Waridi WA BBC: 'Shiko mnyanyua vyuma' aliyekataa kutambuliwa kwa ulemavu wake

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Hebu fikiria kuamka siku moja na kukuta maisha yako yamebadilika kabisa.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Margaret Wanjiku maarufu kama 'Shiko wa Machuma' aliyepoteza miguu yako yote miwili na kuarifiwa kuwa huenda maisha yake yasiwe kama alivyozoea.

Kwake Shiko, ndoto hiyo mbaya iligeuka kuwa uhalisia mwaka 2020 baada ya kupata ajali mbaya ya treni.

Lakini badala ya kuruhusu janga hilo limuamulie yeye ni nani, aliamua kujichagulia mwanzo mpya na leo hii amezungumza na mwandishi wa BBC Asha Juma kama 'Shiko Wa Machuma' aliyemtembelea katika eneo lake la kufanya mazoezi, na kuelezea safari yake ya maisha.

Watu wanapomwona Shiko Wa Machuma leo akinyanyua vyuma vizito, wanaona nguvu za kipekee. Lakini je, unaifahamu simulizi ya binti huyu kijana?

'Ajali iliyobadilisha maisha yangu milele'

.

Shiko wa Machuma ameanza kwa kukumbuka siku ile aliyopata ajali. Anasema walikuwa kumi. Wanaume saba na wanawake watatu waliokuwa wameenda sherehe.

Na baadaye usiku wa manane, waliamua kurejea nyumbani kwa kudandia gari la moshi licha ya wao kufahamu hatari iliyokuwa mbele yao.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Nilijiamini na nikasema wakati gari moshi linapita, lazima nitaruka na kulidandia," anakumbuka Shiko wa Machuma.

Hata hivyo hali haikuwa kama alivyotarajia.

"Nilishindwa kujivuta juu ili kuwa imara. Nikavurutwa chini ya gari moshi na hapo ndipo gari hilo liliponiburuta umbali wa mita 50," Shiko anasema.

"Ghafla nikaanza kuzungumza na Mungu wangu kimoyo moyo".

Siku hii ndio ilikuwa mwanzo wa kuimarika kwa uhusiano Shiko na Mungu wake.

"Nilimwambia Mungu, najua nimekuwa mtoto mbaya, mtukutu, lakini nakuomba kutoka moyoni mwangu, nipe nafasi nyingine nirekebishe tabia zangu. Niwe mtoto mzuri," Shiko wa Machuma anasema.

Shiko anaongezea kwamba alipokuwa hospitali aliamka baada ya siku mbili, na hapo ndipo madaktari walipomueleza kuwa amepoteza miguu yote miwili lakini anasema bado hakuwa anaamini hadi alipotoka hospitali.

"Siku ya kutoka ndio niligundua kuwa maisha yangu hayatarudi kuwa kama nilivyokuwa.

"Kipindi changu kigumu maishani ni kukubali kuwa hakuna siku nitawahi kuwa na miguu yangu miwili tena," anasema Shiko.

Na kama mwanadamu mwingine, kuna wakati alihisi kukata tamaa.

"Nilitamani kujitoa uhai mara mbili tatu hivi," Shiko anasema.

Unyanyuaji wa Vyuma

.

Wakati Shiko akiwa anapitia changamoto zake za maisha anasema kuna kocha ambaye alikuwa akimuona akifanyisha wanawake mazoezi na huo ukawa mwanzo wa chachu ya kile anachokifanya.

Mwingine alikuwa rafiki yake ambaye alimwambia kuwa kila akimwangalia anamuona akiwa na uwezo wa kunyanyua vyuma.

"Yeye ndiye aliyenihusisha kwa mchezo wa unyanyuaji vyuma kitaaluma kila aliponiona, lakini siku ya kwanza kuona jinsi hali ilivyo, nilimwambia siwezi kushiriki mchezo huu," anasema Shiko.

Ameongeza kuwa wakati huo hakuweza kunyanyua hata kilo 10 za chuma lakini hali yake iliendelea kuimarika kadiri alivyoendelea kufanya mazoezi.

"Alinipa motisha wa kunyanyua vyuma na sasa hivi na nyanyua kilo 100," Shiko anasema.

Kile kinachomfurahisha zaidi ni kwamba sehemu yake ya mazoezi, ni sehemu ya kipekee. Hakuna anayemhukumu kwa jinsi alivyo. Na ingawa amefanya mazoezi ya kunyanyua vyuma kwa miezi minane peke yake hadi sasa, ni mengi anayoweza kujivunia.

Mafanikio

Shiko anasema hali haikuwa rahisi wakati anarejea shuleni lakini taratibu alianza kuona kuwa kumbe hata kile anachokipitia sio kitu.

"Kilichonipa nguvu ya kujiamini na imani tena ni wakati niporudi shuleni. Nilipatana na watu wana ulemavu aina zote na wa wengine walikuwa katika hali mbaya hata kuliko mimi. Kuna wale ambao hawakuweza kujilisha wala kujifulia nguo," anasema Shiko.

"Pia, nawakilisha Kenya katika timu ya kunyanyua vyuma na nimetembea sehemu nyingi sana hata nje ya nchi na hili limenifanya nijiamini zaidi," Shiko anasema.

.

Dhana potofu

.

Chanzo cha picha, Margaret Wanjiku

Shiko wa Machuma anasema miongoni mwa changamoto ambazo amepitia ni pamoja na baadhi ya watu kuamua kumtambua kwa ulemavu wake badala ya uwezo wake.

"Wakiniona kwa gari langu la magurudumu wananiona kama mtu ambaye hawezi kufanya mambo mengine. Mfano, mimi sitaki usaidizi lakini mtu anakuja na kunisaidia kusukuma gari langu. Mimi mimi niko sawa," Shiko anasema.

Pia anaongeza kuwa kuna wakati anataka kupanda gari la umma lakini watu hawajui watamsaidia vipi.

"Kingine kinachonikera ni wakati nimevaa nguo yangu nzuri na ni lazima ishike uchafu kwa sababu siwezi kutembea kwa miguu yangu," Shikoo anasema.

Pia anasema sehemu anayofanya mazoezi iko ghorofa ya pili, na kuzipanda sio kazi rahisi. "Mazoezi yanayonifanya kuwa Shiko wa Machuma".

Kingine alichogusia ni wale ambao kwa sababu ya hali yake, wanadhani wanaweza kumtumia vibaya, lakini mwenyewe anasema katu, hawezi kuruhusu hilo kutokea.

Wito wa Shiko ni kwa wote ambao pengine wanaona maisha yamebadilika.

"Cha msingi ni kujipa moyo na kujikubali."

"Maisha yanaweza kubadilika. Jana si leo na kesho haitakuwa leo. Mimi ningejua naenda kupata ajali singeenda," anasema Shiko.

"Dunia haiangalii ni changamoto gani unazopitia kwa sasa bali kile utakachokuwa nacho baadaye, hivyo basi, cha msingi ni kujitia nguvu," anasema Shiko.

Licha ya kwamba changamoto anazopitia ni nyingi, Shiko wa Machuma wa sasa, ni tofauti sana na Margaret wa wakati ule akiwa kitandani hospitali.

"Shiko wa sasa anamshukuru wa zamani kwa sababu hakukata tamaa licha ya magumu aliyopitia kwa sababu sasa hivi anaweza kujizungumzia na kujisimamia.

Shiko wa Machuma, msichana kijana wa miaka 23, aliyekata kutambuliwa kwa ulemavu au kuruhusu utawale kurasa za maisha yake.