Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Nchi iko salama - Inspekta Jenerali wa Polisi Kenya

Hata hivyo, alionya kwamba polisi watawachukulia hatua wale watakaojaribu kusababisha fujo au kuvuruga amani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Asha Juma

  1. Hali ilivyo katika maeneo mbalimbali nchi Kenya

    Vijana wameonekana wakicheza soka katika barabara ya Thika ambayo kawaida huwa nashughuli nyingi.

    Hata hivyo, imeendelea kuwa ya mshikemshike katika maeneo kadhaa nchini Kenya wakati ambapo kuna maandamano ya kuadhimisha kumbukumbu ya waliofariki wakipinga Mswada wa Fedha 2024.

    Milio ya risasi imesikika eneo la Githurai huku polisi wakiwatawanya waandamanaji. Polisi walionekana wakiwafukuza washukiwa wanaodaiwa kuwa walikuwa wakiwapora raia kwenye Barabara ya Thika.

    Ulinzi umeimarishwa mjini Embu huku polisi wakidhibiti mitaa muhimu na kuweka vizuizi kwenye njia kuu za kuingia mjini.

    Maafisa wa usalama waliendelea kuonekana kwa wingi katika eneo la biashara la katikati mwa mji huku wafanyabiashara wakifungua biashara zao kwa tahadhari kutokana na hofu ya uwezekano wa kutokea na vurugu.

    Awali, Polisi wa farasi wamewatawanya waandamanaji katikati ya jiji la Nairobi ambapo idadi kubwa ya maafisa imeendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali.

  2. Kumbukumbu ya maandamano ya Gen Z: Hali ilivyo katika Picha jijini Nairobi

  3. Inspekta Jenerali wa Polisi Kenya asema nchi iko salama

    Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, amesisitiza kuwa nchi imeendelea kuwa salama na yenye utulivu kipindi hiki cha maandamano ya kumbukumbu ya Gen Z kote nchini Kenya.

    Akizungumza na wanahabari siku ya Alhamisi, Kanja alisema kuwa vyombo vya usalama viliruhusu maandamano ya amani ya kuadhimisha miaka miwili tangu maandamano ya tarehe 25 Juni 2024 dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.

    “Nchi yetu iko salama na yenye usalama. Leo, vijana wa Gen Z walikuwa wamepanga maandamano ya kuadhimisha maandamano ya awali, na Waziri wa Mambo ya Ndani alisema kwamba hakuna mtu aliyezuiwa kufanya maandamano ya amani. Ninafurahi kuripoti kwamba nimewaona Wakenya wakifanya maandamano ya amani,” amesema Douglas Kanja.

    Hata hivyo, alionya kwamba polisi watawachukulia hatua wale watakaojaribu kusababisha fujo au kuvuruga amani.

    Jijini Nairobi, eneo la Biashara la katikati mwa jiji (CBD) lilibaki likiwa mahame huku polisi wakiongeza ulinzi na kuweka vizuizi katika barabara kuu zinazoelekea katikati ya jiji hilo.

    Soma Zaidi:

  4. Maafisa wa polisi wakamata waandamaji katikati mwa jiji la Nairobi

    Maafisa wa usalama wamewakamata wanaharakati nje ya barabara ya majengo ya Bunge wakati wa makumbusho ya pili ya Gen Z walioaga dunia katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

    Vile vile, maafisa wa usalama wameshuhudiwa katika sehemu mbalimbali za jijini Nairobi kutawanya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika kukumbuka Gen Z waliopoteza maisha miaka miwili iliyopita katika maandamano ambayo yalishtua nchi.

    Ufikiaji wa eneo la Bunge na sehemu kubwa ya biashara jijini Nairobi uliwekewa vikwazo, huku barabara zikiwa zimefungwa na vikosi vya usalama viliwekwa kwa wingi.

    Waandamanaji kadhaa walikamatwa Kitengela na Rongai, Kaunti ya Kajiado.

    Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Douglas Kanja, pamoja na maafisa wakuu wa usalama, awali walifanya tathmini ya usalama Nairobi na Kitengela na.

    Soma Zaidi:

  5. Wazazi wa waathiriwa wa maandamano ya Gen Z waomba kuweka mashada ya maua

    Wazazi wa waathiriwa wa maandamano ya Gen Z waomba kuweka mashada ya maua

    Wazazi wa waathiriwa wa maandamano ya Gen Z waliofariki dunia katika maandamano ya kupinga mswada wa Fedha wa Mwaka 2024 wameomba kuruhusiwa kuweka mashada ya maua nje ya majengo ya Bunge kwenye ua la waya lililowekwa kuzuia waandamanaji kufika eneo hilo.

    Usalama umeimarishwa katika sehemu mbalimbali za jiji la Nairobi huku wazazi wachache tu na wanaharakati wakifanikiwa kufika nje ya jengo la Bunge kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.

    Wazazi hao waliokuwa wanaongozwa na mwanaharakati wa kutetea Haki za Binadamu Hussein Khalid, waliketi chini barabarani nje ya majengo ya Bunge wakiomba kupewa ruhusa ya kuweka mashada ya maua.

    "Tafadhali polisi sisi ni wazazi. Hatuna nia mbaya. Sisi hatuna wahuni, ni wazazi peke yetu. Tunaomba muturuhusu tuweke maua tu alafu twende zetu," alisema mama wa mwathirika.

    Caroline Mutisya, ambaye mwanawe, Erickson Kyalo Mutisya, aliuawa karibu na Bunge wakati wa maandamano pia alikuwepo kwenye mkusanyiko huo.

    “Nimekuja hapa leo kumkumbuka mwanangu ambaye aliuawa mita 50 tu kutoka majengo ya Bunge na kudai haki kwa kifo chake,” aliiambia BBC.

    Mutisya alisema kuwa uwepo mkubwa wa polisi ulifanya iwe vigumu kwa familia kuzungumza kwa uhuru wakati wa maadhimisho hayo.

    “Nimekuja hapa kumkumbuka mwanangu, lakini sijisikii salama vya kutosha kueleza hisia zangu kutokana na maonyo yaliyotolewa na polisi,” alisema.

    Mzazi mwingine, Jacinta Anyango, alisema kwamba mwanawe wa miaka 12, Kennedy Onyango, aliuawa wakati wa maandamano huko Ongata Rongai, nje kidogo ya Nairobi, ambako polisi na waandamanaji walikabiliana.

    “Kitu pekee ninachotaka ni serikali iwafikishe mbele yetu maafisa waliohusika na kuwaua watoto wetu na waombe msamaha,” alisema. “Haitamrudisha mwanangu, lakini itakuwa na maana kubwa.”

    Alisema ilikuwa jambo la kusikitisha kwamba miaka miwili baadaye, hakuna mtu yeyote aliyewajibishwa kwa vifo hivyo.

    “Rais anatarajia nani atampigia kura mwaka ujao ikiwa ataendelea kutuua kwa njia hii?” alihoji kwa masikitiko.

    Mvutano ulizuka kwa muda mfupi nje ya Bunge wakati kundi dogo la wanaharakati lilipokabiliana na polisi, hali iliyosababisha watu kadhaa kukamatwa.

    Soma Zaidi:

  6. DRC kuwaweka karantini kwa siku 21 wasafiri kutoka nchi nyingine

    Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeamuru wasafiri wanaowasili kutoka maeneo yaliyoathiriwa na Ebola kuwekwa karantini kwa siku 21, baada ya mamlaka ya Ufaransa kuthibitisha daktari aliyerejea nyumbani kutoka DRC ameambukizwa ebola.

    Maafisa walisema daktari huyo, aliyetumwa sehemu ya shirika la ALIMA, alikuwa akihudumu katika kituo cha matibabu cha Rwampara huko Ituri hadi Juni 19.

    Alipitia Kinshasa kabla ya kusafiri kuelekea Ufaransa tarehe 23 Juni.

    Alipofika, alijiwasilisha kwa hiari katika kituo cha afya, ambapo vipimo vya maabara vilithibitisha kuwa ameambukizwa na virusi vya ebola aina ya Bundibugyo.

    Kulingana na Shirika la Afya Duniani na Vituo vya Kudhibiti Magonjwa vya Marekani, Ebola huambukiza mara tu dalili zinapoonekana, na maambukizi hutokea kwa kugusana moja kwa moja na maji maji ya mwili.

    Daktari huyo hakuonyesha dalili zozote akiwa Congo, lakini alizingatiwa kuwa hatarini kutokana na jukumu lake la mstari wa mbele.

    WHO +2 Kinshasa imeitaka Paris kushiriki data kwa ajili ya kufuatilia watu waliotangamana naye na kuahidi ufuatiliaji mkali kwa mujibu wa Kanuni za Afya za Kimataifa.

    Mamlaka zilisisitiza kuwa arifa huanzisha uchunguzi kamili wa magonjwa, na mawasiliano yakifuatiliwa kwa siku 21.

    Mifumo ya ufuatiliaji inasalia amilifu katika viwanja vya ndege vya Bunia na Kinshasa, ikijumuisha utambuzi, kutengwa na uthibitisho wa maabara.

    Takwimu za hivi punde zinaonyesha kesi 1,118 zilizothibitishwa, vifo 291, na waliopona 122 kote Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

    Kiwango cha vifo imefikia asilimia 26, na ufuatiliaji wa watu walioambukizwa ni asilimia 77.

    Rwampara pekee imerekodi zaidi ya maambukizo 200 na vifo 100, na kuifanya kuwa moja ya maeneo hatari zaidi.

    Maafisa wanasema hatua ya karantini inaimarisha udhibiti uliopo na inasisitiza kujitolea kwa DR Congo kukabiliana na mlipuko wake wa 17 wa Ebola.

    Unaweza kusoma:

  7. Tetemeko la ardhi ya Venezuela: Watu 32 wafariki dunia, mamia wajeruhiwa

    Ikiwa ndio mwanzo unajiunga nasi kwa mukhatasari hayo ndio yaliyojiri:

    Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.2 lilitokea kaskazini mwa Venezuela muda mfupi baada ya saa kumi na mbili jioni kwa saa za ndani siku ya Jumatano (23:00 BST), na tetemeko la pili la ukubwa wa 7.5 lilitokea chini ya dakika moja baadaye.

    • Takribani watu 32 wamethibitishwa kufariki na wengine 700 wamejeruhiwa.
    • Majengo katika mji mkuu wa nchi hiyo Caracas yameharibiwa.
    • Kuna hofu kwamba idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka. Utafiti wa Shirika la Jiolojia la Marekani unaonyesha maafa yalitokea kwa 44% kuashiria vifo zaidi ya 10,000.
    • Uwanja mkuu wa ndege nchini humo umefungwa kutokana na uharibifu, baada ya picha kuonyesha watu wakikimbia kupitia zake majengo yake wakati wa tetemeko la ardhi.
    • Marekani imeahidi kutoa msaada wa kimatibabu na wa kibinadamu - Donald Trump alielezea matetemeko hayo kuwa "makubwa sana"
    • Venezuela ilikuwa ikisherehekea sikukuu ya kitaifa Jumatano, na watu wengi walikuwa nyumbani wakati matetemeko hayo yalipotokea.
  8. Wanaharakati na viongozi wa upinzani Kenya wawakumbuka waliouawa katika maadanamano ya Gen Z 2024

    Watetezi wa haki za binadamu na wanachama wa Muungano wa Upinzani wameandamana katikati mwa jiji la Nairobi wakielekea bungeni kuweka mashada ya maua.

    Kiongozi wa PLP Martha Karua, aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwanaharakati Boniface Mwangi na Hussein Khalid ni miongoni mwa walioelekea bungeni.

    Hata hivyo, polisi wamefunga barabara kuu zinazoelekea Bunge la Kitaifa na Seneti.

    Maadhimisho ya Juni 25 yanakuja miaka miwili tangu maelfu ya Wakenya wengi wao vijana kulivunja Bunge wakati wa maandamano ya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya ushuru, katika mojawapo ya changamoto kubwa kwa mamlaka ya serikali katika historia ya hivi majuzi nchini.

    Kilichoanza kama upinzani kwa Muswada wa Fedha kilibadilika na kuwa vuguvugu pana lililochochewa na kufadhaika kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, ukosefu wa ajira, ufisadi na ukatili wa polisi na utawala mbaya.

    Maandamano hayo yaliandaliwa kupitia mitandao ya kijamii na bila uongozi rasmi wa kisiasa, na kuanzisha enzi mpya ya uanaharakati wa vijana nchini Kenya.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema zaidi ya watu 60 waliuawa wakati wa maandamano ya 2024 na ukandamizaji wa usalama uliofuata.

    Wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa 2025, watu wengine 16 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati wa maandamano mapya na mapigano na polisi.

    Waandalizi wanasema matukio ya mwaka huu hayakusudiwi tu kuwakumbuka waliofariki, bali pia kutoa wito wa kuwajibishwa kwa maafisia wa waliohusika na vifo vinavyohusiana na maandamano, majeraha na madai ya unyanyasaji wa polisi.

    Serikali ilisema itaruhusu maandamano ya amani lakini ikaonya kuwa itachukua hatua kali dhidi ya wale watakaofanya uhalifu na ghasia.

    "Kesho ni siku ya kawaida ya kazi na shule," Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen alisema kabla ya maandamano.

    "Serikali inaheshimu haki za kikatiba za Wakenya wote kukusanyika kwa amani kwa sababu yoyote ile, siku yoyote, wakati wowote.

    Watu binafsi au makundi yoyote yanayotaka kutumia maandamano halali kuzua vurugu, kufanya uporaji, kuharibu mali, kuvuruga biashara, au kufanya vitendo vyovyote vya uhalifu, hata hivyo, yatachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria," Murkomen aliongeza.

    Soma zaidi:

  9. Maandamano Kenya: Gachagua adai serikali 'inafadhili wahalifu' kuvuruga maandamano ya kumbukumu ya Juni 25

    Naibu Rais wa zamani wa Kenya Rigathi Gachagua amemshutumu Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen kwa kuandaa na kufadhili wahalifu kuvuruga maandamano ya kumbukumbu ya Juni 25.

    Gachagua amenukuliwa na vyombo vya habari vya ndani akisema matamshi ya Murkomen Jumatano, ambapo Waziri huyo alifichua kwamba alikuwa na ripoti za kijasusi zinazoonyesha wahuni walikuwa wakihamasishwa kufanya uhalifu, yalizidisha tuhuma za umma kuhusu jukumu la serikali katika vurugu zilizopangwa.

    "Nimethibitishwa. Wakenya wana kila sababu ya kuamini kwamba msimamo wangu umekuwa ukweli mtupu; tuna Waziri asiye na ufahamu zaidi anayesimamia usalama tangu uhuru," alisema Gachagua.

    Soma pia:

  10. Kombe la Dunia 2026: Afrika Kusini yafuzu raundi ya pili baada ya kuilaza Korea Kaskazini

    Bao la kipindi cha pili la Thapelo Maseko limeweka historia kwa Afrika Kusini baada ya kufuzu kwa awamu ya muondoano ya Kombe la Dunia kwa ushindi wa mara ya kwanza dhidi ya Korea Kusini dhidi ya Monterrey.

    Alama tatu zinaifanya Afrika Kusini kupanda hadi nafasi ya pili kwenye jedwali, nyuma ya Mexico, na kuiacha Korea Kusini kwa matumaini kwamba itamaliza ikiwa moja ya timu zilizo nafasi ya tatu bora.

    Afrika Kusini sasa itamenyana na Canada huko Los Angeles siku ya Jumapili.

    Maelezo zaidi:

  11. Polisi wafunga barabara kuu Nairobi wakihofia maandamano

    Polisi wameweka vizuizi barabarani na katika sehemu nyingi muhimu za kuingia katikati ya jiji la Nairobi ili kudhibiti harakati kabla ya Maandamano ya ukumbusho wa Gen Z .

    Matatu na magari ya uchukuzi wa umma yanazuiwa kuingia mjini hatua inayosababisha kukwama kwa wasafiri na usumbufu mkubwa wa trafiki.

    Baadhi Wakenya, wakiwemo baadhi ya walionusurika, wanapanga kufanya maandamano nchi nzima na kuwasha mishumaa kuwaenzi mashujaa hao.

    Maandamano ya Juni 25, 2024, ambayo yalishuhudia Bunge la Kenya kuvamiwa na waandamanaji, yameonyeshwa kama kiini cha mabadiliko yasiyoweza kufutika katika utetezi wa raia wa taifa hilo.

    Vijana wa Kenya maarufu Gen Z, walipinga Mswada wa Fedha uliopendekeza nyongeza ya ushuru kupita kiasi, kushinikiza nidhamu miongoni mwa wanasiasa na hata kuondolewa kwa Rais William Ruto na viongozi wengine.

    Miaka miwili baadaye, kumbukumbu za Juni 25 zinaendelea huku familia za takribani watu 19 waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga ushuru zikisubiri haki.

    Mnamo 2025, Wakenya waliadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa maandamano ya Gen Z, tukio ambalo lilisababisha vifo vya watu wengine 16 kutokana na majeraha ya risasi na majeraha ya yaliyotokana na hatua ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na maandamano hayo.

    Soma zaidi:

  12. Kombe la Dunia 2026: Morocco yafuzu kwa hatua ya 32 kwa ushindi wa kusisimua dhidi ya Haiti

    Achraf Hakimi na Ismail Saïbari walifunga mabao ya kipindi cha kwanza na Soufiane Rahimi na Yassine Jassim waliongeza mabao ya kipindi cha pili na Morocco kupata ushindi mnono wa 4-2 dhidi ya Haiti mapema Alhamisi na kufuzu kutoka Kundi C hadi hatua ya 32 kwenye Kombe la Dunia.

    Brazil, ambao walipata nafasi ya kwanza katika kundi kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Scotland pia wamefuzu hatua ya 32.

    Morocco na Brazil tayari walikuwa karibu sana kufuzu baada ya kila mmoja wao kujisanyia alama nne wakati wa mechi mbili za kwanza, na kila mmoja wao alicheza mechi yake ya raundi ya tatu kwa lengo la kupata kufuzu na kunyakua uongozi.

    Wakati huo huo Qatar iliaga Kombe la Dunia la 2026 siku ya Jumatano, kwa kufungwa 1-3 na Bosnia na Herzegovina mjini Seattle, huku Uswizi ikiifunga Canada, moja ya nchi mwenyeji, 2-1 mjini Vancouver, na timu zote mbili zilifuzu kwa hatua ya 32 kutoka Kundi B.

    Qatar ilihitimisha ushiriki wake wa pili katika Kombe la Dunia—baada ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2022—ikiwa na pointi moja, nyuma ya Bosnia na Herzegovina (4), ambao nafasi yao ya kufuzu hatua ya timu 32 bora kama mojawapo ya timu nane bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu imeimarika; huku Uswisi (7) ikiongoza kundi hilo mbele ya Canada (4), ambayo ilishika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao dhidi ya Bosnia.

    Soma zaidi:

  13. Italia yamkosoa Katibu Mkuu wa NATO baada ya Marekani kutumia kambi za Italia katika vita na Iran

    Italia ilikosoa matamshi ya Katibu Mkuu wa NATO kuhusiana na jeshi la Marekani kutumia kambi za kijeshi nchini Italia katika vita na Iran.

    Akijibu ukosoaji wa Donald Trump kwamba washirika wa NATO hawakuunga mkono Marekani vya kutosha, Mark Rutte aliiambia Fox News kwamba Ulaya imekuwa "jukwaa kwa Marekani kuonyesha na kutumia nguvu."

    "Ndege mia tano za Marekani ziliruka kutoka kambi za Marekani nchini Italia ili kusaidia Operesheni Epic Fury.

    Kwa hiyo msaada wetu ulikuwa mpana sana," alisema. Bw. Rutte pia alisema wakati wa vita, kati ya wanajeshi 4,000 na 5,000 walisafirishwa na ndege za Kimarekani kutoka kambi za Ulaya.

    Lakini Wizara ya Ulinzi ya Italia inasema katika taarifa kwamba matamshi hayo yaliwakilisha "picha ya kupotosha kabisa" kwa sababu hayatofautishi kati ya aina za ndege.

    Wizara hiyo ilisisitiza kuwa Italia iliidhinisha tu safari za ndege za "kiufundi, vifaa, na zisizo za kijeshi" za Marekani ndani ya mfumo wa makubaliano yaliyopo na Marekani, na "katika hali ambapo maombi yalifanywa nje ya mfumo huu, kama inavyojulikana, Italia haikutoa idhini."

    Serikali ya Italia imesisitiza kuwa haijaidhinisha matumizi ya maeneo yake na vituo vyake kwa misheni ya moja kwa moja ya kijeshi ya Marekani katika vita na Iran, na kwamba jukumu lake lilikuwa tu kwa msaada wa kiufundi na vifaa.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Trump: Iran inapaswa kukubaliana na kila kitu ninachotaka

    Katika taarifa zake za hivi punde, Rais wa Marekani amesema kuwa, ameridhishwa na mchakato wa maelewano kati ya Iran na Marekani.

    "Nani angefikiria hili lingetokea? Huu ni wakati wa vita na Iran ina tabia nzuri sana. Wanakubali kila kitu ninachouliza na wanapaswa kufanya. Vinginevyo, tutarudi tu na kufanya kile kinachohitajika," Bw. Trump aliwaambia waandishi wa habari, akizungumzia bei ya mafuta inayokaribia $ 70 kwa pipa.

    Katika siku za hivi karibuni, kufuatia mkutano wa timu za mazungumzo za Marekani na Iran nchini Uswizi, ambao ulisuluhishwa na Pakistan, maafisa kutoka nchi zote mbili wametoa kauli kali na zinazokinzana.

    Soma zaidi:

  15. Marekani kuiuzia Uturuki injini za ndege za kivita zenye thamani ya mamilioni ya dola

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, utawala wa Rais wa Marekani Donald

    Trump unanuia kusonga mbele na mpango wa kuiuzia Türkiye makumi ya injini za ndege zenye thamani ya mamia ya mamilioni ya dola.

    Hatua hiyo, ambayo inafanywa licha ya upinzani kutoka kwa Congress, ni maendeleo makubwa kwa Ankara kabla ya mkutano wa kilele wa NATO mwezi ujao, vyanzo vinne vinavyofahamu suala hilo viliiambia Reuters.

    Injini hizi, zinazotengenezwa na General Electric, zitatumia Qa'an, ndege ya kwanza ya kivita ya Türkiye.

    Türkiye, kama mwanachama wa NATO, alianza mradi huu mkubwa mwaka wa 2016 ili kujitegemea zaidi ulinzi.

    Chanzo kimojawapo kilisema dili hilo litakuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 700 na linatarajiwa kukamilika ndani ya siku chache zijazo.

    Soma pia:

  16. Kwa picha: Hofu na wasiwasi katika mitaa ya Caracas

    Picha zilizopigwa saa chache tbaada ya kutokea kwa tetemeko hilo zinaonyesha wakaazi wakiwa wamekusanyika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Venezuela, baada ya nyumba zao kuporomoka na umeme kukatika.

    Wengine wanaonekana wakiwakumbatia ndugu na jamaa zao, huku maafisa wa waokoaji wakipekua vifusi kuwatafuta walionaswa.

    Mamlaka zinahofia tetemeko hilo limesababisha uharibifu mkubwa, lakini kiwango kamili cha uharibifu bado hakijajulikana.

  17. Matetemeko makubwa ya ardhi yakumba Venezuela na kuangusha majengo Caracas

    Mji mkuu wa Venezuela Caracas, umekumbwa na matetemeko mawili makubwa yaliyoachana kwa sekunde chache.

    Tetemeko la kwanza lilikuwa la ukubwa wa 7.2 lililotokea katika eneo la Montalbán, magharibi kidogo mwa Caracas, kulingana na shirika la ufuatiliaji wa Utafiti wa Jiolojia wa Marekani (USGC).

    Sekunde 39 baadaye, tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.5 lilipiga takriban kilomita 10 ndani ya eneo hilo.

    Matetemeko hayo yametajwa kuwa moja ya mitetemeko mikubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo ya Amerika Kusini katika karne moja.

    Majengo yaliporomoka na wakaazi kukimbilia barabarani kutafuta usalama wakati matetemeko ya ardhi yalipotokea.

    Rais wa mpito wa Venezeula Delcy Rodríguez ametangaza hali ya hatari.

    Kuna hofu ya majeruhi na uharibifu mkubwa lakini hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusiana na hilo kufikia sasa. Waokoaji wako mbioni kuwatafuta manusura ambao huenda wamenaswa chini ya vifusi.

  18. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.