Ellen: Binti anayewafuatilia simba 300 wenye vitambulisho Serengeti

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Yusuph Mazimu
- Nafasi, BBC Swahili, Dar es Salaam
- Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa miaka mitatu, Ellen Ponsian, 28 amekuwa akifanya utafiti kufuatilia mwenendo wa Simba ndani na nje ya Hifadhi ya Serengeti. Kwa muda huo, ameweza kuwajua mmoja mmoja, anafahamu familia zao na historia zao. Lakini kazi yake inamuweka karibu na mmoja wa wanyama hatari zaidi barani Afrika.
Usiku mmoja katikati ya pori la Serengeti, Ellen Ponsian alikuwa amelala kwenye hema yake akiendelea na kazi yake ya utafiti.
Ghafla usiku wa manane, simba wakaanza kunguruma karibu na hema lake..
Hakuwa mmoja. Walikuwa watatu.
Kwa mtu mwingine, huo ungekuwa wakati wa hofu kubwa, pengine angeacha kabisa kazi hiyo. Lakini Ellen, ni moja ya matukio ambayo yamekuwa sehemu ya safari yake ya kuwafahamu wanyama hawa.
Kwa miaka mitatu sasa, Ellen amekuwa akifuatilia simba katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Lakini anachofanya si kuwatazama tu. Anajaribu kuelewa maisha yao.
Simba 300 wenye majina na kadi kama za 'kliniki'

Ellen na timu yake wanafuatilia takribani simba 300 katika makundi 23.
"Kuna makundi 23 ninayofuatilia na wenzangu yenye jumla ya simba 300."
Lakini kila mmoja wa simba hao ana utambulisho wake. Taarifa zao zinahifadhiwa kwenye kadi maalumu. Kadi nyeupe ni kwa ajili ya taarifa za simba dume na kadi ya rangi ya njano simba jike. Kadi hizi ni utambulisho na ni kama vitambulisho kwao.
"Kila simba tumempa jina, Yuko aliyekuwa naitwa Moses, tulikuwa na Simba maarufu aliyeitwa Bob Jr."
Hellen na watafiti wenzake wameweka mfumo wa kadi maalumu kwa kila simba.
Kadi hizo hutofautisha madume na majike na kuhifadhi taarifa mbalimbali kuhusu kila mnyama ikiwemo kundi analotoka, jina, umri, lini alionekana kwa mara ya kwanza na hata taarifa za kifo chake ikiwa amefariki.
Kwa Ellen, simba 300 si suala la takwimu tu. Ni simba 300 anaowafahamu mmoja mmoja.
Na kuwafahamu zaidi kunamaanisha wakati mwingine kuwa karibu nao kuliko ambavyo mtu wa kawaida angeweza kuthubutu.
Kazi ya hatari

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Taarifa kutoka kwenye GPS humsaidia Ellen na timu yake kufahamu walipo baadhi ya simba. Kisha safari ya kwenda porini inaanza.
Madaktari wa wanyamapori humlaza simba kwa dawa maalumu kwa dakika 45, na Ellen hutumia muda huo mfupi kumchunguza. Anaangalia meno, alama za mwili, hali yake, vipimo na kukusanya sampuli.
Ni kazi inayohitaji umakini kwa sababu simba huyo atakapotumia dawa ya kuamka, timu inapaswa kuhakikisha anaweza kusimama na kujilinda kabla hawajaondoka.
Lakini hata kwa mtu aliyezoea simba, hatari haikosekani.
"Huyu binti ni jasiri" : Neema Mushi ni miongoni mwa watu wanaovutiwa na kazi ya Ellen Anasema yeye mwenyewe hawezi kuwa na uhakika kama angeweza kufanya kazi hiyo.
"Kwakweli mie siwezi kufanya anachokifanya", anasema.
Kwake, uamuzi wa Ellen kuacha maisha ya mjini na kwenda kufanya utafiti katikati ya wanyamapori unaonyesha ujasiri mkubwa. Anaeleza kuwa katika baadhi ya jamii za Afrika, si jambo la kawaida kumuona mwanamke kijana akichagua maisha ya namna hiyo.
Badala yake, anaweza hata kutafsiriwa vibaya kwa kufanya jambo linaloonekana kuwa si la kawaida.
Lakini Ellen, anasema Neema, ameonyesha kuwa mwanamke anaweza kuanzia popote na kufanya chochote.
Benista Mjaga, anamwona Ellen kwa mtazamo huo huo.
"Huyu binti Hellen ni binti jasiri, ameamua kujifunza tabia za wanyama na kuwafanyia utafiti, akiwapa majina na namba. Ingawa si kazi rahisi…"
Kwa Mjaga anaweza kujaribu kufanya kazi hii lakini ni rahisi kusema hivyo ukiwa mbali na simba.
Ellen mwenyewe amewahi kukutana na hali ambazo zingemfanya mtu mwingine ageuke na kurudi nyumbani.
Na bado anaendelea kurudi. Flora Maruku, Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) , kazi ya Hellen ni mfano wa namna wanasayansi vijana wanavyoweza kutumia utafiti kusaidia uhifadhi.
Utafiti wa zaidi ya miaka 50 wa kufahamu simba

