Kwa nini FVS na si VAR Ligi Kuu Tanzania Bara? Fahamu tofauti

lp

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Mazingira ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) yamebadilika mwaka huu 2026 na maendeleo katika teknolojia yanazidi kuonekana. Ingawa mashabiki na wachambuzi wanatamani kuona teknolojia ya Video ya Kumsaidia Mwamuzi VAR).

Tanzania imeweka historia kwa kuwa taifa la kwanza la Afrika kuanzisha rasmi Usaidizi wa Video katika Mpira wa Miguu (FVS) katika ligi yake ya ndani. Ni mfumo ambao umeanzishwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Kuelewa tofauti kati ya FVS na VAR ni muhimu kwa mashabiki, kwani mifumo hiyo miwili inatumia teknolojia ya video, lakini hufanya kazi kwa falsafa, miundombinu, na itifaki tofauti.

Tofauti ya VAR na FVS

k

Chanzo cha picha, MWANANCHI

VAR, huu ni mfumo ambao unakuwa na maafisa wa kufuatilia video katika chumba cha ufuatiliaji na hufuatilia kila tukio katika mechi. Hufatiliaji mabao, uamuzi wa penalti, kadi nyekundu, kuotea, na michezo ya dhambi.

Wakiona kosa wanampa taarifa mwamuzi uwanjani, na mwamuzi anaweza kukubaliana na ushauri wao au anaweza kusimamisha mpira na kwenda kwenye skrini ya pembeni ya uwanja kutazama marudio ya tukio hilo yeye mwenyewe. Na kisha kufanya maamuzi.

FVS ni mfumo unaotoa nafasi kwa makocha zaidi. Hakuna maafisa wa video waliowekwa kufuatilia kila tukio la mechi. Badala yake, maamuzi ya kumtaka mwamuzi kupitia marudio ya video yapo mikononi mwa makocha wakuu.

Kila timu inapewa idadi maalum ya nafasi za kuomba ukaguzi kwa kila mechi. Ikiwa kocha anaamini mwamuzi amefanya kosa, lazima aombe ukaguzi rasmi kwa kumpa mwamuzi wa nne (wa mezani) kadi ya ombi la ukaguzi.

Katika matumizi ya mfumo huu, timu hupewa nafasi katika mechi za ligi kuu Tanzania bara. Ikiwa ombi litathibitika kuwa sahihi na mwamuzi akabadilisha uamuzi wake, timu haitopungukiwa nafasi hiyo.

Miundombinu ya uendeshaji VAR ni ya gharama zaidi, kwani inahitaji kamera za kiwango cha juu na kamera nyingi (mara nyingi 8+). Lakini FVS inaweza kufanya kazi na kamera 1–4.

Na ikiwa mechi itaenda kwenye muda wa ziada, timu hupewa nafasi moja ya ziada katika mfumo wa VFS.

Mfanano wa VAR na FVS

l

Chanzo cha picha, Getty Images

VAR na FVS zote mbili ni mifumo ya kiteknolojia iliyoundwa ili kuongeza usahihi wa usimamiaji katika mpira wa miguu kwa waamuzi, ili kupunguza makosa yanayohusisha mabao, adhabu, na kadi nyekundu, na makosa katika kumtambua mchezaji.

Zote zinahitaji kamera na skreni pembeni ya uwanja, ambapo mwamuzi mkuu anaweza kufanya mapitio ya picha za tukio kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.

Katika mifumo yote miwili, mwamuzi wa uwanjani ana mamlaka ya mwisho ya kufanya maamuzi. Teknolojia ya video hufanya kazi kama zana ya ushauri pekee.

Mifumo yote miwili imewekewa mipaka, ambapo inashughulikia matukio maalum yenye athari kubwa, mifumo hii haikagui dosari ndogo ambazo haziwezi kuleta athari yoyote katika dakika 90.

Mapinduzi ya Soka la Tanzania

Ingawa VAR ndio mfumo unaotumika katika mashindano kama Ligi Kuu ya England au Ligi ya Mabingwa ya UEFA, inahitaji uwekezaji mkubwa katika teknolojia hiyo na mafunzo.

FVS ni njia mbadala ya VAR. Kwa sababu hiyo Ligi Kuu Tanzania Bara inaboresha maamuzi ya waamuzi wake, ili kuwapa nafasi ya kutoa maamuzi sahihi zaidi.

Siku chache tu tangu mfumo huo uanze katika mechi zilizoanza wikiendi, tayari kadi nyekundu na mikwaju ya penalti imefanyiwa maamuzi kupitia FVS.