Kwa nini baadhi ya wanaume huongeza sehemu zao za siri?

    • Author, James Gallagher
    • Nafasi, Inside Health presenter, BBC Radio 4
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Jason hakutaka kuwa na uume unaofanana na "kopo la Coke" – hilo ni jina la utani kwa uume uliopanuliwa kwa kutumia kiasi kikubwa cha dawa ya kujaza (filler) kiasi cha kufanana na kopo fupi na nene la kinywaji.

"Baadhi ya watu hupitiliza kiasi," Jason aliniambia tulipokutana Manchester.

Utaratibu alioufanyiwa uliongeza unene wa uume wake kwa asilimia 16 – kiasi ambacho yeye na mwenzi wake wanakiridhia sana. Anasema jambo hilo limemfanya " kujiamini zaidi".

"Kila kitu kinafanya kazi kama kawaida," Jason anaeleza – isipokuwa tu kuna "ile sehemu ya ziada ya unene".

Haijulikani ni wanaume wangapi kama Jason wanaofanyiwa utaratibu wa kuongeza ukubwa wa uume kwa njia hiyo.

Na huwezi kutembea mtaani na kupata picha halisi ya hali hiyo kama unavyoweza kuona wazi umaarufu wa utaratibu wa kuongeza ukubwa wa midomo.

Hakuna udhibiti wa kutosha wala rekodi rasmi, kwani mtu yeyote anaweza kuanza kutoa huduma hiyo.

Utaratibu huo wa kuongeza ukubwa wa uume uliibua nadharia ya ajabu ya siri wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi iliyopita.

Kulikuwa na uvumi kwamba wanariadha wanaoruka kwa skis walikuwa wakitumia dawa hizo ili kuongeza ukubwa wa eneo la uso wa mavazi yao, jambo ambalo lingewawezesha kuruka umbali mrefu zaidi.

Hata hivyo, baadhi ya wanaume wamejikuta wakihitaji huduma ya dharura baada ya uume wao kugeuka rangi nyeusi na ngozi kuanza "kuchubuka na kudondoka" kufuatia utaratibu uliofanywa vibaya.

Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo cha Uingereza (British Association of Urological Surgeons) kimetoa tahadhari kwa wanaume wanaofanyiwa taratibu hizo.

Hivyobasi, ni kwa nini wanaume wanafanya hivyo na ni hatari gani zinazohusika?

Jason alizungumza nasi kwa uwazi, lakini bila kutaja jina lake, kuhusu uamuzi wake wa kutumia dawa za kujaza (fillers) ili kuongeza ukubwa wa uume wake.

Aliridhishwa na urefu wa uume wake lakini alitaka "uwiano zaidi" na unene wa ziada ili "kupata muonekano mzuri na wenye uwiano".

"Ukihisi kuna upungufu fulani," anasema Jason, "basi, kwa nini usifanye hivyo?"

Alitumia mwaka mzima kutathmini chaguzi mbalimbali na akaamua kutofanyiwa upasuaji. Alichagua aina ya dawa ya kujaza - *hyaluronic acid* - ambayo haidumu milele, hivyo alijua kuwa hata kama asingependa muonekano huo, dawa hiyo "ingeyeyuka yenyewe baada ya muda".

Jason anasema hakuhamasishwa na dhana ya kiume ya kutaka kuonekana "dume la nguvu" au kujivunia ukubwa - "Siamini katika dhana inayosema 'ukubwa wa uume wako ndio kipimo cha ukubwa wa utu wako kama mwanaume'".

Badala yake, anasema matarajio kuhusu urembo wa wanaume yamebadilika.

"Si wanawake pekee wanaopaswa kwenda na wakati; wanaume pia wanapaswa kufanya hivyo.

"Ni jamii yenyewe inayobadilika. Nadhani namna vyombo vya habari vinavyoonyesha mambo kuna athari kubwa katika maisha ya kila siku sasa," anasema. "Ni kana kwamba huwezi kwenda popote bila kuona mtu mwenye muonekano mkamilifu kama wa kwenye picha."

Ukitembelea tovuti za kliniki zinazotoa huduma za kuongeza ukubwa wa uume - ambazo huuliza maswali kama "je, unaona aibu kwa sababu ya ukubwa wa uume wako?" - utaona jinsi zinavyotumia fursa hii.

