Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mzozo wa Iran: Umoja wa Falme za Kiarabu wasitisha biashara na Tehran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha madai ya Umoja wa Falme za Kiarabu kwamba Tehran imeifyatulia makombora ya balistiki.

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. FIFA imejiharibia yenyewe kwa mpango wa Kombe la Dunia - Mkuu wa Ligi Kuu ya Uingereza

    Mtendaji mkuu wa Ligi Kuu ya England, Richard Masters amekosoa mpango wa Rais wa shirikikisho la soka duniani Fifa, Gianni Infantino wa kuuza hisa za Kombe la Dunia, akisema shirikisho hilo "limebonyeza kitufe cha kujiangamiza.

    Infantino yuko chini ya shinikizo kubwa kuhusu jaribio lake, ambalo baadaye lilishindikana, la kuunda kampuni mpya ya kusimamia haki za kibiashara na tiketi za mashindano yote ya Fifa, ikiwa ni pamoja na Kombe la Dunia, huku asilimia 21 ikipangwa kuuzwa kwa kampuni bnafsi ya uwekezaji.

    Mpango wa Fifa Forward Enterprise (FFE) ulisitishwa baada ya ukosoaji mkubwa wa mashirikisho kadhaa, yanayoongozwa na Uefa, ambayo yametishia kususia mashindano yote ya Fifa.

    Masters aliunga mkono uamuzi wa Shirikisho la Soka la England (FA) kuondoa uungwaji mkono wake kwa Infantino, na akatoa wito wa kupatikana kwa mgombea mpya wa urais wa FIFA ambaye anaweza kuiunganisha dunia ya soka.

    Soma Zaidi Hapa:

  2. Meli ya mafuta ya UAE iliyozuiliwa katika Hormuz inaelekea Bandar Abbas

    Vyombo vya habari vya Iran vinaripoti kuwa meli ya mafuta ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) iliyozuiliwa katika Mlango- wa Bahari wa Hormuz imebadilisha mkondo kuelekea Bandar Abbas.

    Awali, meli hiyo ilikuwa imezuiliwa kaskazini mwa Mlango-bahari wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iran, meli hiyo ilikuwa inaelekea Bandar Jebel Ali, lakini sasa imebadilisha njia yake kuelekea Bandar Abbas.

    Hatua hiyo mpya inakuja wakati Umoja wa Falme za Kiarabu ikitangaza kusimamisha shughuli zote za kibiashara na kifedha na Iran hadi pale itakapotoa taarifa nyingine.

    Wakati wa kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu ililengwa na mashambulizi ya Iran zaidi kuliko nchi nyingine za eneo la Ghuba, lakini baada ya kusaini hati ya makubaliano, Iran haikuishambulia nchi hiyo.

    Soma zaidi:

  3. Waziri wa Ulinzi wa Ukraine aliyefukuzwa kazi aitisha uchaguzi wa urais

    Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Mykhailo Fedorov, ametoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi wakati wa vita, hatua ambayo wengi wanaiona kuwa changamoto kubwa zaidi kwa uongozi wa Rais Volodymyr Zelensky tangu vita dhidi ya Urusi vilipoanza mwezi Februari 2022.

    "Demokrasia haiwezi kushikiliwa mateka na Urusi," alisema Fedorov, aliye na umri wa miaka 35, katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa YouTube siku ya Jumanne, akiongeza kuwa Ukraine inapigana "hasa ​​kwa sababu tunataka kubaki kuwa taifa huru la Ulaya".

    Tangu Urusi Iilipoanza uvamizi wake, Ukraine imekuwa chini ya sheria za kijeshi, hali iliyosababisha uchaguzi kusimamishwa.

    Fedorov, ambaye hakumtaja Zelensky moja kwa moja katika video hiyo, aliondolewa ghafla katika wadhifa wake wa Waziri wa Ulinzi mwishoni mwa mwezi Julai, miezi sita tu baada ya kuteuliwa.

    Zelensky bado hajatoa tamko lolote kuhusiana na video hiyo ya Fedorov, ambaye kufutwa kwake kazi kulichochea maandamano makubwa.

    Fedorov alisifiwa kwa kuimarisha wizara hiyo, kuongoza juhudi za kupambana na ufisadi, na kutumia takwimu kuchambua na kujaribu kuboresha utendaji kaziwakati wa vita.

    Inasadikiwa kuwa kufutwa kwake kulitokana na mvutano kati yake na kamanda mkuu wa jeshi, Oleksandr Syrskyi.

    Katika video hiyo ya YouTube, Fedorov hakuelezea mipango yake ya kisiasa, badala yake alijikita katika umuhimu wa kuwepo kwa "utaratibu halali, salama na unaotekelezeka ambao utaiwezesha Ukraine kurejesha mchakato kamili wa kidemokrasia hata katikati ya vita vinavyoendelea kwa muda mrefu".

    Fedorov ndiye mwanasiasa wa kwanza kigogo kuitisha uchaguzi mkuu ambapo kulingana na sheria za Ukraine,ni marufuku kuandaa uchaguzi wakati wa vita.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Ufaransa yawafukuza wanadiplomasia wawili wa Iran

    Ufaransa imetangaza kuwa inajiandaa kuwafukuza wanadiplomasia wawili wa Iran kutoka nchini humo katika siku chache zijazo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrot alidokeza taarifa hizo Jumanne kwenye mtandao wa kijamii X.

    Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kutangaza kwamba wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Ufaransa waliohusika katika mzozo wa kidiplomasia huko Tehran mwezi Julai hawataruhusiwa kurudi Iran.

    Hapo jana Jumanne Wizara ya Ujasusi ya Iran iliishutumu serikali ya Ufaransa kwa "kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kujaribu kuleta ushawishi."

    Mnamo Julai 20, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alivituhumu vikosi vya usalama vya Iran kwa kukiuka kinga yao ya kidiplomasia kwa "kuwatisha vikali" wawili hao.

  5. Marekani yatangaza vikwazo vipya kwa viongozi wakuu wa ICC

    Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio ametangaza vikwazo dhidi ya Tomoko Akane, Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya kushughulikia kesi za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu ICC.

    Hatua hiyo ni ongezeko la hivi karibuni zaidi la msimamo mkali wa utawala wa Trump katika kampeni yake ya “kuivunja” mahakama hiyo, ambayo imepewa mamlaka na zaidi ya nchi wanachama 120 kuchunguza uhalifu wa kivita.

    Rubio alisema kuwa Marekani ilikuwa ikiweka vikwazo dhidi ya Rais wa ICC, Tomoko Akane wa Japan, na Mwanasheria Mkuu wa Mashtaka wa ICC, Abdoulaye Seye wa Senegal, kwa kushiriki katika juhudi za ICC za “kuwafungulia mashtaka maafisa ambao serikali zao hazijaridhia kuwa wanachama wa mahakama hiyo ya ICC.”

    ICC ilisema inaendelea kuwaunga mkono wafanyakazi wake na inaamini kwamba hatua kama zile zilizotangazwa na Rubio “zinadhoofisha utawala wa sheria.”

    Soma zaidi:

  6. Vita vya Ukraine: Raia 62 wa Ghana wauawa wakiipigania Urusi

    Waziri wa mambo ya nje wa Ghana Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema raia 62 wa nchi hiyo wameuawa wakiipigania Urusi katika vita vya Ukraine huku wengine 15 wakiwa hawajulikani waliko.

    Bwana Ablakwa ambaye yuko Moscow kwa mazungumzo na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov, amewaambia waandishi wa habari kuwa kusajiliwa kwa raia wa mataifa ya kiafrika kupigana katika vita kati ya Urusi na Ukraine kunapaswa kukoma.

    Kulingana na maafisa wa Ukraine, zaidi ya Waghana 272 wamesajiliwa na Urusi tangu mwaka 2022.

    Ukraine inasema takriban Waafrika 2,000 kutoka mataifa 36 ya Kiafrika wanapigana kwa niaba ya Urusi.

    Maafisa wa Urusi wanakanusha kuwa wanawasajili waafrika kinyume na sheria.

    Maelzo zaidi:

  7. Meta yashtakiwa kwa 'kuwateka kimawazo' watoto kwenye Facebook na Instagram

    Matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana na watoto unamulikwa darubini kali katika kesi ambayo imeanza kusikilizwa huko California Marekani.

    Mawakili wa majimbo29 ya Marekani wanaishutumu Kampuni ya Meta kwa kusababisha watoto kutumbukia katika uraibu wa kutumia visivyo mitandao yao ya Facebook na Instagram huku wakiupotosha umma kuhusu hatari zake.

    Meta inakanusha madai hayo, lakini imekiri kwamba baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanakabiliwa na changamoto.

    Majimbo hayo ya Marekani yanataka Meta kutozwa mabilioni ya dola. Mahakama pia inaweza kuamuru mabadiliko katika jinsi Facebook na mitandao mingine ya kijamii inavyofanya kazi.

    Mahakama imesikia hoja kutoka kwa mawakili wanaowakilisha majimbo hayo kwamba Meta ilikusudia kukiteka kimawazo kizazi cha sasa cha watoto kwenye Facebook na Instagram.

    Baraza la majaji huko Oakland, California litatumia wiki sita zijazo kuchunguza madai ya mawakili wakuu kutoka majimbo kadhaa ya Marekani, na mawakili wa kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii, ambao kila mmoja alipinga hoja za mwenzake wakati kesi hiyo ikifunguliwa hapo jana Jumanne.

    Wakili wa jimbo la California alidai Meta iligundua mamilioni ya watoto wenye umri wa miaka 11 na 12 walikuwa kwenye Instagram na haikuchua hatua za kutosha kuwazuia watoto hao. Hata hivyo, Wakili wa Meta alisema ni takriban watumiaji laki moja tu wa umri huo waliogunduliwa na pia alidai uraibu wa mitandao ya kijamii haupo.

    Baada ya wakili wa jimbo la California kusema Meta ilifahamu majukwaa yake yanadhuru afya ya akili ya vijana, upande wa Meta ulisema kampuni hiyo inapuuzwa kutokana na jinsi ilivyochangia vijana wengi zaidi kuwa na wakati mzuri na wanavyonufaika na mitandao hiyo.

    Kesi hiyo inatokana na kesi iliyofunguliwa mwaka 2023 na majimbo 29 ya Marekani, yanayodai ukiukwaji mkubwa wa sheria za Serikali kuu na za majimbo kuhusu kulinda faragha za watoto.

    Si tu kwamba majimbo hayo yanadai mabilioni ya dola kutoka kwa Meta, pia yanaitaka ifanye mabadiliko kwenye Instagram na Facebook, ikiwa ni pamoja na kukomesha idadi ya "likes" na mfumo wa kusogeza mbele maudhui bila kikomo.

    Soma pia:

  8. UAE yasitisha biashara na miamala yote ya kifedha na Iran

    Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imesema kuwa imesitisha shughuli zote za kibiashara na kifedha na Iran hadi itakapotangazwa tena.

    Kwa mujibu wa mashirika ya habari, Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE ilitangaza kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na kuongezeka kwa mivutano katika eneo hilo, mivutano inayodhoofisha amani na usalama.

    Saa chache zilizopita, Wizara ya Ulinzi ya UAE ilisema kuwa Iran ilirusha makombora mawili ya masafa marefu) kuelekea nchi hiyo; moja liliangukia nje ya maji ya eneo la mamlaka ya UAE na la pili liliangukia ndani ya maji ya nchi hiyo.

    Hata hivyo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha madai ya UAE kwamba Iran imerusha makombora kuelekea nchi hiyo.

    Ismail Beqai alieleza katika taarifa kwamba "madai ya Umoja wa Falme za Kiarabu hayana msingi."

    Tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, UAE imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya Iran zaidi kuliko nchi nyingine yoyote katika eneo la mashariki ya kati.

    Hata hivyo, Iran haikuishambulia UAE katika operesheni hiyo baada ya kusainiwa kwa mkataba wa maelewano.

    Soma zaidi:

  9. Natumai hujambo. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.