Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi inakiri makosa ya usajili wa wanajeshi wa akiba, huku upinzani wa umma ukiongezeka
Ikulu ya Urusi imekiri makosa yalifanyika katika harakati zake za kuwakusanya wanajeshi wa akiba kupigana nchini Ukraine, huku kukiwa na upinzani unaoongezeka wa umma.
‘’Kuna matukio wakati amri inakiukwa,’’ msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema, akiongeza kuwa ‘’makosa yote yatarekebishwa’’.
Ripoti nyingi zinasema watu wasio na uzoefu wa kijeshi - au ambao ni wazee sana au walemavu – wanaitwa kujiunga na jeshi.
Amri ya usajili wa wanajeshi wa akiba ya wiki iliyopita tayari imesababisha maandamano makubwa.
Rais Putin alitangaza kile alichokitaja kama usajili wa wanajeshi wa akiba mnamo Septemba 21, huku Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu baadaye akisema wamajeshi 300,000 wa akiba watajumuishwa.
Hata hivyo, ripoti katika vyombo vya habari vya upinzani vya Urusi zilisema kwamba hadi watu milioni moja wangeweza kujumuishwa, aya moja inayoaminika ikihusisha idadi kamili ya wanajeshi wa akiba waliohitajika iliachwa nje katika toleo lililochapishwa la agizo la Bw Putin katika tovuti rasmi ya Kremlin.
Wataalamu kadhaa wa kijeshi katika nchi za Magharibi na Ukraine wanasema uamuzi wa Bw Putin wa kujumuisha wanajeshi wa akiba unaonyesha kwamba wanajeshi wa Urusi wanashindwa vibaya vitani nchini Ukraine - zaidi ya miezi saba baada ya Moscow kuanzisha uvamizi wake.
Tangu kutangazwa kwa tangazo hilo, zaidi ya watu 2,000 wamezuiliwa kutokana na maandamano kote nchini Urusi.
Katika kikao fupi siku ya Jumatatu, msemaji wa Bw Putin, Dmitry Peskov, alikiri kwamba makosa yalikuwa yakifanywa.
Alisema kuwa katika baadhi ya mikoa, ‘’magavana wanafanya kazi kwa bidii kurekebisha hali hiyo’’.
Bw Peskov pia alisema hajui kuhusu maamuzi yoyote ya kufunga mipaka ya Urusi na kuweka sheria za kijeshi nchini humo.
Ripoti za vyombo vya habari hapo awali zilipendekeza hii inaweza kufanywa ili kuzuia waajiri wanaotarajiwa kutoroka nje ya nchi.
Tangu tangazo la usajili wa wanajeshi huo kutangazwa, Warusi wengi wenye umri mdogo wamekuwa wakitafuta kuondoka nchini humo.
Picha za satelaiti zinaonyesha foleni ndefu za magari ya Urusi kwenye mpaka na Georgia.
Katika ishara ya hivi punde ya kuongezeka kwa maandamano ya umma, mtu mmoja alimjeruhi vibaya afisa wa kusajili wanajeshi katika mji wa Siberia wa Ust-llimsk siku ya Jumatatu.
Picha zimeibuka kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha mshambuliaji akimsogelea afisa huyo na kisha kumpiga risasi.
Watu waliokuwa ndani ya jengo hilo wanaonekana wakipiga kelele na kukimbia kwa hofu baada ya mtu mwenye bunduki kuwapigia kelele akiwaambia watoroke.
Mwishoni mwa juma, watu katika eneo linalojitegemea la Dagestan huko Urusi, Caucasus Kaskazini walipambana na polisi kuhusu harakati usajili wa wanajeshi.
Zaidi ya watu 100 walikamatwa wakati wa maandamano katika mji mkuu wa mkoa wa Makhachkala, alisema OVD-Info, mfuatiliaji huru wa haki za binadamu wa Urusi.
Pia kumekuwa na ripoti za mashambulizi kadhaa ya uchomaji moto vituo vya usajili wanajeshi na majengo mengine ya utawala kote Urusi.
Katika tangazo lake kuhusu usajili wa wanajeshi wiki jana, Bw Putin hakutaja ni wanajeshi wangapi wa akiba wanahitajika.
Lakini akizungumza mara baada ya rais, Bw Shoigu alisema wanajeshi wa akiba 300,000 - watu ambao wana uzoefu wa kijeshi na wanaohitaji ujuzi maalum - wataorodheshwa.
Waziri huyo alisema hii ni zaidi ya 1% ya uwezo wa wanajeshi wa akiba ya Urusi milioni 25.
Mchakato huo ungefanyika kwa miezi kadhaa.
Vikomo fulani vya umri na ulemavu vitatumika, amri ya usajili wa wanajeshi wa ziada ilisema.
Hata hivyo, haikutoa maelezo zaidi.
Inaaminika kuwa wanaume wenye umri wa miaka 18-60 - na katika hali zingine hata wazee - wanaweza kusajiliwa.
Baadhi ya wafafanuzi wa Urusi mara moja walitilia shaka ahadi za rais na waziri wake wa ulinzi kwamba mwito huo ungekuwa na ukomo.
Walisema kuwa amri hiyo haikusema chochote kuhusu wasioruhusiwa kujiunga, kama vile kutosajili wanafunzi au makurutu wapya.
Walipendekeza hili lingeachiwa wakuu wa mikoa kuamua ni nani ajumuishwe ili kutimiza idadi.
Mnamo tarehe 24 Septemba, Bw Putin alitoa amri mpya ikisema kwamba, hasa wanafunzi wangetolewa kutoka kwenye sajili.
Kabla ya kuanza uvamizi wake tarehe 24 Februari, Urusi ilikuwa imekusanya takriban wanajeshi 190,000 kwenye mipaka ya Ukraine.