AU yaonya mataifa ya kigeni dhidi ya kuchochea vita Sudan
Umoja wa Afrika, AU, umeonya kuwa kuingiliwa kwa mzozo wa Sudan na mataifa ya kigeni, pamoja na juhudi za kuunda serikali pinzani, kunahatarisha kurefusha vita na kuvuruga umoja wa nchi hiyo.
Onyo hilo limetolewa wakati wa ziara ya siku mbili ya ujumbe wa Baraza la Amani na Usalama la AU nchini Sudan, unaolenga kuhimiza usitishaji wa mapigano, kurahisisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kufufua mazungumzo ya amani.
Katika mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah al Burhan, mjini Khartoum, ujumbe huo umesisitiza kuwa mazungumzo na suluhisho la kisiasa linaloongozwa na Wasudan ndiyo njia pekee ya kufikia amani ya kudumu.
Sudan imekuwa katika vita tangu mwaka 2023. Jeshi linadhibiti sehemu kubwa ya Khartoum na maeneo ya kati ya nchi, huku Kikosi cha Msaada wa Haraka, RSF, kikidhibiti maeneo makubwa ya Darfur.
RSF na washirika wake pia wameunda muungano wa kisiasa unaolenga kuanzisha serikali pinzani.
AU inataka mpito wa kisiasa unaowashirikisha wadau wote na unaoongozwa na Wasudan, ambao hatimaye utawezesha kuundwa kwa serikali ya kikatiba kupitia uchaguzi.
Vile vile wanalenga kuzishinikiza Jeshi la Sudan, SAF, na Kikosi cha Msaada wa Haraka, RSF, kukubali usitishaji wa mapigano, kuhakikisha misaada inawafikia wanaohitaji na kulinda mchakato wa kisiasa utakaowawezesha Wasudan kuamua mustakabali wa nchi yao bila kutawaliwa na makundi hayo mawili yenye silaha.
Ingawa upatanishi unaoongozwa na Waafrika umefanikiwa katika migogoro mingine, mzozo wa Sudan unaendelea kuwa changamoto kubwa. Tofauti na mgogoro wa kisiasa uliotokea Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambapo upatanishi ulioungwa mkono na AU uliwezesha kufikiwa kwa makubaliano ya kugawana madaraka, mzozo wa Sudan unahusisha majeshi mawili yenye silaha nzito yanayodhibiti maeneo tofauti na ambayo bado yanaamini kuwa yanaweza kuimarisha nafasi zao kupitia matumizi ya nguvu.
Ujumbe huo umefika Sudan wakati vita vikiwa katika hatua muhimu. Jeshi la Sudan, SAF, limerejesha udhibiti wa sehemu kubwa ya mji mkuu Khartoum, huku RSF ikiendelea kushikilia maeneo mengi ya Darfur, magharibi mwa nchi.
Kordofan, eneo linalounganisha sehemu za kati, magharibi na kusini mwa Sudan, pia limekuwa kitovu kingine cha mapigano.