Askofu wa Afrika Kusini Desmond Tutu ameaga dunia akiwa na miaka 90

Iliyochapishwa

Askofu wa Afrika Kusini Desmond Tutu, Mshindi wa tuzo ya Nobel ambaye aliisaidia Afrika Kusini kumaliza ubaguzi wa rangi amefariki akiwa na umri wa miaka 90 .

Rais Cyril Ramaphosa amesema kwamba kifo cha muhudumu huyo wa kanisa kimeadhimisha kwa mara nyengine misiba ya kizazi muhimu cha taifa hilo .

Alisema kwamba Askofu Tutu alisaidia katika kurithi taifa la Afrika kusini lililokombolewa .

Tutu alikuwa mmojawapo ya viongozi maarufu nchini humo na Ugenini.

Alishiriki katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi akishirikiana na Nelson Mandela, na kuchochea harakati za kukomesha sera ya ubaguzi wa rangi iliyotekelezwa na serikali ya wazungu wachache dhidi ya weusi walio wengi nchini Afrika Kusini kuanzia 1948 hadi 1991.

Alitunukiwa tuzo ya Nobel mwaka 1984 kwa jukumu lake katika mapambano ya kukomesha mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Kifo cha Tutu kinajiri wiki chache tu baada ya Rais wa mwisho wa enzi za ubaguzi wa rangi FW de Clerk , kufariki akiwa na umri wa miaka 85.

Rais Ramaphosa alisema kwamba Tutu alikuwa kiongozi maarufu wa dini , mwanaharakati dhidi ya ubaguzi wa rangi na mpiganiaji wa haki za binadamu kote duniani.

Alimuelezea kuwa mtu mzalendo , kiongozi mwenye misimamo aliyetoa maana kwa ufahamu wa Biblia kwamba imani bila matendo ni sawa na kifo.

"Alikuwa mtu mwenye ufahamu wa ajabu, mwadilifu na asiyeweza kushindwa dhidi ya nguvu za ubaguzi wa rangi, pia alikuwa mpole na mwenye huruma kwa wale ambao walikuwa wamepitia dhuluma na vurugu chini ya ubaguzi wa rangi, mbali na watu waliokandamizwa kote ulimwenguni."

Alitawazwa kama padre mwaka wa 1960, na kuhudumu kama askofu wa Lesotho kuanzia 1976-78, askofu msaidizi wa Johannesburg na mkuu wa parokia ya Soweto.

Alikua Askofu wa Johannesburg mnamo 1985, na akateuliwa kuwa Askofu Mkuu wa kwanza mweusi wa Cape Town. Alitumia nafasi yake ya hadhi ya juu kuzungumzia ukandamizaji dhidi ya watu weusi nchini mwake, siku zote akisema nia yake ni ya kidini na si ya kisiasa.