Mashambulizi ya Israel yawaua watu sita Gaza, akiwemo mpiga picha wa Al Jazeera
Mashambulizi ya Israel huko Gaza yameua takriban watu sita, akiwemo mpiga picha wa Al Jazeera na mtoto mmoja, kwa mujibu wa maafisa wa afya na waokoaji.
Al Jazeera ilisema “inalaani vikali uhalifu huu wa kikatili wa kulenga na kumuua” mwandishi wake Ahmed Wishah, ambaye aliuawa katika shambulio la bomu lililolenga nyumba moja katikati ya Gaza siku ya Jumamosi.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilidai kuwa Wishah alikuwa “gaidi katika kitengo cha kijeshi cha Hamas ambaye alihudumu kama mpiga risasi wa kuvizia”.
Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, ambayo takwimu zake zinachukuliwa kuwa za kuaminika na Umoja wa Mataifa, inasema jeshi la Israel limeua watu 1,007 tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yalipoanza Oktoba iliyopita.
Al Jazeera ilisema kifo cha Wishah siku ya Jumamosi “kinawakilisha ukiukaji mpya na mkubwa wa sheria zote za kimataifa na kanuni, na kinaonyesha sera inayoendelea ya kuwanyima sauti waandishi wa habari na kunyamazisha ukweli”.
IDF ilisema Wishah katika miezi ya hivi karibuni alikuwa akipanga mashambulizi ya kuvizia dhidi ya wanajeshi wa Israel, bila kutoa ushahidi.
Watu wengine wawili waliuawa pamoja na Wishah katika shambulio hilo lililolenga nyumba katika kambi ya wakimbizi ya Bureij, kwa mujibu wa hospitali ya eneo hilo na shirika la ulinzi wa kiraia linaloendeshwa na Hamas, ambalo hufanya kazi za uokoaji.
IDF pia ilidai kuwa wawili hao waliouawa walikuwa sehemu ya Hamas.
Ndugu yake Wishah, Mohamed, ambaye pia alikuwa mwandishi wa Al Jazeera, aliuawa katika shambulio la Israel mwezi Aprili. IDF ilidai kuwa alishirikiana na Hamas katika makao makuu ya uzalishaji wa makombora na silaha ya kundi hilo, bila kutoa maelezo zaidi.