Nchi 5 bora zaidi kuishi duniani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Je, huwa unahisi kutaka kuacha kila kitu nyuma na kuhamia nchi nzuri ili kuanza maisha mapya?

Utafiti wa 'Expat Insider' wa mwaka 2026 umetoa orodha maalum ya maeneo 31 ya kipekee duniani kote.

Orodha hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia vigezo kama vile ubora wa maisha, uwezo wa kuzoea mazingira mapya, fursa za kazi na maendeleo ya taaluma, uthabiti wa kifedha na uwezo wa kuweka akiba, makazi, pamoja na mahitaji muhimu ya kila siku kama vile huduma za kidijitali.

Mambo mawili muhimu zaidi kwa nchi zilizoshika nafasi za juu mwaka huu yalikuwa 'uwazi na urafiki' wa watu wake pamoja na 'nafuu ya gharama za maisha'.

Kati ya nchi 10 bora, nchi 7 zilikuwa rahisi zaidi kwa mgeni kuhamia na kutulia, huku nchi 5 zikiwa vinara duniani katika masuala ya kupanga matumizi ya fedha na kuweka akiba. Tulizungumza moja kwa moja na watu wanaoishi katika nchi hizo 5 bora. Walituambia sababu za wao kuhamia huko, jinsi walivyotulia na kuzoea maisha, na mambo ambayo watu wapya wanaohamia huko wanapaswa kuyafahamu.

1. Panama

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Panama imedumisha nafasi yake ya kwanza kwenye orodha hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo. Panama inashika nafasi ya kwanza duniani kwa vipengele vyote viwili: kufanya kazi ugenini na kudhibiti gharama za maisha.

Asilimia 87 ya watu wanaoishi Panama wanasema wanafurahia maisha yao kama wageni wanaoishi nchini humo, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa asilimia 70; na asilimia 90 wanasema ni rahisi sana kupanga au kumiliki nyumba huko.

Ariel Barrionuevo alihama kutoka Argentina na kwenda kwenye pwani ya bahari ya Caribea yenye maji ya buluu na safi nchini Panama miaka 8 iliyopita.

Huko, alipata faraja kutokana na sauti tulivu ya mawimbi ya bahari, usingizi mzito na wa kustarehesha, nguvu mpya inayojaza mwili wake kila asubuhi, na furaha ya kweli ya kuishi kwa kufurahia kila wakati.

"Polepole niligundua kuwa hii haikuwa tu hali ya mapumziko ya siku chache," anasema Barrionuevo, ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa hoteli ya La Coralina Island House iliyoko Isla Colon.

"Mahali hapa pana mtindo wake wa kipekee wa maisha ulio tulivu, wa taratibu na wenye uwiano wa ajabu."

2. Mexico

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mexico imeshika nafasi ya kwanza duniani kwa urahisi wa kuzoea na kuishi katika maeneo mapya, na nafasi ya pili kwa ujumla.

Hakuna nchi inayoweza kuishinda Mexico katika kuwafanya wageni wajihisi wako nyumbani. Asilimia 73 ya raia wa Mexico wanaona kuwa ni rahisi kufanya urafiki na wenyeji, ikilinganishwa na wastani wa dunia wa asilimia 39.

Idadi ya wageni wanaoishi nchini humo ambao marafiki zao wengi ni wenyeji wa Mexico ilikuwa mara mbili ya wastani wa dunia.

"Nimepata marafiki wengi zaidi hapa kuliko nilivyopata Chicago," anasema Kirsten Rakuia, mwandishi wa blogu ya 'Sand in My Curls'.

Yeye na mumewe walihamia Puerto Vallarta mwaka wa 2022. Watu wenye urafiki na gharama nafuu za maisha ndivyo vilivyowafanya waamue kuishi hapo.

Anasema kuwa taco (chakula maarufu) kinachouzwa mtaani humo kinagharimu dola moja tu. Gharama zote za upasuaji wa dharura wa kuondoa kidole-tumbo (appendix) alioufanyiwa hivi karibuni na gharama za hospitali hazikufikia dola 4,000.

Ni jambo lisilowezekana kutumia kiasi kidogo kama hicho nchini Marekani.

3. Thailand

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Thailand inashika nafasi ya tatu katika orodha hii ya kimataifa, na watu kutoka kote duniani ndio wenye furaha na kuridhika zaidi wakiwa hapa. Asilimia 86 ya watu wameonyesha kuridhishwa na maisha yao nchini Thailand.

Jambo kuu linalofanya maisha hapa kuwa ya kufurahisha sana ni anasa na ubora wa maisha unaopatikana kwa gharama nafuu.

Thailand ilipata alama za juu zaidi duniani katika utafiti kuhusu nafuu ya gharama, huku asilimia 85 ya watu wakisifu gharama nafuu ya maisha nchini humo, kiwango ambacho ni mara mbili ya wastani wa kimataifa.

Akisimulia uzoefu wake wa kwanza wa kula chakula cha mtaani jijini Bangkok, Bethan Jeentipraphet anasema, "Sisi wote wanne tulikula mlo kamili kwa pauni moja tu, au takriban dola 1.35 ."

Bethan, mama Mwingereza mwenye watoto wawili, alikuja Thailand akitokea Devon, Uingereza, pamoja na mumewe raia wa Thailand mwaka wa 2024, akiwa na nia ya kukaa kwa mwaka mmoja tu. "Lakini ndani ya wiki mbili, niliamua sitarudi tena," alisema.

4. Falme za Kiarabu (UAE)

.

Chanzo cha picha, Getty Images

UAE imerahisisha sana kwa wageni wanaoishi huko (expats) kutulia na kujenga taaluma zao, ikipata alama za juu katika nyanja za fursa za maendeleo ya kazi na kukidhi 'mahitaji ya msingi ya wasio raia', ikiwemo masuala ya visa na lugha.

Utafiti huo ulifanyika mwezi Februari na Machi 2026, kabla na baada ya kuanza kwa mvutano kati ya Marekani na Iran; hivyo, athari za mgogoro huo hazionekani sana katika matokeo hayo.

Hata hivyo, watu wanaoishi huko kwa sasa wanasema kuwa maisha yao ya kila siku yanaendelea kama kawaida na kwa utulivu, kukiwa na marekebisho madogo tu.

Mtaalamu wa masuala ya taswira (image consultant) Michelle Sterling, ambaye amewahi kuishi Dubai na Marekani lakini sasa anapendelea zaidi Dubai, alisema, "Maisha ya kila siku jijini Dubai yanaonekana kuwa ya kawaida na ya utulivu. Ninaamini kuwa Dubai inatoa mtindo wa maisha ulio salama zaidi, wenye faraja zaidi na wa gharama nafuu zaidi."

5. Brazil

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwaka huu, Brazili imeingia katika orodha ya nchi tano bora kwa mara ya kwanza. Brazili imepata alama nzuri sana katika nyanja za furaha, urahisi wa kuzoea mazingira mapya, urafiki wa wenyeji na utamaduni wake tajiri.

Wageni wengi wamesema kuwa wanahisi wako nyumbani kutokana na uchangamfu na ukarimu wa watu wa hapa.

Clint Manning, aliyeondoka Barbados kuanzisha biashara yake mwenyewe jijini São Paulo, anasema, "Hapa, hata ukikutana na mtu mpya siku ya Alhamisi, kufikia Jumamosi unakuwa umekaa nyumbani kwake mkifurahia churrasco (nyama choma).

Mimi natoka Barbados na mtindo wa maisha kule unafanana na huu, hivyo sikuhisi kuwa mgeni hata kidogo nilipokuwa Brazili. Tofauti ni kwamba fursa na ukubwa wa mambo hapa ni mkubwa zaidi kuliko kule."

Anasema kuwa si watu wengi hapa wanaozungumza Kiingereza, na hilo ni jambo zuri. "Ni uzoefu mzuri kwa mtu ambaye kwa kweli anataka kujifunza lugha mpya," anasema.

"Kwa sababu unalazimika kuzungumza Kireno kwa ajili ya kazi na mahitaji ya kila siku. Nilijifunza kuzungumza Kireno kwa ufasaha hapa ndani ya muda mfupi zaidi kuliko muda ambao ungenichukua kwenda Denmark au Ujerumani kujaribu kujifunza lugha hiyo huko."

Imetafsiriwa na Abdalla Dzungu