Habari za hivi punde, Helikopta mbili zagongana wakati wa operesheni ya kuzima moto Ugiriki
Chanzo cha picha, Reuters
Mamlaka nchini Ugiriki zinaendelea na operesheni ya
utafutaji na uokoaji baada ya helikopta mbili zilizokuwa zikishiriki shughuli
za kuzima moto kugongana angani.
Tunachojua kufikia sasa
Helikopta
mbili zilihusika katika ajali, kila moja ikiwa na wahudumu wawili ndani
yake, kwa mujibu wa kikosi cha zimamoto.
Katika
taarifa yake, kikosi hicho kimesema helikopta hizo ni za aina ya Bell na
zilikuwa zimekodishwa na idara ya zimamoto.
Ajali
hiyo ilitokea katika eneo la Psatha, magharibi mwa mji mkuu wa Athens.
Operesheni
ya utafutaji na uokoaji inaendelea huku mamlaka zikiendelea kufuatilia
hali ya wahusika.
Tusichokijua
·Bado haijafahamika ni nini kilisababisha
helikopta hizo kugongana.
·Hali ya wahudumu waliokuwa ndani ya helikopta
hizo bado haijathibitishwa, wala utambulisho wao haujatolewa hadharani.
Ndege iliyokuwa na watalii 13 yaanguka Peru
Chanzo cha picha, EPA
Ndege ndogo
iliyokuwa imewabeba watalii imeanguka nchini Peru, na kusababisha vifo vya watu
wote 13 waliokuwa ndani yake, kwa mujibu wa maafisa wa serikali na vyombo vya
habari vya nchini humo.
Ndege hiyo
ya aina ya Cessna Caravan C-208 ilikuwa ikipaa juu ya eneo maarufu la
kihistoria la Nazca Lines wakati ilipoanguka siku ya Jumamosi. Ilikuwa
imewabeba abiria 11 pamoja na marubani wawili.
Miongoni mwa
waliokuwa ndani ya ndege hiyo walikuwa watalii wawili kutoka Ujerumani, wawili
kutoka Hispania na saba kutoka Italia.
Mamlaka
nchini Peru zimesema chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika, huku uchunguzi
ukiendelea.
Nazca Lines,
ni eneo la Urithi wa Dunia wa UNESCO kusini mwa Peru, na huvutia maelfu ya
watalii kila mwaka. Eneo hilo linajulikana kwa michoro mikubwa ya kale ya
wanyama na maumbo mbalimbali iliyochorwa kwenye mchanga wa jangwani, na watalii
wengi hutumia ndege ndogo kutazama michoro hiyo kutokea angani.
Feri yateketea baharini Indonesia, watu wafariki na wengine hawajulikani walipo
Chanzo cha picha, Getty Images
Watu watano
wamefariki dunia huku wengine 41 wakiripotiwa kutoweka baada ya feri iliyokuwa
imebeba zaidi ya abiria 250 kushika moto ikiwa baharini nchini Indonesia.
Kwa mujibu
wa mamlaka za uokoaji, nahodha wa feri hiyo aliripoti moto huo uliozuka karibu
na kisiwa cha Madura, wakati chombo hicho kikisafiri kutoka Surabaya katika
jimbo la Java Mashariki kuelekea Makassar huko Sulawesi Kusini.
Picha
zilizoonyeshwa na vyombo vya habari vya Indonesia zimewaonyesha abiria wengi
wakiwa wamevaa makoti ya kujiokoa wakisubiri msaada kwenye boti za uokoaji.
Video
nyingine zimeonyesha baadhi ya watu wakishuka kutoka kwenye feri hiyo huku
miali mikubwa ya moto na moshi mzito ukionekana ukifuka kutoka sehemu ya juu ya
feri.
Shirika la
Kitaifa la Uokoaji la Indonesia (Basarnas) limesema moto huo ulianza kati ya
saa 12:00 na 1:00 asubuhi GMT.
Mamlaka
zilisema sehemu kubwa ya feri hiyo ilighubikwa na moto, huku baadhi ya abiria
wakisalia katika sehemu ya mbele ya chombo wakisubiri kuokolewa.
Chanzo cha
moto huo bado hakijafahamika, huku operesheni ya kuwatafuta waliopotea
ikiendelea.
Waziri Mkuu
wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani, amesema serikali yake haitaruhusu ardhi ya
nchi hiyo kutumika kushambulia au kutishia mataifa jirani.
Akiongoza
kikao cha dharura kilichojadili hali ya usalama katika eneo hilo, Sudani
aliamuru kuundwa kwa kamati ya pamoja ya usalama pamoja na kuandaliwa kwa hatua
za kuzuia vitendo kama hivyo kutokea tena.
