Lissu hakuandaa mkutano uliomtia matatani - Heche

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, inaendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche anaendelea kutoa ushahidi wake akiulizwa maswali na Lissu

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Waandishi wa BBC Swahili

  1. Nimesikia Mbowe yuko kwenye uzinduzi wa bwawa, wakati Mwenyekiti wake yuko Ukonga - Lissu

    L

    Chanzo cha picha, CHADEMA

    Mwaka 2005, Rais Benjamin Mkapa aliondoka madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na Jakaya Kikwete. Miaka yake ya kwanza madarakani ilikuwa ya vuguvugu la mageuzi ya kisiasa, Lissu amesema.

    Ameendelea kusema kuwa mwaka 2010, uchaguzi ulifanyika chini ya mfumo huohuo wa uchaguzi, na kulizuka malalamiko makubwa, hususan Zanzibar. Kelele za kudai mabadiliko zikawa nyingi.

    Alipochaguliwa kwa muhula wa pili, Kikwete alisema kulikuwa na haja ya kupata Katiba mpya ili kushughulikia changamoto hizo.

    Mwaka 2014, wakati mchakato wa Katiba Mpya ukiwa kwenye hatua za mwisho chini ya Rasimu ya Jaji Joseph Warioba, CCM ilipinga baadhi ya mapendekezo yake. Baadaye, Kikwete alisema masuala hayo yangejadiliwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

    Mwaka 2015, chini ya mfumo huohuo wa uchaguzi, John Magufuli alichaguliwa kuwa Rais akiwa na Samia Suluhu Hassan kama Makamu wa Rais.

    Majaji, nilisahau kutaja kwamba mwaka 2020 nilirudi kutoka uhamishoni ili kushiriki uchaguzi dhidi ya Magufuli kama mgombea urais wa CHADEMA.

    Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, baada ya matokeo kutangazwa, Tume ya Uchaguzi huchapisha matokeo ya majimbo katika Gazeti la Serikali. Ukiangalia chaguzi zilizopita kabla ya mwaka 2020, utaratibu huo ulikuwa ukifuatwa.

    Hata hivyo, mwaka 2020 matokeo ya urais hayakuchapishwa. Sina uhakika kuhusu uchaguzi uliofuata kwa sababu nilikuwa gerezani, lakini ninaamini kulikuwa na mambo mengi yasiyo ya kawaida.

    Majaji, ukisoma taarifa za waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa pamoja na zile za Umoja wa Afrika, utaona walieleza kuwepo kwa dosari mbalimbali katika uchaguzi huo.

    Ripoti ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 2020 iliwasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021. Kwa mujibu wa Lissu, mijadala kuhusu umuhimu wa mageuzi ya kisiasa na kikatiba iliendelea kujitokeza baada ya uchaguzi huo.

    Baadaye, CHADEMA ilianzisha kampeni ya kudai Katiba Mpya. Katika kipindi hicho, Mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe, alikamatwa na kukabiliwa na kesi ya ugaidi iliyodumu kwa miezi kadhaa kabla ya kuhitimishwa.

    "Jana nimesikia Mbowe yuko kwenye uzinduzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, wakati mimi niko hapa Ukonga," alisema Lissu.

    Soma pia:

  2. CCM imekuwa ikikataa mabadiliko ya katiba na tume huru ya uchaguzi - Lissu

    Lissu: Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 ilifanya wasimamizi wa uchaguzi watoke kwenye mfumo wa serikali za mitaa. Wote ni wateule wa Rais na wanafanya kazi kwa niaba ya Rais. Kwa hiyo, hoja yangu ni kwamba mfumo mzima wa uchaguzi unaonekana kuwa chini ya ushawishi wa CCM.

    Haya yote yapo yameelezwa kwenye pendekezo la katiba ya Warioba ambayo ilifanya utafiti kwenye mfumo mzima wa uchaguzi. Matokeo ya mfumo huu yalianza kujitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa 1995.

    Sasa mbali na uchaguzi, kelele za mamabdiliko zilikuwa kubwa sana na nimewambia nimefafanya utafiti wa masuala haya kwa miaka mine.

    Na moja ya mapendekezo ya kuboresha yalikuwa ni kwamba yafanyike mabadiliko ya kikatiba na kuwe na tume huru ili yaliyojitokeza 1995 yasijirudie tena. Kwasbabu haya masuala ya CCM yanaweza kuleta uvunjifu wa amani.

    Serikali ya rais Mkapa na CCM ikakataa. Mwaka 1998

    Mkapa akaunda tume ya kuchunguza ya Jaji Kisanga na ikapendekeza kuwe na mabadiliko, Mkapa akakataa na CCM.

    Mwaka 2002 maafa yakajirudia tena na wengine wakakimbilia Msumbiji na maeneo mengine.

    Mkapa akaunda tume nyingine na kumuweka mtu wake amabaye mwaka 2005 uchaguzi akataka kugombea urais na wakamwambia 'ebo wewe si upo kwenye tume?'

    Soma zaidi:

  3. Mfumo mzima wa uchaguzi umetengenezwa na CCM - Lissu

    ol

    Chanzo cha picha, X

    Lissu: Tumekuwa tukifanya uchaguzi mkuu tangu mwaka 1957. Uchaguzi wa pili ulifanyika Agosti 1960 na ndio uliozaa Bunge la Uhuru. Tangu miaka ya 1960, Tanzania imekuwa ikifanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano bila kukosa.

    Majaji, kabla ya mwaka 1995, kati ya mwaka 1965 na 1995, nchi ilifanya chaguzi chini ya mfumo wa chama kimoja. Kuna vijana wengi hapa ambao huenda hawaelewi maana ya mfumo huo. Kulikuwa na mgombea mmoja na sanduku moja la kura; wananchi walipiga kura kwa mgombea huyo pekee.

    Baada ya marekebisho ya mwaka 1992 yaliyoruhusu mfumo wa vyama vingi, Tanzania iliingia katika enzi mpya ya ushindani wa kisiasa. Wakati huo, Rais Ali Hassan Mwinyi aliunda tume iliyopendekeza kuwepo kwa Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

    Hata hivyo, Katiba iliyopo sasa ilitungwa katika mazingira ya mfumo wa chama kimoja. Kwa mujibu wa Lissu, mapendekezo yaliyohusu Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na wagombea binafsi yalikataliwa na serikali ya wakati huo pamoja na chama tawala.

    Amesema marehemu Rais Mwinyi aliwahi kuandika katika kumbukumbu zake kwamba walikataa pendekezo la Tume Huru ya Uchaguzi na wagombea binafsi kwa lengo la kuokoa chama, hatua ambayo ilizua mvutano mkubwa kati yake na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

    Lissu amedai kuwa marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 yaliifanya Tume ya Uchaguzi kuwa karibu zaidi na chama tawala kuliko ilivyokuwa hapo awali. Amesema wajumbe wa tume pamoja na wawakilishi wake waliendelea kuwa wateule wa Rais, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.

    Aidha, amesema sheria za uchaguzi zimewaweka wasimamizi wa uchaguzi kutoka ngazi za serikali za mitaa na majimbo kuwa watendaji wanaotokana na mfumo wa uteuzi wa Rais.

    "Kwa hiyo, mfumo mzima wa uchaguzi ni wa CCM," alidai Lissu.

    Soma Zaidi Hapa:

  4. Lissu ahoji muktadha wa kauli zinazounda shtaka la uhaini

    Majaji, kwa mtazamo wangu, kesi hii inahusu uchaguzi. Hati ya mashtaka iliyopo mahakamani inanishtumu kuwa nilikuwa na nia ya kuhamasisha watu kuitishia serikali kwa kuwachochea kuvuruga uchaguzi.

    Maneno ninayodaiwa kuyasema yanahusu uchaguzi. Mashahidi wote 17 wa upande wa mashtaka wametoa ushahidi wao kwa kurejea kauli zangu zinazodaiwa kutolewa kuhusu uchaguzi.

    Nyaraka za ushahidi kuanzia B1 hadi D16 pia zinahusu uchaguzi. Hakuna nyaraka hata moja ambayo haizungumzii suala la uchaguzi.

    Kwa hiyo, Majaji, katika sehemu hii ya ushahidi wangu, naomba nizungumzie uchaguzi.

    Mashahidi PW1, PW2, PW3, na kwa kiwango fulani PW16 na PW17, waliieleza mahakama kwamba kauli ninayodaiwa kuitoa na iliyochapishwa kupitia Jambo TV kwenye YouTube ilikuwa sehemu ya video yenye urefu wa takribani saa tatu.

    PW16 na PW17 walisema video hiyo ilikuwa na urefu wa takribani saa mbili na zaidi. Hata hivyo, kwa ujumla wao wote walikubaliana kwamba video hiyo ilikuwa ndefu.

    Kauli zinazodaiwa kuunda msingi wa shtaka la uhaini hazifikii hata dakika moja. Swali langu ni kuwa, katika muda wote uliobaki wa takribani saa tatu, nilizungumza nini?

    Katika sehemu hii ya ushahidi wangu, nataka kueleza mantiki na muktadha wa kauli nilizozungumza katika kipindi hicho mwaka jana.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Shahidi asitutoe nje ya reli - Serikali

    ll

    Upande wa Serikali: "Sasa ushahidi unaotolewa unatoka nje ya mawanda ya kesi, kwa sababu shahidi analeta masuala yasiyohusiana moja kwa moja na shauri hili. Hii si sehemu sahihi ya kuyajadili.

    Haya masuala ya watu kufa anaweza kuyazungumzia, lakini yanahusiana vipi na kesi iliyopo mbele ya mahakama? Kwa hiyo, naomba majaji, kama inawezekana, wamuelekeze shahidi asitutoe nje ya reli. Hivyo ndivyo sheria inavyotaka."

    Lissu: "Majaji, msingi wa utetezi wangu ni kwamba baadhi ya kesi hizi zimetengenezwa, na hiyo ni sehemu ya tabia ya polisi na waendesha mashtaka.

    Kesi yangu ni uthibitisho kwamba mamlaka yanaweza kutumika vibaya. Sizungumzi mambo haya ili mahakama inionee huruma, bali kuonyesha kwamba kuna tatizo ambalo linahusiana na ushahidi wangu.

    Kusema kwamba tunaweza kutumia wiki mbili kunanitia wasiwasi, kwa sababu wao wamekuwa na mwaka mmoja na miezi kadhaa kuwasilisha upande wao. Leo ninapotaka kutumia muda kujitetea, wanaeleza kuwa napoteza muda. Sipotezi muda, najitetea. Wana wasiwasi gani?"

    Soma Zaidi:

  6. Hii ni mara yangu ya nne kukamatwa chini ya Samia, Lissu amesema

    ol

    Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

    Kuhusu kesi hii, nilikamatwa tarehe 9 Aprili 2025 na kufikishwa mahakamani siku iliyofuata. Hii ni mara yangu ya nne kukamatwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na polisi wake.

    Safari hii nimefunguliwa kesi ya uhaini. Kufikia sasa, tayari nimekaa gerezani kwa miezi 16 na ninaelekea kutimiza mwezi wa 17, sawa na zaidi ya mwaka mmoja na miezi minne.

    Majaji, hiki ni kipindi kirefu zaidi kuwahi kukaa gerezani katika maisha yangu. Pia ni kipindi kirefu zaidi kwa kiongozi wa CHADEMA kushikiliwa gerezani.

    Aidha, hii ndiyo kesi kubwa zaidi kuwahi kufunguliwa dhidi ya kiongozi wa upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini takriban miaka 35 iliyopita. Hakuna kiongozi mwingine aliyewahi kufunguliwa kesi ya aina hii.

    Haya yote yamenitokea mimi binafsi. Ninaamini hakuna kiongozi mwingine wa ngazi ya juu wa CHADEMA aliyepitia mateso na changamoto nyingi kama nilizopitia.

    Nina bahati kwamba, licha ya kujeruhiwa na kubaki na ulemavu wa kutembea kwa kuchechemea, bado niko hai. Wapo wengi tuliowahi kufanya kazi pamoja katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambao wengine wameuawa na wengine hadi leo hawajulikani walipo.

    Kama chama, tumepitia nyakati ngumu sana. Tumebeba maumivu makubwa na tumekumbwa na mateso mengi. Mimi binafsi nimefunguliwa kesi mbalimbali ambazo naamini ni za uongo, zikihusisha polisi na mawakili wa serikali.

    Kesi hii si ya polisi pekee, bali inahusisha pia waendesha mashtaka wa serikali. Katika miaka miwili au mitatu iliyopita, tumezika viongozi wengi wa chama.

    Tumepitia maumivu makubwa sana, na mimi binafsi nimeumizwa sana.

    Soma Zaidi Hapa:

  7. Lissu: Mwaka 2024 ulikuwa mgumu kwa viongozi wa CHADEMA

    p

    Chanzo cha picha, bbc

    Mwezi uliofuata September 7 mkesha wake Mkurugenzi wa Hamasa CHADEMA makao makuu, Ally Kibao akatekwa kwenye busi akiwa anakwenda Tanga, akiwa Tegeta alishushwa kwa nguvu.

    Ukiangalia unaona kabisa ni police kulingana na magari yao, ni polisi ambao ni usalama wa taifa. Kesho yake mzee Kibao akaokotwa akiwa ameuawa maeneo ya ufukweni Ununio, inaelekea aliteswa vibaya sana.

