Moja kwa moja, Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu yaanza

Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu inaendelea leo siku ya Jumatatu ambapo mshtakiwa anatarajiwa kujitetea mbele ya mahakama.

Muhtasari

Moja kwa moja

Elizabeth Kazibure & Rashid Abdallah

  1. Lissu: Nimezuiwa kukutana na mashahidi gerezani

    .

    Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ametoa malalamiko mbele ya mahakama iliyomkuta na kesi ya kujibu katika tuhuma za uhaini, akisema baadhi ya viongozi wa chama chake aliowataja kuwa mashahidi wanazuiwa kumtembelea akiwa kizuizini.

    “Nimekuwa na matatizo makubwa ya haki ya mtu kukutana na mawakili wake na mashahidi wake. Hawa watu nimewataja kama mashahidi wanaotoka Chadema wamepigwa marufuku kunitembelea gerezani,” Lissu amesema.

    Lissu ameiomba mahakama itoe amri ili aweze kukutana na mashahidi wake.

    Soma Zaidi Hapa:

  2. Lissu aomba Samia na viongozi wakuu wa serikali kuwa mashahidi

    .

    Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ameliambia jopo la majaji waliomkuta na kesi ya kujibu kuhusu tuhuma za uhaini kuwa atajitetea mwenyewe.

    Pia, Lissu amesema ataomba mashahidi wafuate, ambao ataiomba mahakama iwapelekee wito wa kuitwa. Amemtaja shahidi wa kwanza kuwa ni Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Rais wa Tanzania.

    Mwingine ni Philip Mpango, ambaye wakati wa matukio yanayolalamikiwa alikuwa mjumbe wa Baraza la Taifa na kiongozi namba mbili serikalini.

    Kassim Majaliwa, wakati matukio hayo yanatokea, alikuwa Waziri Mkuu na kiongozi anayesaidia serikali katika masuala ya usalama wa taifa.

    Lissu pia amemtaja shahidi wa nne, Camillus Wambura, ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania.

    Shahidi wa tano ni Jenerali John Jacob Mkunda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania.

    Shahidi wa sita ni Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS).

    Shahidi wa saba ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ramadhani Kindai.

    Wengine ni John Mnyika, Katibu Mkuu wa CHADEMA, ambaye amesema ndiye mtendaji mkuu wa chama na anaweza kutoa ushahidi, kwani aliandaa mkutano huo na alikuwapo.

    Shahidi wa tisa ni Amani Sam Molugwa, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA.

    John Heche ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA.

    Mwingine ni Brenda Upia, shahidi wa kumi na mmoja, ambaye ndiye aliyewaalika watu wa Jambo TV kwenye mkutano huo.

    Soma Zaidi Hapa:

  3. Lissu ana kesi ya kujibu ya tuhuma za uhaini - Mahakama

    k

    Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa uamuzi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, na kumkuta ana kesi ya kujibu.

    Akisoma uamuzi huo, Jaji Ndunguru, anayeongoza jopo la majaji linalosikiliza shauri hilo, amesema baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka unaowakilishwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), mahakama imejiridhisha kuwa kuna ushahidi wa kutosha unaomfanya Lissu awe na kesi ya kujibu.

    Uamuzi huo unamaanisha kuwa kesi hiyo sasa inaingia katika hatua muhimu ambapo Tundu Lissu atapewa fursa ya kuwasilisha utetezi wake mbele ya mahakama.

    Katika hatua hiyo, upande wa utetezi unaweza kuwasilisha ushahidi pamoja na kuwaita mashahidi wake ili kujibu hoja na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

    Lissu alikamatwa mkoani Ruvuma kabla ya kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam, ambako alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa rasmi mashtaka yanayohusiana na uhaini pamoja na makosa mengine yanayodaiwa kuhusiana na kauli na shughuli zake za kisiasa.

    Upande wa mashtaka umekuwa ukidai kuwa baadhi ya kauli na matendo ya Lissu yalilenga kuzuia au kuvuruga mchakato wa uchaguzi mkuu na kuchochea uasi dhidi ya serikali. Madai hayo ndiyo ambayo yamekuwa msingi wa mashtaka yanayomkabili mwanasiasa huyo.

    Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya Tanzania kutokana na uzito wa mashtaka pamoja na nafasi ya Lissu katika siasa za Tanzania. Mwenendo wa kesi hiyo pia umeibua mjadala mkubwa kuhusu haki za kisiasa, uhuru wa kujieleza na namna sheria za uhaini zinavyotumika katika mazingira ya kisiasa.

    Jumuiya na taasisi mbalimbali za kimataifa zimeonyesha wasiwasi kuhusu mwenendo wa kesi hiyo na zimekuwa zikitoa wito wa kuhakikisha mchakato wa kisheria unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia haki za msingi za mshtakiwa.

    Baadhi yao wamekuwa wakitaka mamlaka kuhakikisha kuwa Lissu anapata dhamana, matibabu na mazingira yote muhimu ya kisheria yanayostahili, huku wengine wakitoa wito wa kuachiwa kwake.

    Hata hivyo, uamuzi wa mahakama kwamba Lissu ana kesi ya kujibu sio hukumu ya kuwa amepatikana na hatia. Ni hatua ya kisheria inayomaanisha kuwa mahakama imeona kuna msingi wa yeye kuitwa kutoa upande wake wa utetezi dhidi ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.

    Kwa sasa, macho yanaelekezwa katika hatua inayofuata ya kesi hiyo, ambapo Tundu Lissu atapata nafasi ya kujibu mashtaka, kupinga ushahidi uliowasilishwa dhidi yake na kuwasilisha ushahidi wa upande wa utetezi.

  4. Maombi yakiendelea mahakamani

    Maelezo ya video, Raia wanaotaka kuingia wanaambiwa mahakama imejaa.

    Raia wanaotaka kuingia wanaambiwa mahakama imejaa.

  5. Kesi ya Lissu: Hali ilivyo ndani ya mahakama

    Maelezo ya video, Kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa Chadema Tundu Lissu nchini Tanzania inatarajiwa kuanza

    Kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa Chadema Tundu Lissu nchini Tanzania inatarajiwa kuamuliwa.

  6. Lissu: Ulinzi umeimarishwa nje na ndani ya mahakama

    .
    .

    Chanzo cha picha, BBC.

    .
    Maelezo ya picha, Ndani ya mahakama

    Ulinzi umeimarishwa huku baadhi ya wafuasi wakizuiwa kuingia mahakamani.

    Raia wanaotaka kuingia wanaambiwa kuwa mahakama imejaa.

    .
  7. Fahamu mambo muhimu kuhusu kesi ya uhaini ya Lissu

    .

    Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CHADEMA, anakabiliwa na kesi ya uhaini nchini Tanzania. Usikilizwaji wa kesi hiyo unaendelea katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, huku upande wa Jamhuri ukiendelea kuwasilisha mashahidi wake. Kufikia jana, mashahidi 17 walikuwa wamefika kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

    1. Kesi ya Lissu inahusu nini?

    Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anakabiliwa na shtaka la uhaini nchini Tanzania.

    Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, na imekuwa ikiendelea kwa awamu huku upande wa Jamhuri ukiwasilisha ushahidi wake.

    2. Lissu alikamatwa lini?

    Lissu alikamatwa Aprili 8, 2025, na siku moja baadaye akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambako alisomewa shtaka la uhaini.

    Hapo ndipo mchakato wa kesi ulipoanzia kabla ya shauri hilo kuendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

    3. Kesi ilifikaje Mahakama Kuu?

    Baada ya hatua za awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi ya uhaini iliendelea katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

    Huko, upande wa Jamhuri ulianza kuwasilisha ushahidi na mashahidi wake katika kuunga mkono mashtaka dhidi ya Lissu.

    Na mpaka sasa, mashahidi 17 wametoa ushahidi wao hadi Agosti 13, 2026.

    4. Kwa nini kesi ilisimama kwa miezi mitano?

    Hili ni moja ya mambo muhimu katika historia ya kesi hiyo.

    Mwezi Februari 2026, Jamhuri iliwasilisha notisi ya kutaka kuongeza ushahidi mpya katika kesi hiyo.

    Lissu alipinga hatua hiyo, na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ikatupilia mbali notisi ya Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi huo mpya.

    Jamhuri haikukubaliana na uamuzi huo. Ilipeleka suala hilo katika Mahakama ya Rufani, ikiomba mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu.

    Kutokana na shauri hilo, Mahakama Kuu ilisimamisha usikilizwaji wa kesi ya uhaini hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi.

    Hivyo, kesi hiyo ilisimama kwa takribani miezi mitano kuanzia Februari 2026.

    5. Nini kilitokea Mahakama ya Rufani?

    Baada ya suala hilo kufikishwa Mahakama ya Rufani, mahakama hiyo ilitoa uamuzi kuhusu hoja iliyokuwa imewasilishwa na Jamhuri.

    Lissu alishinda katika suala hilo, na hivyo kuondoa kikwazo cha kisheria kilichokuwa kimesababisha usikilizwaji wa kesi kusimama.

    Baada ya uamuzi huo, kesi ilirejea Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wake.

    6. Kesi ilianza tena lini?

    Baada ya kusimama kwa takribani miezi mitano, usikilizwaji wa kesi ulianza tena Agosti 10, 2026.

    Tangu kurejea kwake Mahakama Kuu, upande wa Jamhuri umeendelea na uwasilishaji wa ushahidi.

    7. Nini kimejitokeza katika ushahidi wa mashahidi?

    Katika hatua ya sasa ya kesi, Lissu amekuwa akiwahoji mashahidi wa Jamhuri kuhusu ushahidi waliowasilisha na taarifa walizowahi kutoa katika hatua za uchunguzi.

    Katika ushahidi wa Agosti 12, kwa mfano, Lissu alimuuliza shahidi kuhusu tofauti kati ya maelezo aliyowahi kutoa kwa maandishi na majibu ya mdomo aliyoyatoa mahakamani. Shahidi alisema hakuwa ameeleza sababu ya tofauti hiyo kwa maandishi, lakini akiongozwa na wakili wa Serikali alisema alikuwa akijibu maswali kwa namna alivyoulizwa na mshitakiwa.

    Lissu pia aliuliza kuhusu video zilizotumika katika uchunguzi. Shahidi alisema polisi walitazama video iliyokuwa mtandaoni, lakini hawakuangalia video iliyokuwa kwenye kadi ya kumbukumbu (memory card) na flash disk zilizotajwa mahakamani.

    Kuanzia Agosti 10 hadi 12, shahidi wa 16 wa Jamhuri alimaliza kutoa ushahidi. Agosti 13 alianza shahidi wa 17, na leo, Agosti 14, ushahidi unaendelea.

  8. Kesi ya Lissu: Je, Tundu Lissu kuachiwa ama ana kesi ya kujibu?

    .
    Maelezo ya picha, Tundu Lissu

    Uamuzi kuhusu kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa Chadema Tundu Lissu nchini Tanzania unatarajiwa kutolewa hii leo.

    Hii ni baada ya Upande wa mashtaka kufunga Ushahidi wake siku ya Jumatano.

    Hii leo Majaji wa mahakama hiyo wanatarajiwa kutoa uamuzi iwapo Lissu ataachiliwa ama ana kesi ya Kujibu.

  9. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja hii leo

  10. Uamuzi kuhusu kesi ya Lissu Agosti 21

    Upande wa Mashataka unawasilisha:

    Wakili wa Serikali: Kwanza, tunaomba hilo la kulipwa fidia tuliache kwanza.

    Mawasilisho yetu yanatokana na makosa ambayo mshtakiwa ameshtakiwa nayo. Tunaona ana kesi ya kujibu.

    Mshtakiwa alitengeneza nia ya kuzuia uchaguzi na kwa nia ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

    Mahakama yenu haipaswi kuangalia uzito na credibility ya ushahidi katika hatua hii. Haya si maneno yangu, ni maneno ya Court of Appeal of Tanzania, katika kesi ya Philipo Mtonda, Criminal Appeal No. 217.

    Kwa kuzingatia shtaka ambalo mshtakiwa ameshtakiwa nalo, kama ushahidi unatosha kumtia hatiani, na katika hati yetu ya mashitaka, utagundua viini vitatu:

    Kwanza, je, mshtakiwa ni mwenye kosa dhidi ya Jamhuri?

    Pili, je, mshtakiwa alitengeneza nia ya kufanya kosa?

    Na tatu, je, alifanya kitendo kinachohusiana na kosa hilo?

    Kama alivyoeleza PW16, maneno ya mshtakiwa yalilenga kuitishia Serikali, kwa maana kwamba Serikali ndiyo mlizi wa sheria.

    Na kwa maneno yale kulikuwa na nia ya kuvuruga uchaguzi.

    PW3 alisema hivyo, na sisi tunakubaliana kama walivyosema mashahidi wetu.

    Na sisi tunaona mshtakiwa anapaswa kupewa nafasi ya utetezi. Kwa sababu, kwa mujibu wa hati ya mashitaka, nia ya kosa ilithibitishwa kwa kutoa kauli na kuchapisha kauli ili umma uwe instigated (kuchochea umma)

    Na mashahidi wa kutosha tumewaleta hapa mahakamani.

    Kwa hiyo, kitendo cha kutoa na kuchapisha kauli hizo, kama hati ya mashitaka ilivyo, kitendo kile kinaonyesha nia (ya kufanya kosa).

    PW1 alisema walimpa mshtakiwa nafasi (ya kujieleza), ili aoneshe kama kulikuwa na maana nyingine zaidi ya kuitishia Serikali.

    Na mshtakiwa aliomba atoe ushahidi Mahakamani.

    Kwa hiyo, kwa ushahidi wote huo, mshtakiwa atiwe hatiani (kwenye hatua hii apewe nafasi ya kujitetea) na atoe utetezi wake.

    Ni hayo tu, waheshimiwa majaji.

    Jaji Dunstan Ndunguru:

    “Tunachohitaji ni muda tusome (mawasilisho, na tutatoa uamuzi tarehe 21 saa tano asubuhi.”

    Shauri limeahirishwa hadi tarehe 21 Agosti 2026 saa tano asubuhi.

  11. Lissu: 'Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi yangu'

    .

    Lissu: Baada kusikiliza ushahidi wao na mashahidi wao 17 naomba kutoa hoja kwenu majaji kwamba upande wa mashitaka umeshindwa kabisa kuthibitisha kwamba kuna kesi ya uhalifu ya kuiwezesha mahakama hii kumtaka mshitakiwa ajiteteee

    Lissu: asa waheshimiwa majaji 'prima face case' ni ushahdi unaotolewa na upande wa mashitaka na usipojibiwa na upande wa utetezi mahakama inaweza kumhukumu huyo mtuhumiwa, na kwa kesi kama ya uhaini anahukumiwa kifo.

    Kwa hiyo, ili mshtakiwa ahitajike kujitetea, lazima masharti ya kifungu cha 312, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao, yatimizwe; yaani kuwe na ushahidi unaoonyesha kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu. Kama hakuna, mahakama inatakiwa kumwachilia huru.

    Na kwa hiyo, hoja yangu ni hii: Shauri hili, ili likamilike na mshtakiwa aweze kuhukumiwa kwa uhaini na kuhukumiwa kifo, lazima uwe umeonyesha kwamba kulikuwa na kosa la uhaini.

    Lissu: Shitaka ambalo liko mbele yenu, waheshimiwa majaji, ambalo ndilo shitaka la uhaini katika kesi hii, linasema kwamba Lissu alitengeneza maneno ya kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kuchapisha maneno na matendo ya kosa linalodaiwa kuwa linatishia Serikali au Bunge au Mahakama.

    Kwa hayo maneno, Serikali haijatajwa hata mara moja. Bunge wala Mahakama havijatajwa hata mara moja.

    Na kwa ushahidi wa mashahidi wote 17 wa upande wa mashtaka, Serikali haimo.

    Lissu: Maana ya Serikali ni nini?

