Iran inaweza kuendelea na vita kwa muda gani?

M

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Miezi michache baada ya kuanza kwa vita, Iran imepoteza sehemu ya nguvu zake za kijeshi na miundombinu yake, na pia inakabiliwa na shinikizo kubwa zaidi la kiuchumi. Hata hivyo, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado wanaonekana kutokuwa na haraka ya kumaliza vita hivyo.

Iran inaendelea kurusha makombora na ndege zisizo na rubani, imeifanya Mlango wa Bahari wa Hormuz kuwa moja ya njia zake muhimu za kuweka shinikizo, na imekataa kukubali kusitishwa kwa mapigano hata katika vipindi ambavyo mashambulizi ya Marekani yalipungua.

Mfano wa hivi karibuni ni shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan baada ya siku chache za pande zote mbili kupunguza mashambulizi.

Tabia hii inaweza kuwa na sababu kadhaa. Huenda Tehran inataka kuonesha kuwa Marekani peke yake haiwezi kuamua muda na mwelekeo wa vita. Wakati huo huo, huenda bado ina matumaini kwamba vita vikidumu zaidi vitaongeza gharama za kijeshi, kiuchumi na kisiasa kwa Marekani, na hatimaye kuifanya Washington ikubali baadhi ya matakwa ya Iran.

Hata hivyo, nyuma ya hayo kuna swali muhimu zaidi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaweza kuendelea na vita hivi kwa muda gani?

Je, uwezo wa kijeshi wa Iran kuendelea na vita ni upi?

Miezi kadhaa baada ya kuanza kwa vita, bado hakuna taarifa kamili zinazoonesha uwezo wa kijeshi uliobaki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baadhi ya sehemu za viwanda vya ulinzi na vituo vya kutengeneza makombora vimeshambuliwa, lakini hakuna takwimu huru zinazoonesha kiasi cha silaha zilizobaki au kiwango cha uharibifu wa ghala la silaha la Iran.

Baadhi ya tathmini za kijasusi za Marekani, hasa katika miezi ya mwanzo ya vita, zilionesha kuwa sehemu kubwa ya uwezo huo wa kijeshi bado ilikuwa salama.

Shirika la habari la CNN liliripoti mwanzoni mwa mwezi Aprili, likinukuu vyanzo vilivyofahamu tathmini za kijasusi za Marekani, kwamba takribani nusu ya vifaa vya kurushia makombora vya Iran vilikuwa bado vinafanya kazi, na kwamba Tehran ilikuwa na maelfu ya ndege zisizo na rubani za kushambulia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tangu wakati huo, mashambulizi zaidi yamefanyika, hivyo takwimu hizo haziwezi kutumika kuelezea hali ya sasa. Taasisi ya utafiti ya Chatham House pia inasema katika tathmini yake ya hivi karibuni kwamba hakuna taarifa za kuaminika kuhusu kiasi cha makombora ambacho Iran bado inacho.

Njia ambayo Iran inatumia silaha zake pia imebadilika, na mawimbi ya mashambulizi yamekuwa madogo zaidi ikilinganishwa na hatua za mwanzo za vita.

Behnam Bentaleblou, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Foundation for Defense of Democracies, alisema katika mahojiano na BBC Persian kwamba azma na nia ya kuendelea na vita ni muhimu zaidi kuliko uwezo wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu katika mzozo huu.

Alisema, "Moja ya athari kubwa za vita vya siku 40 ni kwamba mashambulizi dhidi ya miundombinu ya viwanda vya ulinzi yamepunguza uwezo wa Iran wa kuzalisha silaha katika siku zijazo. Hata hivyo, sehemu kubwa ya ghala la silaha la Jamhuri ya Kiislamu bado ipo na limeondolewa kwenye maghala ya chini ya ardhi tangu kuanza kwa vita."

Athari za mashambulizi Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Taasisi hiyo imekuwa ikiunga mkono sera ya kuongeza shinikizo na hatua za kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Bw. Bentaleblou alisema: "Utawala wa Iran unajua kwamba unakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa silaha. Kwa sababu hiyo, ingawa unaendelea kurusha makombora mara kwa mara, idadi ya makombora katika kila wimbi la mashambulizi imepungua."

Hata hivyo, uwezo wa kuendelea na vita haupimwi kwa idadi ya makombora ya masafa marefu pekee. Ndege zisizo na rubani na makombora ya cruise ni rahisi na ya haraka zaidi kutengenezwa. Vilevile, makamanda waliouawa tayari wamebadilishwa, na mfumo wa uongozi wa kijeshi haujavurugika. Aidha, Iran bado ina uwezo wa kuvuruga shughuli katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Mohammad Ghaedi, mhadhiri wa mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha George Washington, anaona kuwa mambo matatu ndiyo yanayoamua uwezo wa Iran kuendelea na vita:

Kudumisha uongozi wa kisiasa na kijeshi.

Uwezo wa kutengeneza na kurusha makombora pamoja na droni.

Kudumisha uwezo wa kuvuruga shughuli katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Bw. Ghaedi anaamini kuwa hadi sasa Iran imeonesha uwezo wa kuwabadilisha makamanda wake.

Alisema: "Kwa hiyo, kuwaondoa viongozi na makamanda hakumaanishi moja kwa moja kwamba mfumo wa kufanya maamuzi utavurugika."

Aliongeza: "Idadi halisi ya makombora ya ballistiki yaliyobaki haijulikani, lakini droni na makombora ya cruise ni rahisi na ya haraka kutengenezwa. Huenda Iran ikaendelea kufanya mashambulizi kwa muda mrefu, ingawa kwa kiwango kidogo, na bado ikaendelea kuwa na uwezo wa kuvuruga shughuli katika Mlango wa Bahari wa Hormuz."

Wakati huohuo, mwenendo wa Tehran unaonesha kuwa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu hawaoni kuendelea kwa vita kama jambo linalowadhuru pekee.

Shambulio dhidi ya kambi ya anga ya Mawfaq al-Salti nchini Jordan, baada ya siku kadhaa za kupungua kwa operesheni za Marekani, lilionekana kuwa ishara ya mkakati huo. Hakuna maelezo rasmi yanayoeleza sababu za Tehran, lakini inawezekana kwamba Iran haitaki Marekani iamue peke yake lini vita visimame au vianze tena. Pia, kipindi kirefu cha utulivu kingeipa Marekani muda wa kujipanga upya, kuimarisha ulinzi wake na kujaza tena akiba ya silaha zilizotumika.

Hata hivyo, kuendelea kwa vita pia kuna gharama kwa Marekani. Kuzuia makombora na droni za Iran kumeongeza matumizi ya akiba ya silaha za ulinzi za Marekani, na baadhi ya tathmini za Marekani zimeonya kuhusu kasi ndogo ya kuzibadilisha silaha hizo. Kuongezeka kwa bei ya nishati pamoja na gharama za kuweka majeshi katika eneo hilo pia ni sehemu ya hesabu hiyo.

Mohammad Ghaedi alisema: "Inaonekana Tehran inahesabu kwamba kwa kuonesha uwezo wa kustahimili, inaweza kuongeza gharama za vita kwa Marekani. Wasiwasi kuhusu kupungua kwa baadhi ya akiba ya makombora ya Marekani, gharama kubwa za kuzuia mashambulizi, athari za vita kwa bei ya mafuta, na masuala ya kisiasa ya ndani nchini Marekani, vimeifanya Tehran kuwa na matumaini kwamba inaweza kuilazimisha Washington kukubali baadhi ya masharti yake."

Iwapo hesabu hiyo ni sahihi, lengo la Tehran si lazima kuishinda Marekani kijeshi. Badala yake, kuifanya vita idumu kwa muda mrefu na kuwa na gharama kubwa kunaweza kuwa sehemu ya mkakati wake wa kuongeza shinikizo.

Kwa sasa, hakuna ushahidi unaoonesha kuwa vikwazo vya kijeshi pekee ndivyo vilivyoilazimisha Iran kusitisha vita. Hata hivyo, uwezo wa kuendelea na vita hautegemei tu idadi ya silaha zilizobaki, bali pia mambo mengine ya kisiasa, kiuchumi na kimkakati.

Kutokubaliana mjini Tehran: Vita vinapaswa kuendelea kwa muda gani?

Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Hakuna makubaliano ndani ya mfumo wa kisiasa wa Iran kuhusu kuendelea kwa hali hii. Tofauti ya maoni si kuhusu kupambana na Marekani, bali ni kuhusu vita vya kijeshi vinapaswa kuendelea kwa muda gani na ni wakati gani vinapaswa kubadilishwa kuwa suluhisho la kisiasa.

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran na mkuu wa timu ya mazungumzo, aliwahi kuonya kwamba Jamhuri ya Kiislamu haipaswi kunaswa katika "mtego wa vita vya muda mrefu vinavyochosha." Baada ya kufikiwa kwa makubaliano, aliwakosoa kwa ukali zaidi wapinzani wa mazungumzo. Katika mahojiano ya televisheni aliwaambia "wenye msimamo mkali wanaopinga mazungumzo na Marekani," akisema:

"Hamuisaidii diplomasia wala vita. Acheni kuleta vurugu na msirudie maneno ya Trump. Si jambo jema. Waacheni wananchi waishi kwa amani na wajivunie Iran. Msiharibu haki za taifa kwa sababu ya tofauti zenu za kisiasa na mimi, Qalibaf."

Kwa upande mwingine, wafuasi wa Saeed Jalili na chama cha Stability Front wana mtazamo wa kukata tamaa zaidi kuhusu uwezekano wa kumaliza mzozo kupitia mazungumzo.

Amir Hossein Sabeti, mbunge mwenye msimamo mkali kutoka Tehran, alisema tarehe 2 Juni kwamba vita vingine "ni jambo la hakika," na kwamba hata kama Marekani ingekubali masharti yote ya Iran na kusaini makubaliano, vita bado vingetokea.

Mahmoud Naboyan, mjumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa ya Bunge, pia alikosoa rasimu ya makubaliano ya mazungumzo tarehe 8 Juni. Alisema hakuna muda maalumu uliowekwa wa kufikia makubaliano ya mwisho, na kwamba baadhi ya hatua za kuondoa vikwazo zimeahirishwa hadi hapo.

Hata hivyo, tofauti hizi haziwezi kugawanywa kwa urahisi kuwa makundi mawili ya "wanaounga mkono vita" na "wanaounga mkono amani." Qalibaf pia amesema hatakubali makubaliano ambayo hayatetei haki za Iran. Tofauti kubwa ni kuhusu muda ambao kuendelea kwa shinikizo kunaweza kuipa Tehran nguvu zaidi ya kujadiliana na ni wakati gani gharama za vita zinakuwa kubwa kuliko faida zake.

Ben Taleblou ana mtazamo tofauti kuhusu mahesabu ya Kiongozi Mkuu wa Iran. Anaamini kwamba katika mazingira ya sasa, utawala wa Iran "unaona kuendelea kuishi kwake kunategemea zaidi kuongeza mvutano kuliko kushiriki katika mazungumzo." Kwa maoni yake, vikwazo vya kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kijamii vinavyoikabili Marekani katika kupanua vita vimeifanya Tehran ichague njia hiyo kwa urahisi zaidi. Anaamini kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaelekea kwenye vita vya muda mrefu vinavyopiganwa katika maeneo mbalimbali.