Hali iko vipi katika miji mitano yenye ubora wa juu wa maisha 2026?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ripoti ya hivi punde ya Global Livability Index ya The Economist ilitaja miji bora zaidi duniani.
BBC imezungumza na wakazi wa miji hiyo kuangazia hali ya maisha ya kila siku inayofanya maeneo hayo kuwa ya kipekee kuishi.
Mji mkuu wa Denmark, Copenhagen, unasalia kuwa jiji bora zaidi kuishi duniani kwa mwaka wa pili mfululizo katika Ripoti ya Global Livability Index ya 2026.
Ukadiriaji wa kila mwaka unatathmini miji 173 kote duniani kwa kuzingatia vigezo kama utulivu, afya, utamaduni, mazingira, elimu na miundombinu ili kubaini ile inayofikia ubora wa juu wa maisha.
Vienna, Melbourne, Sydney na Zurich zinakamilisha orodha ya tano bora mwaka huu, zikionyesha utawala wa Ulaya na utendaji mzuri wa Australia.
Ili kujua hali ilivyo katika miji iliyoorodheshwa kuwa na viwango vya juu vya maisha, wakazi wanaelezea kwa nini wanapenda kuishi hapo na mahali powanapeleka wageni ili kuifurahia jiji kama wenyeji.
1. Copenhagen

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mwaka wa pili mfululizo, mji mkuu wa Denmark ulichukua nafasi ya kwanza.
Ulipata alama kamili katika uthabiti, elimu na miundombinu, na mojawapo ya ukadiriaji bora zaidi katika utamaduni na mazingira ya miji yote.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa wakazi wake, hii inatafsiriwa kama kufurahia maisha kwa gharama nafuu, hali ambayo ni sehemu ya maisha ya kila siku.
"Unaweza kuendesha baisikeli kwenda kazini, kutembea bandarini baadaye, na kurejea kwa wakati kwa chakula cha jioni. Hili halifanyiki siku maalum, leo ni Jumanne tu," anasema Laura Amira Kassem, mwanafunzi wa udaktari ambaye ameishi katika jiji hilo kwa miaka minane.
"Mchanganyiko huo wa miundombinu inayokuwezesha kuendesha baiskeli, na mikondo ya maji unayoweza kuogelea, kusema kweli ni kitu ambacho sijawahi kushuhudia mahali pengine popote."
Kassem huanza siku zake kwa kukimbia mapema asubuhi mahali tulivu, kama vile Utterslev Mose au kando ya maziwa, ikifuatiwa na kifungua kinywa, kahawa na, wakati wa kiangazi, kuogelea.
Kuhusu kile kinachoonyesha wageni, ziara yoyote ya kuongozwa huanza katika kitongoji cha kitamaduni cha Nørrebro.
"Soko safi la matunda na mboga mboga, stendi za kebab na maduka ya vito ziko karibu na mikate ya unga, baa za divai asilia na mikahawa midogo," anafafanua.
Kuanzia hapo, anapendekeza kukodisha baiskeli kwenda kuogelea na kunywa kahawa karibu na ufuo wa Nordhavn, ikifuatiwa na chakula cha mchana na smørrebrød, sandwich ya kitamaduni ya mkate wa kiasili, huko Det Gamle Apotek.
Mchana, wakimbiaji wanaweza kujiunga na Loopet, mzunguko wa kilomita 3 kuzunguka Fælledparken, ambapo jumuiya inayoendesha jiji hukusanyika.
"Kila mtu anakaribishwa," anasema Kassem. "Kimbia, kutana na marafiki, na umalize na chakula cha jioni kinachoandaliwa sehemu ya wazi au nje."
2. Vienna