Kuna chaguzi mbalimbali za kuboresha uume. Kuna mbinu za upasuaji na zisizo za upasuaji, pamoja na vifaa au dawa tofauti zinazoweza kudungwa kwenye uume.

Njia inayotumika zaidi ni kudunga dawa yenye umbo la jeli inayojulikana kama *hyaluronic acid* - kiambato kikuu kinachotumika pia katika dawa za kujaza midomo ili kuifanya ionekane minene.

*Hyaluronic acid* ni molekuli ya sukari inayopatikana kiasili mwilini na inajulikana kama kitu kinachovutia na kuhifadhi unyevu kwa sababu ina uwezo wa kushikilia maji.

Dkt. Javed Hussain amekuwa akitoa vijaza uume kwa zaidi ya mwaka mmoja katika kliniki yake huko Prestwich, Greater Manchester.

Hussain alifunzwa kama daktari kabla ya kuhamia katika taratibu za urembo, lakini vijaza uume havihitaji mafunzo yoyote ya kimatibabu kisheria ili kufanya kazi.

Anasema mahitaji yanaongezeka. Amewatibu wanaume wa rika zote - baadhi wakiwa na umri wa miaka 20, huku mteja wake mkubwa zaidi akiwa na umri wa miaka 72.

Mchakato huanza na mashauriano kuhusu afya ya mgonjwa, sababu za kutaka kufanya utaratibu, matarajio kuhusu matokeo, na majadiliano kuhusu hatari.

Siku ya tukio lenyewe, uume hudungwa sindano ya asidi ya hyaluroniki mara tatu - juu na pande zote mbili. Kijaza cha asidi ya hyaluroniki hutolewa kupitia kanula inayoingia kutoka chini yashina la uume na kupanda juu hadi mwisho wa urefu wa uume.

Mjazo huo hupakwa kwa masaji ili kupata muonekano ulio sawa, jambo ambalo mgonjwa huendelea kulifanya akiwa nyumbani.

Kwa gharama ya hadi Pauni 3,500, Hussain anasema wanaume wanaweza kutarajia ongezeko la unene wa kati ya asilimia 10 na 20 kwa kipindi cha miezi sita hadi tisa ijayo.

Lakini kuna hatari. Hizi ni kuanzia zile ndogo kama vile maumivu, michubuko na kutokuwa sawa kwa dutu hiyo, hadi zile kubwa kama vile maambukizi.

Hatari hizi zipo katika taratibu zote zinazotumia dutu ya kujaza. Hata hivyo, kuna hatari pia ya kuharibu sehemu muhimu na mishipa ya damu kwenye uume ambayo ni muhimu kwa ajili ya kusimama kwa uume.

Alipoulizwa kwa nini anajiamini kutoa huduma ambazo zinawatia wasiwasi madaktari wa upasuaji, Hussain anasema "anaelewa kabisa" sababu ya baadhi yao kuwa na wasiwasi.

"Huo wasiwasi unatokana na nia njema," anasema, "lakini wakati huo huo, ushahidi unaendelea kuongezeka na tunapata matokeo mazuri," na kwamba "kuna faida" kwa wanaume.

Hussain anasema ana "mpango wa hatua za haraka," ikiwa ni pamoja na dawa za kuyeyusha mjazo huo mara moja iwapo mambo yataenda vibaya, na anaripoti kuwa "kwa bahati nzuri, hatujawahi kuhitaji kufanya hivyo" - ingawa BBC haiwezi kuthibitisha hilo kwa kujitegemea.

Lakini anakumbuka mgonjwa mmoja aliyemwendea kwa ushauri baada ya kupata matibabu mahali pengine, ambayo yalikuwa "yameharibika vibaya sana."

Anasema aina isiyo sahihi ya mjazo ilikuwa imetumika na "shina la uume lilianza kuwa jeusi" kwa sababu utaratibu huo ulikuwa umeharibu mishipa ya damu kwenye uume na ngozi ilikuwa ikifa. Mwanaume huyo alipelekwa moja kwa moja kwenye kitengo cha dharura.

