Masharti 6 ambayo Iran inatoa kwa Trump ili kufungua Mlango bahari wa Hormuz

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Iran na Oman zote zimesema mazungumzo kuhusu mpango mpya wa kudhibiti trafiki kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz yamekuwa 'chanya' na yako katika hatua ya juu - na kusababisha matumaini ya kuanza tena kwa safari za meli katika mlango huo.

Katika siku za hivi karibuni, mazungumzo yamezingatia njia mpya inayowezekana kupitia mlango-bahari, ambayo Iran na Oman zingeshiriki.

Lakini kadri matumaini yanavyoongezeka, Iran imeorodhesha hadharani mfululizo wa masharti ambayo inasema Marekani lazima iafikie kabla ya njia muhimu ya maji kufunguliwa tena.

Mengi yanapita zaidi ya sehemu za Mkataba wa Makubaliano wa Marekani na Iran (MoU) uliokubaliwa mnamo tarehe 17 Juni, huku mengine yakirudia madai hayo ya Iran .

Je, masharti haya ni yapi? Na je, Marekani inaweza kuyaafikia?

Katika taarifa iliyochapishwa na mtangazaji wa serikali IRIB, Katibu wa zamani wa Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Iran na mshauri wa sasa wa Kiongozi Mkuu, Mohammad Bagher Zolghadr, alionya kwamba Marekani lazima "isahihishe" tabia yake, na kukidhi orodha ya madai. Ilisema kwamba 'marekebisho ya tabia' yanamaanisha yafuatayo:

1. Kukoma kuitisha Iran kwa lugha yoyote au kutukana matakatifu ya taifa hili

Iran inasema Marekani lazima iache kutishia nchi na kutoa hakikisho kwamba vitisho hivyo havitarudi. Hili kwa kiasi kikubwa ni hitaji la kisiasa na usalama. Ingawa kusitisha mapigano kunachukua kizuizi kutoka pande zote mbili, kudai hadharani dhamana dhidi ya vitisho vya siku zijazo kunaonekana kuwa sharti pana la kimkakati badala ya lile lililo wazi katika masharti yaliyoripotiwa hapo awali ya makubaliano ya muda.

2. Kukomesha vita na uchokozi dhidi ya Iran na washirika wake nchini Lebanon, Palestina, Yemen, na Iraq milele

Iran inasisitiza kwamba hatua za kijeshi zitakoma sio tu dhidi ya Iran bali pia dhidi ya washirika wake na vikundi washirika nchini Lebanon, Palestina, Yemen na Iraq. MoU ya June ilizungumzia "Mipaka yote ikiwemo Lebanon" - hii inabainisha nchi zingine na inatafuta dhamana pana za usalama wa kikanda.

3. Kuondoa kizuizi cha majini na kuondoa vikosi vyake (majini na angani) kutoka kote Iran

Chini ya MoU ya Juni kati ya Marekani na Iran, Marekani ilikusudiwa kumaliza kizuizi chake ndani ya siku 30, lakini hii haikuhusiana moja kwa moja na kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari.

4. Lipa fidia kamili kwa uharibifu uliosababishwa na Iran katika vita viwili vya uchokozi

Hii inarejelea vita vya siku 12 mwaka 2025 pamoja na vita vya hivi karibuni. Mifumo ya fidia ilitarajiwa kujadiliwa kama sehemu ya makubaliano ya mwisho baada ya MoU ya Juni. Hata hivyo, sasa Tehran inaunganisha fidia hadharani moja kwa moja na kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.

5. Ondoa vikwazo 'vikali na haramu' dhidi ya taifa la Iran

Ratiba ya kupunguzwa kwa vikwazo tayari ilitarajiwa kuwa sehemu ya mazungumzo kuelekea suluhu ya mwisho. Kwa hivyo Iran haileti suala jipya kabisa hapa. Kilicho kipya, tena, ni msisitizo kwamba kupunguzwa kwa vikwazo kunahusishwa waziwazi na kufunguliwa tena kwa mlango-bahari.

6. Kuachilia mali zilizoganda na zilizoibiwa za watu wa Iran bila masharti

Tena, ombi hili si jipya. Kutolewa kwa mali za ng'ambo ambazo zimezuiwa au kuganda kumejadiliwa hapo awali.

Masharti hayo sita yanapanua masharti ambayo Iran sasa inasema lazima yatimizwe kabla ya mlangobahari huo kufunguliwa tena.

Mchambuzi wa BBC Mashariki ya Kati Sebastian Usher anasema hii inaashiria ugumu wa msimamo wa Iran: "Haya ni masharti ambayo yamekuwepo kama sehemu ya makubaliano ya mfumo wa Mkataba wa Maelewano... lakini muda na utaratibu wake unaonekana kuwa tofauti sana." Anasema Tehran inaweza kuhisi kwamba ina mkono wenye nguvu zaidi kwa sababu Mlangobahari wa Hormuz "bado umefungwa kimsingi".

Hata hivyo, akizungumza na kipindi cha Wikendi cha BBC World Service, Trita Parsi, makamu wa rais mtendaji wa Taasisi ya Quincy, shirika la ushauri wa sera za kigeni la Marekani, anasema anaamini Wairani wanajijua wenyewe kwamba misimamo hii imetiwa chumvi na kwamba kuna uwezekano wa kuiacha.

"Kilichotolewa katika ngazi ya umma sio lazima kiwe kinachoonekana kwenye meza ya mazungumzo," anasema.

Parsi pia anapendekeza kwamba hii inaweza kuwa mbinu ya mazungumzo: "Inaweza kuwa rahisi kwamba wanajaribu tu kuongeza muda wa mchakato huu." Anasema kuna imani miongoni mwa vipengele vingi vya utawala kwamba Iran ilikubali MoU haraka sana mwezi Juni.

Kisha, makubaliano hayo yalidumu siku chache tu kabla hayajavunjika, huku mashambulizi ya kulipiza kisasi yakianza tena siku chache tu baada ya kusainiwa.

Parsi anasema kwamba baadhi ya watu nchini Iran wanasema kwamba kama yangechelewesha mazungumzo hayo kwa muda mrefu zaidi - kusukuma zaidi bei ya mafuta na hivyo kusababisha maumivu zaidi ya kiuchumi duniani - Rais Trump huenda hangekuwa mwepesi kuagiza mashambulizi dhidi ya malengo ya Iran. Inavyoonekana hili si 'kosa' ambalo Iran iko tayari kufanya tena.

Licha ya haya, bado anatabiri kwamba makubaliano juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz yanaweza kuwa siku chache tu kabla.

Wale wanaosubiri kwenye meli au wanaoangalia bei ya mafuta watatumaini kwamba yuko sahihi.