Wakati shahidi akieleza tafsiri hiyo, Lissu alipinga baadhi ya maswali ya upande wa mashtaka, akisema shahidi alikuwa akileta mambo ambayo hayapo kwenye shtaka linalomkabili.
Lissu: "Mimi ni mshitakiwa wa uhaini, sikuwaambia watu wachome na kuchana kura. Haya maneno wanaokoteza na wanayaleta kwa mlango wa nyuma."
Lissu aliwaomba majaji wasiruhusu ushahidi ambao, kwa mtazamo wake, ungeipeleka kesi kutoka kwenye shtaka la uhaini kwenda kwenye madai mengine ambayo hayamo katika hati ya mashtaka.
Baada ya majadiliano, Jaji Dunstan Ndunguru alimruhusu wakili wa Serikali kuendelea na maswali.
Shahidi: "Tulitazama video ya Lissu kwa zaidi ya saa mbili", Kwa ufupi - Kilichojiri Mahakani jana, Agosti 10
Shahidi wa upande wa mashtaka, Kamishna Msaidizi wa Polisi Amini Mahamba, alieleza mahakama kuhusu namna timu yake ilivyofanya uchunguzi wa kauli za Tundu Lissu zilizohusishwa na shtaka la uhaini.
Mahamba alisema baada ya kupokea taarifa kuhusu uchunguzi huo, aliwapangia maofisa majukumu mbalimbali, yakiwemo kukusanya taarifa, kuhoji na kumkamata mtuhumiwa.
Alisema timu yake ilitazama video ya hotuba ya Lissu iliyokuwa imechapishwa kwenye YouTube na Jambo TV.
Wakili wa Serikali: "Mliweza vipi kuiangalia?"
Shahidi: "Tukiwa pale ofisini kuna kompyuta maalumu ambayo anaitumia Inspekta Michael, ndiyo tuliitumia kuangalia hiyo video."
Alisema waliitazama video hiyo kuanzia mwanzo hadi mwisho kwa zaidi ya saa mbili.
Shahidi alisema kwenye video hiyo alimwona Lissu akiwa amevaa vazi rasmi la CHADEMA na akihutubia umma kwa Kiswahili.
Mahamba alisema katika video hiyo alisikia Lissu akizungumza kuhusu kuzuia uchaguzi na kuhamasisha uasi.
Shahidi alidai kuwa kutokana na kauli hizo, timu ya upelelezi iliona Lissu alikuwa na nia ya kuzuia uchaguzi na kuitisha Serikali.
Alisema kauli hizo zilionyesha kile alichokitafsiri kama tishio kwa Serikali na kuvuruga uchaguzi.
Lissu aendelea kumhoji shahidi wa 16 wa Jamhuri katika kesi ya uhaini
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, anaendelea leo, Jumanne Agosti 11, 2026, kumuhoji shahidi wa 16 wa upande wa mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Kesi hiyo, yenye Jalada la Jinai Na. 1 la mwaka 2025, ilianza kusikilizwa Mahakama Kuu baada ya Lissu kushtakiwa kwa shtaka la uhaini linalohusishwa na kauli zake kuhusu kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, akiwa Mbinga mkoani Ruvuma, na siku iliyofuata akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, na kusomewa shtaka la uhaini pamoja na makosa mengine yaliyohusishwa na kauli zake.
Kesi hiyo ilisimama kwa takribani miezi mitano tangu Februari 24, 2026, kabla ya kuanza tena jana, Agosti 10, chini ya Jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.
Usikilizwaji wa kesi hiyo unaendelea kwa mfululizo kuanzia Agosti 10 hadi Septemba 7, 2026.
Jana, shahidi wa 16, Kamishna Msaidizi wa Polisi Amini Mahamba, alimaliza kutoa ushahidi wake wa msingi. Alieleza mahakama kuhusu upelelezi uliofanywa na polisi, ikiwemo namna walivyopitia video ya hotuba ya Lissu iliyochapishwa na Jambo TV na kauli walizodai zilihusisha kuzuia uchaguzi na kuhamasisha uasi.
Mahamba pia alieleza kuhusu majalada ya uchunguzi kutoka mikoa mbalimbali, kukamatwa kwa Lissu na madai ya vitisho dhidi ya baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka.
Leo, Lissu ameanza hatua ya cross-examination, ambapo anamuuliza shahidi kuhusu uadilifu wake kama afisa wa polisi, uzoefu wake wa upelelezi na tofauti kati ya ushahidi alioutoa jana na maelezo yake ya awali.
Endelea nasi hapa kwa taarifa za moja kwa moja kutoka Mahakama Kuu Dar es Salaam.