Vita vya Ukraine: Urusi yadai kushinda kura za maoni katika maeneo iliyoyachukua Ukraine

Iliyochapishwa

Kura katika maeneo manne zinazojulikana kama kura za maoni zimemalizika katika miji ya Ukraine inayoshikiliwa na Urusi kura ambazo Moscow inaweza kutumia kama msingi wa kuchukua maeneo zaidi.

Maafisa walioteuliwa na Moscow katika mikoa hiyo sasa wanadai kuungwa mkono kabisa na wale walioshiriki katika kura zinazozozaniwa za kujiunga na Urusi.

Kura hizo zilishutumiwa na serikali ya Ukraine na washirika wake kama udanganyifu.

kutokana na kushindwa kutambuliwa kimataifa, mchakato haukufuatiliwa kwa uhuru.

Kura hizo zilifanyika katika maeneo ya mashariki yaliyojitenga ya Donetsk na Luhansk.

Kura katika sehemu zinazodhibitiwa na Urusi za mikoa ya kusini ya Kherson na Zaporizhzhia pia zilifanyika.

Wakimbizi waliotawanyika kote nchini Urusi pia waliweza kupiga kura katika vituo vingi vya kupigia kura, ikiwa ni pamoja na Crimea, rasi ya kusini mwa Ukraine iliyotwaliwa na Urusi mwaka 2014. Matokeo machache ya upigaji kura huko yalionyesha idadi kubwa ya watu waliounga mkono kujiunga na Urusi.

Hadi watu milioni nne waliombwa kupiga kura katika maeneo yenye vita, ambayo yanaunda takriban 15% ya eneo la Ukraine.

Mashirika ya habari yanayoendeshwa na utawala unaounga mkono Kremlin huko Donetsk na Luhansk yanaripoti kwamba hadi 99.23% ya watu walipiga kura ya kuunga mkono Urusi asilimia kubwa ambayo itakuwa si ya kawaida katika kura ya aina hii.

Kuna uvumi kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin anaweza kutangaza kunyakua mikoa hiyo minne katika hotuba ya kikao cha pamoja cha bunge la Urusi siku ya Ijumaa.

Mnamo Machi 2014, alitangaza kwamba Crimea imejiunga na Urusi siku chache tu baada ya kura ya maoni sawa na kura ya maoni ambayo haikutambuliwa iliyopigwa sasa.

Iwapo Urusi itatwaa maeneo manne, ambayo Moscow haiyadhibiti kikamilifu, inaweza kupeleka vita katika ngazi mpya na hatari zaidi, huku Moscow ikionyesha jaribio lolote la Ukraine kutaka kuyarejesha kama mashambulizi dhidi ya eneo lake huru.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliishutumu Urusi kwa "kukiuka kikatili sheria ya Umoja wa Mataifa" kwa kujaribu kunyakua maeneo yaliyochukuliwa kwa nguvu.

"Utani huu katika eneo lililochukuliwa hauwezi kuitwa hata kura za maoni za kuiga," alisema Jumanne usiku.

Rais aliongeza kuwa ni "jaribio la kijinga sana kuwalazimisha wanaume katika eneo lililochukuliwa la Ukraine kukusanyika katika jeshi la Urusi ili kuwatuma kupigana dhidi ya nchi yao wenyewe!"

Vikwazo zaidi dhidi ya Urusi

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo vikali zaidi.

"Tunahitaji jibu zito sana, lenye ufanisi na mambo mahususi ambayo yataathiri uchumi wa Urusi. Kadiri mwitikio ulivyo laini kwa kile kinachoitwa kura ya maoni, ndivyo motisha ya Urusi inavyoongezeka na kujumuisha maeneo zaidi," alisema.

Uingereza ilijibu kile kinachoitwa kura za maoni kwa vikwazo vipya kuwalenga maafisa wakuu wa Urusi waliohusika katika kutekeleza kura hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisisitiza tena kuwa nchi za Magharibi hazitawahi kutambua unyakuzi wa Urusi, akiionya Kremlin kuhusu "gharama za ziada za haraka na kali".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna, ambaye siku ya Jumanne alitembelea Ukraine, alielezea uchaguzi huo kama "udanganyifu".

Nchini China, mshirika wa Urusi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Wang Wenbin alisema "uhuru na uadilifu wa eneo la nchi zote lazima uheshimiwe", alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu kile kinachoitwa kura ya maoni.

Rais Putin alitetea kura hizo za maoni akisema ziliundwa kukomesha mateso dhidi ya watu wa kabila la Urusi na wanaozungumza Kirusi na Ukraine shutuma ambazo serikali ya Ukraine inakanusha.

"Kuokoa watu katika maeneo yote ambayo kura hii ya maoni inafanyika ni juu ya akili zetu na umakini wa jamii yetu yote na nchi," kiongozi huyo wa Urusi alisema katika hotuba yake kwenye televisheni.

Matokeo sio ya kushangaza

Matokeo ya kura hizo nne za maoni binafsi hayatashangaza mtu yeyote, hata Ukraine.

Kura za kuunga mkono Urusi ni mwendelezo wa masimulizi ya Kremlin ya kujaribu "kuwakomboa" Waukraine katika maeneo hayo, pamoja na majaribio yake ya kuhalalisha uwepo wake nchini humo.

Ukraine na nchi za Magharibi zimekanusha mchakato huo, na BBC imesikia ushahidi wa askari wenye silaha wakikusanya kura nyumba hadi nyumba, pamoja na madai ya kutofanyika kabisa.

Urusi inatarajiwa kutunga sheria za haraka na mpya kuhusu unyakuzi wa maeneo haya manne yanayogombaniwa, na imetishia matumizi ya silaha hatari zaidi iwapo italengwa katika siku zijazo.

Kile ambacho Kyiv amewahi kusema ni kwamba malengo yake hayajabadilika, bila kujali taarifa (na matokeo ya sasa) ambayo yanatoka Moscow.

Upigaji kura wa mapema ulifanyika kwa muda wa siku nne, huku maafisa wa uchaguzi wakisindikizwa na askari wakitembelea makazi ya watu. Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa Jumanne pekee.

"Kwa sauti yangu, nataka kujaribu kutoa mchango mdogo katika kukomesha vita," Galina Korsakova, 63, kutoka Donetsk aliliambia shirika la habari la AFP.

Kura hiyo ambayo haijatambuliwa ilifanyika wakati vita vikiendelea, na angalau afisa mmoja wa uchaguzi aliuawa, katika shambulio la kombora kwenye mji wa Zaporizhzhia wa Berdyansk.

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine tarehe 24 Februari, makumi ya maelfu ya wapiganaji na raia wameuawa au kujeruhiwa, huku miji na majiji makubwa yakibaki magofu.

Zaidi ya watu milioni 7.4 wa Ukraine kwa sasa wamerekodiwa kuwa wakimbizi, wakiwemo karibu milioni 2.7 nchini Urusi, takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha.