Elon Musk ataka kujenga jiji mwezini, ndoto yake inawezekana?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Hivi karibuni, Elon Musk alitangaza mpango wa kujenga mji kwenye Mwezi; alisema kuwa mpango huo unaweza kutekelezwa ndani ya muda usiozidi muongo mmoja na kwamba mji huo utakuwa na uwezo wa kukua na kuendelea kwa kujitegemea.

Elon Musk alisema kuwa badala ya kujikita katika ujenzi wa mji kwenye sayari ya Mirihi (Mars), kampuni ya SpaceX sasa inaelekeza nguvu zake katika kujenga mji kwenye Mwezi.

Ni nini kilisababisha mabadiliko haya, na ni taarifa gani zinazopatikana kuhusu mpango wa kujenga mji huo kwenye Mwezi?

Kwanini mwezini na sio sayari ya Mars

Bado hakuna mpango rasmi na wa kina unaojumuisha michoro ya kiufundi kwa ajili ya mji huu, bali kuna dhana tu ambayo Elon Musk aliishiriki kwenye mtandao wake wa kijamii wa X.

Alipendekeza mpango wa kuanzisha makazi ya kudumu kwa ajili ya binadamu; makazi ambayo yangeweza kukua na kupanuka kadiri muda unavyosonga kwa kutumia rasilimali za Mwezi na kupitia safari za mara kwa mara kwenda huko.

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa X, Bw. Musk alisema lengo hilo linaweza kufikiwa ndani ya "chini ya miaka 10, huku safari ya kwenda Mars ikichukua zaidi ya miaka 20."

"Dhamira ya SpaceX haijabadilika: kupanua uelewa wa binadamu na maisha nje ya Dunia na kuelekea kwenye nyota," alisema.

Musk alieleza kuwa safari ya kwenda Mars ingewezekana tu ikiwa "sayari hizo zingejipanga sambamba kila baada ya miezi 26, jambo ambalo lingechukua takriban miezi sita."

"Kinyume chake, tunaweza kusafiri kwenda mwezini kila baada ya siku 10, safari inayochukua siku mbili tu; hii ina maana kwamba tunaweza kujenga na kukamilisha mji mwezini kwa kasi zaidi kuliko mji kwenye sayari ya Mars," aliongeza.

Elon Musk alisema kuwa dhamira ya SpaceX bado ni kutimiza lengo lake la muda mrefu la kujenga mji kwenye sayari ya Mars, na kwamba mchakato huo utaanza "katika kipindi cha miaka mitano hadi saba ijayo." "Lakini kipaumbele kikubwa ni kuhakikisha mustakabali wa ustaarabu wa binadamu, na mwezi ni njia ya haraka zaidi ya kufikia lengo hilo," aliongeza.

Mashabiki na wafuasi wa Elon Musk kwenye mitandao ya kijamii walitengeneza na kusambaza kwa haraka michoro na taswira zinazoonyesha jinsi mji huo wa mwezini unavyoweza kuonekana.

Baadhi yao walitumia pia zana ya akili bandia ya Elon Musk, iitwayo Grok.

Kauli za Elon Musk zinaendana na ripoti ya gazeti la Wall Street Journal iliyosema kuwa SpaceX iliwaambia wawekezaji wake kuwa inazipa kipaumbele safari za mwezini na kuahirisha safari ya Mars, huku ikipanga kutuisha mwezini chombo kisicho na rubani mnamo Machi 2027.

Mabadiliko haya yanatofautiana na msimamo wa muda mrefu wa Elon Musk wa kuichukulia sayari ya Mars kama lengo kuu la SpaceX.

Mwaka jana, alisema kuwa kampuni hiyo inapanga kuzindua safari isiyo na rubani kuelekea Mars kabla ya mwisho wa mwaka 2026.

"Hapana, tunaenda moja kwa moja Mars. Mwezi ni kitu cha kutukengeusha tu," Bw. Musk alisema katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X mwezi Januari mwaka jana.

Elon Musk ana historia ndefu ya kuweka muda wa utekelezaji wenye malengo makubwa kwa miradi kama vile magari ya umeme na teknolojia ya magari yanayojiendesha yenyewe, ambayo mara nyingi imeshindwa kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Je, ujenzi huo utafanyika vipi?

Dkt. Seongwoo Lim, mhadhiri mkuu wa masuala ya matumizi ya anga, uchunguzi wa anga na vifaa vya anga katika Chuo Kikuu cha Surrey nchini Uingereza, anaelezea mpango wa SpaceX wa kujenga kituo mwezini kuwa ni wa "matarajio makubwa" lakini si "hadithi za kisayansi."

"Wazo ni kutumia udongo wa mwezini kuzalisha oksijeni, maji na vifaa vya ujenzi—michakato ambayo tayari tuna mifano yake hapa Duniani. Kinadharia, inawezekana," aliambia BBC.

Dkt. Lim anaeleza kuwa changamoto kubwa ni iwapo mifumo hiyo inaweza kufanya kazi kwa ufanisi na uhakika katika mazingira magumu ya mwezini, ambayo yanajulikana kwa kuwa na viwango vya juu sana au chini sana vya joto, vumbi laini, mvutano mdogo wa ardhi na rasilimali chache za nishati. "Kabla hatujategemea mifumo hii, tunahitaji kuifanyia majaribio ya kina kwenye uso wa mwezi," anaongeza.

Anabainisha kuwa mashirika ya serikali yanayoshughulikia masuala ya anga huwa yanachukua hatua kwa "tahadhari" kwa sababu yanategemea fedha za umma na mizunguko ya kisiasa ya muda mrefu, jambo ambalo anasema "linapunguza kasi ya kufanyiwa majaribio kwa mawazo mapya." SpaceX, anasema, "inafanya mambo kwa namna tofauti."

"Iwapo mfumo mpya wa roketi wa kampuni hiyo utafanya kazi kama ilivyopangwa, unaweza kusafirisha vifaa hadi Mwezini mara kwa mara na kwa gharama nafuu zaidi, na hivyo kuharakisha maendeleo," anasema.

Dkt. Ugur Goven, mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Anga za Juu na Nishati katika Chuo Kikuu cha J.D. Goenka nchini India, anasema Mwezi una faida moja muhimu kuliko sayari ya Mirihi (Mars) kwa ajili ya makazi ya awali ya binadamu: uwezo wa kutuma vifaa kwa haraka na kushughulikia dharura kwa ufanisi.

"Kukiwa na tatizo lolote na kuna makazi huko, unaweza kutuma mara moja ujumbe wa msaada," aliambia BBC, akibainisha kuwa safari kutoka Duniani hadi Mwezini kwa kawaida huchukua "siku mbili hadi tatu."

Hata hivyo, Dkt. Lim anaonya kuwa kufikia lengo la kuwa na "mji unaojitegemea kikamilifu Mwezini" bado ni jambo la muda mrefu ujao.

"Ni jambo gumu zaidi kuzalisha chakula bila kupunguza virutubisho vya udongo na kuunda mzunguko ambapo kila kitu kinarejelezwa na kutumika tena," anasema. "Huenda ikachukua miongo kadhaa kufikia hatua hiyo. Kwa hivyo ni maono yanayoweza kutimia, lakini yatatekelezwa hatua kwa hatua, si kwa mara moja."

Clive Neal, profesa wa uhandisi wa ujenzi na mazingira pamoja na sayansi ya jiolojia katika Chuo Kikuu cha Notre Dame nchini Marekani, ambaye pia ni mtafiti wa masuala ya uchunguzi wa Mwezi unaofanywa na binadamu, anakubaliana na hilo.

"Hadi pale utafiti wa kina utakapofanyika ili kubaini rasilimali zilizopo Mwezini na kuthibitika kuwa uchimbaji wake una tija kiuchumi, hatuwezi kujua ni wapi mahali pazuri zaidi pa kujenga mji utakaopanuka taratibu, mji unaohitaji rasilimali zinazoweza kufikiwa na kuchimbwa," aliambia BBC.

Dkt. Lim anaamini kuwa kuna uwezekano "halisi" kwamba "kituo kidogo Mwezini" kinaweza kuzalisha oksijeni yake yenyewe na labda hata kuchimba maji ndani ya miaka 10 ijayo. "Hiyo itakuwa hatua kubwa ya mafanikio," anasema.

Jeffrey Hoffman, mwanaanga wa zamani wa NASA na profesa wa sasa wa uhandisi wa anga na usafiri wa anga katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) nchini Marekani, anaamini kuwa iwapo SpaceX na Blue Origin, kampuni ya teknolojia ya anga inayomilikiwa na mwanzilishi wa Amazon, Jeff Bezos, zitafanikiwa kutengeneza vyombo vya kutua Mwezini, "tunaweza kukidhi mahitaji ya usafirishaji na vifaa kwa ajili ya kituo cha Mwezini hivi sasa."

"Lakini Mars bado ni hatua kubwa mno na ya mbali zaidi," aliambia BBC. Hata hivyo, Profesa Jeffrey Hoffman anasema kuwa uzoefu uliopatikana kutokana na ujenzi wa makazi endelevu Mwezini unaweza hatimaye kutumika kuanzisha kituo kwenye sayari ya Mirihi.

Dkt. Goven anakubaliana na hilo, akiongeza kuwa pindi kituo kitakapokuwa kimeanzishwa Mwezini, itakuwa rahisi zaidi kufika sayari ya Mars, kwani Mwezi unaweza kutumika kama "sehemu ya kurukia" (springboard).

Kuongezeka kwa ushindani

Kauli za Musk zinakuja wakati Marekani ikikabiliwa na ushindani unaoongezeka kutoka China katika jitihada za kuwarejesha binadamu Mwezini ndani ya muongo huu.

Hakuna mtu aliyewahi kukanyaga uso wa Mwezi tangu misheni ya Apollo 17 ya NASA mwaka 1972.

Hivi karibuni, Musk alitangaza kuwa SpaceX imeinunua kampuni changa ya xAI, ambayo yeye pia anaiongoza, katika makubaliano yanayokadiria thamani ya kampuni ya roketi na satelaiti ya SpaceX kuwa dola trilioni 1, na ile ya kampuni ya akili bandia (AI) ya xAI kuwa dola bilioni 250.

Kulingana na Michel Fleury wa BBC jijini New York, hatua hiyo inaweza pia kusaidia lengo lingine la Musk la kuweka vituo vya kuhifadhi na kuchakata data angani kwa ajili ya usindikaji mkubwa wa data za akili bandia.

Mwezi uliopita, Elon Musk alitangaza mipango ya kuweka vituo milioni moja vya data angani; mpango anaotumai utasaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya miundombinu hiyo duniani kutokana na matumizi yanayoongezeka ya akili bandia.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanaendelea kuwa na shaka, wakitaja ukosefu wa hewa ya kupoza vipengele vya kuchakata picha (GPU), ambavyo vina jukumu muhimu katika akili bandia na kazi zinazohitaji usindikaji mkubwa wa data, katika mazingira ya utupu wa anga la juu kama moja ya changamoto kuu.

Katika majibu yake kwa mtumiaji mmoja kwenye mtandao wa kijamii wa X, Elon Musk alisema kuwa NASA itachangia chini ya asilimia 5 ya mapato ya SpaceX mwaka huu.

SpaceX ndiyo mkandarasi mkuu wa mpango wa NASA wa Artemis wa kwenda Mwezini, ambao una jukumu la kuwapeleka na kuwashukisha wanaanga kwenye Mwezi.