Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Miji 10 yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani mwaka wa 2026
Kadiri idadi ya watu duniani inavyozidi kuongezeka, miji inageuka kuwa vitovu vya maendeleo ya kiuchumi, kielimu, na kijamii.
Hali hii imesababisha baadhi ya miji kuwa na mamilioni ya watu, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuliko wakati wowote katika historia.
Ripoti mpya ya World Population Review ya mwaka 2026 imetangaza orodha ya miji yenye watu wengi zaidi duniani mwaka huo.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa miji ya Asia ndiyo inayoongoza katika orodha ya miji yenye msongamano mkubwa zaidi wa watu.
Hata hivyo, jambo lililotuvutia zaidi ni namna jiji la Kano, lililoko kaskazini mwa Nigeria, lilivyofanikiwa kuingia katika orodha ya miji 10 yenye watu wengi zaidi duniani.
Hii ni hali inayoakisi ongezeko la haraka la idadi ya watu na upanuzi wa jiji hilo katika miongo kadhaa iliyopita.
Hata katika sensa ya Nigeria ya mwaka 2006, Kano iliongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu nchini humo.
Katika makala hii, tunaangazia ripoti hiyo na kukuletea orodha ya miji 10 yenye watu wengi zaidi duniani kwa mwaka 2026.
Shanghai
Shanghai, nchini China, ndilo jiji lenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani, kulingana na World Population Review.
Ni jiji lililoko kando ya maji na lenye shughuli nyingi za kibiashara.
Kwa mujibu wa World Population Review, Shanghai ina idadi ya watu inayozidi milioni 24.7.
Ni jiji muhimu sana kwa China, likichangia takriban asilimia 30 ya uchumi wa nchi hiyo.
Delhi
Mji mkuu wa India ni mojawapo ya miji yenye watu wengi zaidi duniani, ukitarajiwa kushika nafasi ya pili katika orodha ya miji yenye watu wengi zaidi duniani ifikapo mwaka 2026, kulingana na *World Population Review*.
Mji huu una umuhimu mkubwa katika masuala ya kisiasa, kibiashara, na kiserikali, kwani ndio kitovu cha utawala nchini India.
Delhi ni mojawapo ya miji inayokua kwa kasi zaidi kutokana na uhamiaji wa watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi.
Ripoti inaonyesha kuwa Delhi ina idadi ya watu zaidi ya milioni 23.3, jambo linaloufanya kuwa mojawapo ya miji mikubwa yenye msongamano mkubwa wa watu duniani.
Mji huu unaendelea kuwa mojawapo ya vitovu muhimu zaidi vya kiuchumi na maendeleo nchini India, ukichukua nafasi muhimu katika maendeleo ya nchi hiyo.
Kinshasa
Mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Kongo) ni mojawapo ya miji yenye watu wengi zaidi na inayokua kwa kasi zaidi barani Afrika.
Kulingana na World Population Review, mji huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa miji yenye watu wengi zaidi duniani ifikapo mwaka wa 2026.
Kinshasa ndicho kitovu cha kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mji huo unajulikana kama mojawapo ya vituo vikubwa vya biashara katika eneo la Afrika ya Kati.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kinshasa ina idadi ya watu zaidi ya milioni 21.8, jambo linaloufanya kuwa mmoja wa miji yenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Mumbai
Mumbai, inayojulikana kama kitovu cha biashara na fedha nchini India, ni mojawapo ya miji yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani.
Jiji hilo, lililoko kando ya Bahari ya Uarabuni, ni makao makuu ya makampuni na taasisi kubwa za kifedha za India.
Mumbai inajulikana kwa tasnia ya filamu ya India, Bollywood, ambayo ni mojawapo ya tasnia kubwa zaidi duniani.
Ripoti ya World Population Review inaonyesha kuwa Mumbai ina idadi ya watu zaidi ya milioni 21.7, jambo linalofanya jiji hilo kuwa mojawapo ya miji yenye msongamano mkubwa zaidi wa watu duniani.
Beijing
Mji mkuu wa China ni mojawapo ya miji yenye watu wengi zaidi duniani na yenye ushawishi mkubwa kisiasa na kiuchumi.
Mji huu ndio kitovu cha serikali ya China, ambapo taasisi kuu za serikali na balozi za kimataifa zinapatikana.
Ripoti inaonyesha kuwa Beijing ina idadi ya watu zaidi ya milioni 21.5.
Licha ya changamoto za msongamano wa watu na uchafuzi wa mazingira, Beijing inaendelea kuwa mojawapo ya vitovu vikuu duniani vya uchumi, teknolojia, na elimu, ikichukua nafasi muhimu katika maendeleo ya China.
Karachi
Karachi, jiji kubwa zaidi nchini Pakistan, ni mojawapo ya majiji yenye watu wengi zaidi duniani na kitovu muhimu cha kiuchumi katika eneo la Kusini mwa Asia.
Jiji hilo, lililoko kando ya Bahari ya Uarabuni, ndilo kitovu cha biashara, viwanda, na fedha nchini Pakistan.
Bandari yake pia ni mojawapo ya bandari zenye shughuli nyingi zaidi nchini humo.
Ripoti inaonyesha kuwa Karachi ina idadi ya watu zaidi ya milioni 21.2.
Shenzhen
Shenzhen ni mojawapo ya miji mikubwa zaidi nchini China na ina uchumi unaokua kwa kasi zaidi.
Jiji hilo, lililoko kusini mwa China karibu na Hong Kong, hapo awali lilikuwa mji mdogo wa wavuvi kabla ya serikali ya China kulitangaza kuwa eneo la maendeleo ya kiuchumi katika miaka ya 1980.
Tangu wakati huo, Shenzhen imekuwa mojawapo ya vituo vikuu vya teknolojia na viwanda duniani.
Ripoti inaonyesha kuwa Shenzhen ina idadi ya watu zaidi ya milioni 20.6.
Jiji hilo pia ni makao makuu ya kampuni kubwa za teknolojia za China, zikiwemo Huawei na Tencent.
Guangzhou
Guangzhou, iliyoko katika jimbo la Guangdong kusini mwa nchi, imekuwa lango la biashara kati ya China na sehemu nyingine za dunia.
Pia inajulikana kwa Maonyesho ya Biashara ya Canton (Canton Fair), ambayo ni mojawapo ya maonyesho makubwa zaidi ya biashara duniani.
Ripoti inaonyesha kuwa Guangzhou ina idadi ya watu zaidi ya milioni 18.5.
Kano
Huu ndiyo mji mkubwa zaidi kaskazini mwa Nigeria na mojawapo ya miji yenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Kano, mojawapo ya miji ya kale zaidi Afrika Magharibi, imekuwa kitovu cha biashara, viwanda, na shughuli za kitamaduni kaskazini mwa Nigeria kwa muda mrefu.
Hali yake kama kitovu cha biashara kwa kaskazini mwa Nigeria na nchi jirani imechangia ukuaji wake wa kiuchumi kwa miaka mingi.
Ripoti inaonyesha kuwa Kano ina idadi ya watu zaidi ya milioni 17.
Idadi ya watu wa Kano na upanuzi wa mji huo vinaonyesha nafasi muhimu inayoshikilia katika uchumi na maendeleo ya nchi.
Chengdu
Chengdu ni jiji la tano kutoka China kuingia katika orodha ya majiji 10 yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani mwaka wa 2026.
Jiji hili linajulikana kwa kuchanganya utamaduni wa kale wa China na maendeleo ya kisasa, na pia ni makazi ya viumbe mbalimbali vya porini, jambo linalolifanya kuwa mojawapo ya maeneo yanayovutia zaidi watalii nchini humo.
Ripoti inaonyesha kuwa Chengdu ina idadi ya watu zaidi ya milioni 15.8.
Chengdu imekuwa mojawapo ya vituo vikuu vya teknolojia, utafiti, na uvumbuzi nchini China.
Jiji hili linaendelea kuvutia wawekezaji na makampuni ya ndani na nje, na hivyo kuimarisha zaidi nafasi yake katika uchumi wa nchi.