Profesa Vaibhav Modgil, daktari bingwa wa mfumo wa uzazi wa wanaume na upasuaji wa mfumo wa mkojo katika NHS jijini Manchester, amewahi kuona wanaume wakifika hospitalini baada ya taratibu hizo kufanywa vibaya.

"Hali hiyo inapotokea, inaweza kuwa na madhara makubwa sana kwa mgonjwa," anasema.

Anakumbuka kuona wanaume waliopatwa na tatizo la "kufa kwa tishu za ngozi (skin necrosis), ambapo sehemu ya ngozi hufa, hubadilika rangi na kuwa nyeusi sana na hatimaye kung'oka yenyewe."

"Kwa hiyo, wanaume huenda huko wakifikiri, 'Oh, matokeo yatakuwa mazuri sana', lakini wanaweza kutoka wakiwa na kutoridhika zaidi kuliko walivyokuwa kabla ya kwenda."

Alex, ambaye hakutaka jina lake halisi litajwe, alisafiri hadi Ujerumani kwa ajili ya utaratibu tofauti wa kuongeza ukubwa wa uume.

Alifanyiwa upasuaji wa kukata kano inayounganisha uume na mfupa wa kinena ili kuufanya uonekane mrefu zaidi. Pia, seli za mafuta kutoka mwilini mwake zilitolewa na kudungwa kwenye uume wake ili kuongeza unene wake.

Alipoamka baada ya utaratibu huo, alihisi maumivu makali kiasi cha kushindwa kusimama.

"Nilipata michubuko mingi na sehemu ya juu ya miguu yangu yote ilibadilika rangi na kuwa ya njano," anasema Alex. "Sikuweza kutembea vizuri kwa takriban mwezi mmoja."

Alex alipatiwa matibabu katika kliniki ya Modgil ambapo hatimaye alithibitishwa kupona. "Watu wengi hawapati bahati hiyo," anasema. "Mimi nilikuwa na bahati."

Alex anasema anajua kuwa uume wake "haukuwa mdogo hapo awali", lakini jamii na filamu za ngono (pornography) zilikuwa zimemshawishi kuwa uume mkubwa ndio "ishara ya uanaume na ndio bora zaidi".

Licha ya kutokuwepo kwa takwimu rasmi kuhusu idadi ya taratibu za kuongeza ukubwa wa uume, Modgil anasema kuwa mwelekeo wa utafutaji mtandaoni, matangazo na mitandao ya kijamii vyote "vinaashiria kuwa idadi hiyo inaongezeka".

Hali hii imesababisha Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo cha Uingereza (British Association of Urological Surgeons) kutoa mapendekezo mapya ya kupinga taratibu hizo.

"Mwongozo tulioutoa hivi karibuni kimsingi unasema hatuwezi kupendekeza kufanyika kwa taratibu hizi kwa sababu ushahidi uliopo ni hafifu sana," anasema Modgil.

Utafiti huo ulichunguza tafiti 36 zilizohusisha wanaume 3,750, lakini ulisema bado haijabainika wazi ni kwa kiwango gani taratibu hizo ni salama.

Hii inatokana kwa kiasi fulani na ukosefu wa taarifa kuhusu athari za muda mrefu za dawa zinazotumika kujaza (fillers) kwenye uume.

Lakini pia kuna wasiwasi kwamba - kama ilivyo kwa dawa za kujaza midomo - hakuna sifa maalum zinazohitajika ili kufanya utaratibu huo.

Modgil anasema kupiga marufuku kabisa "huenda ni hatua kali mno", lakini ikiwa taratibu hizi zitaendelea, basi sekta hiyo "inahitaji sana kudhibitiwa".

Alitoa wito wa kuwepo kwa daftari la kitaifa la kurekodi wakati taratibu za kuongeza ukubwa wa uume kwa njia ya dawa hizo zinapofanyika, na kukusanywa kwa taarifa za muda mrefu ili wanaume waweze kufanya uamuzi sahihi kwa kuzingatia hatari na faida zake.

Kule Manchester, Jason anaridhishwa na matokeo ya utaratibu aliofanyiwa na anatarajia kuurudia tena pale dawa hizo zitakapokwisha nguvu.

Kipindi cha *Inside Health* kiliandaliwa na Gerry Holt.