Waridi wa BBC: Niliacha shule kidato cha pili, niwe mfanyabiashara mkubwa

Chanzo cha picha, Anezylitta
"Niliacha shule nikiwa kidato cha pili," anaeleza Zena Sharif, maarufu kama Scaba.
Miaka 10 iliyopita, nilikuwa ninaishi Kigamboni huku shule yangu ikiwa Upanga. Kutokana na changamoto za usafiri, ilinichukua kati ya saa nne hadi tano kufika shuleni kila siku. Hali hiyo ilinipunguzia hamasa ya kuendelea na masomo ya sekondari.
"Mara nyingi nilikuwa nafika shuleni nikiwa nimechoka na sina ari ya kusikiliza masomo. Baada ya kutoka darasani, nilikuwa nakwenda dukani kwa baba yangu na kukaa naye huku akiendelea na shughuli zake za biashara," anasimulia.
Zena, mama wa watoto wawili mkazi wa jiji la Dar es Salaam amekuwa kivutio kwa wasichana wengi na wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii kutokana na umahiri wake katika taaluma ya ubunifu wa ndani ya majengo (interior design).
Kadri muda ulivyopita, aligundua kuwa elimu ya darasani haikuwa ndoto yake. Badala yake, alivutiwa zaidi na biashara ya baba yake iliyohusisha uuzaji wa vifaa vya ujenzi.
"Niliketi na baba yangu nikamweleza kwamba baada ya kumaliza kidato cha pili sikutaka kuendelea na masomo. Baba alielewa haraka uamuzi wangu, lakini mama yangu alitamani niendelee na shule," anasema.
Zena anakumbuka kuanza kujihusisha na biashara akiwa na umri wa miaka 16 chini ya usimamizi wa wazazi wake. Baba yake alimpa nafasi ya kwanza ya kuonyesha uwezo wake wa kuendesha biashara kwa kumdhamini kupata mkopo benki.
"Baba alisema, 'Ninaweza kukupa pesa, lakini najua hutazirudisha kwa sababu mimi ni baba yako.' Badala yake, alinipeleka benki na kunidhamini. Nilikopeshwa shilingi milioni 40 kama mtihani wa kwanza wa kuonyesha uwezo wangu wa kuendesha biashara."
Anasema baadhi ya wateja walikuwa na mashaka walipomwona akiwa msichana mdogo. Hata hivyo, baada ya kukamilisha kazi zake, wengi walionyesha kuridhishwa na matokeo aliyowapatia.

Chanzo cha picha, Anezylitta
Kwa mujibu wa Zena, mtaji pekee hautoshi kufanikisha biashara.
"Unapotaka kuingia kwenye biashara lazima ujitayarishe kimwili na kiakili. Uaminifu na ubunifu ni muhimu kwa sababu ushindani ni mkubwa. Lazima ujitofautishe ili biashara yako ikue na kuendelea kuvutia wateja."
Licha ya kuacha shule ya sekondari, Zena alidhamiria kuendelea kujifunza kwa njia nyingine. Alitumia mtandao kujifunza kuhusu upangaji wa ndani wa nyumba, hoteli, shule na majengo ya biashara.
"Nilijifunza kupitia safari mbalimbali, na wakati mwingine nililipia mafunzo mafupi katika nchi nyingine ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko."
Zena ambaye sasa ameajiri mamia ya vijana wa kitanzania katika kampuni yake ya ubunifu, anasema vijana wengi wana shauku ya kufanya vizuri na kujiajiri.
Ndoto ya kuwafundisha vijana wa Afrika Mashariki

Chanzo cha picha, Anezulitta
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sasa Zena ana ndoto ya kuanzisha kituo kikubwa cha mafunzo ya ufundi bunifu kitakachowakusanya vijana 1,000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
"Kitakuwa miongoni mwa vituo vikubwa vya mafunzo Afrika Mashariki. Nimetembelea nchi nyingi za Afrika na kugundua kuwa vituo vya aina hii vipo katika maeneo mengine, lakini bado ni vichache Afrika Mashariki."
Anasema wanafunzi watafundishwa kwa vitendo stadi mbalimbali, ikiwemo utengenezaji wa samani, ubunifu wa ndani ya majengo, kazi za alumini, mapambo, utengenezaji wa keki na fani nyingine za ubunifu.
"Kituo hicho kitakuwa na kiwanda, makazi na hata studio ili wanafunzi waweze kufanya majaribio na kukuza vipaji vyao katika mazingira halisi ya kazi."
Zena anashauri wazazi kutambua uwezo wa watoto wao na kuwasaidia kujiendeleza kwenye mambo wanayoweza.
'Mtoto anapoanza kujitambua angalia anapenda nini ili aweze kufanya kitu ambacho anakipenda'.
Mzazi akiweza kufanya hivyo itasaidia watoto kufanya vitu ambavyo wana uwezo navyo.Hii itakuwa rahisi kwa watoto kuanza kujijengea uwezo mapema.
Zena anasema alitamani kufanya kitu cha tofauti jambo ambalo lilimfanya hata nyakati alizokatishwa tamaa kuwa asingeweza alifanya jitihada kuhakikisha kwamba analimudu jambo husika.
'Mitandao ya kijamii imenifungulia milango mikubwa'

Chanzo cha picha, Anezylitta
Zena anasema mitandao ya kijamii imekuwa nyenzo muhimu ya kutangaza kazi zake kuliko kuonyesha maisha yake binafsi.
"Natumia mitandao ya kijamii kujenga chapa ya kazi yangu. Kazi zangu zimeonekana katika nchi mbalimbali, na nimepokea tuzo kutoka Canada. Ninajivunia kuona kazi zangu zikitambulika kimataifa kupitia mitandao."
Anaeleza kuwa zamani ilihitajika kutumia mabango, magazeti au redio kufikia wateja wengi, lakini sasa mitandao ya kijamii imefungua fursa kubwa zaidi.
"Mara nyingi napokea ujumbe kama, 'Zena, uliwezaje? Nifundishe niwe kama wewe.' Maneno hayo hunigusa sana, hasa yanapotoka kwa wasichana na vijana wanaotamani kufuata nyayo zangu."
Kwa Zena, jambo linalompa furaha zaidi ni kuona watu wanaamini uwezo wake na kupata hamasa ya kutimiza ndoto zao kupitia kazi na ubunifu.















