Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yaahirishwa huku Vance akijiondoa katika safari ya Uswizi
Mazungumzo mapya ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran yameahirishwa baada ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, kuahirisha safari iliyokuwa imepangwa kwenda Uswisi.
Ikulu ya White House ilitangaza usiku wa Alhamisi kwamba Vance hangesafiri kuhudhuria mazungumzo hayo na kusema kwamba maandalizi ya kiutendaji hayakuwa “rahisi wala ya kutabirika”.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Marekani kuondoa mzingiro wake wa kijeshi wa majini dhidi ya Iran, kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano kati ya nchi hizo mbili yaliyolenga kumaliza mzozo huo.
Ingawa makubaliano hayo pia yalisema mapigano yanapaswa kusitishwa nchini Lebanon, Wizara ya Afya ya Lebanon ilisema mashambulizi ya Israel yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 18 kusini mwa nchi hiyo usiku kucha.
Jeshi la Israel lilisema limelenga kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, na kuongeza kuwa wanajeshi wake wanne waliuawa.
Wapatanishi walikuwa wanatarajiwa kukutana kwa kile maafisa wa Marekani walichokiita “majadiliano ya kiufundi” kuhusu hatua zinazofuata za utekelezaji wa makubaliano yaliyotiwa saini mapema wiki hii.
Hata hivyo, katika taarifa yake, Ikulu ya Marekani ilisema mipango ya mazungumzo hayo “haikuwa imekamilishwa”. Iliongeza kuwa Marekani inatazamia “kuanza mazungumzo ya kiufundi haraka iwezekanavyo”.
Baadaye, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi ilithibitisha kwamba mazungumzo yaliyopangwa kufanyika katika mapumziko ya milimani ya Burgenstock yameahirishwa, ingawa ilisema maandalizi ya mazungumzo hayo yanaendelea.
Soma zaidi: