Ajenda ya nishati safi ya kupikia Tanzania nini kimebadilika?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kila mwaka, takribani Watanzania 33,000 hupoteza maisha kutokana na athari za uchafuzi wa hewa ya ndani unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa majumbani. Takwimu hizo zinaifanya nishati ya kupikia kuwa zaidi ya suala la jikoni; ni suala la afya ya umma, mazingira na maendeleo ya taifa.

Kwa miongo kadhaa, karibu kaya tisa kati ya kumi nchini Tanzania zimeendelea kutegemea kuni na mkaa kama vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, asilimia 63.5 ya kaya hutumia kuni huku asilimia 26.2 zikitumia mkaa.

Ili kubadili hali hiyo, Serikali ilizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) Mei 8, 2024, ikiwa na lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Kufanikisha azma hiyo, Serikali imepanga kutumia zaidi ya shilingi trilioni 4.6, sawa na takribani dola za Marekani bilioni 1.75, kupitia ruzuku za majiko na mitungi ya gesi, uboreshaji wa miundombinu ya nishati pamoja na kampeni za kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Ukubwa wa uwekezaji huo unaweza kueleweka zaidi ukizingatia kwamba fedha hizo kama utazigawa kwa watanzania wote milioni 61, kila mmoja atapata zaidi ya shilingi 75,000, kaaribu dola 28. Maana yake kwa simu za kitochi, kila mtanzania angalau angepata wastani wa simu mbili.

Hivyo, ajenda ya nishati safi ya kupikia si kampeni ya kawaida ya nishati. Ni moja ya juhudi kubwa zaidi za kubadili maisha ya wananchi, kulinda mazingira na kuboresha afya ya umma kwa wakati mmoja.

Lakini miaka miwili baadaye Je, Tanzania imepiga hatua kiasi gani kuelekea lengo hilo?

Takwimu zinaonyesha mabadiliko

Kwa zaidi ya muongo mmoja, matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania yalikuwa yakiongezeka kwa kasi ndogo. Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa matumizi hayo yaliongezeka kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi asilimia 6.9 mwaka 2021, kiwango kilichokuwa mbali na wastani wa dunia wa asilimia 71.

Hata hivyo, katika miaka michache iliyopita kasi ya mabadiliko imeanza kuonekana. Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia katika Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, anasema matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka asilimia 6.6 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 kwa sasa.

Katika kipindi hicho, serikali imesambaza zaidi ya mitungi 450,000 ya gesi ya LPG kwa ruzuku, kugawa majiko banifu zaidi ya 200,000 na kuanza mpango wa majaribio wa majiko ya umeme kupitia mfumo wa bili za TANESCO.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, anasema ongezeko hilo limetokana na juhudi za kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kiafya na kimazingira za matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuwezesha upatikanaji wake kwa wananchi na taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100.

Lakini nyuma ya takwimu hizo kuna simulizi za wananchi ambao wameanza kuona mabadiliko katika maisha yao ya kila siku. Kwa Geneveve Mhina wa Morogoro, mabadiliko hayo yanaonekana ndani ya nyumba yake.

"Moshi ulikuwa unatusumbua sana hasa wakati wa mvua kuni zinapokuwa mbichi. Sasa tunapotumia gesi nyumba inakuwa safi na watoto hawakai tena kwenye moshi. Kikubwa tunachohitaji ni huduma hizi zipatikane karibu na sisi," anasema.

Mabadiliko hayo yanaonekana pia katika taasisi za elimu. Katika Shule ya Sekondari Lulumba mkoani Singida, Mkuu wa shule hiyo, Yeremia Kitiku, anasema matumizi ya gesi yameongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wanafunzi. "Tangu tuanze kutumia mtambo wa gesi, wanafunzi wanapata chakula kwa wakati na kuingia darasani kwa wakati," anasema.

Kwa wahudumu wa jikoni, manufaa makubwa yamekuwa ya kiafya. "Zamani tulisumbuka sana na moshi. Unakuta kifua kinauma, kichwa kinauma. Moshi ulikuwa mkali kupita kiasi," anasema mmoja wa wahudumu wa shule hiyo.

Mbali na kaya na shule, taasisi nyingine za umma nazo zimeanza kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kambi za jeshi yamefikia asilimia 92.

Tanzania itafanikiwa kufikia lengo?

Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika miaka miwili iliyopita, kinachoulizwa zaidi ni kama Tanzania inaweza kufikia lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034?

Uzoefu wa nchi kama India, Kenya na Ghana unaonyesha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaweza kuongezeka kwa kasi kupitia ruzuku, mikopo nafuu, uwekezaji katika miundombinu na ushiriki wa sekta binafsi. India, kwa mfano, imefanikiwa kuwafikia zaidi ya kaya milioni 95 kupitia mpango wa ruzuku za gesi ya LPG.

Hata hivyo, changamoto bado ni kubwa. Utafiti wa hivi karibuni wa Deborah Andrew Ngusa wa Chuo Kikuu cha Dodoma uliohusisha nchi sita za Afrika na Asia umebaini kuwa kaya nyingi za vijijini bado hukumbana na vikwazo vya kifedha, miundombinu duni, mila na desturi pamoja na changamoto za kiteknolojia katika kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

"Ningetamani serikali ingegawa bure mtungi wa gesi na jiko banifu moja kwa kila kaya masikini vijijini. Kampeni hii ingefanikiwa mara moja," anasema Muhadhi Masisi, mkazi wa Masasi, anayeamini kasi ya mpito huo inaweza kuongezeka zaidi ikiwa kaya maskini zitawezeshwa kupata vifaa vya kuanzia.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, anasema serikali imeanza kukabiliana na changamoto hiyo ya gharama, kupitia ruzuku ya asilimia 50 kwa mitungi ya gesi ya kilo sita na usambazaji wa zaidi ya mitungi 452,000 nchini kote.

"Kuna dhana imejengeka kwamba nishati safi ya kupikia ni ghali kuliko nishati nyingine. Dhana hiyo haina ukweli kwa asilimia 100 kwani teknolojia zilizoboreshwa zinapunguza upotevu wa nishati na hivyo kupunguza gharama kwa watumiaji," anasema.

Pamoja na hatua hizo, wataalamu wanaamini kuwa mafanikio ya ajenda hiyo hayatapaswa kupimwa kwa takwimu pekee. Mtaalamu wa masuala ya maendeleo ya uchumi wa jamii, Raphael Kugesha, anasema:

"Kipimo cha mafanikio ya ajenda hii si asilimia 80 pekee. Ni siku ambayo mwanamke wa kijijini hatahitaji tena kutumia saa kadhaa kutafuta kuni, na mtoto hatalazimika kuvuta moshi kila siku akiwa nyumbani."

Kwa sasa, moshi unaopungua katika mashule, vyuo, taasisi kama magereza, kambi za jeshi na maelfu ya kaya nchini ni ishara kwamba safari imeanza. Lakini mafanikio ya kweli yataonekana pale ambapo kila Mtanzania, bila kujali kipato au eneo analoishi, ataweza kupata nishati safi ya kupikia kwa urahisi, kwa gharama nafuu na kwa usalama.