Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Achana na kadi ya njano au kadi nyekundu unaijua kadi nyeupe iliyoanza kutumika katika soka duniani?
Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili
Hakuna asiyejua kuhusu kadi nyekundu ama kadi ya njano katika mchezo wa soka. Kwa wengi wanaofuatilia soka, kadi nyekundu inafahamika zaidi kwa kuwa hupewa mchezaji ambaye aameonyesha mchezo usio wa kiungwana kama kucheza rafu mbaya, kushika mpira kwa makusudi, kutukana na mengine. Inawahusu pia hata benchi la ufundi.
Kadi ya njano yenyewe inatumika kuonya mchezaji ama bechi la ufundi ama yeyote anayehusishwa na mchezo kwa makosa madogo madogo ya uwanjani ama nje ya uwanja.
Kadi hizi zilianza kutumika miaka zaidi ya 50 iliyopita ikitambulishwa kwa mara ya kwanza kwenye kombe la dunia la mwaka 1970 lililofanyika nchini Mexico ili kupunguza rafu uwanjani zilizoanza kuongezeka katika mechi nyingi za soka wakati huo.
Lakini Januari 21, 2023 imekuwa siku ya kihistoria kwa kadi nyingine ya tatu kuanza kutumika, ni kadi nyeupe.
Imeanza kutumika rasmi kwa mara ya kwanza katika historia ya soka duniani kwenye mchezo wa kombe la ligi huko Ureno kwa timu za wanawake kati ya Sporting Lisbon na Benfica.
N kitu kikubwa kilichofikiriwa kwa muda sasa, lakini inamaanisha nini hasa?
Kadi nyeupe na tafsiri yake
Rangi nyeupe ina maana na uhusiano kadhaa wa kadhaa, ingawa maana zinaweza kutofautiana kulingana na mtu binafsi na tamaduni wanazoishi nazo.
Lakini tafsiri isiyo rasmi kuhusu rangi nyeupe iliyozoeleka mara nyingi rangi nyeupe inawakilisha usafi, kutokuwa na hatia na unyenyekevu.
Hili la unyenyekevu ndilo hasa linalohusisha kwa namna yake kadi nyeupe iliyoanza kutumika katika mchezo wa soka duniani.
Kadi nyeupe inaonyeshwa kutambua na kuhamasisha 'fair play' au uungwana, mchezo mzuri ama jambo zuri katika mchezo wa soka na "imewekwa maalumu kuboresha na kuimarisha nidhamu katika mchezo wa soka", anasema Shaban Shomvi, mmoja wa wacheza soka wa zamani wa Tanzania.
Huko nyuma mchezo mzuri ama jambo zuri la kiungwana katika mchezo huo lilitambuliwa baadaye kwa tuzo kutolewa kwa timu fulani ama mchezaji ama mdau yeyote wa soka, lakini sasa kadi hii itaanza kutambua hilo hapo hapo uwanjani wakati mchezo ukiendelea.
Tukio gani lilisababisha kadi nyeupe kutolewa kwa mara ya kwanza?
Sporting Lisbon na Benfica ni timu hasimu nchini Ureno, ziwe zinakutana timu za wanaume ama wanawake, mechi baina ya timu hizi huwa na upinzani mkali na wakati mwingine uleta vurugu ndani na nje ya uwanja.
Pengine muamuzi Catarina Camposwa aliyechezesha mchezo huo uliozikutanisha timu hizi katika mchezo wa robo fainali ya Taca de Portugal cup kwa wanawake uliopigwa Januari 21, 2023 mjini Lisbon aliona umuhimu wa kuwa nayo na kuitoa kwa sababu ya asili ya upinzani uliopo. Lakini kwa aina ya mchezo huo kuyapata matukio ya 'kiutu' yanayostahili kadi nyeupe iliwezekana.
Mchezo ukiwa unaendelea mmoja wa mashabiki alijisikia vibaya' kuumwa', ikalazimu madaktari wa timu zote mbili kukimbilia jukwaani kumsaidia kuokoa maisha ya mgonjwa huyo, kitendo hicho kilionekana ni cha kiungwana, kimichezo na cha kiutu, kilichomfanya refa au muamuzi Camposwa kuwapa kadi hiyo nyeupe madaktari wa pande zote mbili. Historia ikaandikwa.
Benfica ilishinda mchezo huo kwa mabao 5-0 mjini Lisbon. Lakini ushindi huo wala sio jambo linalozungumzwa, kinachozungumzwa ni kadi nyeupe na uungwana wa madaktari hao wa timu hizo.
Wadau wamepokeaje kadi hii?
Kama ilivyokuwa kwenye michuano ya kombe la dunia lililofanyika Qatar mwezi uliopita, ambapo Shirikisho la soka duniani (FIFA), lilikuwa linaongeza muda wa nyongeza mpaka dakika 10 ili kufidia muda unaopotezwa kwa makusudi na wachezaji, kadi nyekundu pia imepokelewa kwa hisia tofauti lakini kwa ujumla inaonekana kuungwa mkono zaidi.
Wengine kwenye mitandao wamekuwa na mitazamo ya namna hii lakini wapo pia wanaoipinga, mmoja wao ni Neil Fissler, mwandishi wa habari za michezo mahiri Uingereza akisema ni wazo lisilo na maana kwenye historia ya soka.
Lakini wanaounga mkono wanasema ni jambo la kubebwa. 'Nidhamu popote pale iwe uwanjani nje ya uwanja, nyumbani, shuleni hata makazini ni jambo la msingi sana, kadi nyeupe kutumika kila mahali ni msingi wa kuimarisha nidhani', anasema Seif Shangali, mdau wa soka Tanzania na kuongeza' ni muda wa FIFA na nchi wanachama kuifikiria na kuitengenezea sheria na kanuni'.
Nani kaileta na lini itaanza kutumika kwenye ligi kubwa duniani?
Mwaka 2014, aliyekuwa rais wa shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA) Michel Platini aliwahi kutoa wito wa kuanzishwa kwa kadi nyeupe lakini yeye alitaka itumike kama adhabu kwa wachezaji ambao wanakuwa wakorofi uwanjani na kadi hiyo inampa nguvu muamuzi kumtoa mchezaji wa aina hiyo nje kwa dakika 10 kabla ya kumrejesha.
Hiyo ni mbali na kadi ya njano na nyekundu ambayo anaweza akapewa kadi hizo akirejea na kutenda madhambi yanayostahili kadi hiyo.
Hata hivyo wazo lake hilo halikufika popote. Kwa ujumla lilikutana na upinzani mkali na kwa wale waliopinga walionyesha kwamba ni kadi ambayo ingeuwa nguvu ya kadi ya njano, lakini pia ingempa muamuzi asiye muaminifu upenyo wa kuitumia kadi hiyo na kuacha nyingine kwa manufaa ya mahaba yake kwa timu ama mchezaji.
Waliopinga walikuwa na hoja kuwa ni bora kadi nyeupe itambulishe 'fair play' ili kuboresha nidhamu katika soka. Na sasa tunaanza kushuhudia hili likianzia Ureno, moja ya nchi wanachama wa UEFA.
Ni wazi haitaanza kutumika hivi karibuni katika ligi kubwa duniani kama za England, Ujerumani, Hispania, Ufaransa na Italia, lakini kuanzishwa kwake Ureno kutazishtua mamlaka za soka za kimataifa kama UEFA na FIFA, kufikiria upya suala hilo.
Kanuni za FIFA ni muongozo wa kanuni za mataifa wanachama. Hivyo kama FIFA italibeba hili na vyama vya mabara kama UEFA kwa Ulaya, CAF kwa Afrika na vyama vya mabara mengine, huenda siku moja tukashuhudia kadi nyeupe kwenye mifuko ya kila refa au muamuzi duniani.