Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump atishia kutangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump, amesema hivi karibuni atatangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa sehemu ya eneo la Marekani, akidai kuwa Iran imeathirika vibaya na vita vilivyotokea eneo hilo.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. TAZAMA: Majengo yaporomoka Indonesia baada ya tetemeko lenye ukubwa wa 7.7

    Takriban watu 20 wamefariki dunia nchini Indonesia baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 kukumba kisiwa cha Flores mapema Jumamosi.

    Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la Indonesia, BNPB, limesema idadi hiyo ni ya awali huku shughuli za uokoaji na utafutaji wa manusura zikiendelea.

    Tetemeko hilo lilisababisha kuporomoka kwa majengo na miundombinu kadhaa, huku mitetemeko mingine ikifuatia, ikiwemo mmoja wenye ukubwa wa 6.1.

    Video kutoka bandarini Maumere ilionyesha vipande vikubwa vya vifusi vikianguka kutoka kwenye jengo la kituo cha abiria na kuwapiga watu waliokuwa wakisubiri kupanda kivuko.

    Baadhi ya watu walitupwa baharini baada ya daraja la kuingilia kwenye kivuko kuporomoka.

    Arnold Welianto, mkazi wa Talibura, kijiji kilicho karibu na pwani huko Sikka, East Nusa Tenggara, alisema alishtuliwa usingizini na "tetemo kali sana", akiongeza: "Nilishtuka na kuamka, kisha nikakimbilia chumbani kwa mtoto wangu mara moja."

    Gavana wa East Nusa Tenggara, Emanuel Melkiades Laka Lena, amesema baadhi ya waathiriwa walifariki baada ya kuangukiwa na vifusi vya majengo yaliyoporomoka.

    Tetemeko hilo lilitokea katika kina cha takriban kilomita 15, kulingana na shirika la hali ya hewa na jiolojia la Indonesia.

    Onyo la tsunami lilitolewa baada ya tetemeko hilo, na kusababisha wakazi kukimbilia maeneo ya juu na ya ndani. Hata hivyo, onyo hilo liliondolewa takriban saa tatu baadaye baada ya kutogundulika ongezeko kubwa la kina cha maji baharini.

    Mamlaka zimesema takriban watu 2,000 walihama au kuondoka katika maeneo yao kwa hiari kufuatia tetemeko hilo.

    Mbali na vifo, watu kadhaa wamejeruhiwa, huku wawili wakiwa katika hali mbaya na wengine 11 wakipata majeraha madogo.

    Soma Zaidi:

  2. BBC yaomba mahakama kuwashurutisha wanafamilia wa Trump kutoa ushahidi katika kesi ya Panorama

    BBC imeiomba mahakama idhini ya kupata - amri rasmi ya mahakama yaani subpoena - inayowataka wanafamilia wa Donald Trump kutoa nyaraka na ushahidi, huku ikijitetea dhidi ya kesi ya madai ya kashfa ya dola bilioni 10 (pauni bilioni 7.4) iliyofunguliwa na rais huyo wa Marekani dhidi ya shirika hilo la utangazaji.

    Nyaraka za mahakama zinaonyesha kuwa wawakilishi wa timu ya kisheria inayoiwakilisha BBC katika kesi hiyo walijaribu mwezi Mei kuwasilisha amri hizo kwa mwana wa rais, Donald Trump Jr, binti yake Ivanka Trump, na mkwe wake Jared Kushner.

    Rais huyo ameifungulia BBC kesi hiyo kutokana na kipindi cha *Panorama* ambacho kilichanganya sehemu mbili tofauti za hotuba aliyoitoa kabla ya ghasia za Capitol mwaka 2021.

    Katika hati ya hivi karibuni iliyowasilishwa mahakamani, mawakili wa BBC wanahoji kuwa wanafamilia wa Trump walikuwa na "ufahamu wa kibinafsi" kuhusu nia yake ya kutoa hotuba hiyo, jambo linalofanya ushahidi na nyaraka zao kuwa muhimu katika kesi ya madai ya kashfa iliyofunguliwa na rais huyo.

    Ikirejelea ushahidi uliokusanywa awali na kamati ya Bunge la Marekani, hati hiyo inaeleza kuwa Donald Trump Jr na Ivanka Trump walikuwepo wakati baba yao akirekebisha na kutoa hotuba hiyo, na kuongeza kuwa Jared Kushner alimwandalia rasimu ya taarifa ambayo ingelaani matumizi ya vurugu.

    Hati hiyo inaomba mahakama kuruhusu hati za amri ya wito wa kutoa ushahidi (subpoenas) zitumwe kwa barua pepe na barua iliyosajiliwa (certified mail), ikibainisha kuwa majaribio ya kuzifikisha hati hizo kwa mkono hayakufanikiwa.

    Katika tukio moja, kulingana na hati hiyo, mwakilishi wa timu ya mawakili wa BBC alijaribu kufikisha hati ya wito kwa ajili ya Ivanka Trump na Jared Kushner nyumbani kwao Florida, lakini alizuiwa kuingia katika kituo cha ukaguzi cha polisi na baadaye akaambiwa na kitengo malaum cha ulinzi wa rais cha Marekani (Secret Service) kuwa hawaezi kupokea hati hizo.

    Vilevile, kulingana na hati hiyo, mwakilishi alijaribu kufikisha hati ya wito kwa Donald Trump Jr katika jengo la Trump Tower jijini New York lakini akaambiwa na mfanyakazi wa mapokezi kuwa mtu ambaye kwa kawaida hupokea nyaraka kama hizo huenda alikuwa mapumzikoni kwa ajili ya chakula cha mchana.

    Katika jaribio jingine siku mbili baadaye, mwakilishi huyo aliambiwa kuwa "idara ya sheria" haikuwepo siku hiyo, kulingana na hati hiyo.

    BBC tayari iliomba radhi kwa kuhariri hotuba hiyo, lakini imekanusha kwamba uhariri huo unahalalisha madai ya kashfa yaliyowasilishwa na Trump. Mawakili wa Trump wameombwa kutoa maoni kuhusu hatua hiyo ya BBC.

    Soma Zaidi:

  3. Kiongozi wa upinzani Zambia Mundubile ajitangaza mshindi wa uchaguzi wa urais kabla matokeo rasmi

    Mgombea urais wa chama cha NRPUP nchini Zambia, Brian Mundubile, amewaonya Watanzania anaodai wamehusika katika siasa za Zambia, akiwataka kuondoka nchini humo.

    Mundubile amesema Zambia si Tanzania na kwamba mbinu za kisiasa zinazoweza kufanya kazi Tanzania haziwezi kutumika nchini Zambia.

    "Ndugu zangu Watanzania ambao mmekodiwa, tafadhali tokeni katika nchi yetu."

    Amesema chama tawala cha UPND hakiwezi kushinda uchaguzi huo na kukituhumu kutumia kile alichokiita "mbinu ya Tanzania" ili kupata ushindi.

    "UPND hawawezi kushinda uchaguzi huu, hakuna muujiza. Sasa wameamua kutumia mbinu ya Tanzania. Zambia si Tanzania. Hii ni Zambia. Wale wanaofikiri wanaweza kuingiza katika nchi hii mbinu inayofanya kazi Tanzania, hawawezi kufanikiwa kamwe."

    Kauli ya Mundubile imekuja wakati mchakato wa kuhesabu kura katika uchaguzi wa Zambia ukiendelea chini ya ulinzi mkali, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia kusimamisha kwa muda zoezi hilo kufuatia taarifa za mashambulizi dhidi ya maafisa wa uchaguzi na kuibwa kwa kura. Tume hiyo imesisitiza kuwa wagombea hawapaswi kujitangaza washindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa.

    Mundubile, ambaye ni mmoja wa wagombea wakuu wa upinzani, tayari amejitangaza mshindi wa uchaguzi huo, licha ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia kutokuwa imetangaza matokeo ya mwisho.

    Soma Zaidi:

  4. Jason Arday, Profesa wa zamani wa Cambridge aliyekabiliwa na tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma, apatikana amefariki dunia

    Jason Arday, profesa wa zamani wa Chuo Kikuu cha Cambridge aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma, amefariki dunia.

    Huduma za dharura zimesema mwanaume mmoja alipatikana akiwa hajitambui katika eneo la Battersea, kusini mwa London, Ijumaa alasiri.

    Arday alijiuzulu wiki iliyopita kutoka nafasi yake ya profesa wa sosholojia ya elimu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, kufuatia tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma pamoja na maswali kuhusu baadhi ya mafanikio yake. Arday alikuwa amekanusha tuhuma hizo.

    Familia yake imesema katika taarifa kwamba ilikuwa "katika mshtuko" baada ya kumpoteza baba, mwenza, kaka, mjomba na mwana wao waliyemuelezea kuwa wa kipekee.

    Familia hiyo iliongeza: "Kampeni ya taarifa za kupotosha ilikuwa imemlemea Jason, ambaye alikuwa mtu mpole na ambaye daima alitaka kuona mazuri kwa kila mtu."

    Mapema Ijumaa, maafisa wa polisi waliitwa katika anwani hiyo iliyoko Battersea na Huduma ya Ambulance ya London.

