Moto wa harusi ya Iraq: 'Ni kama lango la jehanamu lilifunguka'

Iliyochapishwa

Takriban watu 100 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mkasa wa moto uliotokea kwenye sherehe ya harusi huko Qaraqosh kaskazini mwa Iraq. Watu walioshuhudia tukio hilo wameelezea BBC matukio ya kushtua wakati moto huo ukishika kasi.

Ghaly Nassim mwenye umri wa miaka 19 alikuwa mita chache tu kutoka kwenye jumba la karamu la al-Haitham wakati moto huo ulipozuka Jumanne jioni.

Alikimbia kwenda kuwasaidia marafiki zake watano waliokuwa wamenaswa mle ndani.

"Mlango mmoja ulikuwa umefungwa, kwa hivyo tuliufungua kwa nguvu. Moto mkubwa ulitoka nje ya ukumbi. Ilikuwa kama milango ya jehanamu ilifunguliwa," alisema.

"Hali ya joto ilikuwa isiyostahimilika. Siwezi kuelezea joto kali lililotupiga."

Takriban watu 94 waliuawa na wengine 100 kujeruhiwa katika moto huo, ambao ulizuka wakati wa densi ya kwanza ya bibi na bwana harusi. Maafisa wa ulinzi wa raia waliambia BBC Idhaa ya Kiarabu kwamba wanandoa hao walinusurika, ingawa ripoti za awali zilisema walikuwa wameangamia.

Bw Nassim alielezea matukio hayo kama "msiba halisi".

"Sikuweza kufanya chochote isipokuwa kukimbia kutoka kwa moto," alisema, akionekana kuishiwa nguvu kwenye laini ya simu.

"Baada ya wazima moto kufika, nilikimbilia ndani kuwatafuta marafiki zangu. Niliona maiti 26 zikiwa bafuni. Msichana wa miaka 12 alikuwa ameungua kabisa na kuachwa kwenye kona."

Msemaji wa vyombo vya habari vya Ulinzi wa Raia wa Iraq, Gawdat Abdul Rahman, aliiambia BBC kwamba moto huo ulisababishwa na fataki zilizorushwa ndani ya ukumbi katika mji wa Wakristo wengi.

Utumiaji wa nyenzo za ujenzi zinazoweza kuwaka sana ndani ya ukumbi ulifanya kama kichochezi, aliongeza.

Bw Nassim anaamini kwamba ukosefu wa milango ya kutoka kwa dharura ulifanya mambo kuwa mabaya zaidi, kwani wageni wengi walijaribu kuondoka wakitumia lango kuu la ukumbi, na pengine kusababisha watu wengi kubabaika.

Imeharibiwa 'kwa dakika'

Alisema marafiki zake walikuwa wamehesabiwa na walikuwa salama.

Mmoja wao, Tommy Uday mwenye umri wa miaka 17, alikuwa amesimama karibu na njia ya kutokea wakati moto ulipozuka. Hatua iliyomwezesha kutoka haraka.

"Niliona wingu kubwa jeusi la moshi likitoka kwenye dari, kwa hivyo nilitoka nje haraka," alisema, akiongeza kuwa "mahali penyewe paliharibiwa kwa dakika tano tu".

Takriban miili 50 ilizikwa siku ya Jumatano. Miili iliyosalia inatarajiwa kuzikwa leo Alhamisi. Lakini baadhi ya watu bado wanatafuta jamaa zao.

Ghazwan alitenganishwa na mkewe mwenye umri wa miaka 33, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne na binti wa miaka 13 wakati moto huo ulipozuka.

Binti yake mwingine, ambaye ana umri wa miaka 10, alitoka nje ya ukumbi "mwili wake ukipata majeraha ya moto kwa 98%", dadake Ghazwan Eisan aliambia BBC.

Alisema kuwa kaka yake alikuwa akizunguka hospitali moja hadi nyingine kutafuta jamaa wako wengine.

Hospitali zinahangaika

Ndani ya kituo maalumu cha matibabu cha walioungua mjini Mosul, Dkt Waad Salem aliambia BBC takriban 60% ya waliojeruhiwa waliungua vibaya sana.

"Wengi walipata majeraha ya moto usoni, kifuani na mikononi," alisema na kuongeza kuwa wanawake na watoto ni miongoni mwa walioathirika zaidi.

Muuguzi Mkuu Israa Mohammed aliwatibu majeruhi usiku kucha. Aliiambia BBC kuwa alihudumia takriban wagonjwa 200.

"Nilichoona kilikuwa kigumu na cha kusikitisha sana," alisema.

“Nimeona watu ambao zaidi ya asilimia 90 ya miili yao imiteketea kabisa,” alisema na kuongeza kuwa watoto wasiopungua 50 walithibitishwa kufariki mara tu walipofika hospitalini.

Bi Mohammed alisema kituo chake cha matibabu hakina vifaa vya matibabu na kinatatizika kustahimili wimbi kubwa la waathiriwa.

Kwa wengine kama Bw Nassim na marafiki zake, itakuwa vigumu sana kuondosha mshtuko ambao wameshuhudia.

"Siwezi kuelezea kile nichonahisi," alisema. "Ninafahamu familia ambazo zilipoteza karibu kila mtu. Karibu familia tatu zimepoteza angalau jamaa mmoja katika moto huo. Jamii nzima ina huzuni, sio tu katika jimbo la Ninawi, lakini kote Iraq. Nchi nzima ina huzuni."