    Serikali imetafsiriwa na Katiba, Ibara ya 151. Serikali ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au Halmashauri.

    Hakuna aliyethibitisha hata mmoja kwamba Serikali imetajwa kwenye maneno yanayodaiwa kuwa ya kihaini.

    Uchaguzi mkuu, kwa mujibu wa sheria, unaendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa hiyo, ukiangalia hati ya mashitaka, Serikali haijatajwa na haijatishiwa. Hakuna ushahidi wa kuthibitisha kwamba Serikali ilitishiwa wakati haijatajwa popote.

    Jambo la pili: Hayo maneno yanatengeneza kosa gani kwa mujibu wa sheria za nchi hii?

    Kwenye orodha ndefu ya makosa ya jinai, hakuna kosa la kuzuia uchaguzi wala kukinukisha uchaguzi. Hakuna kosa la aina hiyo kwenye Kanuni ya Adhabu.

    Kwa hiyo, kosa la kufanya kisa cha uhaini halipo, na kwa mujibu wa sheria, nia ya kutenda kosa haipo.

    Kwa hiyo, upande wa mashtaka umeshindwa kabisa kuthibitisha hayo madai.

    Na mahakama ni muhimu ikumbuke kwamba mimi ndiye niliyeshtakiwa pekee katika kesi hii.

    Na sheria inasema maneno ya mtu mmoja hayafanyi uhaini. Na ushahidi uliotolewa haujathibitisha nia ya kutenda kosa la uhaini.

    Kwa hiyo, mtu huyu hatakiwi kuitwa kujitetea. Na nikiitwa kujitetea, nitajitetea kwa kitu gani?

    Kwa hiyo, kwenye hoja hiyo, waheshimiwa majaji, sina kesi ya kujibu. Sina kesi ya kunitaka kula kiapo na kujitetea.

    Kuhusu masuala ya kuchapisha Tundu Lissu anasema:

    Hoja si hiyo tu.

    Ili kuwe na uhaini, lazima kuwe na proof of publication au matendo ya wazi.

    Upande wa mashtaka umefeli. Mimi nilichapisha maneno hayo kwenye mtandao wa Jambo TV. Ushahidi uliotakiwa uwepo ni ushahidi wa Jambo TV.

    Naomba mnielekeze ukurasa wa 135 kwenye rekodi za Mahakama.

    Waliorodhesha (waliwasilisha) ushahidi wa aina tisa na ushahidi wa video, na hawajaleta hata kimoja kati ya vyote 11.

    Mlisema mtaleta video. Iko wapi? Kama hakuna video, hakuna kesi. Hakuna uthibitisho kwamba nilichapisha chochote popote.

    Waheshimiwa majaji, kuhusiana na huo ushahidi wa publication (kuchapisha), hati ya mashitaka inasema mimi ndiye nilichapisha.

    Shahidi wa 17 wa mashtaka alisema nini? Shahidi pekee ambaye ni eyewitness ni PW17. PW17 alinisikia na kuniona.

    Ushahidi wa PW unatakiwa kupewa uzito, na aliambia Mahakama hii kwamba yeye ndiye aliyepiga picha/video hizo.

    Kwenye kilelezo cha 16, amesema:

    “Sisi ndio tulirekodi, tukahifadhi na kusambaza.”

    Na ushahidi wao wala sijamleta mimi.

    Shahidi wao amesema zaidi ya kuhutubia sikufanya kingine chochote.

    Na amesema video hizo ziko hadi leo.

    Kwa hiyo, ni tuhuma ya uongo, na ni ushahidi wao wenyewe.

    Na ushahidi wake unapingana na ushahidi wa nani aliyepublish. Hawana jibu.

    Shahidi wao ameambia mahakama kwamba aliyeitisha mkutano ni Afisa Habari wa CHADEMA.

    Nilimuuliza anaitwa nani, akasema anaitwa Brenda Rupia.

    Na nilipomuuliza, “Uliniona nikipanga viti, nafuta meza?” Akasema, “Hapana.”

    Hakuna proof of publication (hakuna uthibitisho).

    Lissu; Kwa hiyo, ninaomba mfanye uamuzi kwamba hakuna kesi ya kujibu.

    Hakuna kesi ya kusimama mbele ya Mahakama hii na kujitetea.

    Naomba mfanye hivyo leo, nisirudi gerezani.

    Ni hayo tu, waheshimiwa majaji.

  12. Fahamu mambo muhimu kuhusu kesi ya uhaini ya Lissu

    .

    Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CHADEMA, anakabiliwa na kesi ya uhaini Tanzania. Usikilizwaji wa kesi hiyo unaendelea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, huku upande wa Jamhuri ukiendelea kuwasilisha mashahidi wake. Kufikia jana, mashahidi 17 walikuwa wamefika kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

    1. Kesi ya Lissu inahusu nini?

    Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anakabiliwa na shtaka la uhaini nchini Tanzania.

    Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, na imekuwa ikiendelea kwa awamu huku upande wa Jamhuri ukiwasilisha ushahidi wake.

    2. Lissu alikamatwa lini?

    Lissu alikamatwa 8 Aprili 2025, na siku moja baadaye akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambako alisomewa shtaka la uhaini kama Mahakama ya ukabidhi.

    Hapo ndipo mchakato wa kesi ulipoanzia kabla shauri hilo kuendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

    3. Kesi ilifikaje Mahakama Kuu?

    Baada ya hatua za awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi ya uhaini iliendelea katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

    Huko, upande wa Jamhuri ulianza kuwasilisha ushahidi na mashahidi wake katika kuunga mkono mashtaka dhidi ya Lissu. Na Mpaka sasa Mashahidi 17 wametoa ushahidi wao mpaka Agosti 13, 2026.

    4. Kwa nini kesi ilisimama kwa miezi mitano?

    Hili ni moja ya mambo muhimu katika historia ya kesi hiyo.

    Februari 2026, Jamhuri iliwasilisha notisi ya kutaka kuongeza ushahidi mpya katika kesi hiyo.

    Lissu alipinga hatua hiyo, na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam ikatupilia mbali notisi ya Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi huo mpya.

    Jamhuri haikukubaliana na uamuzi huo. Ilipeleka suala hilo Mahakama ya Rufani, ikiomba mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu.

    Kutokana na shauri hilo, Mahakama Kuu ilisimamisha usikilizwaji wa kesi ya uhaini hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi.

    Hivyo, kesi hiyo ilisimama kwa takribani miezi mitano kuanzia Februari 2026.

    5. Nini kilitokea Mahakama ya Rufani?

    Baada ya suala hilo kufikishwa Mahakama ya Rufani, mahakama hiyo ilitoa uamuzi kuhusu hoja iliyokuwa imewasilishwa na Jamhuri.

    Lissu alishinda katika suala hilo, na hivyo kuondoa kikwazo cha kisheria kilichokuwa kimesababisha usikilizwaji wa kesi kusimama.

    Baada ya uamuzi huo, kesi ilirejea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wake.

    6. Kesi ilianza tena lini?

    Baada ya kusimama kwa takribani miezi mitano, usikilizwaji wa kesi ulianza tena Agosti 10, 2026.

    Tangu kurejea kwake Mahakama Kuu, upande wa Jamhuri umeendelea na uwasilishaji wa ushahidi.

    7. Nini kimejitokeza katika ushahidi wa mashahidi?

    Katika hatua ya sasa ya kesi, Lissu amekuwa akiwahoji mashahidi wa Jamhuri kuhusu ushahidi waliowasilisha na taarifa walizowahi kutoa katika hatua za uchunguzi.

    Katika ushahidi wa Agosti 12, kwa mfano, Lissu alimuuliza shahidi kuhusu tofauti kati ya maelezo aliyowahi kutoa wa maandishi na majibu ya mdomo aliyoyatoa mahakamani. Shahidi alisema hakuwa ameeleza sababu ya tofauti hiyo kwa maandishi, lakini akiongozwa na wakili wa Serikali alisema , alikuwa akijibu maswali kwa namna alivyoulizwa na mshitakiwa.

    Lissu pia aliuliza kuhusu video zilizotumika katika uchunguzi. Shahidi alisema polisi walitazama video iliyokuwa mtandaoni, lakini hawakuangalia video iliyokuwa kwenye memory card na flash disk zilizotajwa mahakamani.

    Kuanzia Agosti 10 mpaka 12, shahidi wa 16 wa Jamhuri alimaliza kutoa ushahidi. Agosti 13 akaanza shahidi wa 17, ambapo leo, Agosti 14 ushahidi unaendelea.

  13. Lissu: 'Sina shida na kufungwa kwa kesi'

    .
    Maelezo ya picha, Tundu Lissu

    Lissu: 'Waheshimiwa Majaji nashukuru nimemsikiliza wakili wa serikali Nasoro Katuga kwa umakinj sana, swala la kufunga kesi kwa upande wa mashitaka sina shida nalo nilisema tangu wiki iliyopita ila kama kuna kesi ya kujibu au la wakili wa serkali amesema hakuna kifungu ila kuna kifungu kinachoelekeza nini cha kufanya wakati wa kufunga kesi 312 (1) cha sheria ya mwenendo wa mashitaka (CPA)'

    'Mahakama itarekodi kwamba hakuna hatia kwa vile upande wa mashitaka umefunga kesi yao kilichobaki ni n kunisikiliza mimi na mawakili hawa wa serikali kujibu kama nina hatia au sina hatia ninaomba mtuongoeze'

    Wakili wa serikali Katuga: Ni kawaida kwa mahakama hii kufanya maamuzi kulingana na mazingira ya kesi na mtatoa nafasi kwa pande zote mbili sawa kwa sawa na busara yenu.

    Na tunaona mtuhumiwa hakatai ombi letu la kuwasilisha hoja na ameweka maombi kabla mahakama hii haijaamua . Tunaona yeye yuko tayari. tunaiachiiia mahakama yenu tukufu

    Lissu: Waheshimiwa majaji hili jambo ni dogo na halihitaji mvutano na ombi la kutamka kama kuna hatia au la kisheria linawapa majaji nguvu za kuamua

  14. Habari za hivi punde, Serikali yafunga ushahidi wake dhidi ya Tundu Lissu

    Serikali ya Tanzania imefunga Ushahidi wake kwenye kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu .

    Kupitia wakili wa serikali Nassoro Katuga taatifa ya maombi ya kuufunga ushahidi huo iliwasilishwa mahakamani.

    Serikali imesema kwamba mashahidi ambao mpaka sasa wametoa ushahidi kwa upande wao wanatosha.

    “Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu kuwa upande wa Jamhuri baada ya kupitia ushahidi ambao tayari umewasilisha mahakamani na kuangalia ushahidi uliobakiwa kwa maana mashahidi waliobaki tumeuchambua na kuangalia hoja zilizokubaliwa upande wa jamhuri ukajikuta kwamba unaona ushahidi ambao tayari umeshautoa ni ushahidi toshelezi na kuleta ushahidi zaidi kuthibitisha hoja ambazo zilikubaliwa wakati wa hoja za awali(Preliminary hearing)ni kinyume cha sheria.”

  15. Natumai hujambo na karibu tena katika kikao chengine cha kesi ya Tundu Lissu

  16. Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika: Mfike kwa wingi mahakamani Jumatatu

    Maelezo ya video, Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika awataka wafuasi kuhuduria kwa wingi mahakamani siku ya Jumatatu

    Baada ya kuahirishwa kwa shauri la uhaini linalomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, Katibu mkuu wa Chama hicho John Mnyika amewataka wapenzi na wafuasi wa chama hicho kuhuduria kwa wingi mahakamani siku ya jumatatu kwani ni dakika za mwisho kwa upande wa mashitaka kuwasilisha ushahidi wao.

  17. Kesi imeahirishwa mpaka Jumatatu

    .

