'Taliban hawakuingia Kabul kwa nguvu, niliwaita' - asema rais wa zamani Hamid Karzai

Chanzo cha picha, Getty Images
Aliyekuwa rais wa Afghanistan Hamid Karzai amesema kwamba aliwataka wapiganaji wa Taliban kuingia mji mkuu wa Kabul ili kuzuia ghasia na wizi.
Viongozi wa Taliban walituhakikishia kwamba wapiganaji wake hawataingia mji mkuu wa Afghan, Hamid Karzai aliambia chombo cha Habari cha AP katika mahojiano.
'Lakini rais wa zamani wa Afghanistan Ashraf Ghani aliondoka Kabul ghafla na maafisa wake wakuu na Taliban wasingepatikana'.
Mwezi Agosti mwaka huu , baada ya kuondoka kwa vikosi vya Marekani Taliban ilichukua udhibiti wa Afghanistan na kuiondoa serikali iliokuwa madarakani.
Mmoja baada ya mwengine wapiganaji hao walichukua udhibiti wa maeneo yanayozunguka mji wa Kabul . Wakati huo wapiganaji wa Taliban walihofiwa kuingia mji mkuu wakati wowote.
Baadaye Ashraf Ghani ghafla aliondoka Afghanistan na wapiganaji wa Taliban wakateka mji wa Kabul tarehe 15 Agosti.
Taliban ilisema wakati huo kwamba hawakuwa na nia ya kuingia mjini Kabul, lakini waliingia kuzuia ghasia na wizi katika mji huo.
Hamid Karzai alisema , "Mfumo wa serikali na vikosi vya usalama nchini Afghanistan ulikuwa umepooza . Yeye mwenyewe aliwaomba wapiganaji wa Taliban kuingia Kabul."

Chanzo cha picha, Getty Images
Je mpango uliokuwepo ulikuwaje?
Hamid Karzai aliambia mahojiano hayo kwamba yeye na Abdullah walikuwa wakiwasiliana na viongozi wa Taliban mjini Doha na mpango ulikuwa Taliban kuingia mjini Kabul kwa misingi ya makubaliano na serikali iliokuwepo madarakani.
"Mimi na Abdullah tulikuwa na mipango ya kuzuru Doha tarehe 15 mwezi Agosti kufanya uamuzi wa mwisho wa kisiasa na wapiganaji wa Taliban, alisema.
Kulingana na Karzai ilikuwa wakati wa mchana ambapo uvumi ulienea kuhusu kuondoka kwa rais Ghani nchini humo.
Alipozungumza na waziri wa masuala ya ndani, ilibainika kwamba maafisa wote akiwemo afisa mkuu wa polisi mjini Kabul walikuwa wameondoka mjini humo na kwamba hakuna aliyekuwa madarakani.
Hamid Karzai anasema kwamba iwapo rais Ghani angekuwepo nchini humo kungekuwa na uwezekano wa makubaliano ya kuafikiwa na wapiganaji wa Taliban na kutengeneza mfumo fulani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katiba na bunge
"Afghanistan ipo chini ya udhibiti wa Taliban . jamii ya kimataifa inahitaji kufanya majadiliano na Taliban ili kuzuia hali ya kibinadamu inayoendelea kuzorota.," Karzai said.
"Mara nyengine wanachama wa kundi hilo hawaeleweki. Kwa mfano sio sawa kwamba wanawake wa Afghanistan hawafai kutoka majumbani mwao.''
Karzai alisema aliwapatia Taliban mpango wa kujiondoa katika hali waliopo sasa. Mpango huo unashirikisha kuidhinisha katiba ya aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Mohammad Zahir Shah mbali na kupanga kamati kuu ya wabunge inayohusika kufanya maamuzi makuu serikalini.
Kamati hiyo inaweza kufanya maamuzi kuhusu serikali mpya , katiba na bendera ya kitaifa.
Hatahivyo , alisema kwamba , haki ya wanawake kufanyakazi , haki ya wasichana na wavulana kusoma na wanawake kushiriki katika kila hatua ya maisha yao ni masuala ambayo hawawezi kunyimwa na yanapaswa kulindwa.
Ashraf Ghani na hali ya Taliban
Baada ya kuondoka Kabul, Ashraf Ghani alisema kwamba alikuwa ameamua kuondoka katika mji huo mkuu ili kuzuia vita na umwagijkaji wa damu nchini humo.
Alikuwa amepokea ripoti za ujasusi kwamba Taliban walitaka kumuua. Upande mwengine , Taliban walikuwa wamesema kabla ya kuingia Kabul , kwamba wapiganaji wao watasalia nje ya mji huo na kwamba mazungumzo ya kukabidhi mamlaka yatafanywa.
Baada ya kuuteka mji mkuu, Taliban walitangaza serikali ya muda.
Ilikuwa ikitumia bendera yake nyeupe badala ya ile ya Afghanistan.
Hamid Karzai huenda alikuwa na mapendekezo kwa Taliban , lakini kufikia sasa hajaonesha nia ya kushirikishwa katika serikali ya Loya Jirga.
Hatahivyo, wachambuzi, wanasiasa na jamii ya kimataifa nchini Afghanistan inaamini kwamba serikali ya Taliban sio serikali ya mseto.
Haina ushirikisho wowote wa wanawake.
Taliban inajaribu kutafuta utambuzi kutoka kwa jamii ya kimataifa, lakini kufikia sasa hakuna taifa lililowatambua.