    Katika taarifa, Polisi wa Metropolitan walisema: "Kwa wakati huu, kifo chake kinachukuliwa kuwa kisichotarajiwa, lakini haiaminiki kuwa kilitokana na mazingira ya kutatanisha."

    Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cambridge, Profesa Deborah Prentice, amesema: "Tumehuzunishwa sana kusikia habari hizi za kusikitisha."

    Soma Zaidi:

  5. Burundi yapokonywa haki ya kuandaa mashindano ya magari ya kimataifa mwaka huu

    Shirikisho la Kimataifa la Michezo ya Magari, FIA, limeiondolea Burundi haki ya kuandaa mashindano ya magari ya Kimataifa iliyokuwa imepangwa kufanyika mjini Ngozi mwezi Agosti mwaka huu.

    Baadhi ya taarifa zilizopatikana na BBC Gahuza zinaeleza kuwa uamuzi huo umetokana na mapungufu ya kiutawala yaliyojitokeza katika taasisi ya Burundi iliyokuwa na jukumu la kuandaa mashindano hayo, pamoja na kasoro katika matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mashindano hayo.

    BBC Gahuzamiryango iliwasiliana na viongozi wa taasisi inayosimamia maandalizi ya Rally nchini Burundi ili kupata maelezo yao kuhusu suala hilo. Hata hivyo, hadi habari hii ilipochapishwa, hawakuwa wamejibu.

    Watu walio karibu na waandaaji pamoja na mashindano ya magari nchini Burundi wameithibitishia BBC kwamba FIA imeiondoa Burundi kwenye kalenda ya mashindano ya mwaka huu.

    Hata hivyo, vyanzo hivyo vimesema uamuzi huo umetokana na Burundi kutotekeleza wajibu wake wa kutoa mchango wa fedha unaohitajika kwa ajili ya kuandaa mashindano hayo.

    Mmoja wao alisema kila nchi inayoshiriki katika maandalizi ya mashindano hayo inapaswa kutoa kiasi fulani cha fedha kila mwaka.

    Amesema: "Iwapo nchi haijatoa fedha hizo, FIA huiondoa kwenye kalenda ya mashindano ili iweze kuelekeza fedha zake katika mashindano mengine."

    Kufutwa kwa mashindano hayo hakutaathiri washindani pekee, bali pia kunaweza kuwa pigo kwa wafanyabiashara mbalimbali, wakiwemo wamiliki wa nyumba za kulaza wageni.

    Wafanyabiashara hao wamekuwa wakinufaika na mashindano ya magari kwa kupokea idadi kubwa ya wageni kutoka maeneo mbalimbali ya Burundi pamoja na nchi nyingine.

    Kwa mfano, katika mashindano ya Kimataifa ya magari ya mwaka 2025, washiriki walitoka Burundi, Rwanda, Kenya, Tanzania, Uganda na Zambia.

  6. Arsenal wanalenga kuanza msimu kwa ushindi mkubwa

    Arsenal wataanza msimu mpya wakiwa na azma ya kuonyesha mapema kuwa wana uwezo wa kushindania mataji, baada ya msimu uliopita wenye matokeo mchanganyiko na changamoto kadhaa, huku shughuli zao kwenye soko la uhamisho zikianza kwa utulivu.

    Kikosi cha Mikel Arteta kilianza maandalizi ya msimu kwa ushindi mzuri dhidi ya MK Dons na Girona, kabla ya kupata vipigo kutoka kwa Real Betis na Borussia Dortmund. Arsenal walihitimisha maandalizi yao kwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Como ya Serie A nchini Italia.

    Nje ya uwanja, Arsenal wamekuwa na utulivu katika kipindi hiki cha kiangazi, huku usajili wa Bruno Guimaraes ukiwapa nguvu zaidi baada ya kuimarisha safu yao ya kiungo.

    Iwapo Arsenal wataifunga Manchester City, ambayo inaanza enzi mpya baada ya kuondoka kwa Pep Guardiola, ushindi huo utakuwa ujumbe kwamba bado ni moja ya timu zinazopaswa kuogopwa na wapinzani wao katika mbio za ubingwa.

    Arsenal wataingia msimu huu wakilenga kutetea taji lao, huku ushindi dhidi ya Manchester City ukiweza kuwa mwanzo muhimu wa safari hiyo.

    Soma Zaidi:

  7. Meli ya kivita ya Marekani yaelekea Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya USS Abraham Lincoln

    Meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani imeanza safari kuelekea Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya meli ya USS Abraham Lincoln, ambayo maelfu ya mabaharia wake wameripotiwa kukabiliwa na uhaba wa chakula na mazingira magumu ya maisha wakati wa operesheni yake ya miezi tisa.

    Kulingana na uchunguzi wa BBC, meli ya USS George Washington, iliyokuwa karibu na Malaysia siku ya Alhamisi, huenda ikafika katika eneo hilo ndani ya takriban siku tisa.

    Familia za baadhi ya mabaharia wa USS Abraham Lincoln zimeelezea wasiwasi kuhusu kudorora kwa afya ya akili ya jamaa zao kutokana na hali ngumu wanayokabiliana nayo, huku kukiwa na ripoti za baadhi ya mabaharia wakitaka kujirusha ndani ya bahari.

    Jeshi la Wanamaji la Marekani limekubali kuwepo kwa matatizo ya usambazaji wa mahitaji muhimu kwa wanajeshi hao, lakini limekanusha kuwa wanajeshi hao wanakabiliwa na changamoto za afya ya kiakili.

    USS Abraham Lincoln, ina takriban wanajeshi 5,000.

    Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, Rais wa Marekani Donald Trump alipuuzilia wasiwasi ambao umetolewa na familia za wanajeshi walioko katik meli hiyo ambao wanadai muda wa oparesheni ya meli hiyo imekuwa ndefu sana.

    Soma pia:

  8. Watu wanne wauawa katika shambulizi la makombora la Wahouthi nchini Yemen

    Serikali ya Yemen imewalaumu kundi la wapiganaji la Wahouthi kwa kurusha makombora sita ya kibalistiki katika bandari ya Mocha, kwenye Bahari ya Shamu, hapo jana na kuwaua watu wanne.

    Kulingana na maafisa wa serikali ya Yemen, shambulizi hilo lililenga miundombinu ya kiraia na maeneo ya bandari, huku boti kadhaa za uvuvi zikichomwa moto.

    Kwa upande mwingine, Wahouthi wamesema katika taarifa yao kuwa walilenga vituo vya kijeshi, silaha na ndege za vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia huko Mocha, kwa kuwarushia makombora.

    Tukio hili limetokea wakati mvutano unaendelea kutokota eneo hilo kati ya Wahouthi na Saudi Arabia, Pamoja na mvutano kati ya Marekani na Iran.

    Soma pia:

  9. 'Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa na utaendelea kuwa wa Iran' - Kazem

    Akijibu kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kutangaza Mlango wa Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani, Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, amesema kuwa “Mlango wa Bahari wa Hormuz ulikuwa wa Iran, ni wa Iran, na utaendelea kuwa wa Iran.”

    Kazem Gharibabadi alichapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X na kusisitiza kuwa “Mlango wa Bahari wa Hormuz hauwezi kutekwa kupitia ujumbe uliochapishwa kwenye X au meli ya kubeba ndege za kivita.”

    Waziri huyo aliongezea kuwa Iran “haiogopi vitisho wala maonyesho ya nguvu.”

    Gharibabadi pia alidai kwamba “Marekani hadi sasa imepata kushindwa katika mikakati yake ya vita.”

    Kulingana naye, “Iran pekee ndiyo yenye mamlaka ya kufunga au kufungua Mlango wa Bahari wa Hormuz.”

    Soma pia:

  10. Trump atishia kutangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba hivi karibuni atatangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa sehemu ya eneo la Marekani, akidai kuwa Iran imeathirika vibaya na vita vilivyotokea eneo hilo.

    “Baada ya kuishinda Iran, ambayo sasa imeathirika vibaya,hivi karibuni nitatangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani,” Trump alisema katika mkutano wa kisiasa mjini New York.

    Kauli ya Trump imekuja wakati mkwamo unashuhudiwa kati ya Washington na Tehran kuhusu mlango huo wa bahari.

    Mlango Bahari wa Hormuz ni njia muhimu ambayo hupitisha kiasi kikubwa cha mafuta na bidhaa tofauti duniani.

    Iran imeweka udhibiti katika sehemu kubwa ya mlango huo, na kuzuia meli nyingi za mizigo za kiraia kupita, huku Jeshi la Wanamaji la Marekani likiweka kizuizi katika bandari za Iran katika jaribio la kudhoofisha uchumi wa nchi hiyo.

    “Tumeweka kizuizi. Hakuna meli itakayopita isipokuwa sisi wenyewe tutake ipite,” Trump aliwaambia wafuasi wake.

    Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, amejibu kauli ya Trump mapema hii leo kupitia mtandao wa X na kusema,

    “Mlango huu wa bahari hautafunguliwa wala kufungwa isipokuwa kwa amri ya Iran, na msipo kubali ukweli kuwa mmeshindwa, mtaendelea kujidanganya, na Iran itaendelea kuweka kizuizi.”

    Gharibabadi alisisitiza kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kumilikiwa na Iran, “Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa wa Iran, ni wa Iran, na utaendelea kuwa wa Iran.”

    Soma pia:

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja