Mama wa watoto 4 aliyetafuta penzi juu chini kabla ya kuvunjwa moyo

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

"Niliutoa mwili wangu kwa wanaume kingono mara nyingi nikitafuta kupendwa, hata nilikuwa na toa fedha zangu nipendeke ila nilichokipata ni moyo kuumizwa hata zaidi, simulizi la Grace Destiny.

Grace Destiny ni mama wa watoto wanne na mtoa ushauri nasaha kutoka nchini Kenya.

Lakini hakuanzia hapo kwani anapoangalia nyuma alikotoka maishani mwake hana budi ila kuwa kielelezo katika jamii hususan kwa wanawake ambao wana dhana kuwa ilikuonyesha mwanamume unamvyompenda lazima ushiriki ngono nae.

Ikiwa tunakaribia kusherehekea siku ya wapendanao maarufu kama 'Valentine' Ijumaa hii anakumbuka jinsi ujana wake ulivyokumbwa na pandashuka ya kutafuta penzi ambalo mara nyingi lilimuacha na machungu!.

Shida kuu ya Grace ilianza akiwa msichana mwenye umri wa miaka minne kama alivyoeleza;

"Mama na baba yangu walitengana nikiwa na umri huo, babangu alikuwa ni kipenzi changu kwa hio walipotengana nilihisi kana kwamba penzi langu lilinitoweka", Grace alisema.

Alipokuwa anabalehe akiwa na umri wa miaka 14 Grace alihisi akiwa na upweke mwingi sana kwani anasema kuwa uhusiano wake na mama yake mzazi wakati huo haukuwa wa karibu mno na alichokifanya ni kukimbilia kutafuta mapenzi kutoka kwa wanaume.

Lakini kulingana na simulizi yake, alijitoa kwa moyo wake wote, mwili wake na hata mawazo yake. Tofauti na alichokuwa anatarajia, matokeo yake yalikuwa ni kuvunjika moyo, kutumiwa kimwili na kujihisi kana kwamba yeye ni mchafu mno.

Kwa hio akiwa na miaka 14 aliacha kusoma kwa muda, anasema haya yalifanyika baada ya mamake kujiunga na dhehebu mmoja ambalo lilikuwa na imani potofu ya kuwa elimu haifai mtu akiwa kwa dini hio; kwa hio wakati huo yeye na dadake waliacha shule na kuanza kazi za kawaida za kijini kama vile kulima.

"Mimi sikuwa napenda kulima hata kidogo kwa hio nilitafuta kila sababu nisiwe shambani. Mamangu alikuwa anamgawanyia kila mmoja wetu hekari moja na nusu kulima" Grace aliongeza.

Grace anakumbuka kuwa kutokana na hatua ya mamake mzazi kuingia kwenye dhehebu hilo, alianza kuhisi kana kwamba Mwenyezi Mungu hampendi kwa kuwa aliachishwa shule kutokana na imani za kidini.

Basi akiwa na umri wa miaka 14 aliamua kutoroka nyumbani na kuanza kuishi na jamaa zake kama vile shangazi, kesho kutwa kwa mjomba na baada ya muda alijikuta kwa shangaziye mmoja ambaye alikuwa pia kwenye dhehebu hilo.

Anakumbuka kuwa wakati akiwa kwa shangazi yake, walihudhuria harusi mmoja kule kijijini na kwa kuwa walikuwa vijana nyakati za usiku vijana walijitenga na kuwa na wasaa wa kusifu na kuimba, mara alijikuta akiwa amesalia na kijana mmoja huku wenzake wakiondoka mmoja baada ya mwengine.

Ilikuwa usiku wa manane alijikuta amelala chumba kimoja na kijana huyo na kama anavyosema walishiriki ngono usiku huo kwa mara mmoja tu ilikuwa ni mwaka wa 1995.

Baada ya mwezi mmoja aligundua kuwa alikuwa ameshika mimba na alipomueleza yule kijana mambo yote yaliporomoka kwani juhudi zake za kutumai kuwa angeolewa ziliambulia patupu.

"Wakati nilipokuwa namweleza yule kijana kuhusu uja uzito wangu mamake mzazi alitusikia tukigombana kwa hio alinikaribia na kunieleza kuwa hataki kuniona katika boma lao na hakuna mjadala wa hilo zaidi ya ila kuondoka tu. Niliogopa kurudi nyumbani kwani nilifikiria kuwa mama yangu angenimaliza'', Grace alisema.

Grace aliamua kukodisha chumba kimoja na kuanza maisha. Wakati huo aliamua kufanya vibarua vidogo vidogo vya kulima mashamba ya watu kwa miezi 7 hadi wakati alipojifungua.

Lakini kabla ya kujifungua wakati akiwa na uja uzito wa miezi 8 baba yake mzazi aliyekuwa anaishi Marekani alirejea nchini Kenya na alipopata fursa ya kukutana naye babake alishutuka sana kumuona binti wake akiwa na mimba.

Baba yake alisikitika na wakiwa katika mazungumzo yao, Grace alimweleza kuwa alikuwa na matumaini ya kurejea shuleni baada ya kujifungua mtoto. Jambo ambalo babake mzazi alilikubali na baada ya kujifungua alimlipia karo ya kurejea shule.

Kurejea kwake shuleni hakukuwa kurahisi kwani alikuwa mama na mwanafunzi baadhi ya wanafunzi wenzake walikuwa wanamkejeli mno.

Baada ya kumaliza shule ya upili bado Grace aliendelea kuhangaishwa na haja ya kupendwa au kupendeka hususan na mwanaume tu. Anakiri kwamba kwa kukosa penzi lile la babake mzazi kila wakati alijikuta akitamani penzi la wanamume, hadi ikafikia wakati anatumia fedha kumpatia mpenzi wake pesa ili azidi kumpenda na kukaa naye.

"Nakumbuka kuwa mimi sikuwa na fedha nyingi ila kidogo nilichokuwa nacho nilikuwa nikama nanunua mapenzi kwani nilikuwa nawapatia pesa sana ", Grace alisema.

Grace anasema kuwa sio mara mmoja au mbili ametoa pesa kwa wanaume ambao ni wapenzi wake lakini alichokuwa anasalia nacho ni kuwa wengi wa wapenzi hao walikula pesa zake na mwishowe wakamtonesha kidonda cha penzi lake na kumuacha mpweke.

Hakutoa hesabu kamili ya wanaume ambao ameshiriki nao ngono ila anakiri ni wengi na anasema kuwa kila wakati alitaka tu awe katika mahusiano ya kimapenzi ila kila wakati yalikuwa yanaisha ghafla bin vuu.

Kupitia panda shuka za kutafuta penzi la mwanamume ilifika wakati ambapo Grace aligundua kuwa hangaiko lake kubwa lilitokana na kuwachwa na baba yake mzazi. Alikosa kujipenda na kujithamini ndiposa alikuwa anashiriki ngono na kila mwanamume aliyeonyesha dalili za kuwa na haja na yeye kimapenzi.

Habari njema ni kuwa miaka kadhaa baadaye Grace Destiny na babake mzazi walirejesha uhusiano wao wa mzazi na binti wake, pia grace alianza huduma za kutoa nasana nchini Kenya na kwa sasa anashughulika mno na kutoa nasaha kwa wapenzi hususan kwa wanawake.

Ujumbe wa Grace ni kwamba watu wajipende na wajifahamu pili anaamini kuwapenzi la kweli halisukumwi na tamaa za kimwili kama ngono pekee yake.

Anaonya wanawake wasiwe wa haraka wakati penzi linapoanza badala yake wachukue muda kabla ya kuanza mahusiano ya kimapenzi.