Moja kwa moja, Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu yaanza

Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu inaendelea leo siku ya Jumatatu ambapo mshtakiwa anatarajiwa kujitetea mbele ya mahakama.

Muhtasari

Moja kwa moja

Elizabeth Kazibure & Rashid Abdallah

  1. Mambo muhimu kuhusu kesi ya uhaini ya Lissu

    Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CHADEMA, anakabiliwa na kesi ya uhaini Tanzania. Usikilizwaji wa kesi hiyo unaendelea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, huku upande wa Jamhuri ukiendelea kuwasilisha mashahidi wake. Kufikia jana, mashahidi 17 walikuwa wamefika kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

    1. Kesi ya Lissu inahusu nini?

    Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anakabiliwa na shtaka la uhaini nchini Tanzania.

    Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, na imekuwa ikiendelea kwa awamu huku upande wa Jamhuri ukiwasilisha ushahidi wake.

    2. Lissu alikamatwa lini?

    Lissu alikamatwa 8 Aprili 2025, na siku moja baadaye akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambako alisomewa shtaka la uhaini kama Mahakama ya ukabidhi.

    Hapo ndipo mchakato wa kesi ulipoanzia kabla shauri hilo kuendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

    3. Kesi ilifikaje Mahakama Kuu?

    Baada ya hatua za awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi ya uhaini iliendelea katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

    Huko, upande wa Jamhuri ulianza kuwasilisha ushahidi na mashahidi wake katika kuunga mkono mashtaka dhidi ya Lissu. Na Mpaka sasa Mashahidi 17 wametoa ushahidi wao mpaka Agosti 13, 2026.

    4. Kwa nini kesi ilisimama kwa miezi mitano?

    Hili ni moja ya mambo muhimu katika historia ya kesi hiyo.

    Februari 2026, Jamhuri iliwasilisha notisi ya kutaka kuongeza ushahidi mpya katika kesi hiyo.

    Lissu alipinga hatua hiyo, na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam ikatupilia mbali notisi ya Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi huo mpya.

    Jamhuri haikukubaliana na uamuzi huo. Ilipeleka suala hilo Mahakama ya Rufani, ikiomba mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu.

    Kutokana na shauri hilo, Mahakama Kuu ilisimamisha usikilizwaji wa kesi ya uhaini hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi.

    Hivyo, kesi hiyo ilisimama kwa takribani miezi mitano kuanzia Februari 2026.

    5. Nini kilitokea Mahakama ya Rufani?

    Baada ya suala hilo kufikishwa Mahakama ya Rufani, mahakama hiyo ilitoa uamuzi kuhusu hoja iliyokuwa imewasilishwa na Jamhuri.

    Lissu alishinda katika suala hilo, na hivyo kuondoa kikwazo cha kisheria kilichokuwa kimesababisha usikilizwaji wa kesi kusimama.

    Baada ya uamuzi huo, kesi ilirejea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wake.

    6. Kesi ilianza tena lini?

    Baada ya kusimama kwa takribani miezi mitano, usikilizwaji wa kesi ulianza tena Agosti 10, 2026.

    Tangu kurejea kwake Mahakama Kuu, upande wa Jamhuri umeendelea na uwasilishaji wa ushahidi.

    7. Nini kimejitokeza katika ushahidi wa mashahidi?

    Katika hatua ya sasa ya kesi, Lissu amekuwa akiwahoji mashahidi wa Jamhuri kuhusu ushahidi waliowasilisha na taarifa walizowahi kutoa katika hatua za uchunguzi.

    Katika ushahidi wa Agosti 12, kwa mfano, Lissu alimuuliza shahidi kuhusu tofauti kati ya maelezo aliyowahi kutoa wa maandishi na majibu ya mdomo aliyoyatoa mahakamani. Shahidi alisema hakuwa ameeleza sababu ya tofauti hiyo kwa maandishi, lakini akiongozwa na wakili wa Serikali alisema , alikuwa akijibu maswali kwa namna alivyoulizwa na mshitakiwa.

    Lissu pia aliuliza kuhusu video zilizotumika katika uchunguzi. Shahidi alisema polisi walitazama video iliyokuwa mtandaoni, lakini hawakuangalia video iliyokuwa kwenye memory card na flash disk zilizotajwa mahakamani.

    Kuanzia Agosti 10 mpaka 12, shahidi wa 16 wa Jamhuri alimaliza kutoa ushahidi. Agosti 13 akaanza shahidi wa 17, ambapo leo, Agosti 14 ushahidi unaendelea.

  2. “Hakuna mtu wa CHADEMA atakayekudhuru,”- Lissu

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, iliendelea jana Alhamisi katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, huku shahidi wa 17 wa upande wa Jamhuri akianza kutoa ushahidi wake.

    Shahidi huyo, ambaye utambulisho wake umefichwa, alieleza kuwa ni mwandishi wa habari na kwamba majukumu yake ni kurekodi matukio kwa kutumia kamera. Alieleza Mahakama kuhusu tukio la Aprili 3, 2025 katika makao makuu ya CHADEMA, Mikocheni, ambako alikwenda na wenzake kwa ajili ya kuripoti mkutano wa chama hicho.

    Shahidi alisema walirekodi na kurusha mkutano huo, ambao ulihusu masuala ya uchaguzi na kaulimbiu ya CHADEMA ya “No reforms, no election”. Alisema miongoni mwa viongozi waliozungumza alikuwa Lissu, ambaye kwa mujibu wa shahidi alizungumzia namna ya kuzuia uchaguzi.

    Katika kumuuliza maswali, Lissu alihoji baadhi ya maelezo yaliyotolewa na shahidi huyo katika ushahidi wake na yale aliyoyaandika awali polisi.

    Wakati wa mahojiano hayo, Lissu pia alimwambia shahidi: “Hakuna mtu CHADEMA atakayekudhuru,” akimweleza kuwa licha ya yeye kuwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja, hakuna mwanachama wa chama hicho ambaye atamdhuru. Shahidi baadaye alisema alikuwa na hofu ya kutoa ushahidi hadharani kwa kuhofia huenda wafuasi wa chama hicho wakamdhuru, ingawa alisema hajawahi kutishiwa na mwanachama yeyote wa CHADEMA.

    Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo Ijumaa, Agosti 14, 2026. Lissu pia aliiomba Mahakama iamuru mawakili wake na mashahidi waruhusiwe kumuona akiwa gerezani.

  3. Kesi ya Lissu kuendelea leo Ijumaa

    Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, inatarajiwa kuendelea leo Ijumaa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, baada ya kuahirishwa jana.

    Jana, shahidi wa 17 wa upande wa Jamhuri, ambaye utambulisho wake umefichwa, alianza kutoa ushahidi kuhusu tukio la mkutano wa CHADEMA wa Aprili 3, 2025.

    Shahidi huyo alieleza Mahakama kuwa alifika katika makao makuu ya CHADEMA, Mikocheni, kwa ajili ya kurekodi na kurusha mkutano huo.

    Baada ya ushahidi wa msingi wa shahidi huyo, Lissu alianza kumuuliza maswali na kuhoji baadhi ya taarifa alizotoa pamoja na maelezo yake ya awali kwa polisi.

    Miongoni mwa mambo aliyomuuliza ni kama katika maelezo yake ya polisi aliwahi kusema kuwa maneno aliyoyasema Lissu katika mkutano huo yalikuwa uhaini.

    Leo, Mahakama inatarajiwa kuendelea na hatua inayofuata ya ushahidi wa shahidi huyo, kabla ya kesi kuendelea na mashahidi wengine wa upande wa Jamhuri.

  4. KARIBU KATIKA SIKU YA 5 YA MUENDELEZO WA KESI YA LISSU - IJUMAA 14.08.2026

  5. Shauri limeahirishwa mpaka kesho

    Mawakili

    Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu,imeahirishwa mpaka kesho Ijumaa Agosti 14, 2026, katika Mahakama Kuu Masijala Ndogo Dar es Salaam.

    Katika hatua nyingine, Lissu ameitaka mahakama iamuru mawakili wake na mashahidi waruhusiwe kumuona mahakamani na gerezani.

    "Ninaomba kwa amri ya mahakama waruhusiwe kuniona niko gerezani mwaka na zaidi wale wanaonisaidia waruhusiwe kuniona naomba mtoe maelekezo waruhusiwe kuja kuniona hapa na kule gerezani", alisema Lissu.

  6. "Ninaonewa tu, sina hatia, ninatuhumiwa kurusha matangazo"

    Lissu

    Kielelezo kimepokelewa na kupewa jina D16

    Lissu: Naomba apewe kielelezo D16.

    Shahidi anapewa.

    Lissu: Umesema mlipopangiwa kazi na Boss wako John Marwa ukiwa pamoja na P1 sasa embu soma kwenye kielelezo chako.

    Lissu: Tuendelee, umesema wazungumzaji wakuu kwenye mkutano huo walikuwa Lissu Heche na katibu mkuu hukumtaja jina ? embu angalia kielelezo kama kuna hayo maneno

    Shahidi P: Upo wewe peke yako.

    Lissu: Wala usiwe na wasiwasi nyie watu wangu hatugombani bwana hakuna katibu mkuu wala mnyika si kweli bwana P?

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Sasa shahidi leo umesema baada ya kupigiwa hiyo simu na boss wako ulikutana na afisa wa polisi uleyemkabidhi hiyo kadi na kuandika maelezo embu angalia maelezo yako kama hayo maneno yapo.

    Shahidi P: Haya maelezo hayapo.

    Lissu: Leo kwenye ushahidi wako umeulizwa siku hiyo ya mkutano ueleze muonekano wangu na ukajibu hivi alikuwa amevaa kombat ila rangi sikumbuki waeleze majaji kama yapo kwenye maelezo yako.

    Shahidi P: Hayapo

    Lissu: Uliulizwa walikuwa wanarejelea uchaguzi wa serikali za mitaa kuelekea uchaguzi mkuu yapo hayo maneno hayapo?

    Shahidi P: Hayapo

    Lissu: Umesema ulikuwa na wenzako mkiwa na kamera aina ya sonny NX kwemye maelezo yako mlikuwa na kamera tatu za sonny NX swali langu naomba uwathibitishie majaji kama ndio kamera yemyewe Sony HXA-MX100.

    Shahidi P: Ndio ni kamera hiyo hiyo Nx ni kifupi.

    Lissu: Naomba uthibitishe taarifa huo mkutano ulioelekezwa kuja ku cover alipata mwaliko toka kwa afisa habari wa Chadema.

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Waeleze majaji kama mimi ni afisa habari wa Chadema.

    Shahidi P: Hapana.

    Lissu: Asante usiwe na wasiwasi unafanya kitu cha heshima unatoa ushahidi wa ukweli wa Mungu

    Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu afisa habari Chadema anaitwa Brenda Rupia.

    Shahidi P: Ninafahamu

    Lissu: Kama nimekusikia sawa sasa umesema wewe na wenzako mlipofika HQ Chadema mlikuta wanachama wa chadema na watu wengine viongizi walikuwa hawajafika kweli sio kweli

    Shahidi P: Ni kweli

    Lissu: Waeleze majaji nani alikua anafanya maandalizi ya eneo la mkutano.

    Shahidi P: Sikuzingatia hilo

    Lissu: Waeleze majaji kama mimi nilikuwa sehemu ya wale waliokuwa wanafanya maandalizi kufuta vumbi na kukaribisha wageni.

    Shahidi P: Hapana.

    Lissu: Mtu akikuambia huo mkutano aliyekualika ni Tundu Lissu na aliyefanya maandalizi ni Lissu atakua anasema ukweli au uongo?

    Shahidi P: Si kweli

    Lissu: Sasa shahidi naomba uthibitisje kama ni kweli au sio kweli kina maneno yanayosema mlikua mnarusha matangazo yenu kwenye chaneli yenu ya Jambo na ikiwa yaliandikwa na wewe

    Shahidi P: Ya kwangu.

    Lissu: Naomba nikuhakishie pamoja na kwamba niko gerezani mwaka na zaidi hakuna mtu Chadema atakudhuru

    Lissu: Kuna baadhi ya video tulizirusha kwenye mitandao ya x na youtube ambazo jambo ilirusha mtu akiingia atazikuta zipo?

    Shahidi P: Ndio zipo

    Lissu: Bob Marley Alisema truth is never a sin

    Lissu: Sasa shahidi nimeshitakiwa kwa uhaini na nimekua gerezani tangu ta rehe 10/04/2025 sababu inadaiwa mimi ndio nilirusha hizo video na kuweka kwenye mitandao ya Jambo TV waeleze majaji kama hii tuhuma ni ya kweli ni wewe na wenzako mlirusha au ni mimi.

    Shahidi P: Sisi kupitia wewe.

    Lissu: Nyie ndio mlirusha kupitia mimi.

    Lissu: Waeleze majaji kama nilihusika na kamera zenu.

    Shahidi P: Hapana

    Lissu: Waeleze majaji kama niliwaelekeza kurusha hayo matangazo

    Shahidi P: Hapana.

    Lissu: Je niliwaelekeza baada ya kurusha mbashara mchapishe kwenye mitandao ya kijamii?

    Shahidi P: Hapana.

    Lissu: Ninaonewa tu sina hatia natuhumiwa kurusha tangazo

    Shahidi P: Ni kweli wanakutuhumu lakini ndio maana tuko hapa mahakami ujitetee

    Lissu: Ukisema ni kweli naenda kunyongwa hawa walioshitaki ndio wanachokitaka.

    Lissu: Hebu naomba waeleze majaji kama ni kweli au sio kweli wewe ni shahidi uliyekueko kwenye mkutano huo.

    Shahidi P: Kweli

    Lissu: Shahidi katika kielelezo 16 kuna maneno yanasema hivi yakiyokua yanayoongelewa ni mambo ya uchaguzi na kauli mbiu ya no reforms no election na changamoto zao majimboni.

    Shahidi P: Ni kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama viongozi wakiongea masuala ya uchaguzi na no reforms no election na matatizo ya majimboni kwao wanakuwa wamekosea

    Shahidi P: Hapana.

    Lissu: Kuna maneno yafuatayo nataka uyathibitishe mimi nakumbuka matukio yote yaliyokua yakifanyika kwenye mkutano huo na yako kwenye memory kadi niliyokukabidhi, memory kadi uliyomkabidhi inspekta Chulu ni kweli sio kweli

    Shahidi P: Ni kweli.

    Lissu: Video hizo hatujazifuta wala kuzihariri na mkutano ulifanyika kati ya saa mbili hadi tatu.

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: hiyo memori kadi uliyomkabidhi inspekta Chulu hawajaleta mahakamani wala sijaona wala majaji au leo umeileta mahakamani?

    Shahidi P: Hapana sijaleta

    Lissu: Walileta kitu kingine majaji wakakikataa Kwenye maelezo yako shahidi hakuna uliposema maneno aliyozungumza Lissu ni makosa waeleze majaji kama ni kweli au sio kweli.

    Shahidi P: Ni kweli.

    Lissu: Hakuna mahali umesema alichosema Lissu ni uhaini.

    Shahidi P: Ni kweli.

    Lissu: Hakuna mahali umesema wewe na wenzako kwa kurusha mtandaoni mlikua mnasambaza uhaini.

    Shahidi P: Ni kweli

    Lissu: Ni kweli au sio kweli nyie waandishi wa Jambo hamkuwa peke yenu na walikuwepo waandishi wa vyombo vingine na vyote vilikua vinarusha hayo matangazo.

    Shahidi P: Ni kweli walikuwa wanarekodi.

    Lissu: Waeleze majaji kama vyombo vyote hivyo vilikuwa vinarekodi maneno ya kihaini.

    Shahidi P: Sina hakika sababu mahakama haijathibitisha.

    Lissu: Na kulikuwa na wasikilizaji viongozi wa chadema na watia nia na wote walisikia haya maneno.

    Shahidi P: Kweli

    Lissu: Ieleze mahakama kama wewe na wote waliokuepo mmeshtakiwa kwa kutotoa taarifa baada ya kusikia maneno hayo ya njama za kihaini

    Shahidi P: Hapana

    Lissu: Je, kuna mtu mwingine ameshitakiwa isipokua Lissu?

    Shahidi P: Hapana

    Lissu: Umesema mlikua Dodoma kikazi na mwenzako uliyemtaja kama P2 maelezo ya P2 anasema yeye ni mkazi wa Songea na hajawahi kwenda Dodoma kwenye hizo tarehe yeye akasema alikuwa Songea hiyo wewe unasemaje bwana?

    Shahidi P: Ninachojua nilikua naye Dodoma

    Lissu: Waheshimiwa majaji sina swali jingine ahsante shahdi

    Shahidi anaruhusiwa kutoka. Upande wa jamuhuri hawana maswali ya Dodoso.

    Jaji kama tumekubaliana kuwe na mashahidi wa kutosha tulete mashahidi.

  7. Mliadhibiwa na mamlaka kwa kurusha mkutano wangu: Lissu

    Lissu

    Mahojiano yanaendelea..

    Wakili wa Serikali: Kwa namna unavyokumbuka yale maongezi walikuwa wanazungumzia uchaguzi gani?

    Shahidi P: Serikali za mtaa kuelekea uchaguzi mkuu.

    Wakili wa Serikali: Kwa shahidi huyu waheshimiwa majaji tunaomba tuishie hapa.

    Lissu: Shahidi unanisikia bwana, hujambo?.. ninaomba nikuulize maswali kidogo na uyajibu kwa kweli ya Mungu.

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Iambie mahakama kuwa ninyi waandishi wa Jambo mmefanya kazi na mimi kwa muda mrefu sana.

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Na weleze majaji kama ni kweli au sio kweli mmekuwa mkitangaza mikutano yangu karibu nchi nzima.

    Shahidi P: Kweli.

    Lissu: Na waeleze waheshimiwa majaji mara nyingine nyie jambo TV ni chombo pekee kilichorusha mikutano yangu sehemu mbalimbali nchi hii.

    Shahidi P: Kweli.

    Lissu: Na waeleze majaji kama ni kweli au si kweli hata niliporudi nchini kutoka uhamishoni Ulaya ninyi waandishi wa habari wa Jambo TV mlinisindikiza nyumbani kwetu.

    Shahidi P: Sikumbuki.

    Lissu: Kuna Shedrack Simba na Oscar ni kweli si kweli.

    Shahidi P: Ni kweli.

    Lissu: Hawa nimekua nao katika kila mkutano niliokwenda nchi hii. Waeleze majaji hata siku ninakamatwa Mbinga, waandishi wa habari niliokuwa nao ni Shedrack Simba na Oscar ni kweli au sio kweli

    Shahidi P: Ni kweli.

    Lissu: Na waeleze majaji katika ziara zote hizo mkiwepo tumekuwa tukienda msafara mmoja na hata hoteli tunapofikia na tunakula pamoja ni kweli sio kweli ndugu yangu.

    Shahidi P: Ni kweli

    Lissu: Kama nitakuwa ninakosea waeleze majaji nyie watu wa Jambo na boss wenu tumekuwa na mahusiano ya karibu sana nitakuwa nakosea?

    Shahidi P: Hapana hujakosea.

    Lissu: Waeleze majaji kipindi chote ambacho tumefanya kazi pamoja mmekuwa marafiki zangu.

    Shahidi P: Hujakosea.

    Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji wakati mwingine vyombo vingine vikiogopa kurusha mikutano yangu nyie hamjawahi kuogopa kurusha mikutano yangu ni kweli sio kweli.

    Shahidi P: Ni kweli.

    Lissu: Iambie mahakama kuwa mliadhibiwa na mamlaka kwa kurusha mkutano wangu wa tarehe 3/4/2025

    Shahidi P: Sikumbuki

    Lissu: Hukumbuki mlifunguliwa kesi TCRA.

    Shahidi P: Sikupata taarifa.

    Lissu: Kwa mahusiano yetu mazuri nyie waandishi wa Jambo na boss wenu Marwa waambie majaji kama kuna mwanachadema amekutishia kukudhuru wewe au wafanyakazi wenzako wa jambo TV kwa namna yeyote ile.

    Shahidi P: Hapana.

    Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji tangu uliporusha mkutano mpaka leo kama kuna polisi yeyote au usalama uliyempa taarifa kama mnatishiwa wewe au wafanyakazi wenzako.

    Shahidi P: Hapana sijafanya hivyo.

    Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama una hofu yeyote kama una hofu ya kutoa ushahidi wako hadharani kila mtu akuone na akusikie

    Shahidi P: Nina hofu kutoa ushahidi hadharani

    Lissu: Unahofu gani bwana waeleze kwanini una hofu.

    Shahidi P: Nina hofu sababu hili suala ni nyeti nyie ni viongozi nyie mnaweza msiwe na shida ila wafuasi wanaweza wasinielewe na wakanidhuru.

    Lissu: Kama nimekuelewa vizuri sisi viongozi hatuna shida na hakuna mwanachama aliyekutishia.

    Shahidi P: Ndio

    Lissu: Uliandika maelezo Polisi?

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Waambie kama uliandikia maelezo Dodoma na aliyekuandika ni inspekta wa Polisi Andrew Chulu.

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Waheshimiwa majaji naomba nimsomee maelezo yake, naomba shahidi apewe nakala halisi ya maelezo yake ya Polisi.

    Lissu: Shahidi umepata maelezo?

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Waeleze majaji sehemu ya makazi kama imefichwa.

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Na taarifa za mawasiliano binafsi simu barua pepe anuani?

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Na tarehe yako ya kuzaliwa?

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Na shule ulizosoma zimefichwa vilevile?

    Shahidi P: Ndio

    Lissu: Ulikwenda chuo cha kilimo vilevile imefichwa?

    Shahidi P: Ndio.

    Lissu: Nataka kuepuka uzembe wao hawa waliambiwa wafiche hawakuficha wanakiuka amri ya mahakama

    Lissu anamsomea bila kusoma taarifa binafsi zitakazo fichua utambulisho wa shahidi licha ya kwamba karatasi aliyonayo ina taarifa zote za shahidi .

    Lissu: Je unakubali maelezo yako haya yapokelewe kama kielelezo cha ushahidi mahakamani?

    Shahidi P: Ndio.

  8. Alikuwa akizungumza namna watakavyozuia uchaguzi-Shahidi

    Lissu

    Wakili wa Serikali: Mlikuwa na nani?

    Shahidi P: Nilikuwa na wenzangu watano

    Wakili wa Serikali: Nini kiliendelea siku hiyo na mkutano ulikua wapi

    Shahidi P: Mkutano ulikuwa makao makuu ya Chadema mikocheni, na tulipofika eneo husika tulifunga vifaa vyetu vya kazi tayari kwa tukio sababu kazi ilikuwa inaanza mishale ya saa nne

    Wakili wa Serikali: Bwana P, umesema mlifika kwa ajili ya kujiandaa na matangazo ilikuwa saa nne ya wakati gani

    Shahidi P: Ilikuwa saa nne asibuhi

    Wakili wa Serikali: Wakati mnafika eneo husika hali ilikuwaje?

    Shahidi P: Tulikuta wanachama wengi wa Chadema, waandishi wa habari kabla ya viongozi wa Chadema kufika.

    Wakili wa Serikali: Umetuambia kwamba mlifika na kuweka vifaa vyenu tayari awali ulituambia unafanya matukio ya picha na video siku hiyo ulikua unachukua matukio ya aina gani?

    Shahidi P: Ilikuwa ni kuchukua matukio vilevile kwenda Mbashara.

    Wakili wa Serikali: Unasema mlijiandaa kwa ajili ya kurusha mbashara ilikuwa kwa njia gani?

    Shahidi P: Tulikua tunarusha kwa njia ya kamera sikupeleka mubashara Youtube.

    Wakili wa Serikali: Unaposema Youtube unamaanisha nini?

    Shahidi P: Ni mtandao unaotumika kupakia matukio na kuangalia.

    Wakili wa Serikali: Bwana P, huko mtandaoni mnatambulika kwa jina gani?

    Shahidi P: Ni Jambo TV

    Wakili wa Serikali: Ebu tuambie tukio lilianza muda gani?

    Shahidi P: Saa nne na nusu asibuhi.

    Wakili wa Serikali: Na lilichukua muda gani?

    Shahidi P: Lilichukua saa tatu.

    Wakili wa Serikali: Kwa saa hizo tatu mlirusha matukio gani?

    Shahidi P: Kwa siku husika tulirusha mkutano wa chadema na watia nia wa Chadema kwa ajili ya kuzungumza masuala ya uchaguzi na kuzungumzia kauli mbiu yao ya no reforms no election.

    Wakili wa Serikali: P kwa siku hiyo hujaweza kukumbuka baadhi ya wazungumzaji?

    Shahidi P: Nawakumbuka viongozi wa chadema, mwenyekiti Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu.

    Wakili wa Serikali: Kama unakumbuka miongoni mwa wazungumzaji unakumbuka maneno waliyosema au kauli?

    Shahidi P: Ninayoyakumbuka kwa ujumla ni no reforms no election na namna gani ataenda kuingia kwenye uchaguzi.

    Wakili wa Serikali: Walisema wataingia kwenye uchaguzi kwa namna gani?

    Shahidi P: Walisema bila mabadilko hawatakwenda kwenye uchaguzi mwenyekiti alikuwa akizungumza namna watakavyozuia uchaguzi.

    Wakili wa Serikali: Ukisema mwenyekiti unamaanisha nani?

    Shahidi P: Tundu Lissu.

    Wakili wa Serikali: Bwana P, unaweza kukumbuka baadhi ya maneno unayokumbuka juu ya uchaguzi?

    Shahidi P: Alizungumza mengi kama tutazuia huo uchaguzi na tutakinukisha.

    Wakili wa Serikali: Malengo ya kurusha matukio haya mubashara yalikuwa ni nini bwana P?

    Shahidi P: Malengo yalikuwa ni kuuabarisha Umma.

    Wakili wa Serikali: Chombo chenu kilifikaje eneo la tukio?

    Shahidi P: Tulipata maelekezo toka kwa mkurugenzi wetu kwenda kwa ajili ya kucover habari.

    Wakili wa Serikali: Unaweza kuiambia mahakama tukio lenu la kuchukua na kurusha ilichukua muda gani?

    Shahidi P: Saa tatu.

    Wakili wa Serikali: Baada ya hapo nini kilifuata?

    Shahidi P: Baada ya hapo tuliambiwa waandishi tutoke nje ili viongozi waongee mambo yao ya ndani.

    Wakili wa Serikali: Sasa Bwana P tarehe saba mwezi wa nne 2025 unakumbuka nini kilitokea?

    Shahidi P: Siku hiyo nilikuwa Dodoma kikazi nilipokea simu toka kwa bosi wangu John Marwa akiniambia niende kituo cha Polisi kwa ajili ya kwenda kukabidhi kadi ambayo tulitumia tarehe tatu ambayo ndani mwake ilikua na video za mkutano wa Chadema.

    Wakili wa Serikali: Tarehe ngapi?

    Shahidi P: Tarehe tatu mwezi wa nne 2025.

    Wakili wa Serikali: Ilikuwaje tukio likafika kwenye hiyo kadi ulipaswa ukabidhi?

    Shahidi P: Tukiwa tunatumia kamera tunachokirekodi huwa kinahifadhiwa kwenye kadi na Polisi walikua wanaihitaji hiyo kadi tuliyorekodia tukio la chadema.

    Wakili wa Serikali: Baada ya maelekezo hayo ya Marwa ikawaje?

    Shahidi P: Nilikwenda polisi na kuwasilisha kifaa kichokuwa kinahitajika.

    Wakili wa Serikali: Sasa bwana P iambie mahakama hiyo tarehe 03/04/2024 huyo mtu uliyemtaja kama Tundu Lissu alikuwa katika muonekano gani?

    Shahidi P: Alikuwa kwenye mavazi ambayo rangi husika sifahamu lakini ni kombat zile.

    Unaweza kusoma;

  9. Shahidi wa kificho wa 17 wa Jamhuri anatoa ushahidi wake

    Jaji: Tuendelee

    Wakili wa Serikali: Bwana P unanisikia? nitakuongoza kutoa ushahidi wako wa msingi, ninaomba ujibu kadiri ntakavyokuwa na kuongoza

    Wakili anaendelea

    Wakili: Bwana P unajishughulisha na nini?

    Shahidi P: Mimi ni mwandishi wa habari Jambo Televisheni

    Wakili wa Serikali: Una muda gani sasa?

    Shaid P: Niko tangu 2023 tangu sasa

    Wakili wa Serikali: Majukumu yako ni yapi?

    Shahidi P: Majukumu yangu ni kuchukua matukio ya video na picha

    Wakili wa Serikali: Ujuzi wako kwenye kazi unayofanya ni upi yani ngazi ya elimu yako

    Shahidi P: Nina Diploma ya uandishi wa habari

    Wakili wa Serikali: Ulipata wapi hiyo elimu na mwaka gani

    Shahidi P: Nilipata katika chuo cha DSJ mwaka 2023

    Wakili wa Serikali: Unaweza kuiambia Mahakama unapigaje picha za matukio na video

    Shahidi P: Nafanya haya yote kwa kutumia kifaa cha kamera aina ya Sony AX

    Wakili wa Serikali: Umetuambia kuna matukio ya picha na video kamara Sony A x unaitumia kwenye matukio ya aina gani

    Shahid P: Ax naitumia kwenye video

    Wakili wa Serikali: Na matukio ya picha unatumia nini

    Shahidi P: Natumia kifaa kinachoitwa Cannon kwa ajili ya picha

    Wakili wa Serikali: Baada ya kutujuza kazi unazofanya nikurejeshe tarehe tatu April 2025, ulikuwa na jukumu gani

    Shahidi P: Siku hiyo nilipangiwa kazi na Bosi wangu kwenda kufanya kazi kwenye tukio la CHADEMA ofisi za makao makuu nikiwa na mwenzangu shahidi P1

    Wakili wa Serikali: Boss wenu ni nani?

    Shahidi P: John Marwa

  10. Lissu: "Hii sio kesi ya wizi wa mbuzi ni kesi ya uhaini"

    .

    Kesi imeanza;

    Wakili wa serikali: Tunaomba radhi kwa kuchelewa kwa sababu zisizozuilika shahidi alipata changamoto za usafiri ila kwa uweza wa Mungu tayari amefika na tuko tayari kuendelea waheshimiwa

    Jaji: Mshitakiwa uko tayari?

    Lissu: Majaji naomba msirihusu huu mchezo wa kuchelewa, shahidi anapaswa afike kwa wakati kama Mahakama ilivyoelekeza hii sio kesi ya wizi wa mbuzi ni kesi ya uhaini. Hii kesi inamshitakiwa mmoja leo tuna mwaka na miezi minne kwa utaratibu huo hautafika tukisema tunaanza saa tatu tunaanza saa tatu msikubali waheshimiwa majaji

    Wakili wa serikali: Waheshimiwa tunashahidi wetu mmoja ambaye ni shahidi wa kulindwa

    Shahidi ameshaingia ingia kwenye kisanduku cha siri jaji anamuuliza maswali ya utambulisho ikiwemo umri dini

    Shahidi P: Nina miaka 26, Dini Muislam

    Shahidi anakula kiapo cha uaminifu kulingana na imani yake akiwa ameshika kitabu cha dini (msahafu)

  11. Picha kutoka Mahakamani kesi ikianza punde

    .
    Maelezo ya picha, Lissu ameshaingia na kesi inaanza
    .
    Maelezo ya picha, Mwanasheria wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala (katikati) akiwa na Kaka wa Lissu, Wakili Alute Mughwai na mwanasheria Peter Madeleka (kushoto)
    .
    Maelezo ya picha, Mawakili, akiwemo Nassoro Katuga wa Serikali wakisaliamiana
    .
    Maelezo ya picha, Katibu wa CHADEMA kulia, John Mnyika
  12. Shahidi wa 17 anatarajiwa kuanza kutoa ushahidi katika kesi ya Lissu

    .

    Shahidi wa 17 wa upande wa mashtaka anatarajiwa kuanza kutoa ushahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

    Makarani wa Mahakama wameanza maandalizi na kuweka vipakatalishi vya majaji pamoja na vifaa vingine kwa ajili ya mwenendo wa kesi. Bado Mawakili wa Serikali hawajaingia.

    Baada ya shahidi huyo wa 17 kusikilizwa, upande wa mashtaka utakuwa umesalia na mashahidi 14 wa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

    Kesi hiyo inaendelea mbele ya jopo la majaji watatu katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

  13. Mahakama yawataka mawakili kutozungumza na vyombo vya habari ndani ya viunga vya Mahakama

    .

    Mahakama Kuu ya Tanzania imewakumbusha mawakili kutofanya mahojiano na vyombo vya habari katika viunga vya Mahakama kuhusu mashauri yanayoendelea.

    Taarifa iliyotolewa na Mahakama Kuu na kusainiwa na Msajili wa Mahakama Kuu, C.M. Tengwa, Agosti 12, 2026, imesema mawakili wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Mahakama katika mwenendo wao ndani na nje ya Mahakama.

    Mahakama imesema hatua hiyo inafuatia taarifa kwamba Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kiliwataka wanachama wake kuzungumza na vyombo vya habari katika eneo la Mahakama baada ya mashauri kuahirishwa.

    Hata hivyo, Mahakama Kuu imewakumbusha mawakili kutofanya mahojiano na vyombo vya habari katika viunga vya Mahakama wala kueleza mwenendo wa mashauri yanayoendelea kwa namna inayoweza kuathiri mwenendo wa mashauri hayo.

    Mahakama imesema mwenendo wa mawakili, ndani na nje ya Mahakama, kuhusu mashauri yanayoendelea unapaswa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, taratibu na maelekezo ya Mahakama ya Tanzania.

    Taarifa hiyo imetolewa wakati kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ikiendelea katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam. Kesi hiyo ilianza tena kusikilizwa Agosti 10 na imepangwa kuendelea hadi Septemba 7, 2026.

    Hata hivyo, taarifa ya Mahakama Kuu haijamtaja Lissu, kesi yake wala wakili yeyote kwa jina.

  14. Mambo 7 muhimu kuhusu kesi ya uhaini ya Lissu

    .

    Chanzo cha picha, X

    Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CHADEMA, anakabiliwa na kesi ya uhaini Tanzania. Usikilizwaji wa kesi hiyo unaendelea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, huku upande wa Jamhuri ukiendelea kuwasilisha mashahidi wake. Kufikia jana, mashahidi 16 walikuwa wamefika kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

    1. Kesi ya Lissu inahusu nini?

    Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anakabiliwa na shtaka la uhaini nchini Tanzania.

    Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, na imekuwa ikiendelea kwa awamu huku upande wa Jamhuri ukiwasilisha ushahidi wake.

    2. Lissu alikamatwa lini?

    Lissu alikamatwa 8 Aprili 2025, na siku moja baadaye akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambako alisomewa shtaka la uhaini kama Mahakama ya ukabidhi.

    Hapo ndipo mchakato wa kesi ulipoanzia kabla shauri hilo kuendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

    3. Kesi ilifikaje Mahakama Kuu?

    Baada ya hatua za awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi ya uhaini iliendelea katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

    Huko, upande wa Jamhuri ulianza kuwasilisha ushahidi na mashahidi wake katika kuunga mkono mashtaka dhidi ya Lissu. Na Mpaka sasa Mashahidi 16 wametoa ushahidi wao mpaka Agosti 12, 2026.

    4. Kwa nini kesi ilisimama kwa miezi mitano?

    Hili ni moja ya mambo muhimu katika historia ya kesi hiyo.

    Februari 2026, Jamhuri iliwasilisha notisi ya kutaka kuongeza ushahidi mpya katika kesi hiyo.

    Lissu alipinga hatua hiyo, na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam ikatupilia mbali notisi ya Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi huo mpya.

    Jamhuri haikukubaliana na uamuzi huo. Ilipeleka suala hilo Mahakama ya Rufani, ikiomba mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu.

    Kutokana na shauri hilo, Mahakama Kuu ilisimamisha usikilizwaji wa kesi ya uhaini hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi.

    Hivyo, kesi hiyo ilisimama kwa takribani miezi mitano kuanzia Februari 2026.

    5. Nini kilitokea Mahakama ya Rufani?

    Baada ya suala hilo kufikishwa Mahakama ya Rufani, mahakama hiyo ilitoa uamuzi kuhusu hoja iliyokuwa imewasilishwa na Jamhuri.

    Lissu alishinda katika suala hilo, na hivyo kuondoa kikwazo cha kisheria kilichokuwa kimesababisha usikilizwaji wa kesi kusimama.

    Baada ya uamuzi huo, kesi ilirejea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wake.

    6. Kesi ilianza tena lini?

    Baada ya kusimama kwa takribani miezi mitano, usikilizwaji wa kesi ulianza tena Agosti 10, 2026.

    Tangu kurejea kwake Mahakama Kuu, upande wa Jamhuri umeendelea na uwasilishaji wa ushahidi.

    Kufikia Agosti 12, shahidi wa 16 wa upande wa Jamhuri, ACP Amin Mahamba, alikuwa amemaliza kutoa ushahidi wake na kuhojiwa na Lissu. Akitumia siku 3 Mahakamani

    7. Nini kimejitokeza katika ushahidi wa mashahidi?

    Katika hatua ya sasa ya kesi, Lissu amekuwa akiwahoji mashahidi wa Jamhuri kuhusu ushahidi waliowasilisha na taarifa walizowahi kutoa katika hatua za uchunguzi.