    Jaji Nduguru - Tumesikia hoja ya ahirisho kuhusua afya ya shahidi na tumsikia mshitakiwa juu ya umuhimu wa shauri hili na kwa maelezo ya upande wa Jamuhuri kwamba Jumatatu wataleta mashahidi wao wote basi ni amri ya mahakama siku ya Junatatu wawalete mashahidi wao wote waliobaki, hivyo tunaahirisha shauri mpaka Jumatatu tarehe 17 /08/2026.

  18. "Mashahidi ni binadamu, changamoto inaweza kutokea"- Jamhuri

    Wakili wa serikali: Mashahidi nao ni wanadamu na kwa kuwa ni wanadamu changamoto inaweza kutokea kwa mwanadamu muda wowote. Sisi upande wa mashitaka ni ukweli tunakiri bado tuna mashahidi wengi lakini sio lazima tulete mashahidi wote, sio lazima, tunaleta namna tulivyopanga mpango wetu na vile tulivyojiandaaa.

    Wakili wa Serikali: Na mwenzetu wala asijisikie pengine labda ndio shahidi wa mwisho, kwa hiyo sheria inaruhusu kuahirishwa kwa shauri kwa sababu za msingi na sababu za maradhi ni za msingi kwa hiyo waheshimiwa majaji ni rai yetu tuaomba Mahakama yenu ihairishe shauri mpaka Jumatatu.

    Wakili wa Serikali: Na tutawaleta (mashahidi) wote sababu bado ni ndani ya kipindi hiki na sio kipindi kingine, ni hayo tu waheshimiwa Majaji.

  19. "Nikija kusema aitwe Samia si itachukua miaka mitano?" - Lissu

    .

    Kesi ya Lissu imeanza lakini upande wa mashataka, wanasheria wanaiomba Mahakama ihairishe kwa sababu shahidi wao amepata dharura. Wanaomba Jumatatu wataleta mashahidi wao wote.

    Lissu amesimama na kupinga hoja hiyo.

    Lissu: "Kulikua na amri mliyoitoa mwaka jana siwezi kukumbuka tarehe, kwamba upande wa mashitaka ulete mashahdi wawili kila kesi inaposikilizwa, na hii amri mmeirudia tena juzi jumatano mmeirudia jana, kwamba upande wa mashitaka walete mashahidi wengi.

    Lissu: Sasa waheshimiwa Majaji upande wa Mashitaka hautekelezi amri za Mahakama kwa sababu hamuwachukulii hatua, wanajua mtawakubalia. Lissu: Waheshimiwa majaji kusema maneno haya sio kitu chepesi kwangu ila mmeachia amri zenu kupuuzwa.

    Lissu: Sasa kwa vile mlisema jana na hawajaleta mashahidi naomba msikubali Mahakama kuu ya Tanzania ikageuzwa kama ile iliyomuhukumu Jomo Kenyatta, ikiwakubalia waleta mashitaka kila kitu na kuukatalia upande wa utetezi kila kitu.

    Lissu: Kwanini hawapo tayari kuheshimu amri ya Mahakama. Kama pumzi imekata wafunge ushahidi twende hatua inayofuata. Kama hawako tayari kuendelea wafunge kesi. Msikubali kugeuzwa kama hiyo mahakama niliyoisema.

    Lissu: Again for the record (kwa kumbukumbu) hii ndio kesi kubwa zaidi kwa Jamuhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba, lazima Mahakama ioneshe umuhimu kwa namna inavyosimamia amri zake na maamuzi inayofanya. Hatutembelei njia ambayo haijafagiliwa, kesi ya uhaini ya kwanza ilichukua miezi sita na siku 17 miaka ya 1970. Na ikasafishwa tena miaka ya 1982 na 1983 kesi ilichukua mwaka mmoja na siku 17 chumba hiki hiki.

    Lissu: Leo ni siku ya 495, mwaka mmoja na zaidi ya miezi minne hatujamaliza mashahidi wa upande wa mashitaka nikija kusema aitwe Samia si itachukua miaka mitano, na Philip Mpango na IGP Wambura mtakuwa mmestaafu hawajaitwa. Naomba msiwakubalie walete mashahidi tuendelee na kesi.

  20. Mahakama imeanza, Lissu anazungumza sasa

    .
    .
    .
    .