Tetesi za Soka Ulaya Jumatano: Al Hilal inamfukuzia Kane Bayern Munich

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Wawakilishi wa nahodha wa England Harry Kane,33, wamefanya mazungumzo na klabu ya Al-Hilal ya Ligi ya Pro ya Saudi Arabia, huku mshambuliaji huyo wa Bayern Munich akiwa tayari kuhama hapo baadaye. (Talksport)

Wakati huo huo, mshambuliaji wa Aston Villa na England Ollie Watkins, mwenye umri wa miaka 29, amefikia masharti binafsi na Al-Hilal, japo klabu hiyo ya Saudia bado haijawasilisha ofa rasmi ya uhamisho kwa Villa. (Teamtalk)

Newcastle imeanzisha mazungumzo ya awali na Manchester City kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa Uhispania Nico Gonzalez, mwenye umri wa miaka 24. (The Athletic - usajili unahitaji)

Mpango wa Sunderland wa kumsajili beki wa Toulouse na timu ya taifa ya Ufaransa ya vijana chini ya umri wa miaka 21, Dayann Methalie (20), kwa ada ya pauni milioni 25.7 huenda ukagonga mwamba baada ya tetesi kuibuka kuhusu vipimo vyake vya afya. (Daily Mail)

Ofa ya Coventry ya pauni milioni 8.5 ya kumsajili kiungo wa England Ruben Loftus-Cheek, 30, imekataliwa na AC Milan. (Tuttosport - kwa Kiitaliano)

Real Sociedad wameonyesha nia ya kumsajili kiungo wa West Ham na Mexico Edson Alvarez, 28, huku mpango wa Ajax wa kumsajili ukififia. (Sky Sports)

Ofa ya pili ya Ipswich kwa ajili ya kiungo wa Bayer Leverkusen na Argentina Exequiel Palacios, 27, imekataliwa. (Florian Plettenberg)

Tottenham wanatafakari uwezekano wa kumsajili beki wa Paris St-Germain na Ukraine Illia Zabarnyi, 23, baada ya kumuuza Cristian Romero kwenda Atletico Madrid. (Teamtalk)

Kiungo wa Liverpool na England, Curtis Jones, mwenye umri wa miaka 25, bado ni mlengwa mkuu wa klabu ya Inter Milan, ambayo inaamini kuwa ofa yake ya euro milioni 35 itapokewa. (CaughtOffside)

Klabu ya Wolves imejiunga na kinyang'anyiro cha kumsajili winga wa Brighton, Amario Cozier-Duberry, aliye na umri wa miaka 21; mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England ya vijana chini ya umri wa miaka 20 bado anawindwa pia na Rangers pamoja na klabu yake ya zamani ya Bolton, aliyochezea kwa mkopo. (The Argus)

Klabu ya Malaga inamfukuzia winga Mwingereza Ryan Kent, mwenye umri wa miaka 29, ambaye hajapata klabu tangu alipoondoka Seattle Sounders mwezi Januari. (Fichajes - kwa Kihispania)

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi