Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran na Marekani zakubaliana kusitisha mashambulizi na kufanya mazungumzo Doha - Axios

Kwa mujibu wa Axios Marekani na Iran zinatarajiwa kukutana mjini Doha siku ya Jumanne kutafuta suluhu ya tofauti zao kuhusu Mlango wa Hormuz.

Moja kwa moja

Mariam Mjahid, Lizzy Masinga

  1. Gen Z maarufu kwa kauli ya "Mr Speaker Sir" afikishwa mahakamani kwa kesi ya uvamizi wa Bunge

    Ezekiel Kyama Nzoki, mwanaharakati wa maandamano ya Gen Z anayefahamika kwa kauli ya "Mr Speaker Sir," alifika mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Milimani, Caroline Mugo, Jumatatu, ambapo alikana mashtaka yanayohusiana na maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha wa Juni 25, 2024.

    Kwa mujibu wa mahakama, Nzoki anakabiliwa na shtaka la kuharibu mali katika Majengo ya Bunge kwa makusudi akiwa pamoja na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani.

    Hati ya mashtaka inaeleza kuwa:

    "Ezekiel Kyama Nzyoki, mnamo Juni 25, 2024, katika Majengo ya Bunge ndani ya Kaunti ya Jiji la Nairobi, akiwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, aliharibu kwa makusudi na kinyume cha sheria sehemu za jengo, uzio wa eneo la Bunge, mlingoti wa bendera katika Mausoleum, samani, vifaa vya TEHAMA na skrini za televisheni, vifaa vya jikoni, magari na mifumo ya umeme, vyenye thamani ya shilingi 41,248,570, mali ya Tume ya Huduma za Bunge."

    Nzoki aliachiliwa kwa dhamana binafsi ya Shilingi 100,000 akisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hiyo.

    Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, alifika mahakamani na kumwakilisha Nzoki wakati wa kesi hiyo.

    Nzoki alijulikana sana wakati wa maandamano ya Gen Z baada ya kusambaa kwa video zilizomuonesha akiwa ndani ya ukumbi wa Bunge la Taifa wakati wa uvamizi wa waandamanaji waliokuwa wakipinga Muswada wa Fedha wa 2024.

    Unaweza kusoma;

  2. Kocha wa Korea Kusini ajiuzulu huku rais akiagiza uchunguzi kufuatia kutolewa Kombe la Dunia

    Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Korea Kusini, Hong Myung-bo, amejiuzulu baada ya timu hiyo kushindwa kufuzu hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia.

    Timu hiyo ilikuwa na matumaini ya kusonga mbele kama moja ya timu bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi, lakini matumaini hayo yalitoweka Jumamosi baada ya matokeo ya timu nyingine kukamilika.

    Kuondolewa mapema kwenye mashindano hayo kumezua ukosoaji mkubwa nchini Korea Kusini, huku Rais Lee Jae Myung akiagiza uchunguzi kufanyika kubaini sababu za timu hiyo kufanya vibaya.

    Hong aliomba radhi kwa mashabiki Jumapili na kusema kuwa jukumu la matokeo hayo "linabebwa kikamilifu na mimi kama kocha mkuu."

    Korea Kusini, ambayo ipo nafasi ya 32 katika viwango vya FIFA kwa soka la wanaume na inaongozwa na nyota Son Heung-min, ilipata ushindi mmoja na kupoteza mechi mbili katika Kombe la Dunia, ikimaliza nyuma ya Mexico na Afrika Kusini, ambazo zinashika nafasi ya 15 na 60 mtawalia katika viwango vya FIFA.

    Ukosoaji dhidi ya Hong uliongezeka haraka baada ya Korea Kusini kupoteza bao 1-0 dhidi ya Afrika Kusini Alhamisi.

    Kipigo hicho kiliifanya Korea Kusini kumaliza katika nafasi ya tatu ya Kundi A. Hata hivyo, timu hiyo bado ilikuwa na matumaini ya kufuzu kupitia sheria mpya iliyoanzishwa kufuatia kuongezwa kwa timu za Kombe la Dunia kutoka 32 hadi 48, ambayo inaruhusu timu nane bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu kufuzu hatua ya mtoano.

    Lakini Jumamosi, matumaini hayo yalifutika baada ya matokeo ya mwisho ya makundi mengine kuthibitisha kuondolewa kwao.

    Mashabiki wengi wanamlaumu Hong, ambaye ameinoa timu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita. Jumatatu, kundi rasmi la mashabiki wa timu ya taifa, Red Devils, lilitoa taarifa likimtaka Hong "apige magoti mbele ya taifa zima na aondoke kabisa katika ulimwengu wa soka."

    Unaweza kusoma;

  3. Watu 14 wafariki katika ajali ya helikopta Saudi Arabia

    Watu 14 wamefariki dunia baada ya helikopta kuanguka nchini Saudi Arabia, vyombo vya habari vya serikali viliripoti Jumapili.

    Helikopta hiyo, inayomilikiwa na kampuni kubwa ya mafuta ya serikali ya Aramco, ilianguka katika mji wa pwani wa Ras Tanura mashariki mwa nchi saa 12:00 asubuhi kwa saa za eneo hilo (03:00 GMT), na kusababisha vifo vya watu wote waliokuwa ndani yake, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudia (Saudi Press Agency).

    Shirika hilo lilisema kuwa waathiriwa wote 14 walikuwa raia wa Saudi Arabia, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo.

    Kampuni ya Aramco haikutoa tamko lolote mara moja kuhusu tukio hilo.

    Wizara ya Nishati ya Saudi Arabia imetoa salamu za pole kwa familia za waathiriwa.

    Mji wa Ras Tanura unahifadhi moja ya viwanda vikubwa vya kusafisha mafuta vinavyomilikiwa na Aramco, ambavyo ni miongoni mwa vikubwa zaidi katika Mashariki ya Kati.

    Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa Aramco ilirejesha shughuli za upakiaji wa mafuta ghafi katika eneo hilo Ijumaa, baada ya kusimamishwa kwa karibu miezi minne kutokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.

  4. Takribani watu 30 wameuawa kwa mashambulizi ya Pakistan, Taliban yasema

    Pakistan ilianzisha mashambulizi ya anga na kutuma wanajeshi wa ardhini katika majimbo ya Afghanistan yaliyo mpakani siku ya Jumapili, na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

    Kwa mujibu wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan, takribani raia 36, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa huku zaidi ya watu 160 wakijeruhiwa.

    Serikali hiyo imeyalaani mashambulizi hayo na kuyataja kuwa "kitendo cha woga" pamoja na "uhalifu na ukatili."

    Waziri wa Habari wa Pakistan, Attaullah Tarar, alisema kuwa wanamgambo 29 waliuawa katika mashambulizi yaliyolenga maficho yao. Aliongeza kuwa mashambulizi hayo yalikuwa jibu kwa "mashambulizi ya hivi karibuni ya kigaidi dhidi ya watu wasio na hatia."

    Kwa muda mrefu, Pakistan imekuwa ikiishutumu Afghanistan kwa kuwahifadhi makundi ya kigaidi yanayofanya mashambulizi ya kuvuka mpaka. Hata hivyo, serikali ya Taliban imekuwa ikikanusha madai hayo.

    Unaweza kusoma;

  5. DR Congo yapiga marufuku mikusanyiko ya umma katika maeneo hatarishi ya Ebola

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza marufuku ya mikusanyiko ya umma katika majimbo manne yaliyotajwa kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi ya Ebola, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo.

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Jacquemain Shabani, amesema hatua hiyo inahusu majimbo ya Kinshasa, Tshopo, Bas Uele na Haut Uele, na inajumuisha kusitishwa kwa mikutano, maandamano na mikusanyiko mingine ya watu wengi hadi itakapotangazwa vinginevyo.

    Maafisa wa serikali wanasema hatua hiyo inalenga kuimarisha udhibiti wa Ebola, wakionya kwamba harakati kubwa za watu ndani na karibu na maeneo yaliyoathirika zinaweza kuongeza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo.

    Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa hadi sasa kuna visa 1,203 vilivyothibitishwa vya Ebola na vifo 321, huku kitovu cha mlipuko huo kikiwa katika jimbo la Ituri.

    Majimbo jirani ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini pia yamewekwa chini ya uangalizi maalumu.

    Soma Zaidi Hapa:

  6. Pakistan yashambulia maeneo ya mpakani mwa Afghanistan

    Pakistan imesema imefanya mashambulizi ya anga na ardhini dhidi ya maeneo iliyodai kuwa ni maficho ya wanamgambo wa Kiislamu ndani ya mpaka wa Afghanistan.

    Waziri wa Habari wa Pakistan, Attaullah Tarar, amesema mashambulizi hayo yamefanyika katika majimbo ya Paktia, Paktika na Kunar.

    Maafisa wa Taliban nchini Afghanistan wamesema makumi ya raia wameuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.

    Mashambulizi hayo yamejiri siku chache baada ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu kushambulia kambi ya askari wa Pakistan Rangers katika mji wa Karachi kusini mwa nchi hiyo na kuwaua wanajeshi watatu.

    Islamabad imekuwa ikiishutumu serikali ya Taliban mjini Kabul kwa kuwapa hifadhi na ulinzi wanamgambo wanaoshambulia vikosi vya Pakistan, madai ambayo utawala wa Kabul umeyakanusha vikali.

  7. Polisi Uturuki wakamata zaidi ya watu 50 katika maadhimisho ya watu wa jinsi moja

    Polisi nchini Uturuki wamewakamata watu wasiopungua 50, akiwemo mwandishi wa habari, wakati wa maandamano ya kuadhimisha mshikamano na kutetea haki za watu wa jamii ya jinsi moja LGBTQ+ mjini Istanbul yaliyofanyika licha ya kupigwa marufuku na mamlaka za eneo hilo.

    Waandalizi wa maandamano hayo walisema washiriki walikusanyika katika vitongoji mbalimbali vya Istanbul na kuapa kuendelea na maandamano yao.

    Muungano wa Waandishi wa Habari wa Uturuki ulisema mmoja wa waliokamatwa ni Muberra Unsal, ambaye anamiliki kitambulisho halali cha uandishi wa habari.

    Muungano huo ulisema Unsal alikamatwa licha ya kujitambulisha mara kadhaa kuwa ni mwandishi wa habari.

    Chama cha Wanasheria cha Istanbul kilining'iniza bango kubwa kwenye jengo lake lenye ujumbe: "LGBT ni haki za binadamu."

    Ingawa uhusiano wa watu wa jinsi moja si kosa la jinai nchini Uturuki, maandamano ya kila mwaka ya kuonyesha mshikamano wa jamii hiyo yamekuwa yakipigwa marufuku na kuzuiwa karibu kila mwaka tangu 2015.

    Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amekuwa akiikosoa mara kwa mara jamii ya LGBTQ+, akiihusisha na kupungua kwa kiwango cha uzazi nchini humo.

    Polisi waliimarisha ulinzi katika eneo la Taksim Square mjini Istanbul kwa kuweka vizuizi vya chuma, huku mamlaka za eneo hilo zikipiga marufuku mikusanyiko katika maeneo muhimu ya maandamano na kuzuia huduma za usafiri wa treni katika baadhi ya maeneo ya katikati mwa jiji.

  8. Baadhi ya wanazuoni wa Iran watoa fatwa ya kutaka kuuawa kwa Trump na Netanyahu

    Mgawanyiko usio wa kawaida umeripotiwa ndani ya Baraza la Wataalamu wa Iran, chombo cha juu zaidi cha wanazuoni wa kidini nchini humo.

    Takriban theluthi mbili ya wajumbe wa baraza hilo lenye wanachama 88 walitoa fatwa ya kidini inayotaka kuuawa kwa Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

    Fatwa hiyo ilieleza kuwa ni wajibu wa Waislamu kuwaua viongozi hao wawili iwapo watapata fursa ya kufanya hivyo.

    Hata hivyo, uongozi wa Baraza la Wataalamu umeitaja fatwa hiyo kuwa "isiyo ya kawaida", ukisema maudhui yake yanahitaji mjadala na uchambuzi zaidi.

    Fatwa hiyo, iliyotolewa na wanazuoni wenye misimamo mikali, ilijumuishwa katika barua iliyotumwa kwa umma wa Iran.

    Barua hiyo pia ilisema kuwa Tehran haipaswi kukubali kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz wala kujadili mpango wake wa nyuklia katika mazungumzo na Marekani.

    Maelezo zaidi:

  9. Serikali ya Tanzania yasema kukatika kwa umeme Jumamosi kulizuia janga kubwa zaidi

    Serikali ya Tanzania imesema kukatika kwa umeme nchini kote siku ya Jumamosi kulisababishwa na mfumo wa kiotomatiki wa usalama wa Gridi ya Taifa, ambao ulijizima ili kuzuia uharibifu mkubwa zaidi wa mtandao wa umeme.

    Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Gridi ya Taifa imewekewa mifumo ya kisasa ya kidijitali ya ulinzi ambayo hujitenga au kuzima sehemu za mtandao moja kwa moja inapobaini hitilafu kubwa.

    Amesema teknolojia hiyo imeundwa kuzuia kusambaratika kwa mfumo mzima wa umeme na kulinda miundombinu muhimu.

    Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya hitilafu ya kiufundi kwenye Gridi ya Taifa kusababisha kukatika kwa umeme katika maeneo yote yaliyounganishwa na gridi hiyo.

    Hitilafu hiyo iliathiri shughuli za biashara, usafiri, mawasiliano na huduma nyingine muhimu kwa saa kadhaa, huku maelfu ya wananchi wakikumbwa na usumbufu katika shughuli zao za kila siku.

    Kwa mujibu wa Msigwa, hatua ya mfumo kujizima moja kwa moja inaonesha kuwa miundombinu ya umeme ya Tanzania imejengwa kwa teknolojia za kisasa zenye uwezo wa kubaini hitilafu na kuchukua hatua za haraka bila kusubiri uingiliaji wa kibinadamu.

    Hata hivyo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Umeme na Nishati kuunda kamati ya uchunguzi kubaini chanzo cha hitilafu hiyo na kupendekeza hatua za kuzuia tatizo kama hilo kujitokeza tena.

    TANESCO imetakiwa kuwasilisha taarifa ya awali ndani ya wiki moja ili kuiwezesha serikali kuchukua hatua stahiki, huku uchunguzi wa kina ukiendelea.

    Soma Zaidi:

  10. Rais wa Shirikisho la Soka Saudi Arabia ajiuzulu baada ya timu kutolewa Kombe la Dunia

    Rais wa Shirikisho la Soka la Saudi Arabia, Yasser Al Mashal, amejiuzulu kufuatia kutolewa kwa timu ya taifa ya nchi hiyo katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.

    Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Al Mashal amesema kutofuzu kwa timu hiyo kwenda hatua inayofuata ya mashindano hayo ni matokeo ambayo hayaendani kwa namna yoyote na matarajio na malengo ya taifa hilo.

    "Kutofuzu kwa timu ya taifa kwenda hatua inayofuata ya Kombe la Dunia ni matokeo yasiyoendana na matarajio yetu," aliandika Al Mashal kwenye mitandao ya kijamii.

    "Ninabeba jukumu kamili kwa matokeo haya na naomba radhi kwa wote waliotarajia kuiona timu yetu ikifanya vizuri zaidi.

    Kwa kuamini kwamba uwajibikaji unahitaji kutoa nafasi kwa mwanzo mpya, nimeamua kutoendelea hadi mwisho wa muhula wangu wa uongozi."

    Saudi Arabia ilimaliza mkiani mwa Kundi H ikiwa na pointi mbili, baada ya kutoka sare dhidi ya Uruguay na Cape Verde na kupoteza mechi dhidi ya Hispania.

    Al Mashal alikuwa ameongoza Shirikisho la Soka la Saudi Arabia kwa miaka saba na alihusika kwa kiasi kikubwa katika jitihada zilizoiwezesha Saudi Arabia kupata haki ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2034.

    Saudi Arabia ilikuwa ikishiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo na mara ya saba kwa ujumla. Hata hivyo, maandalizi yake yaliathiriwa na uamuzi wa kumwondoa kocha Herve Renard na kumteua Georgios Donis chini ya miezi miwili kabla ya mashindano kuanza.

    Soma pia:

  11. WHO: Vifo 1,300 Ulaya vyahusishwa na wimbi kali la joto

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema wimbi la joto lisilo la kawaida linaloikumba Ulaya huenda limesababisha vifo vya ziada vya zaidi ya watu 1,300 tangu Juni 21.

    Rekodi za viwango vya joto zimeendelea kuvunjwa katika mataifa kadhaa ya Ulaya, yakiwemo Ujerumani, Poland na Jamhuri ya Czech, huku wimbi hilo la joto kali likiendelea kuelekea mashariki mwa bara hilo.

    Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Tedros alisema joto kali mara nyingi huitwa "muuaji kimya" kwa sababu linaweza kusababisha vifo bila dalili za wazi.

    Aliongeza kuwa nyumba, maeneo ya kazi na shule nyingi barani Ulaya hazikujengwa kuhimili viwango hivyo vya juu vya joto.

    Wizara ya Afya ya Ufaransa imesema takriban vifo 1,000 zaidi ya vilivyotarajiwa vimerekodiwa nchini humo tangu Jumatano, huku idadi kubwa ya vifo hivyo ikiwa ni ya watu wenye umri wa miaka 65 na kuendelea.

    WHO imeonya kuwa Ulaya ndiyo bara linaloongezeka joto kwa kasi zaidi duniani, kwa kiwango cha mara mbili ya wastani wa ongezeko la joto duniani.

    "Mamilioni ya watu barani Ulaya kwa sasa wanaishi chini ya wimbi kali la joto, mamia wamefariki, shule zimefungwa na mifumo ya usambazaji umeme iko chini ya shinikizo kubwa," alisema Tedros.

    Soma Zaidi:

  12. Iran na Marekani zakubaliana kusitisha mashambulizi na kufanya mazungumzo Doha - Axios

    Axios imeripoti kuwa Tehran na Washington zimekubaliana kusitisha mashambulizi katika Ghuba ya Uajemi na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja katika siku chache zijazo mjini Doha, Qatar.

    Mwandishi wa Axios, Barak Ravid, aliandika Jumapili jioni kwamba afisa mmoja mwandamizi wa Marekani amesema Marekani na Iran zimekubaliana kuacha kushambuliana, na kwamba pande hizo mbili zinatarajiwa kukutana mjini Doha siku ya Jumanne kutafuta suluhu ya tofauti zao kuhusu Mlango wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa Axios, mazungumzo hayo yataangazia zaidi suala la Mlango wa Hormuz.

    Iran imehusisha mapigano mapya na Marekani na kile inachodai kuwa ni kuingilia usimamizi wake wa Mlango wa Hormuz.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema wakati wa ziara yake nchini Iraq kwamba kufunguliwa kikamilifu kwa Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa makubaliano na Marekani, ni jukumu la Tehran pekee, na kwamba kuingilia mchakato huo kutavuruga juhudi hizo na kuongeza mvutano katika eneo hilo.

    Maelezo zaidi:

  13. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 29 Juni 2026.