Uchaguzi Kenya 2022: Habari potofu zinazosambaa mtandaoni

Iliyochapishwa

Kampeni rasmi katika uchaguzi wa Kenya sasa inaendelea kabla ya upigaji kura mwezi Agosti.

Tayari, mapendekezo ghushi ya kuidhinishwa kwa wagombeaji wawili wakuu wa urais yanashirikiwa kote mtandaoni.

Tumekuwa tukiangalia baadhi ya machapisho na video za kupotosha za mitandao ya kijamii zinazosambazwa.

Barack Obama hajaidhinisha mgombeaji

Rais Uhuru Kenyatta anastaafu baada ya mihula miwili ya uongozi.

Mmoja wa wanaotarajia kuchukua nafasi yake ni naibu wake, William Ruto.

Video imeibuka, ikidaiwa kumuonyesha aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama, akitangaza kumuunga mkono Bw Ruto.

Video hiyo hata hivyo imebadilishwa na haina uhusiano wowote na uchaguzi wa Kenya - Bw Obama hajaidhinisha mgombea yeyote.

Video hiyo iliyoshirikiwa na watu wengi imetayarishwa ili kumwonyesha Bw Obama akionyesha picha kubwa ya mgombeaji wake mteule, ikiwa na mabango ya uwongo kwenye skrini yanayoonyesha kuwa ni habari ya Habari za BBC, na ilichapishwa kwenye akaunti ya TikTok.

Maandishi yana hitilafu ya kisarufi na rangi za mabango hazilingani.

Video hiyo ya kweli, iliyotumika kama msingi wa hizo ghushi, ilirekodiwa katika Taasisi ya Smithsonian huko Washington mnamo 2018, ambapo Bw Obama alikuwa akionyesha picha yake mwenyewe.

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma

Hakuna mipango ya kuvunja biashara kubwa

Wafuasi wa Raila Odinga, mgombeaji mwingine mkuu wa urais, wamekuwa wakishiriki video ambayo wanadai inamuonyesha mgombea mwenza wa Bw Ruto, Rigathi Gachagua, akisema muungano wake, Kenya Kwanza, - ukichaguliwa - utasambaratisha kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano nchini Kenya, Safaricom.

Mahojiano ya kweli, yaliyotolewa na Bw Gachagua kwa kituo kimoja cha redio nchini, yalichapishwa mtandaoni kwa tafsiri ndogo ya Kiingereza iliyosomeka: "Tutaiua [Safaricom] na kuwapa watu pesa hizo kama takrima."

Lakini akizungumza kwa lugha ya Kikuyu, Bw Gachagua hakusema haya.

Alichosema hasa ni: "Badala ya kuwa na kampuni moja kubwa iitwayo Safaricom inalipa ushuru, ukichukua pesa kutoka kwa kampuni kubwa na kuwapa watu wengi ... ushuru kutoka kwa wengi ukijumlishwa itakuwa kubwa mara 30 kuliko ya kampuni kubwa."

Lilikuwa ni pendekezo la kugawa upya faida ili kusaidia biashara ndogo ndogo, na kwa wazi sio moja ya "kuua" biashara ya ushirika.

Katika hali ya kushangaza ya tukio hili, taarifa kwa vyombo vya habari ilionekana mtandaoni muda mfupi baada ya video hiyo, inayodaiwa kutoka Safaricom, ikilaani hisia zilizotolewa kwenye mahojiano hayo, ambayo yalifikia, ilisema waraka huo, "kuzima [Safaricom] na makampuni mengine makubwa ya kibiashara" .

Taarifa hiyo iliendelea: "Tunataka kushutumu matamshi haya [ya Bw Gachagua] kwa maneno makali iwezekanavyo."

Hata hivyo, taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ilikuwa ya uwongo na Safaricom ilitoa taarifa yake ya kweli kwenye Twitter kuthibitisha hili.

Uidhinishaji mwingine wa uwongo

Wagombea wote wawili wakuu wa urais wanatafuta uungwaji mkono kutoka kwa kabila la Wakikuyu lenye utajiri wa kura. (Ruto anatoka jamii ya Wakalenjin na Odinga ni Mjaluo).

Kwa hivyo, kuidhinishwa na mtoto wa Rais wa zamani wa Kenya Mwai Kibaki - Mkikuyu - itakuwa tuzo inayotamaniwa sana. Akaunti ghushi ya Twitter imeonekana, inayodaiwa kumilikiwa na Jimmy Kibaki, mtoto mkubwa wa rais wa zamani.

Akaunti hiyo ambayo imebadilishwa jina tangu hapo, iliundwa mwezi Februari na hivi majuzi ilituma ujumbe kwenye Twitter kwamba ikimuunga mkono William Ruto kuwania urais.

Akaunti hii ni moja tu kati ya akaunti nyingi ghushi zinazotumia jina la Jimmy Kibaki, na ametoa taarifa akiwataka Wakenya kuzipuuza.

Hapana, Rais Kenyatta hawezi kushiriki

Katiba inaweka kikomo cha rais kwa mihula miwili, ambayo ina maana kwamba Bw Kenyatta hawezi kugombea tena mwaka huu.

Hata hivyo, baadhi ya watumiaji wa mtandaoni, akiwemo angalau mwanasiasa mmoja mashuhuri, wamekuwa wakipendekeza kuwa anaweza kuwa mgombea wa naibu wa rais.

"Nikifikiria tena kwa sauti kubwa :- kifungu cha 137(1) cha Katiba ya Kenya hakimwondoi rais wa sasa kuwania kama naibu rais!" Seneta Ledama Ole Kina aliandika katika Twitter

Ingawa ni kweli kwamba kifungu hiki cha katiba hakikatazi hili waziwazi, kuna kifungu kingine kinachomzuia

Kifungu cha 148 (1) kinasema mtu anayependekezwa kuwa naibu wa rais lazima "awe na sifa za kuteuliwa kuchaguliwa kuwa Rais."

Akiwa amehudumu kwa mihula miwili, Bw Kenyatta hastahiki chini ya sharti hili.