    Majaji wakati marehemu Kibao anatekwa nyara na kuuawa kulikuwa na matukio mengi ya viongozi wa CHADEMA kutekwa na kuawa kilikuwa kipindi kigumu sana 2024.

    Katika kupinga hayo yote chama kilisema kitaandamana tarehe 23 September. Ilipotika asubuhi nikavamiwa na jeshi la polisi mapema asubuhi nyumabani kwangu nikakamatwa. Nikawekwa kituo cha polisi Mbweni.

    Nikakaa Mbweni mpaka usiku, kisha wakanirudisha nyumbani kwangu hawakunifungulia mashtaka.

    Majaji, nakumbuka nilisema nilikamatwa Karatu ili nisiende kuonana na wananchi wa Ngorongoro hiyo ilikuwa Machi 2023. Nilienda kuwekwa kituo cha polisi cha Wilaya ya Monduli waheshimiwa majaji, ili tu kuniharibia mipango yangu

    Soma Zaidi Hapa:

  8. Lissu: Siku niliyopigwa risasi walinzi hawakuwepo

    p

    Chanzo cha picha, mtandao

    Siku niliyoshambuliwa, walinzi wote hawakuwepo na mageti yalikuwa wazi. Nikiwa kwenye eneo la maegesho ya magari, nilipigwa risasi 16, hali iliyosababisha kufanyiwa operesheni 26. Hadi leo, bado nina risasi moja mwilini, karibu na uti wa mgongo.

    Hakuna mtu aliyekamatwa wala kutuhumiwa kuhusika na tukio hilo. Aidha, sijawahi kuitwa na polisi kueleza kilichotokea siku hiyo. Sidhani hata kama polisi walifungua jalada la uchunguzi (RB).

    Majaji, sikufa. Mungu si Athumani. Sikufa. Badala yake, Magufuli alifariki dunia. Baada ya kifo chake, kesi sita zilizokuwa zimefunguliwa dhidi yangu katika Mahakama ya Kisutu zilifutwa mwezi Septemba 2021.

    Baadaye, Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani na kuja na agenda ya 4R.

    Katika kutekeleza agenda hiyo, tarehe 12 Agosti 2024 niliitwa, kwa nafasi yangu ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, kushiriki pamoja na Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

    Jeshi la Polisi lilipiga marufuku maadhimisho ya CHADEMA, lakini ya CCM yaliendelea kufanyika. Nikasema Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kuzuia shughuli hizo na kwamba jukumu lake ni kulinda raia.

    Tarehe 12 Agosti 2024 nilisafiri kwa ndege kwenda Mbeya. Nilipowasili, ilikuwa tayari jioni, ndipo nikaelekea katika ofisi za chama ngazi ya kanda.

    Majaji, siku hiyo nilivamiwa na polisi wakiongozwa na Mkuu wa Operesheni, Awadh Juma. Mimi na viongozi wenzangu tulipigwa na baadaye kukamatwa. Baadaye nilipelekwa mkoani Songwe na kuwekwa mahabusu huko.

    Siku iliyofuata mchana, nilisafirishwa kwa gari kurudishwa Dar es Salaam.

    Nilipofikishwa Dar es Salaam, nilikabidhiwa kwa polisi wa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) na askari kutoka Songwe na Mbeya. Nilipowauliza kosa langu ni lipi, waliniambia walikuwa wakinipeleka nyumbani. Sikufunguliwa mashtaka yoyote. Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kukamatwa chini ya utawala wa Rais Samia.

    Soma Zaidi:

  9. Nilipimwa mkojo kwa mashtaka ya uchochezi - Lissu

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tarehe 29 Julai, nilikamatwa kwa kosa la kumuita Rais Magufuli "dikteta uchwara", siku tatu baada ya kuachiliwa. Nikasafirishwa usiku na kulazwa Kituo cha Polisi Chamwino, ambako kulikuwa na mbu wengi. Baadaye nikaletwa Dar es Salaam na kushtakiwa kwa uchochezi.

    Septemba mwaka huo, nilikamatwa tena na kuletwa Dar es Salaam. Kufikia mwisho wa mwaka 2016, nilikuwa nimekamatwa mara nne na polisi wa Magufuli, huku kesi zote zikisikilizwa katika Mahakama ya Kisutu.

    Kesi ya nne ilifunguliwa mwezi Desemba mwaka huo huo.

    Majaji, mwaka 2017 nilikamatwa tena Dodoma mwezi Februari. Mwezi Aprili kulikuwa na uchaguzi wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

    Wanachama walinitaka nigombee. Siku tatu au nne kabla ya uchaguzi, nilikamatwa na kupelekwa Segerea, ambako nilikaa kwa siku nne.

    Siku ya Ijumaa nikapelekwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Hakimu alisema kesi hiyo ilikuwa na dhamana na akaniruhusu kwenda kugombea urais wa TLS.

    Baada ya uchaguzi wa TLS, nilikamatwa tena mara mbili, mwezi Juni na Agosti. Katika moja ya matukio hayo, nilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupimwa mkojo kwa tuhuma za uchochezi, ingawa hadi leo sijui jambo hilo lilihusiana na nini.

    Soma Zaidi:

  10. Lissu: Polisi walitaka kuvunja chumba cha maiti na kuchukua miili

    p

    Chanzo cha picha, mtandao

    Mwaka 2005, Jakaya Kikwete aliingia madarakani.

    Mwezi Julai 2011, polisi walifanya mauaji katika Mgodi wa North Mara, Nyamongo. Wananchi wa Nyamongo walinipigia simu wakiniomba niende kuwasaidia kwa sababu polisi walikuwa wanawalazimisha kuzika miili ya waliouawa. Nikasafiri kwenda huko na kudai uchunguzi ufanyike kuhusu mauaji hayo.

    Nilipofika Tarime, nilipata taarifa kuwa polisi walitaka kuvunja milango ya chumba cha kuhifadhia maiti ili wachukue miili. Tulikesha nje ya chumba hicho, na ndipo nilipopigwa sana na kujeruhiwa vibaya.

    Baada ya hapo, nilipewa kesi yangu ya pili ya jinai, ambayo nayo ushahidi wake ulikuwa wa mashaka.

    Mwaka uliofuata, 2012, polisi waliua wananchi kadhaa wakati wa maandamano mjini Arusha. Sheria za nchi hii zinaruhusu maandamano, lakini watu waliuawa. Tukaenda kusisitiza haki itendeke, ndipo mimi na wabunge wenzangu, akiwemo Dk. Slaa, tukakamatwa.

    Baadaye, Rais John Pombe Magufuli aliingia madarakani, na kisha Samia Suluhu Hassan.

    Mwaka 2015, wakati wa uchaguzi mkuu Zanzibar, Seif Sharif Hamad alitangazwa kuwa ameshinda, lakini matokeo yakafutwa.

    Ilipotangazwa kuwa uchaguzi wa marudio ungefanyika mwaka 2016, waandishi wa habari waliniuliza maoni yangu. Nikasema kuwa walikuwa wanataka kuleta maafa. Tarehe 26 Juni 2016, nilikamatwa kwa mashtaka ya uchochezi na kupelekwa mahakamani, lakini mashahidi hawakuletwa tena.

    Hata baada ya kupigwa risasi, mashahidi hawakuwahi kuletwa mahakamani.

    Soma Zaidi Hapa:

  11. Lissu akumbuka Krismasi ya kwanza akiwa gerezani

    Majaji, tuanze na utawala wa Marehemu Rais Mkapa, mwaka jana wakati wa Krismasi mwanangu mmoja alinitumia ujumbe akisema kuwa upo gerezani umetukumbusha, Krisimasi ya kwanza baba yao alipokuwa gerezani.

    Nilikamatwa tarehe 23/12/2002, siku mbili kabla ya Krismasi kosa la uchochezi. Nilitengenezewa kesi ya uchochezi. Nilikaa Shimoni siku mbili na nikapelekwa mahakamani siku ya Krisimasi. Kesi hii nilikaa nayo kwa miaka 6 hawaleti mashahidi kila siku tunachunguza upelelezi unaendelea.

    Baada ya miaka 6 mahakama mkazi kisutu ilitupilia mbali kesi kwa kukosekana mashahidi. Hiyo ilikuwa wakati wa Mkapa

    2005 akaingia Rais Jakaya Kikwete.

    Mnamo 2011 Julai Polisi walifanya mauaji kwenye mgodi Nyamongo, wananchi wa nyamongo walinipigia simu wakisema niende nikawasadie maana polisi walikuwa wanalazimisha wazike, nikasafiri kwenda kule na kudai uchunguzi kufanyika wa mauaji yale.

    Nilipofika Tarime nilapata taarifa kuwa polisi wanataka kuvunja milango ya chumba cha maiti, wachukue maiti, tukaka nje ya mlango nilipigwa sana nikaumizwa vibaya sana.

  12. Ndani ya Chadema mimi ndiye kiongozi niliyeshtakiwa mara nyingi - Lissu

    ;pp

    Majaji, mnamo 1997, serikali ya Rais Benjamin Mkapa, ilipanga karibu eneo lote karibu na mto Rufiji kwa mwekezaji mmoja wa Irish ili afuge samaki aina ya kamba.

    Sasa mkapa na serikali walimgawia hekari elfu 20,000 misitu ya mikoko na maeneo ya wananchi ili afanye hiyo. Kama mpango huo ungefanikiwa basi kusingekuwa na huo msitu leo hii. Na tafiti za kitaalam zilisema zingeathiri watu 120,000 wa Rufiji.

    Mimi na wenzangu na wanaharakati wa haki za binadamu tukaingia kwenye mapambano kuzuia hilo balaa lisitokee. Tulisakamwa sana na Rais Mkapa na serikali yake tuliitwa mujahidina. Tukafanya kampeni kubwa na kumkimbiza raia huyo wa Ireland na kutetea wananchi. Hiyo ilikuwa 1997/98.

    Sio rufiji tu nimekuwa mstari wa mbele kupigania haki za ardhi na hifadhi za wanyama pori, Ngorongoro, Onyoro, Tarime, Masa Mashariki upande wa magharibi ma Mashariki na Serengeti.

    Miaka 3 iliyopita nilikamatwa Karatu ili nisiende kuwaona Wamasai ambao nimekuwa nikiwapigania tangu 1996.

    Ukanda Mashariki wa ziwa Tanganyika na ukanda wa pwani pamoja na ukanda wote wa ziwa Victoria nimepigania haki za wavuvi, kwenye mpaka wa Uganda kumekuwa na ukandamizaji wa haki za Uvuvi, watu wanauawa.

    Lakini majaji kipekee kabisa ninajulikana kwa kupigania haki za wananchi kwenye maeneo yenye madini. Kwa takriban miaka 10 tangu1999, mimi ndiye nilikuwa nazungumzia masuala ya madini na haki za wananchi katika maeneo ambayo serikali ya Mkapa iliwapa wawekezaji kutoka nje, mgodi wa Geita, Iiyamuro, ambao Julai na Agosti 1999 kulitokea mauaji makubwa ya wachimbaji wadogo ambapo serikali ya mkapa ilipeleka wanajeshi kukabiliana nao.

    Majaji nataka nimalizie kwa kusema kila mahali palipokuwa na ukandamizaji nchi hii, ukandamizaji wa haki za wananchi nimejitahidi kuwa sehemu ya kupinga huo ukandamizaji. Kauli Mimi yangu imekuwa upinzani dhidi ya ukandamizaji ni utiifu kwa Mungu.

    Sasa majaji, maisha ya aina hii, msimamo wa aina hii imekuwa na alama kubwa sana kwangu na napenda nizungumzie hili.

    Majaji, kesi hii, kesi ya uhaini, na kama ambavyo nimesema mbele yenu uhaini kwenye sheria ndio kosa kubwa kuliko yote kwenye sheria ya muungano, idara ya 24 ya katiba.

    Kama mkishawishika na ushahidi waliotoa mawakili wa serikali adhabu pekee ni kifo.

    Sina hakika na watu wengine nje ya Chadema lakini naweza kusema ndani ya Chadema mimi ndiye kiongozi niliyeshtakiwa mara nyingi kuliko mwanachama mwingine yoyote

    Majaji na kesi zote ambazo nimefunguliwa na serikali mawakili na polisi zimekuwa kesi za kisiasa zilitokana na misimamo na kauli zangu za kisiasa.

    Soma Zaidi Hapa:

  13. Lissu asema kesi ya uhaini ni kwa sababu ya harakati za kupigania demokrasia

    l

    Lissu: Kwa leo majaji, naomba nianze kwa kuzungumza juu ya mchango wangu kama mwanaharakti wa haki za binadamu na demokrasia katika nchi hii. Na ushahidi huu utathibitisha kuwa kesi hii ni kwa sababu ya msimamo wangu wa miaka hiyo yote.

    Ni kesi inayotokana na harakati za kupigania demokrasia katika nchi hii. Ni kwa sababu ya msimamo wangu na kazi ninayoifanya na ninaendelea kufanya na sio kwa sababu mimi ni mhaini.

    Kwa kuanzia naomba kusema kuwa nimetumia maisha yangu yote ya utuzima nikipigania haki za binadamu na demokrasia. Si kuanza jana au juzi, ilianza nikiwa sekondari mwaka 1988, harakati kutetea wanafunzi wa kidato cha nne wakati nipo kidato cha sita.

    Na majani katika mahakama hii kuna watu wana fahamu kwani tulikuwa darasa moja. Na niliulizwa kwanini nawatetea wakakata sipo kidato cha nne. Bado kidogo nifukuzwe.

    1989/90 nikiwa naenda jeshini, vyama vingi vikaanza, vyombo vya usalama polisi jeshi wote walikuwa CCM na naamini wote hawa bado wana misimamo ya CCM.

    Msimamo wa jeshi ulikuwa hapana vyama vingi. Na mimi nilikuwa kikosi cha jeshi namba 841, niligombana sana na wakubwa wa jeshi waliokuwa wanasema hatutaki vyama vingi. Nikawambia kuwa Julius Nyerere, alisema "kuwa wasioruhusu mageuzi ni wajinga" kwahiyo sauti ya Mwalimu hamjaisikia, hilo likaleta ugomvi sana.

    Nilipigania nchi hii kuwa ya demokrasia. (Rais mstaafu mwendazake) Ali Hasan Mwinyi alipoteua tume kuhusu mfumo wa vyama vingi au chama kimoja, inaitwa tume ya rais ya mundo wa vyama vingi au chama kimoja Tanzania. Francis Nyalali alikuwa mwenyekiti.

    Ilipoundwa mwaka 1991 nilikuwa mmoja ya wa Watanzania waliokwenda kutoa maoni ya Tanzania kurudi TZ kurudi kwenye vyama vingi.

    Kama niliposema mfumo wa vyama vingi uliporudisha nilikuwa tayari kuacha shule Uingereza kuja kugombea maana nilikuwa na shauku na masuala ya ustawi wa nchi hii.

    Majaji, kwa miaka yote iliyofuata mpaka leo nimepigania demokrasia takriban na mfumo huru wa uchaguzi, sijawahi kupumzika, nje ya kupigania demokrasia nimepigania haki za wananchi wa kawaida Tanzania kwa miaka mingi

    Soma Zaidi Hapa:

  14. Mashirika ya kikanda na kimataifa yalaani kesi hii - Tundu Lissu

    KL

    Lssu: Ijumaa wakati nazungumza siku ya kwanza niliwaleza kuwa hii ni kesi ya kisiasa, nilisema kuwa jamii za Kimataifa zimelaani kesi hii na mashtaka yote, nilitaja Jumuiya ya Madola, EU, hizo zote ni za Kimataifa, nilisahau kusema kuwa kuna jamii za kikanda pia zimelaani na hii ni kwasababu wasije kusema ni wazungu peke yao sio peke

    Lissu: Mara baada ya kesi hii taasisi za nchi jirani na za ndani zilitoa matamko za kualaani mashtaka haya na ya kuyaita ya uonevu na matumizi mabaya ya uendeshaji wa mfumo wa mahakama

    East African Law Society, wanasheria wa SADC (SADC Lawyers Association), muungano wa wanasheria Afrika (pan African lawyers union), Chama cha mawakili wa Zambia, Chama cha mawakili wa Kenya, Chama cha Mawakili wa Watanganyika ambacho nilikuwa rais wake kwa muda mfupi 2017.

    Taasisi nyingine ni tume ya wanasheria duniani, Amnesty International regional office for eastern and Southern Africa, pamoja na Uganda Law society.

    Majaji kauli za kulaani mashtaka haya pia zilitolewa vilevile na Democrats Union of Africa (DUA) ambayo ni inajumuisha vyama barani afrika wenye mrengo sawa na wa CHADEMA.

    Lissu: na vile vile platforms of African democrats ambalo ni jukwaa la vyama vya democracy kutoka nchi 17 za Afrika,

    Lissu: Majaji kwa kipekee kabisa tarehe 30/07/2025 Tume ya Haki za Binadamu na Wananchi Afrika, makazi yake Arusha Tanzania, ambayo ni chombo mahususi cha Umoja wa Afrika cha kusimamia haki za binadamu na za wananchi barani Afrika kilifanya kikao cha dharura kujadili mashtaka hayo.

    Likapitiaha azimio linaloitwa Azimio kuhusu hali ya haki za binadamu katika Jamhuri ya muungano Tanzania. Azimio Hilo linazungumzia masikitiko makuu kukamatwa kwangu na kufunguliwa kwa kesi hii na tume ilisema serikali ya Tanzania ina wajibu wa kufuata matakwa ya mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na wananchi.

    Soma Zaidi Hapa:

  15. Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu yaanza

    Jaji: naomba tuendelee

    Upande wa utetezi upo tayari?

    Lissu: Mheshimiwa jaji nipo tayari.

  16. Leo kinatarajiwa nini?

    Leo Lissu anatarajiwa kuendelea na ushahidi wake wa kujitetea.

    Macho pia yataelekezwa kwenye hatua ya mahakama kuhusu baadhi ya mashahidi ambao Lissu ameomba waitwe, hasa viongozi wakuu wa serikali aliowataja katika orodha yake.

    Kesi hii inaendelea katika hatua ya utetezi baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa Lissu ana kesi ya kujibu. Uamuzi huo haukumaanisha kwamba amepatikana na hatia, bali kwamba mahakama iliona kuna msingi wa yeye kuitwa kujibu ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.

  17. Lissu alianza ushahidi wake

    Baada ya majaji kutoa maamuzi kuhusu baadhi ya mashahidi wa upande wa serikali, Lissu alianza kutoa ushahidi wake.

    Katika sehemu ya ushahidi wake, alizungumzia pia muda aliokaa kizuizini, akisema kukaa gerezani hakujapunguza heshima yake bali kumeiongeza.

    Alidai pia kuwa taasisi mbalimbali za kimataifa zimeeleza kuwa mashtaka yanayomkabili yana sura ya kisiasa.

    Lissu aliendelea kueleza uzoefu wake katika siasa na masuala ya uchaguzi, akisema mashtaka yanayomkabili yanahusiana na kauli alizotoa kuhusu uchaguzi.

  18. Kesi ya Lissu: Kilichotokea Ijumaa

    ll

    Chanzo cha picha, bbc

    Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, inaendelea leo Jumatatu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, baada ya kuahirishwa Ijumaa wakati Lissu akiendelea kutoa ushahidi wake wa kujitetea.

    Ijumaa ilikuwa siku muhimu katika kesi hiyo baada ya Mahakama Kuu kumkuta Lissu ana kesi ya kujibu, hatua iliyofungua rasmi hatua ya utetezi.

    Lissu aliamua kujitetea mwenyewe na alianza kwa kueleza historia yake ya kisiasa, uzoefu wake kama mwanasheria na mshiriki katika masuala ya uchaguzi Tanzania.

    Katika ushahidi wake, Lissu alisisitiza kuwa ana uzoefu wa muda mrefu katika masuala ya uchaguzi, akisema ameshiriki katika chaguzi mbalimbali kama mpiga kura, mgombea na wakili wa wagombea na wabunge.

    Alieleza pia historia yake ya kisiasa, akiwemo nafasi yake kama Mwenyekiti wa CHADEMA, ubunge na uongozi katika chama hicho, kabla ya kuhusisha kesi inayomkabili na kile alichokiita mapambano ya kisiasa kuhusu Katiba mpya na mfumo wa uchaguzi.

    Mashahidi aliowaomba Lissu

    Kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake, Lissu aliwasilisha orodha ya mashahidi 11 ambao aliomba mahakama iwaite kutoa ushahidi.

    Miongoni mwao ni Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Philip Mpango, aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi Camillus Wambura, Mkuu wa Majeshi Jenerali John Mkunda na Mkuu wa TISS.

    Upande wa mashtaka ulipinga baadhi ya mashahidi hao, ukisema ushahidi wao haukuwa muhimu kwa sababu baadhi ya mambo wanayoweza kueleza tayari yalishatolewa na mashahidi wa serikali.

    Hasa, upande wa serikali ulipinga kuitwa kwa Rais Samia, ukisema Mahakama haina mamlaka ya kutoa wito wa kumtaka Rais kufika mahakamani kutoa ushahidi.

    Lissu alipinga hoja hiyo na kusisitiza kuwa hakuna mtu anayeweza kutoa ushahidi kwa niaba ya mwingine, akitaka mahakama ilinde haki yake ya kuwasilisha utetezi.

  19. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya kesi ya Tundu Lissu, tarehe 24/08/2026

  20. Kesi ya Lissu imeahirishwa kwa muda hadi jumatatu

    G

    Kesi inayomkabili kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu, imeahirishwa hadi Jumatatu saa tatu asubuhi, baada ya Lissu kuendelea kutoa ushahidi wake mahakamani.

    Baada ya kueleza msimamo wake kuhusu masuala ya uchaguzi na uzoefu wake wa kisheria, majaji walimweleza Lissu kuwa wanatumaini atakuwa amekamilisha ushahidi wake ifikapo Jumatatu.

    Hata hivyo, Lissu aliwaambia majaji kuwa hataweza kumaliza ushahidi wake katika muda huo.

    Kesi hiyo inaendelea baada ya mahakama kuu kuamua Tundu Lissu ana kesi ya kujibu.

    Soma Zaidi Hapa: