Yanga v Simba: Dabi ya Seleman Mwalimu leo?

Chanzo cha picha, TheCitizen
Yanga na Simba zinakutana leo Jumatano katika Uwanja wa New Amaan Complex kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, lakini kabla hata ya mpira kuanza, jina la Seleman Mwalimu limeuteka mchezo huo na kuufanya kuwa zaidi ya pambano la kutafuta taji la kwanza la msimu.
Mwalimu, ambaye hadi siku mbili kabla alikuwa mchezaji wa Simba, amehamia Yanga katika dakika za mwisho kuelekea mchezo huu. Uhamisho huo umeibua mjadala mkubwa, hasa kutokana na uwezekano wa mchezaji huyo kukutana na waajiri wake wa zamani akiwa amevaa jezi ya watani wao wakubwa.
Mjadala huo umefika hadi kwenye mkutano wa waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, ambapo TFF ilijaribu kuuweka pembeni wakati mwandishi alipouliza kuhusu usajili wa Mwalimu.
Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo, alijibu: "Nadhani tusizungumze hayo yanayohusiana na usajili, tupo hapa kwa ajili ya dabi ya Yanga vs Simba."
Lakini licha ya jaribio hilo, sakata la Mwalimu limeendelea kutawala mazungumzo kuelekea mchezo huo. Kwa upande wa mashabiki wa Simba, uamuzi wa mchezaji huyo kuhamia moja kwa moja kwa watani wao umeongeza machungu na kuufanya uhamisho huo kuwa sehemu ya vita ya kisaikolojia kabla ya mchezo.
Mwalimu na vita ya kisaikolojia
Kwa baadhi ya wachambuzi, Yanga tayari imepata faida kabla ya mpira kuanza kutokana na namna uhamisho wa Seleman Mwalimu ulivyobadilisha mazingira ya mchezo. Mchambuzi wa soka Frank Vegullah anaona upande wa Yanga ukiingia kwenye mchezo ukiwa na nguvu zaidi kisaikolojia.
"Kwa namna saikolojia zilivyokaa za mashabiki, wachezaji, viongozi, upepo uko kwa Yanga zaidi," anasema Vegullah.
Kwa mashabiki wa Simba, jambo linaloumiza zaidi si kumpoteza Mwalimu pekee, bali namna alivyoondoka na kwenda moja kwa moja kwa watani wao wakubwa. Kwao, kama angehamia klabu nyingine, huenda uhamisho huo usingekuwa na uzito mkubwa kama ulivyo sasa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Haji Manara, aliyewahi kuwa msemaji wa Simba na Yanga, anaona Yanga imepata faida ya kisaikolojia kupitia usajili huo na kuelekea mchezo huo, akieleza kuwa athari za uhamisho huo zimeenda zaidi ya suala la kuongeza mchezaji kwenye kikosi.
Manara anaongeza kuwa ingawa masuala ya kisaikolojia si rahisi kuwekwa mbele katika mchezo wenyewe, hali iliyotokana na uhamisho huo imeathiri mazingira ya Simba. "Ingawa mechi yenyewe saikolojia huwa haiwekwi sana, lakini hali katika kambi ya Simba imevurugika," anasema.
Kauli hizo zinaifanya mechi ya leo kuwa na vita mbili: moja ya kutafuta Ngao ya Jamii ndani ya uwanja, na nyingine ya kisaikolojia ambayo tayari imeanza kabla ya filimbi ya kwanza. Kwa Simba, changamoto ni kuzuia sakata la Mwalimu lisigeuke kuwa mzigo kwa wachezaji, wakati Yanga inaweza kutumia mazingira hayo kama kichocheo cha kujiamini.
Na kama Mwalimu ataruhusiwa kucheza dhidi ya timu yake ya zamani, presha hiyo inaweza kufikia kiwango kingine kabisa. Katika hali hiyo, kila mguso wake wa mpira, kila shangwe na kila tukio litakalomhusu linaweza kuwa sehemu ya simulizi kubwa kuliko Ngao ya Jamii yenyewe.
Dabi inayovuka mipaka ya Tanzania

Chanzo cha picha, MickyJr
Mchezo wa Yanga na Simba hauzungumzwi Tanzania pekee. Safari hii Ngao ya Jamii imevuta pia macho kutoka Afrika Kusini, hasa kutokana na uhusiano mkubwa uliopo kati ya soka la nchi hizo mbili.
Makocha wa timu zote mbili wanatoka Afrika Kusini; Steve Barker anaiongoza Simba, huku Manqoba Mngqithi akiwa kocha wa Yanga. Aidha, wachezaji kadhaa wenye historia ya kucheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini wamejiunga na vilabu hivyo, jambo linaloongeza shauku nchini humo.
Mwandishi wa habari za michezo kutoka Afrika Kusini, Mthokozisi Dube, amefika Zanzibar kufuatilia mchezo huo na anasema Kariakoo Derby tayari ina jina kubwa hata nchini kwao.
"Mechi hii ni kubwa hata Afrika Kusini," anasema Dube, akiwataja nyota kutoka nchini humo wanaocheza Simba Rushine de Reuck pamoja na nyota mpya, Neo Maema miongoni mwa majina yanayoongeza mvuto wa mchezo huo.
Dube anaeleza kuwa wachezaji kama Rushine wamejenga jina katika soka la kimataifa, baada ya kucheza katika ligi mbalimbali, ikiwemo Afrika Kusini, Israel na Ureno. Hivyo, kuhamia Tanzania kwao pia kunaifanya ligi ya Tanzania kuanza kufuatiliwa zaidi na mashabiki wa Afrika Kusini.
Ngao ya Jamii na historia ya Kariakoo Dabi
Lakini nyuma ya sakata la Mwalimu na mvuto wa kimataifa, bado kuna taji linalosubiriwa. Yanga na Simba zinakutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii baada ya kumaliza msimu uliopita zikiwa na mataji mawili tofauti.
Yanga waliibuka mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania, huku Simba wakitwaa Kombe la CRDB Federation Cup. Kwa sababu hiyo, mchezo huu unakuwa pia kipimo cha kwanza cha nguvu za timu hizo kuelekea msimu mpya wa 2026/27.
Katika Ngao ya Jamii ya mwaka uliopita, Yanga iliifunga Simba 1-0, bao likifungwa na Pacome Zouzoua. Hata hivyo, Pacome hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana na majeraha, hivyo Yanga italazimika kuanza msimu bila mchezaji aliyeamua pambano hilo mwaka jana.
Kwa upande mwingine, Simba inaingia kwenye mchezo ikiwa na sura mpya na kocha mpya, huku Yanga ikiwa nayo ikianza ukurasa mpya chini ya Manqoba Mngqithi. Hivyo, licha ya historia ndefu ya Kariakoo Derby, mchezo wa leo unaweza kutoa picha mpya kabisa ya ushindani wa msimu huu.
Na hatimaye, macho yatakuwa kwa Seleman Mwalimu. Je, atapata nafasi ya kukutana na timu yake ya zamani akiwa upande wa Yanga? Kama atacheza, swali halitakuwa tu kama ataifunga Simba, bali pia atajisikiaje kuvaa jezi ya Yanga dhidi ya klabu aliyokuwa akiichezea hadi siku chache zilizopita?
Ngao ya Jamii itatafutwa ndani ya dakika 90, lakini vita ya Mwalimu tayari imeanza kabla ya filimbi ya kwanza.














