Nani anayedhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz sasa baada ya makubaliano?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Makubaliano yamefikiwa kati ya Marekani na Iran ili kumaliza mzozo katika Mashariki ya Kati.

Aidha, mazungumzo yanaendelea kati ya nchi hizo mbili ili kutekeleza makubaliano ya kudumu ndani ya siku 60 zijazo.

Njia hii ya maji imeathirika tangu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yalipoanza. Kwa kawaida, takriban asilimia 20 ya mafuta duniani hupita katika mlango-bahari huu.

Kukwama kwa usafirishaji kupitia Mlango-bahari wa Hormuz kumesababisha kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta na gesi duniani; hali hii imeshuhudiwa hapo awali wakati wa vita ambapo Iran na Marekani zilishambuliana meli au kuwekeana vikwazo vya kuzuia usafirishaji.

Mambo 14 ambayo Marekani na Iran zimekubaliana kuhusiana na makubaliano hayo pia yanajumuisha suala la Mlango-bahari wa Hormuz.

Suala la nne na la tano la Mkataba wa Makubaliano unaozungumziwa kati ya nchi hizo mbili ni kuhusiana na Mlango Bahari wa Hormuz.

Kwa mujibu wa sula la nne, Marekani "itaanza kuondoa kizuizi chake cha majini... na itamaliza kuondoa kizuizi hicho ndani ya siku 30."

Vilevile, Iran "itafanya kila juhudi kuhakikisha meli za kibiashara zinapita kwa usalama kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz kwa muda wa siku 60 bila malipo yoyote."

Mlango wa bahari wa Hormuz ni nini?

Mlango-Bahari wa Hormuz ni mlango wa bahari unaounganisha Ghuba ya Oman na Ghuba ya Uajemi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria za Umoja wa Mataifa, nchi zina haki ya kudhibiti mipaka yao ya baharini hadi maili 12 za baharini (maili 13.8) kutoka pwani zao.

Katika hatua yake nyembamba zaidi, Mlango-Bahari wa Hormuz na njia zake za meli ziko kabisa ndani ya bahari ya Iran na Oman, ndiyo maana nchi zote mbili zinaidai.

Jeshi la Iran linashikilia nguvu katika eneo hilo, na njia nyembamba zaidi za baharini ziko ndani ya maji ya Iran, ikiruhusu Iran mara nyingi kuchukua fursa ya nafasi yake ya kimkakati ya kudhibiti usafirishaji wa meli.

Kwa sababu hiyo, iliaminika pia kuwa Iran ilikuwa ikikusanya ushuru kutoka kwa meli zinazopita eneo hilo wakati wa vita, ingawa Rais wa Marekani Donald Trump alikanusha hilo.

Kama njia ya asili ya maji kupitia Iran na Oman, meli tayari hupita kwa uhuru kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz bila malipo.

Chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari, meli zimehakikishiwa kupita kwa usalama katika maji ya nchi nyingine, lakini si Iran au Marekani iliyoidhinisha mkataba huo.

Wataalamu wanasema Marekani inaamini kuwa kupita bila vikwazo kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz ni sehemu ya sheria za kimila za kimataifa.

Baadhi ya mifereji iliyotengenezwa na binadamu, kama vile Panama na Suez Canals, hutoza ushuru na ada kwa huduma fulani.

Wakati wa mzozo huo, Iran imejaribu kudai mamlaka yake juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz, ikiwa ni pamoja na kuanzisha "Mamlaka ya Mlango-Bahari wa Ghuba ya Uajemi," ambayo ilisema itasimamia "vibali vya kupita kwa usalama."

Wakati Iran ilipodai kuudhibiti Hormuz

Mwezi uliopita, Iran ilidai kwamba ilikuwa ikipanua kwa kiasi kikubwa eneo linalozunguka Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao ina udhibiti wa kijeshi, ili kuthibitisha uhuru wake juu ya njia hii muhimu ya biashara.

Ramani iliyochapishwa na "Mamlaka ya Mlango-Bahari wa Ghuba ya Uajemi" iliyoanzishwa hivi karibuni ya Iran ilidai "uangalizi wa vikosi vya kijeshi vya Iran" katika eneo la zaidi ya kilomita za mraba 22,000.

Ilienea hadi kwenye maji ya eneo la Oman na UAE, ambayo yalikuwa yamepuuza madai ya Iran ya udhibiti kama "vipande vya ndoto tu."

Mamlaka mpya ya Iran pia ilisema kwamba usafiri wote kupitia mlango-bahari "unahitaji uratibu na idhini na Mamlaka ya Mlango-Bahari wa Ghuba ya Uajemi."

Marekani na washirika wake wa Ghuba wamekataa mara kwa mara majaribio ya Iran ya kudhibiti mlango-bahari, na wameonya meli zisizingatie sheria za Iran.

Anwar Gargash, mshauri wa kidiplomasia wa rais wa UAE, alisema kwamba Iran "inajaribu kutakasa ukweli mpya uliotokana na kushindwa wazi kijeshi, lakini majaribio ya kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz au kunyakua uhuru wa baharini wa UAE si kitu zaidi ya vipande vya ndoto."

Nani anatawala sasa baada ya makubaliano?

Marekani na washirika wake wa Ghuba wamekataa mara kwa mara majaribio ya Iran ya kudhibiti mlango huo wa bahari.

Akitangaza mpango huo na Iran siku ya Jumapili, Rais wa Marekani Donald Trump alisema mkondo huo utakuwa 'bure kwa kile taifa kupita' .

Shirika la Habari la Fars la Iran liliripoti kuwa chini ya makubaliano mapya na Marekani, hatimaye Iran itasimamia Mlango-Bahari wa Hormuz kwa uratibu na Oman, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa "ada ya huduma" kwa meli zinazopita kwenye njia ya maji.

Hata hivyo, haijulikani ni kwa aina gani ya huduma ada hizo zitapaswa kulipwa.

Naveen Das, mchambuzi mkuu wa mafuta katika kampuni ya uchanganuzi ya biashara ya Kpler, aliiambia BBC kwamba mfumo wowote mpya wa malipo wa kutumia mkondo huo "utaongeza kizingiti kingine" kwa sababu ya idadi ya meli zinazoweza kupita kila siku, ambayo inaweza kusababisha "vikwazo vya vifaa au vikwazo".

Naveen Das alisema zaidi kwamba maswali mengi bado yamesalia, kama vile, "Ni nani anayeitekeleza? Je, itatekelezwa vipi? Je, ada zitakusanywa vipi? Nchi nyingine za Ghuba zina maoni gani kuhusu hilo?"

Mengi ya maswali haya yanaweza kujibiwa wakati wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani ili kuafikiana kuhusu makubaliano ya kudumu, lakini wataalamu wanasema hakuna uwezekano kwamba Tehran itaruhusu meli kupita kwenye Mlango wa Hormuz kwa uhuru kama ilivyokuwa kabla ya mapigano kuanza.

"Jambo muhimu ni kwamba wakati mlango wa bahari unaweza kufunguka haraka kutoka kwa mtazamo wa kisiasa au usalama, mfumo wa meli za kibiashara una uwezekano wa kurejea katika hali ya kawaida polepole zaidi," anasema Dimitris Ampatzidis wa Kpler.