Pia aliagiza
vyombo vya usalama kuhakikisha sheria zinafuatwa kuimarisha amani na usalama,
pamoja na kulinda mamlaka ya Iraq na uhusiano wake mzuri na nchi jirani.
Taarifa
iliyotolewa baada ya kikao hicho ilisema vikosi vya usalama vya Iraq vimewekwa
katika hali ya tahadhari ili kuzuia jaribio lolote la kutumia ardhi ya nchi
hiyo kuhatarisha usalama wa mataifa ambayo Baghdad imeyataja kuwa "marafiki
na ndugu zake."
Rubio: Mabadiliko ya utawala wa Iran hayamaanishi kuipindua serikali
Chanzo cha picha, Reuters
Waziri wa
Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa mazungumzo kuhusu "mabadiliko
ya utawala" nchini Iran hayamaanishi lazima kuiondoa serikali iliyopo
madarakani, bali yanahusu kubadili tabia na mwelekeo wa uongozi wake.
Akizungumza
na Fox News, Rubio alisema huenda kusiwe na mabadiliko ya utawala kwa maana ya kupindua
serikali, lakini akaongeza kuwa sera na mwenendo wa utawala wa Iran vinapaswa
kubadilika.
Rubio alidai
kuwa kwa miaka mingi Iran imekuwa ikifuata sera za kupanua ushawishi wake nje
ya mipaka yake, akisema lengo lake si kuitawala Iran pekee bali pia kuwa na
nguvu kubwa katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Alisisitiza
kuwa hali hiyo inapaswa kubadilika, na kwamba njia pekee ya kuilazimisha Iran
kubadili mwelekeo wake ni kuiwekea gharama ambazo haiwezi kuendelea kuzibeba.
Kwa mujibu
wa Rubio, kubadili jinsi serikali ya Iran inavyojiendesha ni jambo tofauti na
kuangusha utawala wake, kwani mabadiliko ya tabia na sera ni mchakato unaoweza
kuchukua muda mrefu
Rubio
alisema makubaliano ya nyuklia yanaweza kufikiwa na kufuatiliwa kwa urahisi,
lakini kuifanya Iran iachane na sera zake za ushawishi katika Mashariki ya Kati
ni kazi ya muda mrefu, jambo linalomaanisha kuwa shinikizo dhidi ya Tehran
linaweza kuendelea kwa kipindi kisichojulikana
Kwa nini Iran inaficha hata sauti ya kiongozi wake mpya?
Chanzo cha picha, Getty Images
Gazeti la Hamshahri,
linalomilikiwa na Manispaa ya Tehran, limesema sababu ya kutotolewa kwa sauti ya
Mojtaba Khamenei, kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni hofu ya
uwezekano wa kufuatiliwa na huduma za kijasusi kupitia teknolojia za kisasa.
Gazeti hilo
linaeleza kuwa mwangwi unaopatikana kwenye rekodi za sauti unaweza kutoa
taarifa kuhusu eneo au chumba ambako sauti hiyo ilirekodiwa.
Gazeti la Hamshahri
pia limedai kuwa mashirika ya kijasusi yanaweza kutumia mabadiliko madogo ya
mfumo wa umeme uliopo kwenye rekodi za sauti kubaini nchi, tarehe, muda na hata
eneo husika lilipofanyika rekodi hiyo.
Mbali na
hilo, aina ya kifaa kilichotumika kurekodi sauti nayo inaweza kutoa taarifa
muhimu. Kila simu au kifaa cha kurekodi kina sifa zake za kipekee ambazo
zinaweza kutumika katika utambuzi kama alama ya vidole.
Gazeti hilo
limeongeza kuwa sauti za mazingira kama upepo, ndege, wadudu au mifumo ya
uingizaji hewa zinaweza kusaidia kubaini eneo la kijiografia la aliyerekodiwa.
Tangu Mojtaba
Khamenei ateuliwe kuwa kiongozi wa tatu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,
hajaonekana hadharani, hakuna picha mpya wala sauti yake iliyotolewa, huku
vyombo vya habari vya Iran vikichapisha tu ujumbe wa maandishi unaodaiwa kutoka
kwake.
Bin Salman aisihi Marekani kuyapa kipaumbele mazungumzo badala ya vita
Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika
rasmi la habari la Saudi Arabia, Axios, limethibitisha kuwa Mwanamfalme Mrithi Mohammed
bin Salman amefanya mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump, ambapo
viongozi hao walijadili hali ya usalama na maendeleo ya hivi karibuni katika
eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, Bin Salman alisisitiza umuhimu wa kuipa kipaumbele njia ya
mazungumzo na diplomasia ili kupunguza mvutano unaoendelea kuongezeka katika
ukanda huo.
Mwanamfalme
huyo pia alitoa wito wa kufanyika kwa juhudi zote zinazowezekana ili kurejesha
utulivu, akisema hali hiyo inaweza kufungua njia ya suluhisho za kidiplomasia
huku ikilinda usalama na uthabiti wa eneo hilo.
Aidha,
alionya kuhusu hatari ya kuenea kwa vita ambayo inaweza kuathiri si tu
Mashariki ya Kati bali pia usalama na uthabiti wa kimataifa.
Rais Trump
alikuwa amesema mwishoni mwa Jumamosi kuwa shambulizi kubwa la kijeshi dhidi ya
Iran lilikuwa limepangwa, lakini baadaye akatangaza kwamba Marekani na Israel
zitasitisha kwa sasa hatua hiyo baada ya ombi kutoka Iran na baadhi ya mataifa
ya Mashariki ya Kati ili kutoa nafasi kwa mazungumzo.
Mashambulizi ya Israel gaza yaua wapalestina wanane usiku mmoja
Chanzo cha picha, Getty Images
Wapalestina takriban
wanane waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel yaliyolenga majengo ya
makazi katika Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia Jumapili, na kufanya idadi ya
waliouawa katika kipindi cha siku mbili za mashambulizi kufikia 16, kwa mujibu
wa vyanzo vya ulinzi wa kiraia na afya vya Gaza.
Msemaji wa
ulinzi wa kiraia, Mahmoud Bassal, alisema mwanaume mmoja na mke wake waliuawa
huku watu wengine wanne wakijeruhiwa baada ya helikopta ya jeshi la Israel
kushambulia nyumba kusini mwa Deir al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza.
Aliongeza
kuwa mzee mmoja na mtoto mmoja waliuawa katika shambulio jingine lililolenga
jengo la makazi magharibi mwa Mji wa Gaza.
Katika tukio
tofauti, watu watatu, akiwemo mtoto mmoja, waliuawa baada ya jengo la makazi
kushambuliwa kaskazini-magharibi mwa Khan Younis, kusini mwa Gaza.
Vituo vya
afya na ulinzi wa kiraia pia viliripoti kuwa Wapalestina wengine wanane
waliuawa katika mashambulizi mengine ya Israel yaliyofanyika siku ya Jumamosi.
Miongoni mwa
maeneo yaliyolengwa ni ghala la kuhifadhi dawa na vifaa tiba la Hospitali ya
Al-Aqsa Martyrs mjini Deir al-Balah, ambapo Wizara ya Afya ya Gaza ilisema
shambulio hilo lilisababisha uharibifu mkubwa.
Awali, Wamarekani walitahadharishwa kujiandaa kuondoka mashariki ya kati
Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya
Marekani ilichukua hatua na kuwatahadharisha raia wake walioko Mashariki ya
Kati kuwa waangalifu na kuwa tayari kuondoka endapo hali ya usalama katika eneo
hilo itazidi kuwa mbaya.
Tahadhari
hiyo imetolewa wakati kulipokuwa na ripoti kwamba Rais Donald Trump huenda
akapanga mashambulizi mapya makali dhidi ya Iran mwishoni mwa wiki.
Katika
taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa vituo vya
kidiplomasia vya Marekani, ikiwemo vile vilivyo nje ya Mashariki ya Kati,
vimewahi kulengwa hapo awali.
Pia ilionya
kuwa Iran na makundi yanayoiunga mkono yanaweza kulenga maslahi ya Marekani au
maeneo yanayohusishwa na raia wa Marekani duniani kote.
Awali, Iran
iliishutumu Marekani kwa kuongeza mvutano katika eneo hilo, ikionya kuwa nchi
yoyote itakayoshirikiana na Washington anaweza "kumezwa na vita"
hivyo.
Hata hivyo,
baadaye, Trump alisitisha mpango wa kufanya mashambulizi dhidi ya Iran kwa
sharti kwamba makubaliano yafikiwe "haraka" kati ya pande hizo mbili.
Kupitia
ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema aliamua "kufuta
shambulio hilo, mradi tu iwezekane kufikiwa kwa MAKUBALIANO kwa haraka",
ambayo yatajumuisha kufunguliwa mara moja kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz na
kumalizika kwa kile alichokiita "tishio la nyuklia la Iran."
Licha ya vikwazo, meli ya Urusi yatua Mali na magari ya kijeshi
Vikosi vya
Urusi na Mali vinavyopambana na waasi kaskazini mwa Mali vimepokea msafara
mkubwa wa magari ya kijeshi, ambayo yanaonekana kusafirishwa na meli ya mizigo
ya Urusi iliyowekewa vikwazo, uchunguzi wa BBC Verify umebaini.
Msafara
mkubwa wa magari ya kivita ulionekana ukiwasili jijini Bamako katika video
zilizothibitishwa na kuonyeshwa na televisheni ya taifa ya Mali tarehe 25
Julai. Waandishi wa habari waliripoti kuwa msafara huo ulisafiri kutoka bandari
ya Lomé nchini Togo.
Kwa mujibu
wa taarifa za ufuatiliaji wa meli zilizochambuliwa na BBC Verify, meli ya
mizigo ya Urusi Mikhail Britnev, ambayo imewekewa vikwazo, ilitia nanga katika
bandari ya Lomé tarehe 9 Julai. Picha za satelaiti zinaonyesha kuwa meli hiyo
huenda ilikuwa imebeba malori ya kijeshi, magari ya kubeba wanajeshi yenye
silaha pamoja na magari mepesi ya kivita yanayofanana na yale yaliyoonekana
jijini Bamako.
Taarifa za
ufuatiliaji wa meli zinaonyesha kuwa meli Mikhail Britnev iliondoka katika
bandari ya Baltiysk nchini Urusi tarehe 18 Juni, ikapitia Bahari ya Kaskazini
kabla ya kuingia katika Mfereji wa Uingereza."
BBC Verify
imeelezwa kuwa meli hiyo ilisindikizwa kupitia mfereji wa Uingereza na manowari
ya kivita ya Urusi ya daraja la Ropucha. Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imekataa
kutoa maoni kuhusu taarifa hizo.
Wachambuzi
wanasema usafirishaji huo unaonyesha kuwa Urusi inaongeza msaada wake kwa utawala
wa kijeshi wa Mali, ambayo imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi makubwa kutoka
kwa waasi wanaoongozwa na kundi la jihadi la Jama'at Nusrat al-Islam
wal-Muslimin (JNIM) pamoja na waasi wa Kitouareg. Mashambulizi hayo yamewezesha
waasi hao kuteka maeneo makubwa kaskazini mwa nchi.
Urusi
imekuwa ikiisaidia serikali ya kijeshi ya Mali tangu kuondoka kwa vikosi vya
Ufaransa mwaka 2022, ikipokea malipo ya fedha pamoja na upendeleo wa kufikia
migodi na machimbo ya dhahabu nchini humo.
Awali, kundi
la mamluki la Wagner lilikuwa likifanya operesheni zake Mali, lakini shughuli
hizo baadaye zilichukuliwa na Africa Corps, kikosi kinachosimamiwa na Wizara ya
Ulinzi ya Urusi.
Serikali ya
kijeshi ya Mali imepata pigo mara kadhaa katika uwanja wa mapambano katika wiki
za hivi karibuni.
Siku ya
Jumatano, shirika la Amnesty International liliitaka kufanyika uchunguzi wa
uhalifu wa kivita kufuatia madai ya kuuawa kwa takriban wanajeshi 19 wa Mali
baada ya kuvamiwa mapema mwezi huu.
Uganda yafanikiwa kudhibiti Ebola huku DRC ikiendelea kupambana na mlipuko huo hatari
Chanzo cha picha, Getty Images
Uganda imefanikiwa kudhibiti Ebola na kwa sasa haina
maambukizi ya ugonjwa huo, huku hali ikiwa tofauti nchini DRC ambako mlipuko
unaendelea kuenea na idadi ya vifo vilivyothibitishwa ikizidi 1,500.
Maafisa wa afya nchini Uganda wanasema mafanikio hayo
yametokana na utambuzi wa haraka wa wagonjwa, ufuatiliaji wa waliokutana na
maambukizi, pamoja na kuweka wagonjwa kwenye vituo maalum vya matibabu kabla ya
ugonjwa kusambaa kwenye jamii.
Kati ya wagonjwa 20 waliothibitishwa kuwa na Ebola nchini
Uganda tangu mwezi Mei, wengi walikuwa wametokea DRC. Hata hivyo, mamlaka
zinasema hatua za haraka zilisaidia kuzuia maambukizi makubwa ndani ya nchi.
Wakati huo huo, DRC inaendelea kukabiliana na changamoto za
usalama, uhamaji wa watu na ugumu wa kufuatilia mawasiliano ya wagonjwa, hali
ambayo imechangia kuenea kwa virusi hivyo katika baadhi ya maeneo
yaliyoathirika.
Licha ya kutangaza kutokuwa na wagonjwa wa Ebola kwa sasa,
Uganda imeendelea kuimarisha uchunguzi mpakani na imetuma wahudumu wa afya
nchini DRC kusaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko huo, huku ikisisitiza kuwa
tishio la ugonjwa huo bado halijaisha.
Watu watatu
wamefariki dunia na wengine 21 kujeruhiwa baada ya bomu lililotengenezwa kienyeji
kulipuka katika mgahawa wa Kiitaliano jijini Moscow, kwa mujibu wa vyombo vya
habari vya serikali ya Urusi vilivyonukuu maafisa wa usalama.
Mlipuko huo
ulitokea majira ya saa nane usiku kwa saa za Moscow katika eneo la Kudrinskaya,
karibu na katikati ya jiji.
Kamati ya
Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi ya Urusi (NAK) imesema mwanamke aliyekuwa
amebeba vilipuzi alijaribu kuingia ndani ya mgahawa huo lakini akazuiwa na
mlinzi wa usalama. Kifaa hicho kililipuka na kusababisha vifo vya mwanamke
huyo, mlinzi pamoja na mteja mmoja wa mgahawa huo.
Mgahawa huo,
uliopo ndani ya moja ya majengo maarufu ya enzi ya Stalin jijini Moscow,
ulikuwa ukiandaa hafla binafsi wakati wa tukio hilo.
Mamlaka
hazijatoa taarifa kuhusu orodha ya wageni waliohudhuria hafla hiyo wala kueleza
ni nani aliyelengwa na shambulio hilo.
Mashahidi
wamesema waliona watu wakitolewa eneo la tukio wakiwa wamejaa damu kufuatia
mlipuko huo.
Ripoti za
awali zilidai mlipuko ulitokea jikoni, lakini baadaye uongozi wa mgahawa
ulisema kuwa "tatizo lilitokea nje ya jengo."
Video
iliyochapishwa na shirika la habari la RIA ilionyesha maafisa wa usalama wenye
silaha nzito wakiwa eneo la tukio, ambalo lilikuwa limezingirwa na kuzuiwa kwa
umma.
Katika miaka
ya hivi karibuni, maafisa kadhaa waandamizi wa jeshi la Urusi wameuawa ndani na
maeneo ya karibu na Moscow, huku serikali ya Urusi ikiilaumu Ukraine kwa
mashambulizi hayo.
Mashambulizi yasitishwa: Trump aitaka Iran kufanya makubaliano haraka
Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa
Marekani, Donald Trump, amesema amesitisha mpango wa kufanya mashambulizi dhidi
ya Iran kwa sharti kwamba makubaliano yafikiwe "haraka" kati ya pande
hizo mbili.
Kupitia
ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema aliamua "kufuta
shambulio hilo, mradi tu iwezekane kufikiwa kwa MAKUBALIANO kwa haraka",
ambayo yatajumuisha kufunguliwa mara moja kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz na
kumalizika kwa kile alichokiita "tishio la nyuklia la Iran."
Trump
alisema uamuzi huo ulifikiwa kwa ushirikiano na Israel. Kauli hiyo
imekuja wakati vyombo vya habari vya Marekani vikiripoti kuwa Marekani ilikuwa
ikifikiria kufanya mashambulizi mapya na makali dhidi ya Iran mwishoni mwa
wiki.
Awali, Iran
iliishutumu Marekani kwa kuongeza mvutano katika eneo hilo, ikionya kwamba
taifa lolote la kikanda litakaloshirikiana na Marekani "litamezwa na vita"
hivyo.
Katika
ujumbe wake, Trump alisema Marekani iko "tayari kabisa kwa hatua za
kijeshi" dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akidai kuwa nguvu, uwezo wa
kijeshi na vitisho vya Marekani vinafikia kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu
Vita vya Pili vya Dunia.
Hata hivyo,
alisema aliamua kusitisha mashambulizi hayo baada ya kuombwa na Iran pamoja na
baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati kusubiri ili kutoa nafasi kwa mazungumzo
ya kufikia makubaliano.
Trump pia
alidokeza kuwa hatua imepigwa katika mazungumzo hayo, akisema kuwa "misingi
ya makubaliano tayari umefikiwa."
"Hatua
hii itajumuisha kufunguliwa mara moja, kikamilifu na bila masharti kwa Mlango
wa Hormuz, pamoja na kumaliza tishio la nyuklia la Iran," Trump aliandika.