Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani na Iran zaanza siku ya pili ya mazungumzo nchini Uswisi yanayolenga kuimarisha makubaliano ya mpito ya kumaliza mzozo

Mazungumzo ya Marekani na Iran kuhusu kufikia makubaliano ya mwisho ya kusitisha vita yanaendelea nchini Uswisi.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Netanyahu asema: “Sifanyi kila kitu ambacho Trump anataka”

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa watu wengi hudhani yeye na Rais wa Marekani, Donald Trump, hufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu katika kila jambo, lakini si kweli kwamba kila mara wanaafikiana.

    Netanyahu aliongeza kuwa si wakati wote hufuata matakwa ya Marekani, akisisitiza kuwa Israel hufanya maamuzi yake kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa.

    Kauli hiyo imekuja baada ya Trump pamoja na Makamu wa Rais wa Marekani, J. D. Vance, kumkosoa hadharani.

    Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Sera uliofanyika mjini Jerusalem, Netanyahu alisema hataruhusu Iran kupata silaha za nyuklia na kwamba majeshi ya Israel yataendelea kuwepo kusini mwa Lebanon kwa muda wowote utakaoonekana kuwa wa lazima kwa usalama wa nchi yake.

    Akihutubia Mkutano wa JNS mjini Jerusalem, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema:

    "Nchini Marekani, watu husema kwamba Rais Trump hufanya kila ninachomwambia afanye. Nchini Israel, watu hudhani kwamba mimi hufanya kila anachotaka Trump. Lakini hakuna kati ya mambo hayo yaliyo ya kweli."

    Netanyahu alitumia kauli hiyo kusisitiza kwamba yeye na Rais wa Marekani, Donald Trump, wanafanya maamuzi kwa kujitegemea kulingana na maslahi ya nchi zao, na si kwamba mmoja humwelekeza au kumdhibiti mwingine.

    "Sisi ni viongozi wa mataifa huru na yenye fahari. Wakati mwingine maoni yetu hutofautiana. Kila mmoja wetu anasimamia maslahi ya nchi yake. Mimi ninasimamia maslahi na usalama wa Israel."

    Netanyahu aliendelea kusema:

    "Mara nyingi mawazo yetu yanaendana. Lakini wakati mwingine hayaendani. Tunaheshimu mamlaka ya kila mmoja, uongozi wa kila mmoja, na dhamira ya kila mmoja kwa wananchi wake."

    Kauli hiyo ya Benjamin Netanyahu ilikuwa ikisisitiza kwamba licha ya uhusiano wa karibu kati ya Israel na Marekani, yeye na Rais wa Marekani, Donald Trump, hawakubaliani katika kila jambo na kila mmoja hufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya taifa lake.

    Unaweza kusoma;

  2. Polisi wa Australia wakamata tani 2.7 za kokeni iliyofichwa kwenye maghala ya siri

    Polisi wa Australia wamekamata tani 2.7 za kokeni, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa nchini humo.

    Dawa hizo za kulevya, zenye thamani inayokadiriwa kufikia dola za Australia milioni 816 (takriban pauni milioni 433), ziligunduliwa Ijumaa katika vyumba vya siri vilivyofichwa chini ya sakafu bandia ndani ya makontena matatu ya usafirishaji kwenye eneo la Londonderry, magharibi mwa mji wa Sydney.

    Wanaume wawili wenye umri wa miaka 21 na 25 walikamatwa eneo la tukio baada ya kudaiwa kujaribu kuwatoroka polisi. Wameshtakiwa kwa kumiliki kiasi kikubwa cha dawa za kulevya zilizoingizwa nchini kinyume cha sheria.

    Polisi wanasema kokeni hiyo ilisafirishwa kwa magendo kuingia Australia kupitia mji mdogo wa Midge Point, ulioko Kaskazini mwa jimbo la Queensland, kwa maagizo ya kundi la uhalifu uliopangwa.

    Wanaume hao wawili waliwekwa rumande baada ya kufikishwa mahakamani Jumamosi, na wanaweza kukabiliwa na kifungo cha maisha gerezani iwapo watapatikana na hatia.

    Polisi walisema uvamizi huo ulikuwa sehemu ya operesheni iliyopewa jina la Operation Minjiang, ambayo ilianzishwa mwezi Mei baada ya kilo 40 za kokeni kupatikana zikielea majini karibu na sehemu ya kushushia boti katika Midge Point.

    Wiki iliyopita, watu wengine sita katika majimbo ya Queensland na New South Wales walikamatwa na kushtakiwa kutokana na uchunguzi ulioanzishwa kufuatia ugunduzi huo.

    Aidha, chombo kikubwa cha majini kinachoshukiwa kuwa sehemu ya mtandao wa usafirishaji wa dawa hizo kwa magendo kimezuiliwa katika visiwa vya Solomon.

  3. Trump: Lazima Iran isitishe vikosi washirika vyake nchini Lebanon

    Mara tu baada ya matamshi ya J. D. Vance kabla ya mkutano wa pande nne uliofanyika nchini Switzerland, Rais wa Marekani, Donald Trump, aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social:

    "Iran lazima mara moja izuie makundi yake washirika nchini Lebanon, ambayo yamekuwa yakifadhiliwa kwa kiasi kikubwa, kuendelea kusababisha matatizo. Ikiwa Iran haitafanya hivyo, tutaishambulia tena kwa nguvu zaidi kuliko tulivyofanya wiki iliyopita."

    Mazungumzo kati ya Iran na Marekani yanaendelea nchini Uswisi, yakihusisha pia uwepo wa wawakilishi kutoka Qatar na Pakistan.

    Lengo la mazungumzo hayo ni kutafuta makubaliano ya mwisho yatakayosaidia kupunguza mvutano wa kikanda, kusitisha mapigano yanayohusisha washirika wa Iran katika eneo hilo, na kujadili masuala ya usalama pamoja na mpango wa nyuklia wa Iran.

    Unaweza kusoma;

  4. Starmer anatafakari mustakabali wake wa kisiasa huku shinikizo la kumtaka ajiuzulu likiongezeka

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, anaripotiwa kutafakari mustakabali wake wa kisiasa wakati kukiwa na shinikizo la kutaka atangaze kujiuzulu.

    Hali hiyo imekuja baada ya mshirika wake wa karibu katika Baraza la Mawaziri, Peter Kyle, kusema kuwa Waziri Mkuu alikuwa akizingatia "uhalisia wa kisiasa" kufuatia ushindi wa Andy Burnham katika uchaguzi mdogo wa Makerfield wiki iliyopita, ambao umefungua njia kwake kuwania uongozi wa Chama cha Labour.

    Baada ya matokeo hayo, Starmer amekabiliwa na wito mpya kutoka kwa baadhi ya mawaziri waandamizi wakimtaka kuweka wazi ratiba ya kuondoka kwake madarakani ili kumpisha Burnham.

    Katika pigo jingine kwa kiongozi huyo wa Labour, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema kuwa Starmer "atajiuzulu kama Waziri Mkuu", huku akikosoa utendaji wake akiwa madarakani.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema Starmer "ameshindwa vibaya" katika sera za uhamiaji na nishati, na akasisitiza tena wito wake wa kufunguliwa zaidi kwa uchimbaji wa mafuta katika Bahari ya Kaskazini.

    Trump aliongeza:

    "Namtakia kila la heri!"

    Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza iliiambia BBC kwamba viongozi hao wawili, ambao walikutana mara ya mwisho katika mkutano wa viongozi wa G7 nchini Ufaransa wiki iliyopita, hawakuwa wamezungumza mwishoni mwa wiki.

    Mara baada ya ushindi wa Burnham, Starmer aliendelea kusisitiza kwamba angepambana na jaribio lolote rasmi la kuondolewa kwenye uongozi wa chama.

    Hii ina maana kuwa kama kutakuwa na changamoto ya uongozi, uchaguzi wa ndani wa Labour utahitajika, ambapo wanachama wa chama pamoja na wafuasi wa vyama vya wafanyakazi vinavyoshirikiana na Labour wataamua mustakabali wa chama hicho.

    Unaweza kusoma;

  5. Kiongozi wa Hezbollah: Haiwezekani kwa majeshi ya Israel kuendelea kubaki nchini Lebanon

    Kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, alijibu kauli za Waziri Mkuu wa Israel siku ya Jumapili kuhusu majeshi ya Israel kuendelea kubaki katika eneo la usalama kusini mwa Lebanon, akisema:

    "Haiwezekani kwa majeshi ya Israel kubaki nchini Lebanon."

    Aliongeza:

    "Hakuna eneo la usalama kwa Israel. Tuna jeshi la taifa ambalo lina jukumu la kulinda nchi, na sisi tunashirikiana nalo."

    Kiongozi huyo wa Hezbollah alisema katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja kwenye televisheni kwamba Israel ni "nchi adui" na kwamba "lazima iondoke nchini Lebanon."

    Pia alilaumu Marekani kwa kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Israel nchini Lebanon, akisema kuwa Marekani inabeba jukumu la hali hiyo kuendelea.

    Unaweza kusoma;

  6. Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran inatarajiwa kuendelea usiku kucha

    Mazungumzo kati ya Marekani na Iran ya kufikia makubaliano ya mwisho ya kumaliza vita yanatarajiwa kuendelea usiku kucha nchini Uswisi, afisa mwandamizi wa Marekani anayeshiriki katika mazungumzo hayo amesema.

    Mazungumzo hayo yalianza Jumapili, kufuatia makubaliano ya wiki iliyopita ya kufikia suluhu ndani ya siku 60.

    Jumapili usiku, mwanadiplomasia huyo wa Marekani alisema kwamba majadiliano yalikuwa yakijikita katika kufafanua baadhi ya ujumbe zilizokuwa hazieleweki kutoka Iran kuhusu kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, utekelezaji wa usitishaji mapigano kusini mwa Lebanon, pamoja na baadhi ya vipengele vya makubaliano ya nyuklia.

    Mapema, Rais wa Marekani, Donald Trump, alikuwa ametishia kuishambulia Iran ikiwa haitaisimamisha Hezbollah huku mapigano kati ya kundi hilo na Israel yakiendelea nchini Lebanon. Iran ilipuuzilia mbali onyo hilo, ikisema iko tayari kupigana.

    Afisa huyo alisema ujumbe wa pande zote mbili, ambao unakutana katika mji wa Lucerne nchini Switzerland, utatumia matokeo ya mazungumzo ya leo kama msingi wa mazungumzo ya kiufundi yatakayoendelea.

    Makubaliano ya awali ya wiki iliyopita yanajumuisha ahadi ya kufikia makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60, pamoja na kusitishwa kwa mapigano katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon, na kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Hata hivyo, tangu wakati huo kumeshuhudiwa kuongezeka kwa mapigano kati ya Hezbollah na majeshi ya Israel kusini mwa Lebanon, pamoja na mashambulizi ya anga ya Israel ambayo wizara ya afya ya Lebanon imesema yamesababisha vifo vya raia kadhaa, wakiwemo wanawake na watoto.

    Kuongezeka huko kwa mzozo kuliipelekea Marekani kutangaza usitishaji mpya wa mapigano kati ya Israel na Hezbollah siku ya Ijumaa.

    Lakini mapigano na mashambulizi ya anga yaliyoendelea yaliifanya Iran kutangaza Jumamosi kwamba imeufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ingawa takwimu za ufuatiliaji wa meli zinaonesha kuwa vyombo vya majini vimeendelea kupita katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Unaweza kusoma;

  7. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo.