Yafahamu magonjwa mawili yanayowahangaisha wanawake kupata watoto

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Polyendocrine Metabolic Ovarian Syndrome (PMOS), ambalo zamani lilijulikana kama Polycystic Ovary Syndrome (PCOS), ni hali ya kiafya inayoathiri ovari na kuvuruga homoni na huwapata wanawake, hasa wale walio katika umri wa kujifungua. Hali hii huathiri hedhi, ngozi, uzito, na uwezo wa kupata ujauzito.

Tatizo hili hutokea pale kunapokuwa na ukosefu wa uwiano wa homoni mwilini mwa mwanamke, hali inayozuia mayai kukua na kuachiliwa ipasavyo.

Hali hii pia inahusiana na mchakato wa ovari kuachilia yai (ovulation).

Fibroidi ni tatizo ambalo baadhi ya watu hulifananisha na 'ugonjwa wa kulala' (kutokana na mwenendo wa dalili zake kutoonekana dhahiri kwa muda mrefu).

Ni uvimbe unaojitokeza katika mfuko wa uzazi wa mwanamke na kukua hadi kufikia hatua ya kusababisha matatizo mengine.

Tofauti kati ya PMOS na fibroids ni ipi?

Dkt. Bilal Suleiman, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake anayefanya kazi katika Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Abuja, Gwagwalada, alisema kuna mambo kadhaa yanayotofautisha magonjwa haya:

  • Kwanza, PMS ni tatizo linaloathiri ovari, huku fibroids (uvimbe wa nyuzi-misuli ya kizazi) zikiwa ni tatizo linalojitokeza ndani ya mfuko wa uzazi (uterasi).
  • -Pili, daktari anasema kuwa homoni inayohusishwa na fibroids inaitwa estrojeni; hii ni homoni inayopatikana kwa wanawake wengi na humsaidia mwanamke kuwa na sifa kamili za kike. Kiwango kikubwa kupita kiasi cha homoni hii husababisha ukuaji wa uvimbe ndani ya mfuko wa uzazi. Kuhusu PMOS, homoni inayohusishwa nayo ni androjeni. Hii ina maana kwamba homoni zinazohusika katika matatizo haya ni tofauti.
  • -Tofauti ya tatu inayotofautisha matatizo haya ni katika hali ya kutokwa na damu ya hedhi kwa wanawake. Mwanamke mwenye fibroids atagundua kuwa anatokwa na damu nyingi—wakati mwingine kwa mkupuo mmoja—na siku za hedhi huongezeka. Kwa mwanamke mwenye PCOS, hedhi yake huwa haifuati utaratibu maalumu; yaani inaweza kuja leo kisha ikakatika, au ikaja wiki hii na kukatika, kisha ikarudi tena baada ya wiki mbili.

Wakati mwingine, mwanamke anayekabiliwa na ugonjwa huu anaweza kukosa hedhi kwa miezi miwili au mitatu, tofauti na wale wenye uvimbe kwenye nyumba ya uzazi (fibroids) ambao hupata hedhi ya kawaida kila mwezi.

Daktari Suleiman anasema kuwa wakati mwingine mwanamke mwenye PCOS anapopata hedhi—hasa ikiwa alikosa kwa miezi miwili au mitatu—hutokwa na damu nyingi, hali amabyo humfanya kulazimika hata kufanyiwa upasuaji wa kuondoa kizazi. Hata hivyo, uvimbe wa nyumba ya uzazi hausababishi kutokwa na damu kila wakati.

Aliongeza, "Mwanamke anayeugua maradhi ya PCOS asipopati hedhi kwa miezi miwili hadi mitatu, wakati mwingine hudhani kuwa ana mimba."

Daktari huyo anasema kuwa jambo lingine linalotofautisha magonjwa haya ni kwamba kwa mwanamke aliye na uvimbe wa nyuzi za misuli ya kizazi (fibroids), uvimbe huo unapokuwa mkubwa zaidi, unaweza kubana kibofu cha mkojo au bomba linaloungana na njia ya haja kubwa.

Kulingana naye, hii ina maana kwamba mwanamke anapohitaji kwenda haja ndogo katika hatua hii, atahisi maumivu au atapata kiasi kidogo tu cha mkojo; vilevile, anapokwenda chooni, kwa kuwa uvimbe huo umelibana bomba linaloungana na njia ya haja kubwa, atashindwa kujisaidia haja kubwa bila kupata shida. Hata hivyo, PCOS—ambayo si uvimbe—haisababishi matatizo haya kwa sababu huathiriwa zaidi na kemikali mwilini.

Uhusiano kati ya PMOS na Fibroid

Dk Bilal Suleiman, anasema kuna baadhi ya mambo ambayo magonjwa hayo yanahusiana au kufanana navyo.

Ya kwanza alisema, "magonjwa haya yote yanahusiana na matatizo ya uzazi, akimaanisha ugumba, ingawa alisema kuwa fibroids haihusiani moja kwa moja na ugumba."

Hata hivyo, katika hali nyingi, ikiwa inakua kubwa sana katika uterasi, mtoto hawezi kupandwa, na wakati mwingine tube ambayo hubeba manii kwenye yai inaweza kuzuiwa na fibroids.

Hii itafanya kuwa haiwezekani kwa mwanamke kupata mjamzito.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Daktari alisema kuwa PCOS ni ugonjwa unaoathiri ovari za mwanamke, kiasi kwamba hawezi kutoa yai kabla ya hedhi yake. Kwa kawaida, mwanamke hutoa yai moja kila mwezi, lakini mwanamke anayakabiliwa na maradhi ya PCOS halitoi, hali inayomzuia kupata ujauzito.

Bingwa huyo wa magonjwa ya wanawake alisema kuwa jambo linalofanya magonjwa haya kuhusiana na kwamba mwathiriwa hutokwa na damu nyingi, hasa wakati wa hedhi. Alisema kuwa yote husababisha mwanamke kuvuja damu zaidi ya kawaida, na wakati mwingine kusababisha kuvuja damu kupita kiasi.

Hata hivyo, Dkt. Bilal anasema kuwa magonjwa hayo hayahusiani na saratani ya shingo ya kizazi, na kwamba baadhi ya dawa zinazotumiwa kudhibiti uvujaji wa damu kwa wagonjwa wenye matatizo haya ni zilezile.

Je, ni zipi dalili za magonjwa haya?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Dkt. Bilal anasema kuwa baadhi ya wanawake wana uvimbe wa nyuzi za misuli ya kizazi (fibroids) lakini hawajui kama wanao, kwa sababu uvimbe huo unaweza kuwa mdogo sana usio na madhara yoyote. Hata hivyo, uvimbe huo ukianza kukua au mwanamke akianza kuhisi dalili nyingine mwilini mwake, anamshauri kwenda hospitalini kwa uchunguzi, kubaini kama anao.

Alisema, "Miongoni mwa dalili ambazo mwanamke anaweza kuziona ni kuvimba kidogo kwa sehemu ya chini ya tumbo lake—yaani eneo la uke—ambapo ukiguswa huhisiwa kuwa mgumu au imara na hauumi; na iwapo uvimbe huo ni mkubwa sana, husababisha kutoka damu nyingi wakati wa hedhi."

"Inaweza pia kuzuia mimba au kusababisha mimba kuharibika. Na iwapo uvimbe huo (fibroids) utakuwa mkubwa sana, unaweza kubana kibofu cha mkojo cha mwanamke, na kusababisha ashindwe kukojoa au apate shida wakati wa kukojoa, na hatimaye kushindwa kuhifadhi mkojo. Pia, kunaweza kutokea maumivu ya nyonga iwapo uvimbe huo utakuwa mkubwa mno."

Kwa mwanamke mwenye tatizo la PCOS, dalili zake—kama daktari alivyoeleza—zinajumuisha utasa na *amenorrhea* (hali ambapo mwanamke hukaa miezi kadhaa bila kupata hedhi), pamoja na kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi.

Dkt. Bilal pia anaongeza kuwa dalili nyingine za PCOS ni pamoja na chunusi, hasa usoni, na kuota kwa nywele kwa mtindo unaofanana na wa wanaume. Mwanamke mwenye PCOS anaweza kumea masharubu au ndevu zikianza kuota hatua kwa hatua, pamoja na kuota kwa nywele kifuani au nywele za sehemu ya mbele ya mwili kuenea hadi kufikia eneo la sehemu za siri.

Pia wanaweza kupata msongo mkubwa wa mawazo, kutokwa na jasho wakati ambapo kwa kawaida hawapaswi kutokwa na jasho, na hali hiyo ikizidi kuwa mbaya, sauti yao inaweza hata kubadilika na kuwa kama ya mwanamume.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Daktari alisema kuwa wanawake wenye uzito uliopitiliza wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kupata tatizo la PCOS; ndiyo maana mara kwa mara wanashauriwa kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia lishe na mazoezi, kwani hata wakipewa dawa, huenda zisifanye kazi ipasavyo.

Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya wanawakepia anasema kuwa mwanamke aliye na uvimbe wa kizazi (fibroids) anaweza kupona kwa sababu huo ni uvimbe unaoweza kuondolewa, lakini mwanamke aliye na maradhi ya PCOS hawezi kupona kabisa—kama ilivyo kwa ugonjwa wa kisukari—isipokuwa kwa kutumia dawa. Hii ni kwa sababu tatizo hilo linahusisha mfumo wa kemikali mwilini, ingawa dawa hutolewa ili kupunguza ukali wa dalili zake.

Imetafsiriwa na Ambioa Hirsi