Chanzo cha picha, Getty Images
Huenda mji mkuu wa Austria ulipoteza nafasi ya kwanza kwa Copenhagen mwaka jana, matokeo yake bora katika nyanja za afya na elimu yanauweka katika nafasi ya pili.
Kwa wakazi wake, ubora wa maisha jijini Vienna unatokana na urahisi wakufikia sehemu yoyote jijini—iwe ni kwa usafiri wa umma au kwa miguu—na kufurahia maelezo madogo madogo ya safari hiyo.
"Utaratibu wangu wa kila siku ni kwenda kazini nikipita kwenye barabara ya Ringstrasse, nikitumia moja ya treni za umeme (trams) maarufu za hapa," anasema Franziska Hochmüller, mfanyakazi katika Ofisi ya Utalii ya Vienna.
"Badala ya kuangalia simu yangu, napenda kusoma kitabu au kungalia tu majengo mazuri ninayopita. Ni jambo dogo linalonikumbusha kila siku jinsi mambo ya 'kawaida' yalivyo ya kipekee jijini Vienna."
"Katika wilaya namba 1 hadi 9, usafiri wa umma hauhitajiki sana," anaongeza Roland Eggenhofer, kutoka idara ya mauzo na masoko ya MOTTO Hotel.
Anapenda kuwapeleka wageni katika wilaya ya 6 na 7, hasa maeneo ya Neubaugasse na Spittelberg, kutokana na uuwepo wa migahawa, maduka ya mitindo na mazingira tulivu, pamoja na soko la Naschmarkt lilo na vyakula mbalimbali vya kimataifa.
Wakati wa vuli, anapendekeza kutembelea *Heuriger*—aina ya baa ya divai iliyoko kwenye mashamba ya mizabibu viungani mwa jiji—ili kuonja glasi ya divai ya ndani ya Vienna.
Ili kuelewa vyema maisha ya Vienna, Hochmüller anawashauri wageni kutembelea soko la Kutschkermarkt katika wilaya ya 18, ambalo huwa na soko la wakulima kila Jumamosi, pamoja na migahawa na maeneo ya kunywa kahawa.
"Kuona familia, wapenzi na wazee wakifanya manunuzi yao ya wiki au wakifurahia kahawa tu ni jambo la kawaida sana jijini Vienna," anasema.
Baada ya miaka kadhaa kuishi jijini humo, mdundo wa maisha bado unamvutia Hochmüller.
"Hata katika jiji kubwa, daima kuna fursa ya kupunguza kasi ya maisha," anasema.
"Iwe ni kwenye mkahawa, bustanini au ukingoni mwa Mto Danube, muda hupita kwa namna tofauti jijini Vienna."
3. Melbourne

Chanzo cha picha, Getty Images
Melbourne iliishinda mpinzani wake wa pwani, Sydney, na kushikilia nafasi ya tatu kutokana na alama zake za pamoja za utamaduni na mazingira kufikia 96—moja ya alama za juu zaidi katika orodha hiyo.
Kwa wakazi wake, utajiri huu wa kitamaduni unaonekana ubora wa vitongoji vyake, ambapo kila eneo lina sifa ya kipekee.
"Melbourne ni jiji kubwa ambalo, mienendo ya wakazi wake ni kama ya mji mdogo," anasema Anne Marie Lennon, meneja mkuu wa hoteli ya Crowne Plaza Carlton, ambaye amewahi kufanya kazi Uingereza, Ireland na Australia.
"Hapa, watu wana shauku ya kweli ya kukufahamu. Kisha kuna utamaduni, chakula, muziki, mitindo na sanaa. Kila kitongoji kina mazingira na utambulisho wake."
Lou McGregor, raia wa Scotland anayeishi Melbourne kwa miaka 20, anakubaliana na hilo.
"Footscray ni kitongoji changu na ni mojawapo ya maeneo bora zaidi ya kula na kunywa jijini: mchanganyiko wa tamaduni, vyakula na mazingira yenye uchangamfu wakati wote," anasema.
"Fitzroy ina baa ndogo za kuvutia na maduka ya bidhaa za zamani; St Kilda ni mahali pazuri pa kutembea kando ya ufukwe, na Carlton haina mpinzani kwa kufurahia vyakula vya Kiitaliano na kutembea katika mitaa yake mizuri ya zamani."
McGregor anapopokea wageni, huwapeleka kwenye chumba cha kusomea chenye umbo la kuba katika Maktaba ya Jimbo (State Library), eneo la sanaa ya mtaani inayobadilika-badilika la Hosier Lane, Jumba la Sanaa la Kitaifa la Victoria (National Gallery of Victoria), pamoja na vichochoro na maeneo ya maduka yenye sifa ya kipekee.
"Hiyo ndiyo Melbourne kwangu: jiji lenye udadisi na ubunifu, lililojaa matukio madogo yasiyotarajiwa kila kona," anasema.
Ili kupata taswira ya maisha ya kila siku jijini Melbourne, Lennon anapendekeza wageni watembelee Hifadhi ya Princes (Princes Park) yenye ukubwa wa hekta 39.
"Watu wanaotembea na mbwa, wanaokimbia kwa mazoezi, familia, na watu waliokaa tu na kupumua hewa safi. Ni mahali tulivu na halisi. Hiyo ndiyo Melbourne ninayoishi kila siku, na sichoki kamwe nayo," anahitimisha.
"Unaweza kutembea kilomita 2 na kuhisi kana kwamba umeingia katika ulimwengu tofauti kabisa."
4. Sydney

Chanzo cha picha, Getty Images
Jiji la Sydney linashikilia nafasi ya nne sawa na Melbone likiwa na alama kamili katika nyanja za afya na elimu.
Hata hivyo, wakazi wanasema kuwa urahisi wa kufurahia mazingira ya asili, mitaa yenye mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali, na mtindo wa maisha wa nje ndivyo vinavyofanya jiji hili kuwa mahali pazuri pa kuishi.
"Sydney inafanya mambo kuwa rahisi kwa sababu, popote ulipo, huwezi kuwa mbali na mandhari ya kuvutia, iwe ni bandari, Milima ya Blue (Blue Mountains), au fukwe," anasema Steve Kamper, Waziri wa Ajira na Utalii wa New South Wales.
"Mchanganyiko wa tamaduni, mitaa yake, vyakula vya kipekee, na mtindo wa maisha hufanya Sydney kuwa mahali pa pekee. Ni jiji la kimataifa, lakini bado linatoa hisia ya kuwa mkusanyiko wa jamii za wenyeji."
Ili kugundua hili, Kamper anashauri kwenda nje ya maeneo ya kawaida ya watalii kama vile Harbour Bridge au Bondi, na kutembelea vitongoji vya magharibi mwa jiji.
"Burwood ndiyo Sydney inayojulikana na kupendwa na wenyeji," anasema.
"Ni eneo lenye uchangamfu, lililojaa vyakula vitamu, na ni mojawapo ya maeneo bora zaidi ya kujionea utamaduni mseto wa Sydney."
Pia anapendekeza kuwapeleka wageni kutazama mechi ya soka la 'Australian Rules'; anasema, "ni maeneo machache sana duniani yanayotoa burudani ya michezo kama Sydney."
Baada ya kuishi katika mabara manne, mbunifu wa vito kutoka Ufaransa, Julie Livni, bado anavutiwa sana na Sydney.
"Watu hawasubiri wikendi ili kwenda ufukweni au kuogelea; wanajumuisha shughuli hizo katika ratiba yao ya kila siku," anaeleza.
Kwa upande wake, ubora wa maisha huanza na matembezi ya kila siku alfajiri kutoka Bondi hadi Bronte akiwa na marafiki zake.
"Kama mfanyabiashara na mama wa watoto wawili, maisha huenda kwa kasi sana, hivyo saa hiyo moja kando ya bahari ni njia yangu ya kutulia na kuachana na msongo wa mawazo," anasema. "Ni njia bora zaidi ya kuanza siku."
Kwa kawaida yeye huwapeleka wageni wake kwenye ufukwe wa Tamarama kutazama jua likichomoza, kisha kunywa kahawa Bondi, na baadaye kupanda feri kutoka Rose Bay.
"Si lazima kwenda mahali fulani mahususi, bali ni kwa ajili ya kufurahia kutazama jengo la Opera House na bandari ukiwa majini," anasema, huku akisimama kupata chakula cha mchana katika mgahawa wa Uncut Seafood.
"Sydney pia ina mchanganyiko mkubwa wa tamaduni, vyakula vya hali ya juu na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, lakini bado inadumisha hali ya utulivu na amani," anaongeza.
"Ni mchanganyiko wa kipekee unaopatikana jiji kubwa."
5. Zurich

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya kushuka kutoka nafasi ya pili ya pamoja mwaka wa 2025 hadi nafasi ya tano mwaka huu, wakazi wanasema kuwa mchanganyiko wa ufanisi na urahisi wa kufikia maeneo ya asili ndio msingi wa ubora wa kipekee wa maisha jijini Zurich.
"Zurich isingekuwa vile ilivyo bila ziwa na mito yake. Kila siku napita kando ya Ziwa Zurich, Mto Limmat, au Mto Sihl na kutenga muda kwa ajili yangu mwenyewe," anasema Manuela Leonhard, mkazi wa asili wa Zurich na mtayarishaji wa maudhui.
"Maji yake ni safi na yako wazi kabisa, na tuna zaidi ya chemchemi 1,200 za maji ya kunywa kote jijini."
Ili kuwaonyesha wageni sababu inayomfanya aipende sana Zurich, huwapeleka Lindenhof, ngome ya zamani ya Warumi ambayo sasa imebadilishwa kuwa uwanja wa wazi juu ya kilima unaotazama Mto Limmat na mji wa kale uliopo pande zote mbili za mto huo.
Pia anapendekeza maeneo ya wazi (materaso) ya ETH Zurich na Chuo Kikuu cha Zurich kwa ajili ya kutazama mandhari nzuri ya jiji zima.
"Na huwa nawapeleka kutembea katika mji wa kale, ambao ndio moyo wa Zurich, wenye mitaa midogo na maduka madogo," anaongeza.
Hata baada ya kuishi maisha yake yote Zurich, Leonhard bado anashangazwa na jinsi jiji hilo linavyotunzwa kwa ustadi mkubwa.
"Haijalishi ni tukio gani kubwa linalofanyika Zurich, asubuhi iliyofuata haiwezekani kutambua kilichotokea usiku uliopita," anaelezea.
"Hilo hunishangaza kila wakati."














