Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini Ceuta na Melilla ni sehemu ya Uhispania wakati ziko Afrika?
- Author, José Carlos Cueto
- Nafasi, BBC
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Ni maeneo pekee ya Umoja wa Ulaya amayo yako katika bara la Afrika na mipaka yao yamekuwa kitovu cha migogoro mingi ya uhamiaji na mizozo ya kidiplomasia.
Tunazungumzia Ceuta na Melilla, miji miwili ambayo ni mali ya Uhispania kwa zaidi ya miaka 500, lakini Morocco imekuwa ikidai kuwa nni maeneo yake tangu ilipopata uhuru mwaka 1956.
Sheria za kimataifa haziyataji maeneo hayo kuwa makoloni, na Umoja wa Mataifa (UN) unaunga mkono mtazamo kwamba ni majimbo ya Uhispania.
Katika siku za hivi karibuni, maelfu ya wahamiaji wamevuka mpaka kutoka Morocco na kuingia Ceuta, na kusababisha serikali ya Uhispania kutuma jeshi kudhibiti hali hiyo.
2025 kulikuwa na mvutano kati ya nchi hizo mbili kuhusu madai ya Morocco kuwa ni eneo lake. Mvutano huo ulitulia baada ya serikali ya kisoshalisti ya Pedro Sánchez kutoegemea upande wowote kuhusu eneo la Sahara Magharibi.
Ceuta na Melilla
Melilla ni mali ya Uhispania tangu karne ya 15. Ceuta tangu karne ya 17.
Mwaka 1415, Ceuta ilikuwa mojawapo ya bandari kuu za kiuchumi na kimkakati za ulimwengu wa Kiislamu na kwa karne nyingi ilidhibitiwa na nasaba mbalimbali za Berber na Waarabu.
Lakini mwaka huo huo ilitekwa na Ureno, wakati wa upanuzi wa Wakristo ambao baadaye ulimaliza ufalme za Kiislamu uliokuwa umetawala Rasi ya Iberia kwa miaka 700.
Zaidi ya karne moja baadaye, 1580, Ureno na Uhispania ziliungana katika nasaba ya pamoja inayojulikana kama Umoja wa Iberia, na Ceuta ikawa sehemu ya milki ya Uhispania. Mara tu Muungano ulipovunjika 1640, Uhispania iliendelea kuidhibiti Ceuta.
Kwa upande wa Melilla ilinyakuliwa na Mwanamfalme wa Castile 1497. Kwa amri ya Wafalme Wakatoliki, Ferdinand II wa Aragon na Isabella I wa Castile, meli zilikwenda kwenye mji huu wa bandari kama sehemu ya utanuzi wa Uhispania, kwani miaka mitano nyuma, walikuwa wameushinda ufalme wa mwisho wa Kiislamu kwenye rasi ya Granada.
Kwa Waislamu wengi, Ceuta na Melilla ni ukumbusho mchungu wa kushindwa na kudhalilishwa mikononi mwa mamlaka ya Kikristo ya Ulaya.
Ceuta na Melilla kwa Uhispania
Uwepo wa Uhispani katika maeneo haya ya Afrika Kaskazini ulitokana na upanuzi wa Uhispania.
Kwa taifa hili kuwa na uwezo wa kufikia Bahari ya Mediterania kupitia Mlango-Bahari wa Gibraltar ni kipaumbele cha kimkakati.
"Ceuta na Melilla zilipata thamani kubwa kutokana na ukaribu wao na peninsula na uwezo wa kudhibiti njia ya maji kupitia Mlango-Bahari wa Gibraltar," anasema mwanahistoria Manuel Torres Soriano, kutoka Chuo Kikuu cha Pablo de Olavide cha Seville, Uhispania.
Ceuta, upande wa pili wa mlango bahari na umbali wa kilomita 14 tu kutoka pwani ya peninsula, ilitumika kama kitovu cha mtiririko wa biashara na watu kati ya pwani zote mbili.
"Melilla, kwa upande mwingine, ilishughulikia hitaji la bandari na kituo cha kuendeleza mapambano dhidi ya uharamia. Hili lilikuwa tatizo kubwa kwa usalama wa Uhispania," Torres aliongeza.
Tangu wakati huo, na baada ya karne tano za uwepo wake, Uhispania inaona miji hii miwili kama sehemu muhimu ya eneo lake.
"Sasa, kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, Ceuta na Melilla ni maeneo ya Hispania kama eneo lingine lolote kwenye rasi," anasema Torres.
Katika nusu ya kwanza ya karne ya 20, jiografia ya Ceuta na Melilla ilikuwa muhimu tena kwa shughuli za kijeshi za Uhispania.
Kati ya 1912 na 1956, Uhispania na Ufaransa zilikuwa na jukumu la kulinda eneo la Afrika Kaskazini ambalo lilijumuisha maeneo makubwa ya Morocco ya leo.
Uhispania ilipewa sehemu za kaskazini na kusini mwa nchi. Hata hivyo, Ceuta na Melilla zilitengwa kutoka eneo hili la ulinzi na kubaki na hadhi yao kama maeneo ya Uhispania.
"Miji yote miwili ikawa kitovu cha utawala wa kikoloni wa Uhispania wakati wa kuikoloni Morocco. Maeneo hayo yalikuwa ni viituo vya utawala na kijeshi ya kudhibiti eneo la Morocco," anaelezea Torres.
Utawala wa Kihispania huko Afrika Kaskazini haukuisha hadi 1956, wakati Morocco ilipopata uhuru wake. Na eneo la kusini lilikabidhiwa kwa Morocco mwaka 1958.
Lakini Ceuta na Melilla zilibaki kuwa maeneo ya Uhispania.
Madai ya Morocco
Tangu kupata uhuru, Morocco imekuwa ikidai mara kwa mara kukomeshwa kwa kile wanachokiona kama uvamizi wa Uhispani huko Ceuta na Melilla.
Madai yao ni sehemu ya dhana ya Morocco Kubwa, ambapo Wamoroko wanadai uhuru juu ya maeneo haya na mengine ya eneo la Afrika Kaskazini, ikiwa ni pamoja na Sahara Magharibi.
Lakini Morocco ilipowasilisha kesi ya Ceuta na Melilla kwa Umoja wa Mataifa kama maeneo yasiyojitawala yanayosubiri kuondolewa ukoloni, kesi yake ilitupiliwa mbali.
Samir Bennis, mchambuzi wa siasa wa Morocco, anasema, baada ya uhuru kutoka Hispania na Ufaransa, Morocco ilidhani kwamba suala la Ceuta na Melilla litatatuliwa kwa amani katika siku zijazo.
Hivi sasa, Uhispania inakataa kabisa kufanya mazungumzo yoyote kuhusu miji hii miwili na inasisitiza kwamba ni ya Uhispania kwa zaidi ya karne tano na ni sehemu muhimu ya Jimbo la Uhispania.
Sheria za kimataifa zinasemaje?
Wataalamu walizungumza na BBC Mundo wanasema kuna siasa nyingi zinazozunguka madai ya Morocco kwa Ceuta na Melilla, na si suala la kisheria tu.
Kwa kweli, miji hii miwili si maeneo pekee ambayo yamezikutanisha Uhispania na Morocco.
Karibu na pwani ya Morocco, Uhispania pia inadhibiti mwamba wa Vélez de la Gomera, mwamba wa Alhucemas, visiwa vya Chafarinas na kisiwa kidogo cha Perejil.
Tofauti na Ceuta na Melilla, hakuna raia katika maeneo haya. Vélez de la Gomera ina kambi ya kijeshi, lakini hakuna raia.
"Kwa Morocco, ingekuwa rahisi zaidi kudai maeneo yasiyokaliwa na watu kuliko Ceuta na Melilla," anasema Jamie Trinidad, mtaalamu wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza.
"Utetezi wa kisheria wa Uhispania ni kwamba maeneo haya yalikuwa Uhispania muda mrefu kabla ya Morocco kuwa nchi. Na, chini ya sheria, maeneo haya hayazingatiwi kuwa makoloni kwa sababu yameunganishwa kikamilifu kama sehemu huru ndani ya Katiba ya Uhispania," mtaalam huyo aliongeza.
"Kwa upande wa kisheria, ni wazi kabisa kwamba maeneo hayo ni ya Uhispania. Itakuwa vigumu sana kwa Morocco kubadilisha hadhi hiyo, ingawa naamini wataendelea na madai yao kama mkakati wa kisiasa," anasema Trinidad.
Msomi huyo anaamini Sahara Magharibi ni muhimu zaidi kwa Morocco kuliko Ceuta na Melilla, na ingawa wanaungwa mkono na mashirika kama vile Umoja wa Afrika, lakini madai yao yanatokana zaidi na suala la kihisia kwani ni "maeneo mawili ya mwisho ya Ulaya katika bara la Afrika".
Maisha yakoje Ceuta na Melilla?
Kama miji inayojiendesha yenyewe, Ceuta na Melilla zina mamlaka sawa na jamii zingine zinazojiendesha za Uhispania kama vile Catalonia, Basque, au Andalusia. Hata hivyo, mfumo wao ni mseto zaidi kati ya baraza la mtaa na mamlaka inayojitawala.
Licha ya wakaazi wake wengi kuwa na asili ya Morocco na ukuaji wa Uislamu, Torres anaelezea kwamba hadi sasa hakuna tatizo la la utambulisho.
Wahispania kutoka Ceuta na Melilla wenye asili ya Morocco wana fahari na utambulisho wao kuwa ni Wahispania kutokana na hali nzuri ya maisha na upatikanaji wa haki na uhuru, mambo ambayo hawayapati katika upande wa pili wa mpaka," Torres alisema.
"Kwa mtazamo wa wengi, madai ya Morocco ni kama tishio, na si kitu kinachoweza kuzingatiwa," anaongeza.
Hata hivyo, miji yote miwili wakati mwingine huhisi imeachwa na serikali ya Uhispania. Yote miwili inaorodheshwa miongoni mwa miji ya maisha ya chini kabisa nchini kwa upande wa utajiri wa kila mtu, kulingana na data kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu.
Na uchumi wa wakazi wao unategemea sana biashara ya kuvuka mpaka na magendo ambazo zimeenea pande zote mbili za mpaka kwa miongo kadhaa.
Tatizo la wahamiaji
Zaidi ya hayo, ndio sehemu pekee ya kuingilia EU kutoka Afrika, na kuifanya miji hii kuwa shabaha ya maelfu ya wahamiaji kila mwaka.
Hali ambayo baadhi wanaamini imetumiwa na Morocco kama silaha ya kisiasa.
Katika majira ya kuchipua ya mwaka 2021, wahamiaji wapatao 8,000 walivuka mpaka kwa siku moja. Wakati huo, kulikuwa na uvumi kwamba walinzi wa Morocco waliwaacha tu wapite.
Tukio hilo lilisababisha mgogoro mkubwa wa kidiplomasia kati ya Uhispania na Morocco, na kusababisha serikali ya Uhispania kutuma vikosi vya ziada kwenye mipaka yake.
Karibu mwaka mmoja baadaye, wahamiaji 23 walifariki na wengine walijeruhiwa wakati umati mkubwa ulipojaribu kuvuka kuingia Melilla, ingawa mashirika ya haki za binadamu yaliongeza idadi ya vifo hadi 37.
Tukio hilo lilitokea wakati kikosi kikubwa cha wanajeshi wa Morocco kilipojaribu kuwazuia wahamiaji hao kwa kutumia fimbo, gesi ya vitoa machozi, na risasi za mpira.
Machi 2020, Morocco ilifunga mipaka yake na miji hii miwili kutokana na janga la virusi vya korona na haikufunguliwa tena hadi miaka miwili baadaye. Wakati wa vikwazo hivyo, uchumi wa majirani zao uliathirika zaidi, na kufichua utegemezi wao kwa nchi hiyo ya Afrika.
Kituo cha Uchunguzi cha Ceuta na Melilla kimekuwa kikihimiza serikali ya Uhispania kuchukua hatua madhubuti za kubadilisha mfumo wa kiuchumi wa miji hii, kupunguza utegemezi kwa Morocco, na kuzuia migogoro ya siku zijazo.