Kwa nini uume ni kipimo muhimu cha afya ya mwanaume

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Tatizo la kushindwa kusimamisha uume linaweza kuwa ishara ya awali ya mshtuko wa moyo, kiharusi, kisukari na hata maradhi ya kupoteza kumbukumbu.

Watafiti wanasema ni wakati wa wagonjwa na madaktari kulichukulia suala hili kwa uzito zaidi.

Tatizo la kushindwa kusimamisha uume linaweza kuelezwa kama janga la kimya kimya.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 40 hukumbwa na hali hii kwa kiwango fulani. Hata hivyo, wengi wao husita kuzungumzia tatizo hilo, hata na watu wao wa karibu.

Linapojitokeza katika mazungumzo, mara nyingi suala hili huchukuliwa kama mzaha badala ya kuonekana kama ishara ya mapema ya matatizo makubwa ya kiafya yanayoweza kujitokeza baadaye. Lakini utafiti unaozidi kuongezeka unaonyesha kuwa afya ya uume inaweza kuwa kiashiria muhimu cha afya ya jumla ya mwanaume.

Wataalamu wanaeleza kuwa tatizo la kushindwa kusimamisha uume linaweza kuwa ishara ya magonjwa mbalimbali makubwa, yakiwemo kisukari, magonjwa ya moyo, kiharusi na maradhi ya mfumo wa fahamu yanayosababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na kukumbuka.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya ya ngono, Emmanuele Jannini wa Chuo kikuu cha Rome Tor Vergata, tatizo la kushindwa kusimamisha uume ni kama "kengele ya tahadhari ya mapema" inayoweza kuashiria kuwepo kwa matatizo makubwa ya kiafya mwilini. Jannini, ambaye hivi karibuni alihariri kitabu cha kitaaluma kinachochambua ushahidi uliopo kuhusu suala hili, anasema kuwa uchunguzi wa mapema na wa kina wa tatizo hilo unaweza kuwasaidia madaktari kubaini magonjwa hatari yanayowakabili wanaume kabla hayajafikia hatua mbaya.

Hata hivyo, wanaume wengi husita kuzungumzia afya yao ya kingono kutokana na aibu au hofu, hali inayowafanya kukosa fursa muhimu za kugundua na kutibu matatizo ya kiafya mapema.

Haya ndiyo unayohitaji kujua kuhusu dalili na ni wakati gani unapaswa kumuona daktari.

Tatizo la mzunguko wa damu

Kama ilivyo kwa magonjwa mengi, kiwango halisi cha kuenea kwa tatizo la kushindwa kusimamisha uume hutegemea namna linavyofafanuliwa na kupimwa. Kwa sababu hiyo, tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa kiwango chake duniani miongoni mwa wanaume watu wazima kinatofautiana kutoka asilimia 3 hadi asilimia 76.5, tofauti kubwa sana.

Hata hivyo, mojawapo ya tafiti kubwa na za kina zaidi iliwahusisha takribani watu 1,200 kwa kutumia dodoso za kina na kubaini kuwa asilimia 39 ya wanaume wenye umri wa miaka 40 walikumbwa mara kwa mara na kiwango fulani cha udhaifu wa nguvu za kiume. Kiwango hicho kiliongezeka hadi asilimia 67 kwa wanaume wenye umri wa miaka 70.

Aidha, wanaume wenye tatizo la kushindwa kusimamisha uume walibainika kuwa na uwezekano mkubwa kwa asilimia 59 wa kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo na uwezekano mkubwa kwa asilimia 34 wa kupata kiharusi.

Kwa namna nyingi, tatizo la kushindwa kusimamisha uume ni tatizo la mfumo wa mzunguko wa damu.

Ndani ya uume kuna miundo miwili yenye tishu laini kama sifongo inayojulikana kama corpora cavernosa, ambayo kwa kawaida huwa imelegea. Mwanaume anapopata msisimko wa kingono, ubongo hutuma ishara zinazolegeza misuli inayozunguka mishipa ya damu ya uume, na hivyo kuruhusu damu nyingi kuingia katika miundo hiyo miwili.

Miundo hiyo inapojazwa damu na kupanuka, huanza kujinyoosha na kubana mishipa inayorudisha damu kutoka kwenye uume, jambo linalosababisha damu kubaki ndani yake.

Kama puto linalojazwa hewa, uume huongezeka ukubwa na kuwa mgumu. Kitu chochote kinachopunguza kiasi cha damu kinachoingia kwenye uume kinaweza kuathiri uwezo wa mwanaume kupata au kudumisha usimamo wa uume.

Mara nyingi tatizo hili hutokana na sababu za kisaikolojia. Hali ya msongo wa mawazo inayohusisha homoni za adrenalini na cortisol inaweza kusababisha mishipa ya damu kubana, na hivyo kuzuia corpora cavernosa kujaa damu na kuwa ngumu.

Viwango vya juu vya msongo wa mawazo pia vinaweza kuathiri uzalishaji wa homoni ya testosterone, jambo linaloweza kupunguza hamu ya kufanya ngono na kupunguza msisimko wa kingono. Aidha, watu wenye matatizo ya tezi na homoni kama hypogonadism huwa na uzalishaji mdogo wa testosterone, hali ambayo inaweza pia kuchangia tatizo hili.

Mbali na hayo, msongo wa mawazo mara nyingi huambatana na hali ya kutawanyika kwa fikra, jambo linaloweza kumfanya mtu ashindwe kuzingatia tendo la ndoa.

Kwa mtazamo wa mageuzi ya binadamu, hali hii ina sababu yake. Ikiwa msongo wa mawazo unasitisha msisimko wa kingono, mwili huhifadhi nguvu na rasilimali zake kwa ajili ya kujiokoa wakati wa hatari.

"Kama mazingira yana hatari, ni muhimu kutozaliana," anasema Emmanuele Jannini.

Kiashiria cha magonjwa ya moyo na ubongo

Katika baadhi ya matukio, kushindwa kusimamisha uume kunaweza kuwa ishara ya tatizo kubwa zaidi la kiafya.

Mojawapo ya sababu kuu ni ugonjwa wa kuziba na kukakamaa kwa mishipa ya damu, unaojulikana kama atherosclerosis. Hali hii hupunguza mtiririko wa damu mwilini na kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo.

Kwa kuwa mishipa ya damu ya uume ni midogo kuliko sehemu nyingi za mwili, mara nyingi huathirika mapema zaidi. Ndiyo maana matatizo ya usimamo wa uume yanaweza kuonekana miaka kadhaa kabla ya mtu kupata dalili za ugonjwa wa moyo.

Utafiti uliohusisha zaidi ya watu 154,000 ulibaini kuwa wanaume wenye tatizo hili walikuwa na uwezekano mkubwa kwa asilimia 59 kupata ugonjwa wa mishipa ya moyo na asilimia 34 kupata kiharusi.

Wataalamu wanasema kuwa uwezo mzuri wa kusimamisha uume ni ishara kwamba mfumo wa mishipa ya damu unafanya kazi vizuri.

Pia kuna ushahidi unaoonyesha kuwa hali hii inaweza kuhusishwa na hatari kubwa ya kupungua kwa uwezo wa kufikiri na kukumbuka. Tafiti zimebaini kuwa wanaume waliogundulika kuwa na tatizo la kushindwa kusimamisha uume walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata maradhi ya kupoteza kumbukumbu katika miaka iliyofuata.

Uhusiano wake na kisukari

Kisukari ni mojawapo ya magonjwa yanayohusishwa kwa karibu sana na tatizo hili.

Viwango vya juu vya sukari kwenye damu vinaweza kuharibu mishipa ya damu na neva. Hali hiyo hupunguza uwezo wa damu kufika katika sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo uume.

Watafiti wanasema wanaume wenye kisukari aina ya pili wana uwezekano mara tatu zaidi wa kupata tatizo la kushindwa kusimamisha uume kuliko wale wasiokuwa na kisukari.

"Uhusiano kati ya ugonjwa wa kisukari na upungufu wa nguvu za kiume ni mkubwa sana," anasema Bogdan Vlacho, mtafiti katika Taasisi ya Utafiti ya Sant Pau huko Barcelona, ​​nchini Uhispania. "Wanaume walio na kisukari cha aina ya pili wana uwezekano wa mara tatu zaidi wa kupata tatizo la kukosa nguvu za kiume kuliko wale wasio na kisukari."

Kwa wagonjwa wa kisukari, hali hii inaweza pia kuwa ishara ya matatizo mengine makubwa yanayoendelea kujitokeza, yakiwemo uharibifu wa neva, matatizo ya macho yanayoweza kusababisha upofu, na kuchelewa kupona kwa vidonda.

Katika tathmini ya hivi karibuni ya ushahidi wa kisayansi, Bogdan Vlacho pia alibaini kuwa watu wenye kisukari na tatizo la kushindwa kusimamisha uume wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata neuropathi ya pembeni (peripheral neuropathy), yaani uharibifu wa neva katika mikono na miguu, ikilinganishwa na wale wenye kisukari pekee.

Pia wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata retinopathi, hali inayoharibu retina ya jicho na inaweza kusababisha upofu, pamoja na kuchelewa kupona kwa vidonda, jambo ambalo katika baadhi ya visa huweza kupelekea kukatwa kwa kiungo.

Hata hivyo, uchunguzi wa kubaini tatizo la kushindwa kusimamisha uume miongoni mwa wagonjwa wa kisukari bado si sehemu ya kawaida ya huduma za afya.

"Kuna ushahidi unaoonyesha kuwa wataalamu wa afya mara nyingi hawazungumzi na wagonjwa kuhusu suala hili," anasema Santiago Martinez, daktari bingwa wa magonjwa ya homoni katika University of Barcelona nchini Hispania, ambaye alishiriki kuandika tathmini hiyo ya tafiti mbalimbali.

Kwa nini wanaume wanapaswa kutafuta msaada

Licha ya kuwa tatizo hili ni la kawaida, wanaume wengi husita kutafuta msaada wa kitabibu kutokana na aibu na hofu.

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa ni muhimu kuzungumza na mtaalamu wa afya mapema. Mbali na kusaidia kutatua tatizo lenyewe, uchunguzi unaweza kubaini magonjwa mengine hatari kabla hayajafikia hatua mbaya.

Matibabu kama sildenafil, inayojulikana zaidi kwa jina la Viagra, yanaweza kusaidia kuongeza mtiririko wa damu kwenye uume.

(Viagra awali ilitengenezwa kama dawa ya kutibu matatizo ya mfumo wa moyo na mishipa kwa wagonjwa wenye shinikizo la juu la damu, kabla watafiti hawajagundua athari yake ambayo sasa imeifanya ijulikane duniani kote.)

Kwa mujibu wa utafiti uliochambua zaidi ya wagonjwa 885,000, dawa hizi zinaweza pia kusaidia kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya kupoteza kumbukumbu. Utafiti huo ulibaini kuwa matumizi yake yalihusishwa na kupungua kwa hatari ya kupata ugonjwa wa Alzheimer's disease kwa takribani mara mbili.

Angalau, ikiwa mgonjwa atamweleza daktari kuhusu tatizo la kushindwa kusimamisha uume, daktari anaweza kufanya uchunguzi wa vihatarishi vya kawaida vya magonjwa ya moyo, kama vile shinikizo la juu la damu na kuziba au kukakamaa kwa mishipa ya damu (atherosclerosis). Aidha, anaweza kutoa ushauri kuhusu masuala kama unene uliopitiliza, ambao unaweza kuchangia kudhoofika kwa afya ya moyo na mishipa ya damu.

Aidha, mabadiliko ya mtindo wa maisha kama kufanya mazoezi, kupunguza uzito, kuacha kuvuta sigara na kudhibiti kiwango cha sukari mwilini yanaweza kuboresha hali hiyo kwa kiasi kikubwa.

Kwa ujumla, wataalamu wanaonya kuwa kushindwa kusimamisha uume si suala la kupuuzwa wala la kufanyiwa mzaha. Mara nyingi ni ishara ya mapema kwamba kuna tatizo kubwa la kiafya linaloendelea kujitokeza mwilini. Kulitambua na kulifuatilia mapema kunaweza kusaidia kuzuia madhara makubwa zaidi na hata kuokoa maisha.

Hata hivyo, Santiago Martinez na Bogdan Vlacho wanasisitiza kuwa utafiti kuhusu athari za matibabu haya katika kutibu tatizo la kushindwa kusimamisha uume bado uko katika hatua za awali. Kwa sasa, bado haijathibitishwa kikamilifu iwapo matibabu hayo yanaweza pia kupunguza hatari ya matatizo mengine ya kiafya yanayohusishwa na hali hiyo.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid