Ariana Grande kusitisha kwa muda shughuli zake za hadharani kutokana na kufuatiliwa mara kwa mara

Chanzo cha picha, Getty Images
Ariana Grande anatarajiwa kujiondoa katika shughuli zinazomfanya aonekane hadharani na hatahusika tena katika tamasha la muziki litakalofanyika London baada ya kuhitimisha ziara yake ya *Eternal Sunshine* mwezi ujao.
Mwakilishi wa mwimbaji huyo kutoka Marekani, mwenye umri wa miaka 33, aliambia jarida la *People* kuwa "atapunguza kujionyesha hadharani" mara ziara hiyo itakapomalizika, kufuatia kuonekana kwake kusababisha "uchunguzi na mjadala usioisha wa umma".
Kampuni inayoandaa toleo jipya la tamasha la muziki la Stephen Sondheim, *Sunday in the Park with George*—ambalo linatarajiwa kuonyeshwa katika ukumbi wa Barbican mwaka wa 2027—ilithibitisha kuwa hatahusika tena katika tamasha hilo na kwamba wanaelewa na kuunga mkono uamuzi wake kikamilifu.
Muonekano wa mwili na afya ya Grande vimekuwa mada ya uvumi katika miaka ya hivi karibuni.
Uvumi huo umeongezeka tangu kutolewa kwa albamu yake mpya, *Petal*, siku mbili zilizopita na kuonekana kwake katika vifaa vya kuitangaza albamu hiyo.
Mwakilishi wake alisisitiza kwa jarida la *People* kuwa Grande anatarajia kuhitimisha ziara yake "kwa mafanikio makubwa, akiwa na afya njema na furaha, na kisha kuchukua mapumziko yanayostahili kutokana na kazi na shughuli zinazomfanya aonekane hadharani, ambazo zimesababisha uchunguzi na mjadala usioisha wa umma".



























