Uchaguzi Kenya 2022: William Ruto - Kutoka kuwa muuzaji wa kuku hadi kuidhinishwa kuwa mgombea wa urais

    • Author, Na Evelyne Musambi
    • Nafasi, BBC News, Nairobi
  • Iliyochapishwa

Maisha ya utotoni ya William Ruto ni mfano halisi wa maisha ya watoto wengi masikini Wakenya.

Alikwenda shule miguu peku, ambapo alivaa kwa mara ya kwanza viatu akiwa na umri wa miaka 15. Aliuza kuku na karanga kando ya barabara katika maeneo ya kijijini kwao katika mkoa wa Bonde la ufa (Rift Valley).

kwa hiyo sio jambo la kushangaza kwamba anajielezea kama kiongozi wa masikini wakati anapogombea kiti cha urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 9 Agosti.

Bw Ruto anawania kiti hicho chini ya Muungano unaofahamika kama Kenya Kwanza, akitoa ahadi ya kukuza uchumi.

Kiwango rasmi cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wenye kati ya umri wa miaka 18 na 34 ni karibu 40%, na uchumi hautoi ajira za kutosha kuweza kuwaajiri vijana 800,000 wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka.

Kwahiyo amebuni usemi "Hustler nation" , akimaanisha vijana wanaohangaika kutafuta riziki .

Bw Ruto ameahidi mfumo wa kiuchumi unaowainua watu wenye pato la chini , akisema utawanufaisha masikini ambao wanakabiliwa na gharama ya mzozo wa maisha ambao umeikumba dunia kufuatia janga na Corona na vita ya Ukraine.

Hili ni jaribio la kwanza la mwanaume huyu mwenye umri wa miaka 55 la kugombea urais. Ana tumaini la kushinda kwenye uchaguzi wa Agosti 9 sawa na alivyoshinda ubunge wa jimbo la Eldoret Kaskazini mwaka 1997.

Alijiunga na siasa katika mwaka 1992, ambapo alifunzwa , kama alivyosema na aliyekuwa rais wa Kenya wakati huo Daniel Arap Moi.

Bw Ruto alikuwa sehemu ya tawi la vijana la chama kilichotawala wakati mmoja cha Bw Moi , na alikuwa mmoja wa wanaharakati waliopewa jukumu la kuhamasisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi katika mwaka huo huo.

Kwa sasa ana sifa ya kuwa mzungumzaji mwenye mamlaka mwenye uwezo wa kukusanya umati mkubwa katika mikutano ya kisiasa, na mwenye kufanya vyema katika mahojiano na vyombo vya habari.

Mara nyingi huanza kuzungumza kwa kusema "Rafiki yangu", matamshi yanayomsaidia kuanzisha uhusiano na wapiga kura.

Kuhama miungano

Baada ya kushikilia nyadhifa mbali mbali za uwaziri- ikiwa ni pamoja na waziri wa elimu-alipanda cheo na kuwa Naibu wa rais baada ya uchaguzi wa mwaka 2013.

Bw Ruto aligombea uchaguzi huo kama mgombea mwenza wa rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta, ambapo aliwashangaza Wakenya wengi kwasababu walikuwa katika pande zinazopingana kisiasa katika uchaguzi uotangulia.

Ulikuwa ni muungano wa manufaa, kwani wote wawili walikuwa wameshitakiwa na mahakama ya Kimataifa ya uhalifu kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu baada ya kushutumiwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ulioibua mgawanyiko mkubwa, ambapo watu 1,200 waliuawa. Katika uchaguzi huo, Bwana Ruto alikuwa ameunga mkono mgombea wa upinzani raila Odinga-ambaye sasa ni hasimu wake kisiasa-huku Bw Kenyatta akimuunga mkono aliyekuwa rais wakati huo -Mwai Kibaki katika azma ya kuwania tena urais.

Muungano wao, ulioipachikwa jina la ''bromance'', ulizaa matunda kwani wanaume hao wawili walichukua mamlaka, yaliyowaweka katika nafasi imara ya kuondokana na tisho lililowakabili wote kutoka mahakama ya ICC- mafanikio ambayo waliyapata wakati mwendesha mashitaka alipomuondolea mashitaka Rais Kenyatta katika mwaka 2014 na Jaji akatupa nje kesi dhidi ya Bw Ruto mwaka 2016.

Hatahivyo Muungano wao ulivunjika katika mwaka 2018,wakati Bw kenyataa- katika mabadiliko mengine makubwa ya kisiasa alipoamua - kufanya maridhinao na Bw Odinga, na kuondoa matumaini ya Bw Ruto kwamba rais anayeondoka mamlakani angemuidhinisha kama mrithi wake katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea kwa sasa.

Washirika wa rais wanamlaumu Bw Ruto kwa kukosa utiifu, madai ambayo anayakanusha, lakini amekiri kutofautiana, kwa kusema kuwa yeye na rais ''wanamtizamo tofauti wa siasa.''

Bw Ruto, amesalia kuwa mamlakani, kutokana na vipengele vya katiba vnavyomuwezesha Naibu rais kubakia mamlakani hadi muhula wake unapomalizika.

Mmiliki wa ardhi kubwa na mkulima makini

Ufuasi ya kikabila una fursa kubwa katika siasa za kenya na bw Ruto anatoka katika kabila la tatu kwa ukubwa , la Kalenjin, ambapo limekwisha kuwa na rais mmoja tu, hayati daniel Arap Moi, ambaye alikuwa rais wa muda mrefu zaidi aliyeitawala Kenya.

Amemuoa Rachael, ambaye kwa mara ya kwanza walikutana katika mikutano vijana ya kanisa.

Wana watoto sita. Kijana wao mkubwa Nick, wakati mmoja alibarikiwa na wazee wa Kikalenjin, jambo lililochochea uvumi kwamba alikuwa anatayarishwa kwa ajili ya kuchukua wadhifa wa kisiasa, huku binti yao, June, akifany akazi katika wizara ya mambo ya nje.

Bw Ruto anapenda ukulima , jambo ambalo limemfanya awe mkulima wa mahindi, ufugaji wa ng'ombe na kuku.

Anamiliki ardhi kubwa katika maeneio ya magharibi na kpwani ya Kenyana pia amewekeza katika sekta ya utalii.

bw Ruto amekuwa akihusishwa na kashfa za ufisadi katika serikali na vyanzo vya utajiri wake vimekuwa vikiibua tetesi nyingi.

Mwezi Juni mwaka 2013, Mahakama ya juu zaidi ilimuamuru asalimishe shamba la heka 100, na kulipa fidia kwa mkulima ambaye alimshutumu kunyakua ardhi wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Alikanusha kufanya kosa lolote, na anaendelea kuwaomba kura vijana, akiwaahidi kuwapatia fursa ya kuboresha maisha yao, kama alivyofanya yeye.