Makumi ya spishi mpya za wanyama zagunduliwa nchini Angola

Chanzo cha picha, Nicky Bay
Wanasayansi wamegundua makumi ya spishi mpya wakati wa utafiti wao katika mojawapo ya maeneo ya Afrika ambayo bado hayajafanyiwa uchunguzi wa kutosha kuhusu bioanuwai.
Utafiti huo, uliopewa jina la Cassai Life Atlas, ulibaini spishi nane mpya za kereng'ende, spishi tatu mpya za panzi, pamoja na takriban spishi 60 mpya za nondo na vipepeo katika uwanda wa juu nchini Angola.
Wataalamu kutoka The Wilderness Project waliongoza msafara huo na kugundua viumbe pamoja na aina za mimea ambazo hapo awali hazijatambulika na sayansi.
Miongoni mwao ni mende wa matunda(fruit beetles) wenye ukubwa unaokaribia kiganja cha mkono wa binadamu, pamoja na buibui wadogo wenye alama za bluu zinazong'aa.
"Matokeo ya utafiti yalionyesha bioanuwai kubwa zaidi kuliko tulivyotarajia," alisema Rob Taylor, kiongozi wa msafara huo na mtaalamu wa ikolojia ya uhifadhi.
"Idadi ya baadhi ya viumbe ilikuwa ndogo, kwa sehemu kutokana na mifumo hii ya ikolojia kuwa na virutubishi vichache. Hata hivyo, utofauti wa spishi maalumu na zisizo za kawaida ulikuwa wa kushangaza."
Uwanda wa juu wa Lisima nchini Angola kwa muda mrefu umechukuliwa kuwa mojawapo ya maeneo makubwa ya Afrika ambayo bado hayajafanyiwa utafiti kikamilifu kuhusu bioanuwai.
Eneo hilo pia lina umuhimu mkubwa wa kiikolojia unaovuka mipaka yake, kwani mifumo ya ikolojia na jamii zilizo umbali wa maelfu ya kilomita kutoka eneo hilo hutegemea maji yanayotoka katika uwanda huo.
"Uelewa wa kina kuhusu bioanuwai ya eneo hili ni muhimu ili kuhakikisha mfumo mzima unalindwa kwa ufanisi," alisema Taylor.

Chanzo cha picha, Nicky Bay
Utafiti huo unatoa taswira ya kina zaidi kuwahi kupatikana kuhusu eneo ambalo kwa kiasi kikubwa bado halijafanyiwa uchunguzi na wanasayansi, na umebainika kuwa na spishi za kipekee kama buibui taji (Crowned crab spider)

Chanzo cha picha, Nicky Bay
Wataalamu walirekodi makundi 47 ya panzi, nzige na nyenje, ambapo makundi matatu kati yao yalikuwa hayajawahi kujulikana na wanasayansi.

Chanzo cha picha, Nicky Bay
Nge na mende pia waligunduliwa na sasa wanasubiri kufanyiwa uchunguzi wa maabara ili kubaini utambulisho wao.

Chanzo cha picha, Nicky Bay
Nyoka aina ya bush viper, ambaye ana sumu kali, ni miongoni mwa spishi 23 za wanyama wanaotambaa waliorekodiwa katika eneo hilo.

Chanzo cha picha, Nicky Bay
Buibui huyu aina ya ladybird orb-web, ambaye anaaminika kuwa spishi mpya, hutumia kujificha kama njia ya kujilinda dhidi ya kuuliwa, kwani ladybird hutoa sumu kwa wanyama wanaowawinda.












