Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanawake wanaonufaika na utalii kupitia urithi wa utamaduni wao Zanzibar
Kwa wanawake wengi katika jamii za pwani ya Tanzania, talaka inaweza kuwa mwanzo wa changamoto mpya za kijamii na kiuchumi.
Kwa baadhi yao, hali hiyo huambatana na hukumu za jamii, kutengwa na wakati mwingine kupoteza matumaini ya kuanza maisha yao upya.
Lakini kwa Maskat Shineni, mkaazi wa Zanzibar na mwanzilishi wa kikundi cha Mamas of Zanzibar, talaka haikuwa mwisho wa safari yake bali mwanzo wa safari mpya ya kujijenga na kuwasaidia wanawake wengine.
"Ukiwa mtalaka, mara nyingi watu wanakuona kama hukufaa vya kutosha au kuna kosa ulilofanya lililosababisha ndoa kuvunjika," alisema.
Anasema licha ya kutokuchukua maneno ya watu kwa uzito mkubwa, maisha baada ya talaka yalikuwa na changamoto nyingi.
"Unajikuta una watoto, uko peke yako na unatakiwa kutafuta namna ya kupata kipato ili kuwahudumia. Hapo ndipo wanawake wengi huumia kwa sababu hawajui waanzie wapi."
Kutoka maumivu hadi matumaini
Maskat anasema msaada wa wazazi wake pamoja na kujiamini mwenyewe vilimsaidia kusimama tena.
Akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika sekta ya utalii na hoteli, alianza kutafuta njia ya kugeuza changamoto zake kuwa fursa.
Ndipo alipokuja na wazo la kuanzisha Mamas of Zanzibar, kikundi kinachowaunganisha wanawake wa Zanzibar kuwakaribisha wageni, kuwafundisha mapishi ya vyakula vya asili na kuwaonyesha utamaduni wa Zanzibar.
"Niliianzisha Mamas of Zanzibar ili nijiondoe kwenye mawazo ya kwamba sitoweza au nitabaki peke yangu. Nilihitaji kitu cha kunipa matumaini na kunifanya niangalie mbele," anasema.
Mwanzoni aliwashirikisha majirani zake wachache kuhusu wazo hilo.
"Nilikuwa naogopa hata kuwaambia kwasababu sikujua kama nitafanikiwa. Lakini waliposikia wazo langu, walikaa kikao chao na siku iliyofuata wakaniambia tuendeleze jambo hili na wataniunga mkono."
Wanawake 40 na safari ya kujikomboa kiuchumi
Leo, kikundi hicho kina takribani wanawake 40.
Kupitia shughuli za utalii wa kitamaduni, wanawake hao hupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani na kuwaonyesha mapishi ya kizanzibari, matumizi ya viungo mbalimbali na maisha ya kila siku ya Wazanzibari.
Maskat anasema lengo lake si kuwapa wanawake ajira pekee, bali kuwajengea kujiamini na uwezo wa kusimama wenyewe.
"Kumsaidia mwanamke mmoja ni kama umeisaidia jamii nzima. Kuna watoto na familia nyingi zinazofaidika."
Anakumbuka mmoja wa wanawake wa kwanza kujiunga na kikundi hicho ambaye wakati huo alikuwa akihangaika kulipa kodi ya nyumba.
Kupitia kipato alichopata, aliweza kuhudumia watoto wake, kununua kiwanja na baadaye kujenga nyumba yake mwenyewe.
"Ukianzisha kitu halafu kikawasaidia watu, unapata zaidi ya kile ulichotoa. Hilo hunipa faraja kubwa sana," anasema Maskat.
"Sasa naweza kujitatulia matatizo yangu"
Salma Makame Khamis ni mmoja wa wanachama wa Mamas of Zanzibar.
Anasema kabla ya kujiunga na kikundi hicho alikuwa ameacha kazi ya kuwaongoza watalii na kubaki nyumbani baada ya kuolewa.
"Baadaye nilikuja hapa na kuendelea na kipaji changu. Nimefurahi kuwa na kina mama wenzangu ambao tunasaidiana na kushirikiana," anasema.
Kwa mujibu wake, kipato anachopata kimemwezesha kusaidia familia yake na kujitegemea zaidi.
"Ninaweza kutatua matatizo yangu kwa kutumia pesa yangu mwenyewe. Hilo limeniongezea kujiamini."
Kwa upande wake, Subira Mikidadi Sharifu anasema maisha yake yalikuwa magumu kabla ya kujiunga na kikundi hicho.
"Nilikuwa sina kazi na maisha yalikuwa magumu sana. Lakini tangu nijiunge na Mamas of Zanzibar najisikia amani na nina uwezo wa kukabiliana na changamoto zangu."
Naye Mwanaisha Hemedi Juma anasema kipato anachopata sasa kimemwezesha kuwasomesha watoto wake katika shule binafsi na kusaidia maendeleo ya familia.
"Maisha yangu ya sasa na ya zamani ni tofauti kabisa. Ninajivunia kuwa naweza kuwahudumia watoto wangu na kushiriki katika maendeleo ya familia."
Utalii unaowaunganisha wageni na jamii
Kwa Maskat, chakula ni daraja muhimu linalowaunganisha watu kutoka tamaduni tofauti.
"Nilitaka kuonyesha kwamba Zanzibar ni zaidi ya fukwe na hoteli. Zanzibar ni watu wake pia."
Anasema kupitia shughuli zao, wageni hupata nafasi ya kujifunza kuhusu vyakula vya asili, matumizi ya viungo maarufu vya Zanzibar na maisha ya kila siku ya wanawake wa eneo hilo.
"Ni muhimu kuhifadhi urithi wetu wa vyakula kwasababu wanawake ndio wanaojua siri za jikoni. Tunapowafundisha wageni ni kama tunadumisha utamaduni wetu."
Kwa mujibu wake, wanawake wengi wa Zanzibar huona watalii wakifika kisiwani lakini mara chache hupata nafasi ya kushirikiana nao moja kwa moja.
"Ni wakati wa wanawake wa Zanzibar kushiriki zaidi katika sekta ya utalii na kuonyesha utamaduni wetu, mavazi yetu na maisha yetu."
Mtazamo wa jamii kuhusu wanawake waliotalikiwa
Baadhi ya wakazi wa Zanzibar waliozungumza na BBC wanasema bado kuna mtazamo wa kuwalaumu wanawake pale ndoa zinapovunjika.
Mwanamume mmoja aliyetoa maoni yake anasema jamii mara nyingi huwanyooshea wanawake vidole bila kujua chanzo halisi cha migogoro ya ndoa.
"Ndoa ikivunjika si lazima mwanamke ndiye awe chanzo. Wanaume pia wana mchango katika matatizo yanayoweza kusababisha ndoa kuvunjika."
Naye mwanamke mwingine anasema kuachika hakupaswi kumfanya mwanamke kupoteza haki zake wala kuonekana hana thamani.
"Mwanamke anatakiwa kuwa jasiri na kuendelea kutafuta njia za kujipatia kipato na kujenga maisha yake."
Talaka Zanzibar: Takwimu zinasemaje?
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makaazi ya Tanzania ya mwaka 2022, kuna ongezeko la talaka na wanandoa kutengana katika baadhi ya maeneo ya Tanzania, huku Kusini mwa Unguja kukiwa miongoni mwa maeneo yaliyoonesha viwango vya juu vya hali hiyo.
Kwa Maskat, hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuwepo kwa mifumo ya kuwasaidia wanawake wanaopitia changamoto mbalimbali za maisha.
"Jamii isiwatazame kwa jicho kali wajane au wanawake waliotalikiwa. Wakati mwingine wanahitaji mtu wa kuwainua tu. Msaada mdogo unaweza kubadilisha maisha ya mtu kabisa."
Ndoto ya baadaye
Licha ya mafanikio aliyoyapata, Maskat anasema bado ana ndoto ya kupata eneo kubwa zaidi litakalokuwa kituo cha kuwasaidia wanawake wengi zaidi.
Kwa sasa shughuli za Mamas of Zanzibar zinafanyika nyumbani kwake.
"Ningependa iwe sehemu ya kimbilio kwa wanawake wanaopitia changamoto mbalimbali. Wale ambao hawajawahi kufanya kazi, ambao hawakusoma, na hata waliosoma lakini wanahitaji fursa ya kuanza upya."
Anasema jambo kubwa analojivunia ni kuona wanawake wakiondoka wakiwa na furaha, matumaini na kujiamini zaidi.
"Usikate tamaa. Tafuta kile unachokipenda na ukipiganie. Ukiamini unaweza, utaweza," anashauri wanawake wanaoanza maisha upya baada ya talaka au changamoto nyingine.
Kwa Maskat, Mamas of Zanzibar si mradi wa utalii pekee, bali ni njia ya kuhifadhi utamaduni wa Zanzibar na kuwapa wanawake nafasi ya kujenga upya maisha yao.