Jinsi pombe inavyochangia kasi ya kuzeeka

Chanzo cha picha, PA
Kuacha pombe kunaweza kuongeza miaka katika maisha yako kwa kupunguza kasi ya mwili kuzeeka.
Mwaka uapoanza huwa unaonekana kuwa wakati mwafaka wa kuacha kunywa pombe na si kwa sababu tu ya desturi maarufu ya 'Dry January' yani Januari bila pesa.
Kadiri majira ya baridi yanavyoendelea, wengi wetu tunahisi hamu ya kupunguza muda wa kunywa vinywaji baridi kama bia na kokteli, na badala yake kutumia muda mwingi kufurahia kahawa ya maziwa yenye viungo na vikombe vya chai.
Hata hivyo, huu pia ni msimu wa kukaa kwa muda mrefu kwenye baa, jambo linaloathiri vibaya akiba yetu ya fedha. Kama tunavyojua sote, tabia ya kuendelea kunywa pombe kwa namna hii inaweza pia kuharibu mahusiano yetu na kuathiri afya zetu.
Lakini, linapokuja suala la afya, hali halisi ni tata zaidi kuliko inavyoonekana. Si ini, ubongo na moyo pekee vinavyoweza kufanya kazi vizuri zaidi pale unapoishi bila pombe.
Kwa kweli, mwili wako wote unaweza kunufaika. Hii ni kwa sababu pombe huharakisha mchakato wa kuzeeka, na kusababisha kwa kasi kudhoofika kimwili.
Kuacha pombe kunaweza kusimamisha mchakato huo, na kukukinga dhidi ya matatizo ya utendaji kazi wa ubongo,kupungua kwa uwezo wa mwili, kupunguza hatari ya magonjwa mengi, na hata kuongeza muda wa kuishi.
Muhimu zaidi ni hali viungo vya ndani
Kuacha kunywa pombe hakutasitisha muda wala kukufanya uwe kijana tena kwa kurudisha nyuma umri, kama inavyotokea katika kipindi cha *Doctor Who*.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hii ni kwa sababu hatuzungumzii muda wa kawaida wa kalenda hapa, bali muda wa kibiolojia. Kwa maneno mengine, suala si idadi ya kiwango ambapo dunia imekuzungusha kuzunguka Jua, bali ni uchakavu ambao mwili wako hupitia kadiri miaka inavyosonga.
Wazo ni kwamba maisha , pamoja na mikazo yake yote, sherehe, mazoezi, vinywaji baridi kama soda, chipsi, televisheni, likizo na keki ,huathiri mwili. Tabia zetu huacha alama mwilini mwetu, na hivyo tunazeeka.
Lakini wakati baadhi ya watu wakibaki na ujana na afya njema kwa miaka mingi, wengine huingia haraka katika hali ya ngozi kukunjamana, kupungua kwa uwezo wa akili, na kuathirika na magonjwa yanayohusiana na uzee. Huo ndio uzee wa kibiolojia.
Dkt. Anya Topiwala, mtafiti mkuu wa masuala ya kliniki katika Idara ya tiba ya magonjwa ya akili yani Saikiatri ya Chuo Kikuu cha Oxford, anaeleza, "Unaweza kuwa na umri wa miaka 35 kulingana na tarehe ya kuzaliwa, lakini ikiwa umeishi maisha yenye afya njema, unaweza kuwa na umri mdogo zaidi wa kibiolojia.
"Na kinyume chake, ikiwa umekuwa ukivuta sigara sana na kula vyakula visivyofaa, unaweza kuwa na umri wa kibiolojia wa miaka 40."
Wanasayansi wanaweza kutumia zana mbalimbali kukadiria umri wetu wa kibiolojia, na wamegundua kuwa watu wanaokunywa pombe nyingi huonekana kuwa na umri mkubwa zaidi kuliko watu wengine wa rika lao.

Chanzo cha picha, Stefania Pelfini la Waziya via Getty
Angazia telomeres zako
Mojawapo ya njia ambazo wanasayansi wanaweza kupima umri wa kibiolojia, na kuchunguza uhusiano wake na pombe ni kupitia kitu kinachoitwa 'telomeres'.
"Telomeres ni ncha za kromosomu zako," anaeleza Topiwala. " vinasaba au DNA yetu imepangwa katika kromosomu, na seli zetu zinapogawanyika, kromosomu hizi hunakiliwa. Hata hivyo, unakili huo huwa haukamiliki kikamilifu katika ncha za telomeres.
"Kwa hivyo, kadiri muda unavyopita, telomeres hizi huzidi kuwa fupi. Zinapofikia hatua ya kufupika kupita kiasi, seli hufa."
Hii ina maana kwamba wanasayansi wanaweza kupima urefu wa telomeres za mtu ili kubaini ni mara ngapi seli zake zimegawanyika na hivyo kukadiria umri wake,kwa mtazamo wa kibiolojia.
Mnamo mwaka wa 2022, Topiwala na timu yake katika Chuo Kikuu cha Oxford walifanya utafiti kuhusu uhusiano kati ya pombe na urefu wa telomeres kwa watu wazima zaidi ya 245,000 nchini Uingereza.
"Tulibaini kuwa kadiri watu walivyokunywa pombe zaidi, ndivyo telomeres zao zilivyokuwa fupi zaidi," anasema Topiwala. "Wale waliokunywa pombe walikuwa wameharakisha mchakato wao wa kuzeeka kibiolojia."
Kwa wastani, washiriki walioripoti kunywa takriban pombe kwa wiki kiasi sawa na glasi 10 za divai walionekana kuwa na umri mkubwa kwa hadi miaka miwili kuliko wale waliosema walikunywa kiasi kidogo kwa wiki kama glasi mbili za divai.
Wanasayansi hawana uhakika kamili kuhusu sababu inayofanya pombe iathiri telomeres zetu, lakini Topiwala anasema tunajua tayari kuwa pombe huharibu inasaba au DNA kwa kufuta, kuvunja na kupanga upya sehemu zake, hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa utaratibu unaohusika ni uleule.
Muda unapoyoyoma
Telomera si njia pekee inayotumiwa na wanasayansi kupima umri wa kibiolojia. Wanaweza pia kutumia kitu kinachoitwa saa za epijenetiki (epigenetic clocks).
Hebu fikiria vinasaba au DNA yako kama kitabu cha mapishi. Kitabu kipya kabisa cha mapishi huwa katika hali safi na isiyo na alama yoyote,lakini kama wewe ni mpishi makini, unaweza kuchagua kuandika dondoo pembeni mwa maelekezo ya mapishi uliyowahi kuandaa, au kuweka vibandiko na alama za kurasa, ili kurahisisha mambo wakati ujao utakapohitaji kuandaa chakula cha jioni.
Hali hiyo inafanana kidogo na kile kinachotokea kwa DNA yako kadiri muda unavyopita. Mwili wako huongeza alama ndogo za kemikali zinazoitwa 'methyl groups' ili kubadilisha jeni zinazotumiwa na seli zako, mchakato unaojulikana kama 'methylation'.
Kadiri tunavyozeeka, mpangilio wa alama hizi hubadilika taratibu, katika mchakato unaoitwa 'epigenetic drift'.
Kwa mfano, tunaweza kuona kitabu cha mapishi kilichojaa michoro na madokezo yaliyochomekwa humo, na kuhitimisha kuwa kimetumika sana. Vivyo hivyo, wanasayansi wanaweza kuchunguza mifumo hii ya methylation ili kukadiria umri wa mtu, kulingana na ni jeni zipi ambazo zimewashwa au kuzimwa.
Kuna mbinu mbalimbali ambazo wanasayansi wanaweza kutumia kufafanua mifumo hiyo. Hizi huitwa saa za epigenetic, na zile zinazojulikana zaidi ni PhenoAge na GrimAge.
PhenoAge kifupi cha Phenotypic Age au Umri wa Kifizikia hutumia mifumo yako ya methylation kukadiria umri wako wa kibiolojia. Kwa upande mwingine, GrimAge hukadiria ni lini unaweza kufariki dunia, ndiyo maana inaitwa hivyo.
Kwa kutumia zana hizi, wanasayansi wameweza kuchunguza jinsi pombe inavyochangia kuzeeka kwetu. Kwa mfano, utafiti wa mwaka 2021 ulichambua data za DNA methylation kutoka kwa washiriki 28,000 nchini Uingereza kwa kutumia PhenoAge na GrimAge.
Waligundua kuwa kadiri mshiriki alivyokunywa pombe nyingi, ndivyo ilivyokuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na umri wa kibiolojia ulio juu zaidi ya umri wake halisi.
Wakati huo huo, utafiti kama huo wa mwaka 2023 uligundua kuwa watu wazima nchini Marekani wenye umri wa miaka 44 au zaidi, ambao walikuwa wamekunywa pombe nyingi katika maisha yao, walionyesha dalili zaidi za kuzeeka kwa kasi ikilinganishwa na watu wazima wenye umri mdogo au wale waliokunywa kiasi kidogo.
Kwa kweli, kwa kila kinywaji cha pombe ambacho mshiriki wa umri wa kati au mkubwa alikunywa kwa siku, wastani wa miezi saba hadi tisa ya ziada iliongezwa kwenye umri wao wa kibiolojia.
Athari hii ya kuzeeka ilikuwa kubwa zaidi ikiwa washiriki walikunywa pombe kali kama vile wiski au vodka badala ya bia au divai.
Pombe na ubongo

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanasayansi hawahitaji kila mara zana tata za kupima mabadiliko ya kijenetiki au saa za epigenetic ili kuona jinsi pombe inavyoharakisha mchakato wa kuzeeka. Hii ni kweli hasa kwa ubongo, huku tafiti zikionyesha kuwa unywaji mwingi wa pombe unahusishwa na hatari kubwa ya kupata magonjwa ya akili yanayotokana na uzee.
Kadiri tunavyozeeka, wengi wetu hupata tatizo la kupungua kwa uwezo wa utendaji kazi wa ubongo hali hiyo ya ubongo kupunguza kasi ya utendaji kazi ambayo inaweza kusababisha magonjwa ya kuharibika kwa seli za ubongo kama vile shida ya kupoteza kumbukumbu na uwezo wa kufikiri .
Na katika utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Topiwala, uliowahusisha zaidi ya watu wazima laki tano nchini Marekani na Uingereza, timu yake iligundua kuwa wale walioripoti kunywa pombe nyingi kwa kipindi cha miaka kadhaa walikuwa na hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa wa dementia.
Hii inafuatia utafiti ambao kundi hilo hilo lilichapisha mwaka wa 2017, ambao ulionyesha uhusiano kati ya unywaji wa pombe na hatari ya dementia miongoni mwa watu wazima 550. Katika utafiti huo, hakuna hata mmoja wa washiriki aliyekuwa akinywa pombe kupita kiasi cha wastani.
Profesa David Nutt – mkurugenzi wa kitengo cha neuropsychopharmacology katika Chuo cha Imperial College London, ambaye hakushiriki katika utafiti wa Topiwala , anaelezea utafiti huo wa mwaka 2017 kama "ushahidi bora zaidi wa kuzeeka kwa kasi" unaohusishwa na pombe ambao wanasayansi wanao.
"Unaonyesha kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya unywaji wa pombe na kupungua kwa ukubwa wa ubongo kwa kipindi cha takriban miaka 40," anasema. "Watu hawa si walevi sugu. Wanaendelea na maisha yao ya kawaida na kufanya kazi kama watumishi wa umma. Lakini pombe ina athari hii mbaya."

Chanzo cha picha, THOM LEACH / SCIENCE PHOTO LIBRARY via Getty
Nutt anaeleza kuwa, katika utafiti wake mwenyewe, amelinganisha ubongo wa watu wenye uraibu wa dawa mbalimbali, ikiwemo pombe, heroini, kokaini na bangi.
"Pombe ndiyo dawa inayohusishwa zaidi na kupungua kwa ukubwa wa ubongo," anasema. "Ni watu walio katika hatua mbaya zaidi ya uraibu wa pombe pekee ndio wanaoonyesha uharibifu wa ubongo unaoweza kuonekana wazi."
Kwa hakika, Nutt anaongeza kuwa picha za skani ya ubongo za watu wenye matatizo makubwa ya matumizi ya pombe zinafanana kabisa na zile za watu wenye ugonjwa wa Alzheimer, "kwa sababu ubongo wao unakufa."
Kuna sababu mbalimbali za jambo hili. Nutt anaeleza kuwa pombe ni sumu, hivyo inaweza kuua seli moja kwa moja na pia kuharibu DNA iliyo ndani yake,jambo linalofupisha telomeres na kuongeza hatari ya kupata saratani.
Pombe pia husababisha uvimbe mwilini, hali inayopelekea kuchakaa zaidi kwa mwili. Viwango vya juu vya uvimbe kwenye ubongo vinaaminika kuwa sababu kuu ya hatari ya kupata shida ya akili.
Si hayo tu, bali mwili hubadilisha pombe kuwa kemikali iitwayo acetaldehyde, ambayo, kulingana na Nutt, "hufanya ubongo wako kuwa kama kitu kilichohifadhiwa kwenye siki ,na pia hufanya hivyo kwa ini na moyo wako."
Acetaldehyde ni kaboni moja tu tofauti na formaldehyde, kemikali inayotumika kuhifadhi miili ya marehemu.
"Kwa hivyo, acetaldehyde inakuhifadhi kabla hata hujafa," anasema Nutt, na kuongeza, "jambo ambalo hutaki litokee," kwa sababu kemikali hiyo husababisha protini kwenye ubongo kushikamana pamoja. Hali hiyo ingefaa kama ungekuwa maiti iliyohifadhiwa ya Misri , lakini ikiwa bado unataka kutumia protini hizo kwa muda mrefu zaidi, itafanya utendaji kazi wa mwili kuwa wa taratibu.
"Maiti zilizohifadhiwa mummies zimekuwepo kwa maelfu ya miaka, lakini hazifanyi kazi wala kuitikia mambo kwa haraka," anasema.
Hatimaye, unywaji wa pombe unaweza kusababisha shinikizo la juu la damu, hali inayoongeza hatari ya kupata mshtuko wa moyo, magonjwa ya moyo, na aina ya shida ya akili inayotokana na matatizo ya mishipa ya damu.
Athari zinazochochea mambo mengine
Pombe inaweza kuharakisha kuzeeka kwa miili yetu kibaolojia na kuongeza kasi ya kudorora kwa utendaji wa ubongo kunakotokana na umri lakini hayo si yote.
Pia inaweza kuathiri mambo mengine ambayo nayo yanaweza kuathiri umri wetu wa kibaolojia na muda tutakaoishi.
Dkt. Jeevan Fernando, daktari na mshirika wa shirika la hisani la Alcohol Change UK, anasema, "Kupunguza unywaji wa pombe kunaboresha ubora wa usingizi, viwango vya nishati, ukali wa akili na hali ya hisia," jambo linaloweza kusaidia "kuweka misingi imara ya kujenga tabia njema za kiafya, kama vile mazoezi na lishe bora, zinazoongeza muda wetu wa kuishi."
Mambo haya yote ni muhimu kwa muda wetu wa kuishi, na hii ndiyo sababu kuu inayofanya unywaji wa pombe kuhusishwa moja kwa moja na muda unaotarajiwa wa kuishi. Mwaka 2024, utafiti uliohusisha watu wazima milioni 2.4 barani Ulaya ulibaini kuwa wale waliokunywa pombe zaidi waliishi muda mfupi zaidi ,hata baada ya wanasayansi kuzingatia mambo mengine katika uchambuzi wao, kama vile uvutaji wa sigara.

Chanzo cha picha, Oscar Wong via Getty
Hakuna kiasi chochote cha pombe kilicho salama
Basi, ni kiasi gani cha pombe tunachoweza kunywa kwa usalama bila kuhatarisha madhara haya mabaya? Jibu fupi ni, hakuna kiasi chochote. Angalau, ndivyo Topiwala anavyoamini.
"Ni vigumu sana kuthibitisha hili, lakini nimefikia hitimisho kwamba hakuna kiwango salama cha matumizi ya pombe," anasema. "Hiyo ina maana kwamba ni suala la ni kiasi gani cha hatari uko tayari kukubali ili kupata burudani itokanayo na unywaji. Ikiwa unataka kuepuka kabisa hatari inayotokana na pombe, basi usinywe."
Nutt anakubaliana na hilo, akiongeza: "Kadiri unavyokunywa kidogo, ndivyo unavyoishi muda mrefu zaidi." Hata hivyo, anasema, kadiri unavyokunywa pombe nyingi ndivyo madhara yanavyokuwa makubwa zaidi ,hivyo, kunywa kiasi kidogo tu ni jambo "salama kiasi."
Kwa upande wa vipimo, hiyo inamaanisha kunywa ndani ya viwango vinavyopendekezwa kwa wiki. Nchini Uingereza, Huduma ya Afya ya Taifa (NHS) inashauri kutokunywa zaidi ya vipimo 14 vya pombe kwa wiki. Hiyo ni sawa na pinti sita za bia au glasi nane za divai.
Nchini Marekani, Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vinapendekeza kutokunywa zaidi ya vinywaji viwili vya pombe kwa siku kwa wanaume, na kutokunywa zaidi ya kinywaji kimoja kwa siku kwa wanawake.
Nutt ana ushauri zaidi. Anasema kwamba, ikiwa unakunywa kiwango kamili cha vipimo 14 vya pombe kwa wiki, ni vyema kugawanya kiasi hicho katika siku zisizopungua tatu ,na kuhakikisha una siku moja au mbili kwa wiki ambazo hunywi pombe kabisa.
"Kunywa pombe kupita kiasi kwa mkupuo mmoja ni hatari kwa ubongo," Nutt anaeleza, "na kutokunywa kabisa kunasaidia ini kupata nafuu."
Ikiwa unakunywa divai na mwenzi au rafiki wakati wa mlo, anashauri kutumia chupa moja tu. Ukifungua ya pili, kuna uwezekano mkubwa wa kunywa kupita kiasi. Nutt anashauri kutokunywa kiasi kikubwa kiasi cha kupata maumivu ya kichwa na madhara mengine ya baada ya kunywa .
Na anaongeza: "Usinywe kinywaji ambacho hakikuletei faida. Hiyo ina maana, usinywe peke yako."
Pombe huharibu ubongo, lakini kushirikiana na marafiki kuna faida za kiafya; hivyo Nutt anashauri kutoka na marafiki lakini ukachagua vinywaji visivyo na kilevi, ili kupata faida hizo kwa ukamilifu.
Kwa njia hiyo, utabaki kijana na mwenye uchangamfu kwa muda mrefu iwezekanavyo, bila kulemewa na athari za pombe.















