Je, Naibu Rais wa Kenya atamudu joto la kisiasa linalomfuata?

    • Author, Profesa Hezron Mogambi,
    • Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu Cha Nairobi
  • Iliyochapishwa

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto na nia yake ya kuwania Urais mwaka wa 2022 imepandisha joto la kisiasa nchini Kenya mapema zaidi ya mwaka mmoja na nusu kabla wakati wenyewe na kuzua maswali mengi.

Akiwa ameshtuliwa na kuja pamoja na kuungana kwa wanasiasa wakuu nchini Kenya wanaoonekana kutaka kupinga azma yake ya kutaka kuwa Rais pamoja na kuondolewa kwa washirika wake wa kisiasa kwenye nyadhifa kwenye serikali na bungeni, safari ya William Ruto kuelekea mwaka wa 2022 inaonekana kukumbwa na changamoto nyingi.

Kabla ya hapo, kuanzia mwaka wa 2013 wakati wawili hawa walionekana kama "mapacha wa kisiasa", hali ilikuwa shwari kwani walikuwa wameahidiana kwamba watasaidiana kisiasa hadi kila mmoja wao kutawala Kenya. Hali sasa ni tofauti kati ya wawili hawa.

Hali ngumu na chanzo

Matatizo haya yote yalianza mnamo Machi mwaka wa 2018 wakati Rais Uhuru Kenyatta alikubaliana kufanya kazi na Raila Odinga baada ya kuwa mahasimu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017, makubaliano ambayo sasa William Ruto anayaona kama yenye nia mbaya-mpango wa kumzuia asiwe Rais wa Kenya. Baadaye, wawili hawa waliunda jopo la maridhiano ambalo limetayarisha ripoti yake ambayo inakisiwa huenda ikatumika kama msingi wa kura ya maoni. Kura hii inapingwa na William Ruto.

Ushirikiano wa Rais Kenyatta na Raila Odinga umepelekea Bwana Ruto kuonekana kama ambaye ametengwa kwenye shughuli za serikali na hata za chama tawala cha Jubilee. Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta ameonekana akiwa na uhusiano mzuri na Raila Odinga kwenye siasa na katika bunge la Kenya ambapo vyama vyao vinashirikiana.

Katika hali hii ngumu anamojikuta, William Ruto anashindwa cha kufanya maana anaonekana kupigana na mkubwa wake kisiasa, Rais Kenyatta, jambo ambalo wengi wanaamini linaweza kumletea balaa kisiasa kwa sababu ya athari zinazoweza kutokea. Kwa upande mwingine, kwa sababu ya kuwa na azma ya kuwania kiti cha rais wa Kenya, ni lazima ashiriki kwenye shughuli za kisiasa ili kuendelea kujizolea umaarufu nchini.

Hali hii imepelekea Bwana Ruto kukosa kufika kwenye mikutano muhimu ya baraza la mawaziri na hata mingine ya chama cha Jubilee ambako yeye ni msaidizi kama naibu wa Rais Kenyatta.

Rungu la kisiasa ambalo Bwana Ruto alirushiwa miezi kadhaa iliyopita na Rais Kenyatta kwenye bunge la seneti na bunge la kitaifa ambapo wandani wake wa karibu waliondolewa kwenye nyadhifa muhimu na uhusiano wa karibu na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kunampa changamoto mpya anapopanga siasa zake kwa njia tofauti na alivyopanga hapo awali ili kupigania Urais mwaka wa 2022. Katika mabunge yoye mawili ya Kenya, nyadhifa ambazo washirika wake walikuwa nazo sasa haziko na ushawishi wake pia umepunguzwa kisiasa.

Haya yanatokea kwa sababu ya makubaliano yaliyotiwa saini kati ya vyama vya Kanu na uhusiano wa kisiasa na chama cha Raila Odinga, ODM hali ambayo inamnyima idadi ya wabunge ili kupigana na kufanya maamuzi ya kisiasa kwenye mabunge hayo mawili.

Katika kile kinachoonekana kuwa ishara kubwa kwamba uhusiano baina ya Rais Kenyatta na Raila Odinga huenda ukawa hata mkubwa zaidi kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2022, wazee wa jamii ya Agikuyu wapatao 700 na wanasiasa wengine kutoka eneo la Mlima Kenya walimtembelea na kumwombea Raila Odinga nyumbani kwake Kang'o Ka Jaramogi katika kaunti ya Siaya. Ziara hii inatafsiriwa kuwa mpango wa Bwana Raila Odinga kuwania Urais mwaka wa 2022.

Kura ya maamuzi

Jambo lingine kuu ni msukumo uliopo kwa sasa wenye nia ya kufanywa kwa kura ya maamuzi ambayo wandani wa Bwana Ruto wanaiona kama njama ya kumwondoa kwenye kinyanganyiro au kumfanya asiwe na ushawishi wowote wa kisiasa iwapo atawania na kushinda kiti cha Urais mwaka wa 2022.

Bwana Ruto amekuwa akifanya kampeini ambazo zinaonekana kama zenye kupinga kuwepo kwa kura ya maamuzi, yenye nia ya kuongeza nyadhifa za uongozi kwenye ngazi ya kitaifa kama mazoezi tu ya kura ya mwaka wa 2022. Hata hivyo, uwanja wa kisiasa nchini Kenya umekuwa ukibadilika kila kukicha na mabadiliko haya huenda yakaendelea na kubadili sura ya siasa za Kenya kwa kuwa matokeo ya kura ya maamuzi, iwapo itafanyika, huenda yakaipa mwelekeo siasa ya mwaka wa 2022.

Kumekuwepo na mpango wa kuhakikisha kuwa, kadri muda unayoyoma kuelekea uchaguzi wa mwaka wa 2022, nguvu na ushawishi wa Bwana Ruto unaendelea kupunguzwa ndani na nje ya serikali. Hatua hizi ambazo zinatekelezwa na serikali ambayo Bwana Ruto ndiye naibu Rais zina nia ya kumpuguzia ushawishi na ndoto yake ya kupigania Urais mwaka wa 2022, kuwatoa pumzi wandani wake wa kisiasa, na kuwatawanya ili kumfanya bwana Ruto kufikiria upya kuhusu kupigania Urais mwaka wa 2022.

Tatizo jingine ambalo anakumbana nalo bwana Ruto ni seneta wa Baringo Gideon Moi huku kukuwa na madai kwamba seneta huyu anafanya kazi na upinzani ili kufanya kibarua chake cha kutafuta Urais mwaka wa 2022 kuwa kigumu zaidi.

Purukushani kwenye chama cha Jubilee

Halafu kuna changamoto inayomkosesha usingizi bwana Ruto kwa sasa - ile ya chama chake cha Jubilee - jambo ambalo limekifanya chama chake kufunga afisi zake kwa sasa kwa sababu ya mzozo wa uongozi baina yake na maafisa wakuu wa wa chama .

Kwa sasa hatima yake kwenye chama hicho tawala haijulikani maana inavyoonekana maafisa wengine wakuu wakiongozwa na Rais Kenyatta kwenye chama hicho wamemtenga na hana afueni kisiasa.

Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe, ambaye ni rafiki wa karibu wa Rais Kenyatta amenukuliwa akisema mara nyingi kwamba tofauti za kisiasa baina ya Rais Kenyatta na naibu wake zimefikia viwango ambapo haziwezi kutatuliwa na kwamba hawawezi kufanya kazi tena pamoja kwenye chama hicho kama ilivyokuwa hapo awali tangu mwaka wa 2013. Je, atajiondoa kwenye chama tawala cha Jubilee?

Kumekuwepo na ripoti za kisiasa kwamba, kwa hakika, wandani wa Rais Kenyatta wamekuwa wakipanga jinsi ya kupeleka hoja ya kutokuwa na imani bungeni na naibu Rais wa Kenya ili kumwondoa afisini. Je, hili litafanyika na kufaulu ama hali itakuwaje. Likifanyika, hatima ya kisiasa ya Bwana Ruto itakuwaje?

Kando na haya, William Ruto mwenyewe amekuwa akijipanga na kuunda mtandao wa marafiki wa kisiasa tangu mwaka wa 2017 ingawa jambo hili limekuwa likimkera Rais Kenyatta ambaye amekuwa akisisitiza kuwa ni wakati wa kufanya kazi na si siasa. Ingawa yanayomkumba kwa sasa yanaonekana kuwa mazito ikizingatiwa kuwa yeye ni msaidizi wa Rais Kenyatta ambaye hajaonekana kupendezwa na siasa anazozifanya.

Hata hivyo, Bwana Ruto mwenyewe ameonyesha kutotishwa na changamoto zinazomkumba na badala yake amekuwa akifanya kampeini zake akikutana na Wakenya wa kila tabaka hasa akiwalenga wale anaotaja kuwa wametengwa kwenye jamii kama vijana na akina mama, maskini na kuwapa msaada wa kufanya biashara ama ala za kufanyia kazi zao na makundi mengine kama ya kanisa na kijamii kwenye afisi zake na kwake nyumbani jijini Nairobi.

Katika hatua ambayo ilimpunguzia nguvu za kisiasa, Rais Kenyatta alimteua waziri Fred Matiangi kuwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri kwenye utekelezaji wa mipango ya serikali - kazi ambayo, kimsingi, bwana Ruto anafaa kuwa anaifanya. Juma lililopita waziri Matiangi pia alitwikwa jukumu jingine kama mwenyekiti wa watakaoshughulikia usalama na utulivu nchini Kenya.

Kampeini za Ruto

Changamoto nyingine inayomkumba bwana Ruto kupigania Urais wa Kenya ni kwamba ameifanya ngome ya kisiasa ya Rais Kenya ya Mlima Kenya ngome ambayo angetaka kupata uungwaji mkono zaidi bila kutafuta usaidizi wa Rais Kenyatta. Hali hii ya "kuvamia" ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta imewakasirisha wengi wa wandani wa Rais Kenyatta na Rais mwenyewe. Hata hivyo, Bwana Ruto anafahamu kuwa hawezi kupata usaidizi wa kundi linaloonekana kumpinga na ndipo akaanza kampeini ya kuwafikia wananchi wa mashinani moja kwa moja.

Bwana Ruto alitumia urafiki wake na baadhi ya wabunge na wawakilishi wodi wa sehemu za Mlima Kenya anakotoka Rais Kenyatta na kufanya shughuli nyingi za kisiasa na kidini tangu mwaka wa 2013. Hali hii imemfanya kuwa na umaarufu kwenye sehemu hii, jambo linalowaudhi baadhi ya maafisa wakuu serikalini na kwenye chama cha Jubilee.

Katika sehemu ambazo zinaonekana kuwa kinyanganyiro cha kisiasa kitakuwa kikali na ambako kutakuwa na kupigania umaarufu kama vile Nairobi, Nakuru, Kirinyaga, Kiambu, Murang'a na Kajiado tayari kinyanganyiro kinaonekana kitakuwa kikali. Katika sehemu hizi zote, Bwana Ruto amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara na akielekeza macho yake kwenye sehemu za pwani ya Kenya ambako ndiko ngome ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga na chama cha cha ODM.

Bwana Ruto amekuwa akijaribu kila njia kuhakikisha kuwa sehemu ya Mlima Kenya anakotoka Rais Kenyatta iko nyuma yake kisiasa kwa sababu anahitaji kura za sehemu hii ili kuweza kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda Urais mwaka wa 2022.

Aidha, jambo hili linatokana pia na shauku ya kisiasa kwamba ahadi za kisiasa si za kuaminiwa maana ahadi aliyompa Rais Kenyatta ya kumuunga mkono kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2022 yaonekana imeyeyuka bayana kwa haraka.

Kura za eneo la Mlima Kenya

Tatizo lililopo kwenye kura za Mlima Kenya ni kuwa kuna ushahidi wa kihistoria unaoonyesha kuwa tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini Kenya mwaka wa 1992, jamii ya Agikuyu haijawahi kumpigia mwaniaji kutoka nje ya jamii hiyo kura nyingi kwa pamoja.

Katika mwaka wa 1992, sehemu ya Mlima Kenya iligawanyika katika upigaji kura baina ya Mwai Kibaki na Ken Matiba. Katika mwaka wa 1997, Matiba hakung'ang'ania Urais, na wapigaji kura wake wote wakahama na kumpigia kura mpizani wake,Mwai Kibaki.

Katika mwaka wa 2002, kura ya sehemu hii iligawanyika kati ya Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, ambaye hakuwania Urais mwaka wa 2007 lakini akimpigia upatu na kuhakikisha Rais alikuwa Mwai Kibaki. Mwaka wa 2013, eneo la Mlima Kenya lilipiga kura kwa kauli moja kwa Uhuruto.

Kile ambacho hali hii inatuonyesha ni kuwa wakati mwaniaji wa Urais kutoka sehemu ya Mlima Kenya atakapojitokeza akiwa na uwezo wa kuleta matumaini kwa jamii ya eneo hili, uungwaji mkono wa kisiasa ambao Bwana Ruto anaonekana kuwa nao unaweza kupotea kwa haraka sana. Pia, Bwana Ruto ana tatizo jingine la kuhakikisha kuwa yule atakayemchagua kama naibu wake katika kinyangayiro hicho anatoka eneo hili.

Hali hii inatokana na ukweli kwamba Bwana Ruto amekuwa naibu wa Rais Kenyatta na utakuwa wakati mzuri wa "kurudisha mkono". Lakini hili nalo lina ugiligili wake kwenye siasa za Kenya kwa sababu Wakenya wa maeneo mengine wanaweza kuona kwamba Jubilee ama hali iliyopo Kenya ni utamaduni wa kisiasa wa kubadilisha Urais kwenye jamii mbili tu - Wakikikuyu na Wakalenjin.

Kinachodhihirika ni kwamba, joto la kisiasa linavyoendelea kupanda nchini Kenya kuhusiana na uchaguzi wa mwaka wa 2022, naibu Rais William Ruto anajikuta katika hali ngumu ya kufanya maamuzi muhimu ambayo huenda yakafanikisha azma yake ya kuwania urais ama kuivunja azma