    Katika ushahidi wa Agosti 12, kwa mfano, Lissu alimuuliza shahidi kuhusu tofauti kati ya maelezo aliyowahi kutoa wa maandishi na majibu ya mdomo aliyoyatoa mahakamani. Shahidi alisema hakuwa ameeleza sababu ya tofauti hiyo kwa maandishi, lakini akiongozwa na wakili wa Serikali alisema , alikuwa akijibu maswali kwa namna alivyoulizwa na mshitakiwa.

    Lissu pia aliuliza kuhusu video zilizotumika katika uchunguzi. Shahidi alisema polisi walitazama video iliyokuwa mtandaoni, lakini hawakuangalia video iliyokuwa kwenye memory card na flash disk zilizotajwa mahakamani.

    Jana, Agosti 12, shahidi wa 16 wa Jamhuri alimaliza kutoa ushahidi. Baada ya hapo, upande wa Jamhuri uliomba kesi iahirishwe kwa kuwa haukuwa umejiandaa na shahidi mwingine, na Jaji Dunstan Ndunguru akaahirisha kesi hadi leo, Agosti 13.

    Kwa hiyo, leo macho yanaelekezwa Mahakamani kujua hatua inayofuata katika ushahidi wa upande wa Jamhuri.

  15. Kesi ya uhaini ya Lissu kuendelea leo: Nini kinatarajiwa Mahakamani?

    .

    Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, inatarajiwa kuendelea leo katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, baada ya kesi hiyo kuahirishwa jana. Upande wa Jamhuri ulisema haukuwa umejiandaa na shahidi mwingine.

    Kesi hiyo iliahirishwa jana baada ya shahidi wa 16 wa upande wa Jamhuri, ACP Amin Mahamba, kumaliza kutoa ushahidi wake. Upande wa Jamhuri uliomba muda zaidi kwa sababu haukuwa umejiandaa na shahidi mwingine.

    Jaji Dunstan Ndunguru aliahirisha kesi hiyo hadi leo saa tatu asubuhi.

    Kwa hiyo, kinachofuatwa leo ni hatua itakayochukuliwa na upande wa Jamhuri baada ya shahidi huyo kumaliza ushahidi wake.

    Jana, Lissu aliomba mahakama izingatie agizo la kuwa upande wa Jamhuri uje na mashahidi wawili, akisema kuchelewa kwa kesi hiyo si kwa sababu yake na kwamba yeye anaendelea kukaa gerezani bila hatia.

    BBC itaendelea kufuatilia kinachoendelea Mahakamani leo na kukuletea kila hatua kwenye ukurasa huu.

  16. Kesi ya Lissu: Mambo muhimu yaliyojiri Mahakamani jana

    .

    Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, iliendelea jana katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, huku shahidi wa 16 wa upande wa Jamhuri, ACP Amin Mahamba, akimaliza kutoa ushahidi wake. Lissu alimuuliza shahidi maswali kuhusu ushahidi wake, matukio ya Oktoba 2025 na madai yanayohusishwa na uchaguzi na Katiba.

    Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa na Lissu ni kuhusu tofauti zilizopo kati ya maelezo ambayo shahidi aliwahi kutoa polisi na yale aliyoyasema mahakamani. Shahidi alikiri kuwa hakuwa ameeleza sababu za tofauti hizo.

    Lissu pia alimuuliza shahidi kuhusu madai ya maandalizi ya vurugu wakati wa uchaguzi wa Oktoba 2025 na hatua zilizochukuliwa dhidi ya watu waliodaiwa kuhusika.

    Katika sehemu nyingine ya dodoso, Lissu aliuliza kuhusu ushahidi wa video uliotumika katika uchunguzi. Shahidi alisema polisi walitazama video iliyokuwa mtandaoni, lakini hawakuangalia video iliyokuwa kwenye memory card na flash disk iliyotajwa Mahakamani.

    Lissu pia alimuuliza shahidi kama ushahidi wake ulikuwa unathibitisha kwamba yeye ni mhaini. Shahidi alijibu: “Sijasema hivyo.”

    Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi, upande wa Jamhuri uliomba kesi iahirishwe kwa sababu haukuwa umejiandaa na shahidi mwingine.

    Jaji Dunstan Ndunguru akaahirisha kesi hadi leo saa tatu asubuhi.

  17. KARIBU KATIKA MUENDELEZO WA KESI YA LISSU LEO ALHAMIS 13.08.2026

  18. Kesi yahahirishwa mpaka kesho Alhamisi Agosti 12, 2026

    ..

    Upande wa Jamuhuri wameomba ahirisho la kesi kwa sababu hawakujiandaa na shahidi mwingine

    Lissu: Ninaomba ile amri ya Mahakama ya kuwa wanapaswa kuja na mashahidi wawili, tumechelewa sana na sio kwa sababu zangu ni kwa sababu zao, mimi naendelea kukaa gerezani na sina hatia. Kuanzia kesho waje na mashahidi wa kutosha

    Jaji: Shauri lina ahirishwa mpaka kesho saa tatu asubuhi...

  19. Shahidi wa 16 wa Jamhuri amaliza kutoa ushahidi wake

    .

    Upande wa Serikali, Katuga, unamuuliza Shahidi, Mahamba

    Katuga: Naomba ufafanuzi waambie majaji yale maneno yaliyoko kwenye hati ya mashitaka tutakinukisha, kuna neno serikali wafafanunulie majaji ulimaanisha nini

    Shahidi: Nilipotamka neno serikali lipo nilimaanisha serikali ndio nyenye mamlaka ya kutekeleza na kusimamia sheria za nchi kwa hiyo kutamka maneno kama hayo kwamba utauzia uchaguzi au utavuruga uchaguzi ni kuitishia serikali kwani ndio ina wajibu wa kulinda amani ya nchi

    Katuga: Tuendelee kujikita hapo hapo uliulizwa ni nani aliyechapisha mtandaoni ukamkomalia ukamwambia ni wewe na akaenda mbele akuuliza je akina P na P1 walifanya nini ukasema wao walisambaza na yeye ndio alichapisha ifafanulie Mahakama ulimaanisha nini?

    Shahidi: Nilimaanisha kwamba mshitakiwa alikuwa akiongea mbele ya waandishi wa habari ambao walikuwa wakirusha yale matangazo tunaamuni kwamba hiyo ilikuwa ni nia yake na kama alikuwa hataki asingewaruhusu

    Katuga: Ndio maana ukakomaa ni wewe ni wewe?

    Shahdi: Ndio

    Katuga: Uliulizwa haya maneno kunzia uchaguzi, kukinukisha je yamo kwenye kifungu cha 39/2 B

    Shahdi: Yale maneno aliyotamka mshitakiwa tafsiri yangu ni kwamba kulikuwa na hiyo nia ya kuitishia serikali

    Katuga: Umeulizwa sana hapa mambo ya Katiba na ukaulizwa kudai Katiba ifafanulie mahakama haya madai na kosa hili la uhaini au nini majibu yako kwenye hili la katiba na uhaini

    Shahidi: Havihusiani

    Katuga: Kuna maswali mengi uliulizwa juu ya mambo ya Oktoba 2025 mkaambiwa wewe na polisi mlifanya vurugu ulimaanisha nini

    Shahidi: Sio kweli kwamba Polisi ilihusika kwenye vurugu ni wazi kwamba baada uchunguzi tuliofanya ulibaini kwamba kulikuwa na maandalizi ya awali

    Lissu anaingilia:...Mimi sikuuliza hilo swali na kwakuwa shahidi anajibu kitu kipya nitaomba ni rudie kufanya dodoso

    Katuga: Umeulizwa na mshitakiwa ushahidi uliosoma Mahakamani na ule uliandika polisi leo ukaulizwa je unataka ushahidi wako Mahakamani usiaminiwe ukasema ndio na uliandika Polisi ukasema ndio ukasema huajelezea sababu ya utofauti wa ushahidi wako wa kuandika na kuongea fafanua ulimaanisha nini uliposema sijaeleza

    Shahidi: Kweli sijaeleza sababu ya hiyo tofauti ila majibu ya hapa mahakamani yalitokana na maswali niliyokuwa ninaulizwa na mawakili hapa mahakamani

    Katuga: Waheshimiwa majaji ni hayo tu kwa shahidi huyu .

    Jaji Nduguru: Shahidi umemaliza kutoa ushahidi wako unaweza kwenda...

  20. Lissu amuuliza shahidi: “Ni ushahidi wako kwamba mimi ni mhaini?”Ajibu: “Sijasema hivyo”

    .

    Lissu hiyo taarifa ipo Mahakamani najua kuna taarifa ilikataliwa sababu haikuandaliwa na mtaalamu ilikataliwa

    Shahidi: Tuendelee

    Lissu Mpaka sasa wewe ni shahidi wa 16 nyie wote hakuna aliyewasilisha ushahidi wa video na hakuna kidhibiti hata kimoja zaidi ya stori

    Shahidi: Ni sahihi

    Lissu: Twende kwenye mkutano wangu uliyosababisha yote haya juu ya msimamo wangu na chama changu juu ya uchaguzi na katiba

    Shahidi: Sina hakika kama ulizungumzia katiba

    Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu madai ya mfumo wa uchaguzi na katiba ni madai ya siku nyingi

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Waeleze majaji kama una fahamu mwaka 1992, Tume ya Nyalali ilipendekeza itungwe katiba mpya itakapofikia Septemba 1993

    Shahidi: Sijawahi kusikia

    Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu mapendekezo hayo ya Jaji Nyalali yalikataliwa na CCM chini ya serikali ya Rais Mwinyi

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Rais Mkapa marehemu aliunda tume ya Jaji Robert Kisanga mwaka 1998, walipendekeza kuwe na Katiba mpya na Rais Mkapa akasema hakuwatuma waangalie hayo ya katiba

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Rais Mkapa akaunda Tume nyingine ya Jaji Mark Bomani nayo ikapendekeza katiba mpya na Mkapa na CCM yake wakakataaa

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Rais Kikwete akaunda tume ya Jaji Warioba na wakaanda rasimu ya Katiba mpya na mapendekezo ya mabadiliko kwenye mfumo wetu wa uchaguzi, Rais Kikwete naye akataaaa waeleze majaji

    Shahidi: Sijawahi kusikia

    Lissu: Waleze majaji kuwa tunafanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano

    Shahdi: Ni sahihi

    Lissu: Tangu 1995 watazamaji wa uchaguzi huo kutoka nje kimataifa na kikanda kila kwenye uchaguzi mkuu wamependeza kwa serikali itungwe katiba mpya na mabadiliko kwenye mfumo wetu wa uchaguzi

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Waeleze majaji mwaka 2015 ilani ya CCM ilikua na ahadi kuwa watakamilisha mchakato wa katiba mpya

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Waeleze majaji hata mwaka 2020, CCM ya Magufuli iliahidi mchakato wa katiba mpya utakamilika

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Hata alipokuja Samia naye alikataaa

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Kila uchaguzi mkuu lazima kuwe na mauaji ya raia

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Baada ya hotuba yangu ya tarehe tatu wewe na Jeshi mlichukua hatua ya kunitafuta na kuniuliza nilimaanisha nini

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Kwa yote haya katika historia yetu ya miaka 35, No Reforms No Election ilikuwa sahihi kwenye mazingira haya

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Jaji Chande anasema hivi ghasia za baada ya uchaguzi mkuu zilitokana na matatizo ambayo yamekueko kwa muda mrefu ikiwemo madai ya katiba mpya, mfumo wa uchaguzi. Maelfu ya watu wameuawa sababu ya kutotatuliwa kwa muda mrefu, je nakosea

    Shahidi: Unakosea

    Lissu: Kwa hiyo hata Jaji Chande na tume yake wamekosea?

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Hayo unayosema ni makosa yangu waeleze majaji kama unafahamu kikosi kazi cha kamati ya haki za binadamu umoja wa mataifa kimetoa taarifa baada ya uchunguzi wa miezi tisa imesema kukamatwa kwangu ni kinyume cha sheria na nilipwe fidia

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu tarehe 10 Juai, Kamati ya Mawaziri wanaowakilisha Jumuiya ya Madola imetoa taarifa inayoitaka serikali ya Tanzania kuniachilia huru ndani ya mwezi mmoja na wasipofanya hivyo kwenye kikao cha Septemba, watachuku hatua stahiki dhidi ya serikali ya Tanzania

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Swali langu la mwisho bwana askari kama Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola wote wanasema niachiliwe na ni ushahidi wako kwamba mtu huyu anayepiganiwa na Taasisi zote hizi ni mtu mbaya mhaini na anayestahili kunyongwa

    Shahidi: Sijasema hivyo

    Lissu amemaliza kumuhoji shahidi wa 16, Mahamba