Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ebola: DR Congo yazindua kampeni ya chanjo ya Ebola Butembo
Kampeni ya chanjo ya Ebola imeanzishwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa huo mwezi huu, Shirika la Afya Duniani - WHO limesema.
DR Congo imethibitisha visa vinne vya ugonjwa wa Ebola tangu kutangazwa kwa mlipuko mwingine wa virusi hivyo Februari 7 huko Butembo.
Wafanyakazi wa afya katika vituo vya afya ambako mgonjwa wa kwanza wa Ebola alitibiwa walikuwa wa kwanza kupata chanjo, WHO imesema.
Taarifa hizo zinawadia baada ya Guinea iliyopo Afrika Magharibi kutangaza mlipuko wa ugonjwa huo.
Awali, mlipuko wa Ebola huko DR Congo ulitangazwa Juni 2020.
Na ulikuwa umesababisha vifo vya watu 2,287 tangu Agosti mwaka 2018.
Takriban dozi 8,000 za chanjo ya Ervebo, ambazo zilikuwa zimehifadhiwa baada ya mlipuko, zinatumiwa katika kampeni ya sasa hivi ya kutolewa kwa chanjo, mwandishi wa BBC Emery Makumeno ameangazia hilo kutoka mji wa Kinshasa.
Ervebo ilikuwa chanjo ya kwanza ya Ebola kuidhinishwa na Utawala wa Chakula na Dawa ya Merekani (FDA) Desemba 2019.
Pia, nchi ya Guinea Jumapili ilitangaza mlipuko mpya wa Ebola, kufuatia kuthibitishwa kwa visa saba vya maambukizi ya virusi hivyo na vifo vitatu.
Waathirika walianza kuugua ugonjwa wa kuharisha, kutapika na kuvuja damu baada ya kuhudhuria mazishi ya muuguzi mmoja karibu na mji wa Nzérékoré.
"WHO inafuatilia kwa karibu hali hiyo na imechukua tahadhari na pia inawasiliana na wazalishaji [wa chanjo] kuhakikisha dozi za chanjo zinapatikana haraka iwezekano kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo," Shirika la habari la AFP limemnukuu Alfred George Ki-Zerbo, mwakilishi wa WHO nchini Guinea.
Kati ya mwaka 2013 na 2016 zaidi ya watu 11,000 walifariki dunia katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwasababu ya janga la Ebola ambalo llilianza nchini Guinea.
Rais wa Liberia George Weah ameweka mamlaka ya afya katika hali ya tahadhari kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.
Mwandishi wa BBC Umaru Fofana nchini Sierra Leone anasema kuwa nchini humo kuna hofu zaidi ya ugonjwa wa Ebola kuliko corona.
Amesema uwepo wa chanjo mpya kidogo ni faraja - na kwamba kuna hitaji la dharura la hifadhi ya chanjo 500,000 kupitia Gavi - muungano wa chanjo kimataifa.
Nchi hizo tatu zina idadi ya watu jumla ya milioni 22.5 na kusababisha wasiwasi kuwa watengenezaji wa chanjo hiyo huenda wakawa na muda kidogo kutengeneza chanjo nyingi ikiwa kutakuwa na haja ya kufanya hivyo wakati ambapo chanjo za virusi vya corona ndio zinazopewa kipaumbele, mwanahabari wa BBC amesema.
Ebola ni nini?
- Ebola ni virusi ambavyo awali vilisababisha kifo ghafla, mwili kudhoofika kabisa, maumivu ya misuli na kuwashwa kwenye koo
- Pia dalili hizo zinaandamana na kutapika, kuharisha na kutoka damu kwa ndani na nje
- Watu wanapata maambukizi wakikutana moja kwa moja na walioathirika kwa njia ya ngozi, mdomo na pua, kwa njia ya damu, kutapika, choo au majimaji ya mwilini ya mtu mwenye ugonjwa wa Ebola
- Wagonjwa wanafariki dunia kutokana na ukosefu wa maji mwilini na kushindwa kufanyakazi kwa viungo vya mwili