Trump azindua ndege ya kifahari ya Air Force One iliyotolewa kama zawadi na Qatar
Rais Donald Trump amezindua ndege mpya aina ya Boeing 747-8 ya kutumiwa kwa safari za rais maarufu kama Air Force One ambayo ilitolewa kama zawadi "isiyokuwa na masharti" na serikali ya Qatar kwa Marekani mwaka jana.
Jeshi la Marekani limekamilisha marekebisho ya ndege hiyo ya kifahari, ambayo imekadiriwa kuwa na thamani ya $400m (£300m).
"Ndege hii iligeuzwa kuwa Ikulu ya White House katika kiwango cha kifahari ambacho hakuna mtu amewahi kukishuhudia," Trump alisema katika hotuba yake katika kituo cha Joint Base Andrews siku ya Ijumaa.
Jeshi la wana anga la Marekani lilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba ndege hiyo itaanza safari za majaribio ya mwisho, kabla ya kuanza kutumiwa kumsafirisha rais.
Jeshi pia lilisema kuwa marekebisho ya ndege hiyo yalijumuisha uboreshaji wa mifumo ya usalama, mawasiliano na teknolojia, na kwamba waliondoa vitisho vyovyote vinavyowezekana kuwepo katika ndege hiyo.
Mnamo Mei 2025, familia ya kifalme ya Qatar ilitoa zawadi ya ndege ya kifahari aina ya Boeing 747-8 kwa idara ya ulinzi ya Marekani ili itumike kama sehemu ya safu ya ndege zinazoitwa Air Force One, ambazo hutoa huduma za usafiri kwa rais.
Wakati habari hizo zilipofichuliwa mwaka jana, zilizua mjadala kutoka pande zote mbili za kisiasa Marekani, wakiwemo baadhi ya washirika wa Trump. Wakosoaji waliteta kuwa kukubali mchango huo wa thamani ya juu kunaleta mgongano wa kimaslahi na huenda ni kinyume cha katiba.
Ingawa sheria ya Marekani inaonyesha kwamba maafisa wa Marekani wanaweza tu kupokea zawadi chini ya $480, Ikulu ya White House imesisitiza kuwa kukubali ndege hiyo ni halali, na kuahidi kwamba itatolewa kama zawadi kwa maktaba ya rais Trump mara tu atakapoondoka madarakani.
Kabla ya kuongezwa kwa ndege hiyo ya Qatar, safu ya Air Force One ilijumuisha ndege mbili za 747-200B ambazo zimekuwa zikitumika tangu 1990.
Jeshi lilisema ndege hiyo mpya itatumiwa na rais kwa muda wa mpito hadi Boeing iwasilishe ndege zake mbili za VC-25B ambazo zimepangiwa kwa matumizi ya muda mrefu ya Air Force One, lakini kumekuwa na ucheleweshaji katika utengenezaji wake.
Pia unaweza kusoma: