Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran na Marekani zaanza tena mashambulizi ya kulipizana

Baada ya mashambulizi hayo ya pande zote mbili, Marekani na Iran zilishutumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Wanaharakati wanne wa Kenya hawajulikani waliko tangu maandamano ya Alhamisi

    Wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wameipa serikali saa 24 kuwapatikana kwa wanaharakati wanne waliopotea katika eneo la Mathare, wakionya kuwa kutofanya hivyo kutachochea maandamano mapya siku ya Jumanne.

    Miongoni mwa waliopotea ni Davis Lichuma, mwanaharakati wa haki za kijamii wa Mathare, ambaye alitoweka Juni 25 wakati wa maadhimisho ya miaka miwili tangu maandamano ya Gen Z.

    "Mathare lazima iwe mahali salama kwa kila mtu. Hatupo katika hali ya utulivu. Tunaipa polisi na serikali saa 24 kumleta Lichuma. Wasipofanya hivyo, nchi hii haitatawalika," alisema Olal.

    Kesi nyingine iliyotajwa ni ya Maximilian, maarufu kama Maxy, ambaye alitoweka Juni 20 baada ya majirani kudai kamera za ulinzi zilinasa gari lisilo na namba za usajili likimchukua nje ya nyumbani kwake alipokuwa akijiandaa kwenda kazini.

    Mwanaharakati wa haki za binadamu Hussein Khalid amesema mazingira ya matukio hayo yanaashiria kuhusika kwa maafisa wa usalama, akisisitiza kuwa Kenya si taifa la polisi na kwamba maafisa wa usalama hawapaswi kutenda nje ya sheria bila kuwajibishwa.

    Wakati huo huo, makundi ya kutetea haki za kiraia yamesema watu wengine sita waliopotea wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka miwili tangu maandamano ya Gen Z wamepatikana wakiwa hai baada ya kudaiwa kuteswa na kutelekezwa katika maeneo mbalimbali ya Nairobi.

    Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamu Kenya, baadhi yao walipatikana katika Barabara ya Lang'ata na wengine karibu na Uwanja wa Talanta, na kwa sasa wanapatiwa matibabu hospitalini.

    Waziri wa Usalama nchini Kenya Kipchumba Murkomen, alisema kuwa watu 355 wamekamatwa wakati wa maandamano yaliyofanyika kote leo nchini Alhamisi, huku akiwapongeza Wakenya kwa kudumisha amani wakati wa kumbukumbu ya miaka miwili tangu maandamano ya Gen Z.

    Soma Zaidi Hapa:

  2. Afisa wa Marekani athibitisha mashambulizi ya Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani

    Afisa mmoja wa Marekani amethibitisha kuwa Iran ilirusha makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Marekani katika nchi jirani, zikiwemo Bahrain na Kuwait.

    Awali, Wanajeshi wa Iran (IRGC) walitangaza kuwa walishambulia vituo muhimu vya kijeshi vya Marekani, vikiwemo Kambi ya Anga ya Ali al Salem nchini Kuwait na makao makuu ya Jeshi la Wanamaji la Marekani la Fifth Fleet nchini Bahrain.

    Katika taarifa yake, IRGC ilisema ilitekeleza mashambulizi hayo kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani, na kwamba yalikuwa ni jibu la mashambulizi ya awali ya Marekani.

    IRGC ilidai kuwa ililenga vituo vinane vya kijeshi vya Marekani, huku ikiituhumu Washington kwa kushambulia vituo vitano vya majini vya Iran kwa kile ilichokiita kisingizio cha vikosi vyake kuzuia meli katika Mlango wa Hormuz.

    Hata hivyo, maafisa wa Marekani bado hawajatoa taarifa kuhusu kiwango cha uharibifu au iwapo kuna watu waliojeruhiwa au kuuawa.

    IRGC pia ilisema kuwa, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, Iran ina jukumu la kudhibiti usafirishaji wa meli katika Mlango wa Hormuz na kuonya kuwa itachukua hatua kali dhidi ya meli yoyote itakayoona inakiuka sheria.

    Maelezo zaidi:

  3. Iran na Marekani zarejea kushambuliana tena

    Iran na Marekani zarejea kushambuliana baada ya wanajeshi wa Iran kusema wameshambulia miundombinu ya kijeshi ya Marekani katika kambi mbili za kijeshi nchini Kuwait na Bahrain, kulipiza kisasi kwa kile ilichokiita mashambulizi dhidi ya vituo vitano vya pwani vya Iran.

    Bahrain na Kuwait zimethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait imelaani vikali shambulio jipya la Iran, ikisema ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya nchi hiyo.

    Kwa mujibu wa Idhaa ya BBC Persian, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani mashambulizi ya Marekani na kusisitiza kuwa Iran ina haki ya kulinda mamlaka na uhuru wake wa kujitawala.

    ''Marekani haijawahi kuheshimu ahadi zake'', Iran yaituhumu Marekani kwa kukiuka makubaliano.

    Saa chache kabla ya mashambulizi hayo, Rais wa Marekani Donald Trump alisema jeshi la Marekani lilikuwa limelenga maghala ya makombora na ndege zisizo na rubani pamoja na vituo vya rada vya Iran, akidai hatua hiyo ilikuwa ni jibu kwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Trump pia alionya kuwa iwapo italazimika kutumia nguvu za kijeshi kwa kiwango kikubwa zaidi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakuwepo tena.

    Kwa upande wake, jeshi la Iran wameonya kuwa watatoa jibu kali kwa shambulio lolote jipya, hata kama litakuwa dhidi ya malengo wanayoyaita madogo.

    Maelezo zaidi:

  4. Muhoozi aamuru kufungwa kwa NTV Uganda na vyombo vingine vya habari

    Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kuwa kituo cha televisheni cha NTV Uganda na gazeti la Daily Monitor havitafunguliwa tena bila kibali chake.

    Kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa X, Muhoozi alisema kuwa vyombo hivyo viwili vya habari vitafungwa kuanzia leo.

    Katika ujumbe mwingine, alisema haamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda na kwamba vyombo vya habari vinapaswa kuongozwa kwa kuzingatia misingi ya mapinduzi.

    ''Kuanzia sasa vyombo vyote vya habari vya Uganda vitafuata sheria'', ameandika Muhoozi.

    Kufikia alfajiri ya Jumapili, watazamaji wa NTV Uganda na Spark TV walikumbana na skrini tupu zenye ujumbe ulioonyesha kuwa matangazo ya vituo hivyo hayapatikani.

    Shughuli za gazeti la Daily Monitor pamoja na vituo vya redio vya KFM na Dembe FM ziliathiriwa na operesheni hiyo.

    Hadi wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda, Jeshi la Polisi la Uganda na Tume ya Mawasiliano ya Uganda havikuwa vimetoa taarifa rasmi kueleza sababu za operesheni hiyo au msingi wa kisheria wa kufungwa kwa vyombo hivyo vya habari.

    'Bado hatujaelezwa kufungwa kwa vyombo vya habari Uganda kutaendelea hadi lini', Daily Monitor ilichapisha kauli hiyo kwa mtandao wa X.

    Tukio hilo limezua upya hofu kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda, ambako taasisi huru za habari zimewahi kukumbwa na shinikizo na vikwazo vya serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

  5. Netanyahu asema makubaliano ya Israel na Lebanon ni pigo kwa Iran na Hezbollah

    Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, ameyakaribisha makubaliano yaliyofikiwa kati ya Israel na Lebanon kwa upatanishi wa Marekani, akiyataja kuwa "ushindi wa kihistoria" na kusema ni "pigo kwa Iran na Hezbollah."

    "Jana, baada ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Israel na Lebanon, tulifikia makubaliano ya kihistoria yanayoinufaisha serikali ya Israel. Makubaliano haya ni pigo kwa Iran na Hezbollah," Netanyahu alisema katika hotuba iliyorushwa na televisheni.

    Netanyahu pia alisisitiza kuwa majeshi ya Israel yataendelea kuwepo katika eneo aliloliita "ukanda wa usalama," ambalo ni eneo lililoanzishwa na vikosi vya Israel ndani ya Lebanon, takribani kilomita 10 kutoka mpakani.

    Waziri Mkuu huyo alisema: "Tutabaki katika eneo hili hadi Hezbollah na makundi mengine tunayoyachukulia kuwa ya kigaidi yatakapovuliwa silaha."

    Aliongeza kuwa Marekani na Lebanon zinatambua haki ya Israel kuendelea kuwa na ukanda wa usalama ndani ya ardhi ya Lebanon kwa muda utakaohitajika ili kuhakikisha usalama wake.

    Soma Zaidi:

  6. Ethiopia mwenyeji mkutano wa kimkakati kujadili mwelekeo mpya wa diplomasia ya umma Afrika

    Watu zaidi ya 600, wakiwemo viongozi wa kimataifa, wanadiplomasia, watunga sera, wabunifu, wafanyabiashara, wasomi na wawakilishi wa mashirika ya kiraia kutoka Afrika na sehemu nyingine za dunia, wanatarajiwa kukutana jijini Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 29 na 30 Julai kwa ajili ya mkutano wa World Public Summit Africa.

    Mkutano huo wa kimataifa unalenga kuimarisha diplomasia ya umma na kuongeza mchango wa Afrika katika kuunda mustakabali wa dunia.

    Rais wa Ethiopia, Taye Atske Selassie anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo wenye kauli mbiu “ Dunia mpya: Afrika itavyobadili mwelekeo wa siku zijazo” ambao unakuja wakati ambapo mataifa ya Afrika yanazidi kutafuta nafasi kubwa zaidi katika maamuzi ya kimataifa.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jukwaa la World Peoples Assembly, mfumo wa awali wa kidiplomasia unaozingatia serikali kwa serikali pekee haukidhi tena mahitaji ya dunia ya sasa badala yake, wanasisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi, asasi za kiraia, taasisi za elimu, sekta binafsi na wadau wa utamaduni katika kujenga mahusiano ya kimataifa.

    "Mkutano huu unaakisi mtazamo mpya wa ushirikiano wa kimataifa unaoweka mbele ushirikiano kati ya watu, kuheshimiana na malengo ya pamoja ya maendeleo," inaeleza taarifa ya waandalizi.

  7. Timu ya taifa ya Iran yaaga Kombe la Dunia

    Mchezo wa hatua ya makundi wa Kombe la Dunia kati ya Algeria na Austria ulimalizika kwa sare ya mabao 3 kwa 3, matokeo yaliyofuta kabisa matumaini ya mwisho ya timu ya taifa ya Iran kufuzu hatua ya mtoano.

    Marko Arnautović aliifungia Austria bao la kwanza katika dakika ya 28, kabla ya Algeria kusawazisha kupitia Belkhali katika dakika ya 45.

    Marcel Sabitzer aliirejeshea Austria uongozi katika dakika ya 55, lakini Riyad Mahrez akaifungia Algeria bao la pili la kusawazisha.

    Algeria ilipata bao la tatu katika dakika ya 90+3, lakini Austria ilisawazisha tena katika dakika ya 90+5.

    Kutokana na matokeo hayo, Iran ilishindwa kujipanga miongoni mwa timu zilizofuzu kama washindi wa makundi au miongoni mwa timu bora za nafasi ya tatu, na hivyo kuaga rasmi Kombe la Dunia.

    Maelezo zaidi:

  8. Idadi ya waliofariki dunia katika matetemeko ya ardhi Venezuela yafikia 1,400

    Siku tatu baada ya matetemeko mawili makubwa ya ardhi kuikumba Venezuela, juhudi kubwa za uokoaji bado zinaendelea. Idadi ya vifo vilivyothibitishwa imevuka watu 1,400, huku watu wengi wakiendelea kutoweka.

    Wakati huo huo, hali ya kutoridhishwa na mwitikio wa serikali inaongezeka miongoni mwa wananchi.

    Mwandishi wa BBC aliyepo mjini La Guaira, eneo lililoathirika zaidi, anasema hali ni mbaya, huku idadi isiyojulikana ya wakazi ikihofiwa kuwa bado imekwama chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.

    Makundi ya kimataifa ya kutoa misaada pia yamewasili katika eneo hilo, na timu za uokoaji kutoka Mexico, Brazil na mataifa mengine zinaendelea kufanya kazi usiku na mchana kusaidia shughuli za uokoaji na utoaji wa misaada.

    Maelezo zaidi:

  9. DRC watinga hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia

    Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, maarufu kama Leopards, imefuzu kwa mara ya kwanza katika hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia baada ya kuichapa Uzbekistan mabao 3 kwa 1 mjini Houston.

    Yoane Wissa alifunga mabao mawili, huku Fiston Mayele akiongeza bao moja, na kuiongoza DR Congo kubadili matokeo baada ya kujikuta nyuma mapema.

    Ushindi huo ulizua shamrashamra kubwa katika Kinshasa, ambapo mashabiki walisherehekea hatua hiyo ya kihistoria ya timu yao kufuzu kwa mara ya kwanza zaidi ya hatua ya makundi.

    Kwa taifa ambalo lilikuwa halijashiriki Kombe la Dunia tangu mwaka 1974, mafanikio hayo yana uzito mkubwa, yakirejesha fahari na matumaini katika nchi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiusalama.

    Matokeo hayo yameandika historia, yakikomesha kusubiri kwa miaka 52 tangu DR Congo iliposhiriki kwa mara ya mwisho Kombe la Dunia, na sasa Chui watakutana na timu ya England katika hatua ya 32 bora jijini Atlanta Jumatano ijayo.

    Soma pia:

  10. Trump aonya Iran itaangamizwa kabisa ikiendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kwamba ndege za kivita za Marekani zimeshambulia maghala ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran pamoja na vituo vya rada katika maeneo ya pwani.

    Trump amesema mashambulizi hayo yalifanyika kujibu kile alichokitaja kuwa "ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha mapigano" na akaonya kwamba ikiwa Marekani italazimika "kukamilisha" operesheni zake za kijeshi, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakuwepo tena.

    Kwa upande mwingine, Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) imetangaza kwamba imelenga vituo vya kijeshi vya Marekani katika kambi ya Ali al Salem nchini Kuwait na makao makuu ya Kikosi cha Tano cha Jeshi la Wanamaji la Marekani nchini Bahrain kwa kutumia makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani.

    IRGC pia imeonya kwamba itachukua hatua kali zaidi dhidi ya meli inazozitaja kuwa "zinazokiuka" masharti yaliyowekwa.

    Baada ya mashambulizi hayo ya pande zote mbili, Marekani na Iran zilishutumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Katika taarifa yake, Centcom ilisema: "Iran ilipewa fursa ya kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini ilichagua kutofanya hivyo wakati vikosi vyake viliporusha ndege isiyo na rubani ya kujitoa mhanga iliyogonga meli ya mafuta ya MT Kiku," meli iliyosajiliwa nchini Panama.

    Maelezo zaidi:

  11. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya taarifa zinazochipuka kote duniani.