mojawapo ikiwa ni marekebisho ya kikatiba na kisheria ya kuwezesha uchaguzi huru na wa haki, yaliwasilishwa na mimi.
Lissu: Uchaguzi huru wa mwaka gani?
Mnyika: Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024. Mapendekezo hayo yalihusu kufanyika kwa marekebisho ya kuwezesha uchaguzi huru na wa haki tuliyoyaita Minimum Reforms.
Lissu: Baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo, nini kiliendelea?
Mnyika: Rais aliahidi kwamba mchakato wa mazungumzo utaendelea, na akaahidi kuunda timu ya watu watano ikiongozwa na Abdulrahman Kinana ambaye wakati huo alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM. Sisi kwa upande wetu, aliyekuwa mwenyekiti wetu pia aliahidi kuunda timu ya watu watano, na aliunda.
Lissu: Mazungumzo hayo yaliendelea hadi lini?
Mnyika: Mazungumzo yaliendelea hadi tulipojibiwa na upande wa pili kwamba marekebisho hayo yasubiri hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Hata yale tuliyoyaita Minimum Reforms, kama kuwa na tume huru ya uchaguzi, matokeo ya urais kupingwa mahakamani, maamuzi ya tume kufanyiwa mapitio, na tume kuwa na watumishi wake huru. Walieleza kuwa mradi yanagusa marekebisho ya Katiba, yasubiri mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Nzengeli: Waheshimiwa majaji, muda si rafiki na tumepokea maombi kutoka kwa watu wa usalama. Tunaomba tuishie hapo kutokana na muda.
Jaji: Mshitakiwa, wewe umechoka?
Lissu: Ombi linahusu masuala ya kiulinzi, sasa mimi siwezi kufahamu, lakini tukubali tu kwamba saa kumi na moja hii inatosha.
Jaji: Tunaahirisha hadi siku ya Jumatatu saa tatu asubuhi.




