Lakini nyuma ya uwezo wa Ellen kumtambua simba mmoja mmoja kuna historia ndefu ya utafiti.
Mradi wa Simba Serengeti, unaoratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kupitia Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Serengeti, umefuatilia idadi, tabia na mienendo ya simba kwa zaidi ya miaka 50.
Kwa sasa, mradi huo unafuatilia takribani simba 300 katika makundi 23, huku Ellen akiwa miongoni mwa watafiti wanaoendeleza kazi hiyo.
Teknolojia imekuwa sehemu muhimu ya utafiti huu. Hellen na watafiti wenzake hutumia VHF/GPS satellite collars kufuatilia mienendo ya simba na kujua maeneo ambayo makundi yao yanapatikana.
Lakini taarifa hizi si kwa ajili ya kuwajua simba walipo pekee.
Zinasaidia watafiti kuelewa jinsi wanavyoishi, wanaishi kwa muda gani, wanatembea wapi, wanakabiliwa na vitisho gani na hatua gani zinaweza kuchukuliwa kuwalinda.
Na kazi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania.
Kwa mujibu wa TAWIRI, Tanzania ina zaidi ya simba 17,000, idadi inayoiweka kileleni Afrika kwa wingi wa simba.
Kwa hiyo, kazi ya Ellen si kumjua tu simba mmoja.
Ni sehemu ya juhudi kubwa za kuhakikisha kizazi kijacho kinaendelea kuelewa na kulinda wanyamapori hawa.
Serikali imewekeza katika utafiti huo, na kwa TAWIRI, Elleni sehemu ya kizazi kipya cha wanasayansi wanaotarajiwa kuendeleza kazi hii.
Mkurugenzi wa TAWIRI, Dkt. Eblate Mjingo, anasema tangu walipomwajiri Hellen walitambua shauku yake ya kufanya utafiti wa ikolojia ya simba.
"Siku ya kwanza tu tulipomuajiri Ellen tulijua anapenda sana Ikolojia ya Simba. Anafurahia kuona watafiti vijana wakikua na kuchukua nafasi katika sayansi ya uhifadhi akisema taarifa za watafiti kama Ellen zinasaidia sana uhifadhi na utalii.
Hellen bado ana safari ndefu. Kesho, kuna uwezekano mkubwa atafungua tena kompyuta yake, aangalie taarifa za GPS na kutafuta mmoja wa simba 300 anaowafuatilia.
Na ikiwa taarifa zitampeleka tena porini, atachukua vifaa vyake na kwenda. Iwe kuna hatari ama hakuna, anatekeleza wajibu wake kwa mnyama anayempenda.
Kwa sababu mahali ambapo wengi wetu tungeona hatari, Ellen anaona maisha yake, kazi yake na wanyama ambao amekuja kuwajua mmoja mmoja.
Wakati mimi na wewe tunaweza kuogopa hata paka, Ellen anaishi karibu na simba kila siku-pamoja na ukali wao.













