Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, watu wenye mapaja manene wanaweza kuishi muda mrefu zaidi?
"Lo! Sijui yangeonekana vizuri zaidi kama yasingekuwa na mafuta mengi hivi?" Hayo ndiyo mawazo yaliyokuwa yakimjia Tasha Thompson, mkimbiaji kutoka Uingereza, kila alipotazama mapaja yake.
Katika baadhi ya tamaduni, kuwa na miguu myembamba kwa muda mrefu kumekuwa kukithaminiwa kama sehemu ya viwango vya urembo.
"Ikiwa huwezi kufikia kiwango hicho cha uwembamba wa mapaja, unaweza kujihisi kama umefeli hivi," Thompson aliiambia BBC World Service.
Hata hivyo, tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, kuwa na mapaja makubwa, ambayo mara nyingi hukosolewa, kunaweza kusaidia kuongeza muda wa maisha.
Utafiti mkubwa uliohusisha watu 25,000 ulibaini kuwa kwa kila ongezeko la sentimita 5 katika mzunguko wa paja, hatari ya kufariki kutokana na sababu yoyote ilipungua kwa 18%.
Lakini je, hii inamaanisha kwamba tunapaswa kujaribu kuongeza ukubwa wa mapaja yetu?
Kuna faida gani za kuwa na mapaja yenye mafuta mengi?
Wataalamu wanaamini kuwa sababu iliyowafanya washiriki katika uchanganuzi wa tafiti mbalimbali wa mwaka 2020 kuishi muda mrefu zaidi huenda ni kwa sababu walikuwa na misuli mikubwa zaidi ya miguu, ambayo ilichangia ukubwa wa mapaja yao.
"Kuna ushahidi mkubwa sana kwamba misuli, ambayo ni mojawapo ya aina tatu za tishu mwilini, inahusishwa kwa kiwango kikubwa sana na afya na maisha marefu," anasema Claire Steves, Profesa wa Uzee na Afya katika King's College London nchini Uingereza.
Kuwa na misuli mingi zaidi husaidia kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu, jambo linalopunguza hatari ya kisukari, magonjwa ya moyo na magonjwa mengine sugu.
Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2009 uliochapishwa katika British Medical Journal, kuwa na mapaja madogo au membamba kunahusishwa na ongezeko la hatari ya kupata magonjwa ya moyo na kufariki kwa wanaume na wanawake.
Vilevile, kuwa na mapaja yenye nguvu huwasaidia watu wazee kuepuka udhaifu wa mwili na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kujitegemea bila kutegemea wengine.
"Misuli iliyo sehemu ya mbele ya paja huwa muhimu sana kwa shughuli za mwili tunapozeeka. Baada ya yote, ndiyo misuli inayotusaidia kuinuka kutoka kwenye kiti na kutembea," anaeleza Steves, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya wazee katika Guy's and St Thomas' Hospital mjini London.
Imebainika pia kwamba nguvu inayozalishwa na miguu inaweza kusaidia kudumisha afya ya ubongo tunapozeeka.
Utafiti uliofanywa kwa kupima nguvu za miguu za zaidi ya mapacha 300 wa kike ulibaini kuwa pacha aliyekuwa na nguvu zaidi za miguu mwanzoni mwa utafiti alikuwa na uwezo bora zaidi wa kufikiri na kukumbuka, pamoja na muundo imara zaidi wa ubongo, miaka 10 baadaye.
Sababu ni nini?
Misuli inayofanya kazi huzalisha kemikali maalum. Wanasayansi wanaamini kuwa kemikali hizo hupunguza uvimbe kwenye ubongo na kulinda mtandao wa neva, hivyo kusaidia kulinda ubongo tunapozeeka.
"Wakati huohuo, shughuli za mwili pia zina athari kubwa sana kwenye mfumo wetu wa kinga," anaongeza Profesa Steves, ambaye alifanya utafiti huo.
Utafiti mwingine uliofanywa na King's College London uliwachunguza watu wazee wenye shughuli za mwili ambao walikuwa wakiendesha baiskeli mara kwa mara na kubaini kuwa walikuwa na mifumo ya kinga iliyokuwa na sifa zinazofanana na ya watu wenye umri wa miaka 20.
Ninawezaje kufanya mapaja yangu yawe na nguvu zaidi?
Mkufunzi wa mazoezi Elizabeth Davis anasema kwamba ili kuishi muda mrefu, watu hawapaswi kujaribu kubadilisha umbo la mapaja yao, bali kuongeza misuli yao.
Mwandishi wa kitabu Training for Your Old Lady Body anaongeza:
"Ikiwa kwa miaka mingi umekuwa ukitamani mapaja yako yawe madogo, makubwa au yenye umbo tofauti, sasa ni wakati wa kuachana na mawazo hayo. Badala yake, zingatia ni kiasi gani mapaja yako yanaweza kufanya na kustahimili shughuli mbalimbali."
Anaeleza kuwa mapaja yanaweza kuwa na nguvu sawa bila kujali kama ni madogo au makubwa.
Sayansi pia imethibitisha kwamba nguvu ni muhimu zaidi kuliko ukubwa. Utafiti wa mwaka 2006 uliohusisha watu wenye umri wa miaka 70 na zaidi ulibaini kuwa, kuwa na misuli dhaifu ya miguu kulihusishwa zaidi na ongezeko la hatari ya kufariki kuliko kuwa na mapaja madogo.
Kwa mujibu wa Davis, ikiwa unataka kujenga nguvu katika mapaja yako, njia bora ni kufanya mazoezi ya kunyanyua vitu vizito. Kuinua vitu vizito huongeza msongamano wa mifupa, jambo ambalo pia husaidia kuzuia osteoporosis, ugonjwa unaodhoofisha mifupa na kuifanya iwe rahisi kuvunjika.
Davis anashauri kufanya mazoezi ya miguu mara mbili au tatu kwa wiki ni mwanzo mzuri.
"Jambo muhimu ni kuanza katika kiwango unachoweza kumudu na kuongeza hatua kwa hatua kadri muda unavyokwenda," anasema.
Kuinua uzito huenda isiwe aina yako ya mazoezi unayoipenda zaidi, lakini anawahimiza wateja wake kuiona kama sehemu muhimu ya ratiba yao ya kila siku ambayo haiwezi kuepukika.
"Sipendi sana kupiga mswaki. Lakini nafanya hivyo kwa sababu najua ni muhimu kwa afya ya kinywa," anasema.
Davis pia anawahimiza watu kufurahia faida ndogo na za vitendo wanazopata kutokana na mazoezi ya kujenga nguvu katika maisha yao ya kila siku.
"Mara nyingi nasikia watu wakisema mambo kama: 'Nilimbeba mjukuu wangu kwa takriban mita 100, na sikuchoka kabisa'... 'Nilivuta mfuko wa mboji hadi kwenye gari na kuuweka kwenye buti bila shida yoyote.'"
Je, mafuta kwenye mapaja yana faida zozote kiafya?
Kwa mujibu wa Profesa Steves, mafuta yaliyoko kwenye mapaja si hatari kama mafuta yanayohifadhiwa katika sehemu nyingine za mwili. Mafuta yanayozunguka tumbo, hasa, yanaweza kuwa tatizo kubwa.
Mafuta haya ya tumboni, yanayojulikana kama mafuta ya ndani ya tumbo (visceral fat) na ambayo hujikusanya kuzunguka viungo vya ndani, huongeza hatari ya kupata magonjwa kama kisukari cha aina ya 2, ugonjwa wa moyo na ini kushindwa kufanya kazi, pamoja na MASH, hali hatari ya ugonjwa wa ini yenye mafuta ambayo huongeza hatari ya saratani.
Lakini tafiti zimebaini kuwa mafuta kwenye mapaja na makalio yanaweza hata kuilinda miili yetu, kwa sababu seli za mafuta katika maeneo hayo zina uwezo wa kuzuia asidi za mafuta huru ambazo zinaweza kuwa na madhara mwilini.
Hii inamaanisha kuwa kuwa na mafuta sehemu ya chini ya mwili, hususan kwenye eneo la mapaja, kunaweza kusaidia kupunguza kiwango cha LDL, kinachojulikana kama kolesteroli "mbaya", kuongeza HDL, inayojulikana kama kolesteroli "nzuri", na kupunguza viwango vya sukari kwenye damu.
Mafuta haya pia yanaweza kutumika kama akiba ya nishati wakati wa ugonjwa, jambo ambalo linaweza kuwa muhimu hasa kwa watu wazee.
Aina nyingine kuu ya tishu inayopatikana kwenye mapaja ni mifupa. Tunapozeeka, misuli na nguvu zake zinaweza kupungua kutokana na hali inayoitwa sarcopenia.
Hali hii inaweza kuharakisha ukuaji wa osteoporosis, ugonjwa unaopunguza msongamano wa mifupa na kuifanya iwe dhaifu na rahisi kuvunjika.
Kwa hiyo, kujenga mfumo imara wa mifupa kupitia mazoezi kama vile kuinua uzito ni muhimu sana tunapozeeka, anasema Steves.
Jivunie nguvu zako
Kwa Tasha Thompson, mwanzilishi wa kikundi cha michezo cha Black Girls Do Run, kuzingatia kile ambacho mapaja yake yanaweza kufanya kumemsaidia kubadilisha mtazamo wake kuyahusu.
Kuwa na binti pia kumemfanya abadilishe maneno anayoyatumia kuyaelezea mapaja yake.
"Siyaiti tena mapaja yangu kuwa yana mafuta au ni makubwa. Sasa nayaita mapaja yenye nguvu," anasema Thompson, ambaye amekamilisha mashindano ya mbio za masafa marefu ya ultramarathon pamoja na triathlon.
"Sote tuna maumbo na ukubwa tofauti... Kinachojali zaidi si jinsi miili yetu inavyoonekana, bali kile ambacho miili yetu inaweza kufanya," anaongeza.
Imetafsiriwa na Faidha Ngaga